31-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kukiri Kuidhulumu Nafsi Kwa Makosa Na Kuomba Maghfirah

 

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

31-Kukiri Kuidhulumu Nafsi Kwa Makosa Na Kuomba Maghfirah

 

 

"رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي"

 

Rabb wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu”[Al-Qaswas: (16)]

 

Ni du’aa ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam).  Ni du’aa muhimu ambayo inabidi tuizingatie.  Inabainisha litakiwalo kwa mtu kushikamana nalo wakati wa fitnah na misukosuko, na namna ya kuamiliana na hali kwa mujibu wa Manhaj ya Allaah isiyo na kombo na njia iliyonyooka ambayo mwenye kushikamana nayo hatopotea duniani na wala hataishia pabaya aakhirah.

 

Sababu ya du’aa hii ni kuwa Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimuua Mkoptik kwa makosa bila kukusudia.  Ni pale Muizrael ambaye ni katika watu wake alipomwomba amsaidie dhidi ya Mkoptik.  Muwsaa akampiga ngumi moja akafa pale pale.  Akalichukulia hilo ni dhambi kwa kuua nafsi ambayo Allaah Hakumwamuru kuiua.

 

Katika du’aa hii, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) ameanza kwa kukiri kosa lake na kuonyesha majuto.  Majuto yake yalimsukuma kunyenyekea kwa Mola wake na kumwomba maghfirah.  Na kwa kuwa kosa lenyewe si la kukusudia, basi bila shaka alijua kwamba Allaah Atamsamehe, lakini pamoja na hivyo akaomba maghfirah.  Hii ndiyo hali ya Nabiy wa Allaah.  Basi vipi hali yetu sisi tunaofanya madhambi usiku na mchana bila kujali wala kuhisi lolote?!

 

Bila shaka kila mmoja wetu anatakikana asimame na kuitaamuli hali yake na hatima yake.  Kila mtu atawajibishwa kwa kila dogo na kubwa.  Leo ni matendo hakuna hisabu, na kesho ni hisabu hakuna matendo.

 

 

Tunayojifunza kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Kukiri kosa ni toba pamoja na kulijutia, kuachana nalo kabisa na kuweka azima ya kutolirudia tena.

 

 

2-  Kukiri kwanza kosa na kukiri kuidhulumu nafsi kabla ya du’aa, ni katika viwajibisho vya kujibiwa du’aa.

 

 

3-  Aliyefanya dhambi anatakiwa aharakie kutubia na kurejea kwa Allaah hapo hapo.

 

 

4-  Kukiri kwamba mtu kaidhulumu nafsi yake na kuomba maghfirah toka kwa Allaah, ni katika nyenendo za Manabii na Mitume.  Ni kama walivyosema baba na mama yetu Aadam na Hawwaa:

 

"قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنْفُسَنَا وَإِنْ لَمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"

 

Wakasema:  Rabb wetu!  Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”.  [Al A’araaf: (23)].

 

5-  Du’aa hii inadulisha namna ambavyo Allaah Anapenda kuikubali tawbah ya Mja Wake na kumghufuria.  Muwsaa baada tu ya kuomba du’aa hii, Allaah Alimsamehe kosa lake.  Aayah kamili inasema:

 

قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

 

Akasema:  Rabb wangu!  Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, basi Nighufurie; Akamghufuria.  Hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [Al-Qaswas: (16)].

 

 

6-  Kutawassal kwa Jina la Rabbu kunanasibiana na du’aa za haja zote.

 

 

Share