35-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Usaidizi Dhidi Ya Mafisadi

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

35- Usaidizi Dhidi Ya Mafisadi

 

 

"رَبِّ انصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ"

 

(Luutw) akasema:  Rabb wangu!  Ninusuru dhidi ya watu mafisadi. [Al-‘Ankabuwt:  (30)].

 

Hii ni du’aa ya Nabiy Luutw (‘Alayhis Salaam).  Nabiy huyu alitumwa kwa watu waliokuwa wamejumuisha kati ya ushirikina, ukafiri na kitendo kibaya mno cha kuchukiza.  Walikuwa wakiwaendea wanaume kinyume na maumbile kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na yeyote katika waliotangulia.  Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ametuhadithia ulinganio wa Nabiy huyu.  Watu hawa walikaidi na kuukataa ulinganio huo hata mkewe ambaye ndiye mtu wa karibu zaidi.  Alipokata tamaa, Nabiy Luutw aliwaapiza baada ya kuzidi kubobea kwenye uchafu wao na ukafiri.  Na hata walithubutu kuwataka kimatamanio Malaika wa adhabu walipomjia Nabiy Luutw na habari ya furaha wakiwa katika maumbile ya kibinadamu.  Alipoona hali hiyo, Nabiy Luutw alielekea kwa Mfalme, Mwenye uwezo na Mwenye Kusikia kila kitu na kuomba akisema: “Rabb wangu!  Ninusuru”.

 

Alimwomba Allaah Amnusuru wasiweze kufikia dhamira yao kwa kuwateremshia adhabu iliyoahidiwa.  Akatawassali kwa Jina Tukufu la Allaah la Rabb lenye maana ya ulezi, usimamizi, kuleta manufaa, kuondosha madhara, na kudabiri mambo.  Akawaelezea watu wake kuwa ni mafisadi kwa kuwa ufisadi wao huo ulifungua njia kwa vizazi vilivyofuatia hadi leo kama hali tunavyoiona. Kampeni zimechachamaa kuhalalisha jambo hilo ili kionekane kitu cha kawaida, ndoa za jinsia moja zinatangazwa hadharani bila kukemewa na hata baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wamehudhuria kwenye mikutano au minasaba mikubwa na wake zao waume.

 

Na kutokana na kitendo hicho chao kibaya na kichafu mno cha kuwaingilia wanaume, Allaah Aliwaadhibu adhabu kali mno ya kuupindua mji wao juu chini, chini juu:

 

"فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ"

 

Basi ilipokuja Amri Yetu, Tuliupindua (mji wao) juu chini, na Tukauteremshia mvua ya mawe ya udongo mgumu uliookwa yenye kuandamana”.  [Huwd: (82)].

 

Kama walivyopindua maumbile asili, Allaah Naye Akapindua miili yao, nyumba zao na mji wao kiujumla kama adhabu inayowafikiana na matendo yao.

 

Katika kisa hiki, kuna mazingatio na maelekezo kwetu kwamba tukimbilie kwa Allaah kuomba hifadhi, na tujilinde Kwake kutokana na munkarati potoshi zenye kuharibu moyo, akili, mwili na silka salimu.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Hakuna mwenye uwezo wa kuhifadhi isipokuwa Allaah Pekee.

 

 

2-  Mwombaji anatakiwa aepukane na mafisadi ili yasimkute yaliyowapata watu wa Luutw, na pia amwombe Allaah Amsaidie kufanikisha hilo.

 

 

3-  Umuhimu wa kutawassali kwa Allaah kwa kuwaapiza mafisadi.  Ni kama lilivyodulisha tamshi: “Ninusuru”, na hakusema: “Nilinde”, na hii inaonyesha hatari yao kubwa, na kwamba mwenye kunusuriwa na watu hao, basi kwa hakika amenusuriwa nusra ya nguvu kutoka kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

Share