37-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kutimiziwa Nuru Na Kughufuriwa

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

37-Kutimiziwa Nuru Na Kughufuriwa

 

 

 

"رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ"

 

“Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza”.  [At-Tahriym: (66)].

 

Du’aa hii yenye manufaa ni ya Waumini Siku ya Qiyaamah wakati nuru ya wanafiki itakapozimika (tunajilinda kwa Allaah na hilo).  Na nuru hii, ni moja kati ya alama ambazo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atawatambua kwayo umati wake.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَنَا أَوَّلُ مَنْ يُؤْذَنُ لَهُ بِالسُّجُودِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَأَوَّلُ مَنْ يُؤْذَنُ لَهُ أَنْ يَرْفَعَ رَأْسَهُ، فَأَرْفَعُ رَأْسِي فَأُنْظِرُ بَيْنَ يَدَيَّ، فَأَعْرِفُ أُمَّتِي مِنْ بَيْنِ الْأُمَمِ))، فَقَالَ رَجُلٌ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، فَكَيْفَ تَعْرِفُ أُمَّتَكَ مِنْ بَيْنِ الْأُمَمِ؟ مَا بَيْنَ نُوحٍ إِلَى أُمَّتِكَ؟ قَالَ: ((غُرٌّ مُحَجَّلُونَ مِنْ أَثَرِ الْوُضُوءِ، ولَا يَكُونُ لِأَحَدٍ مِنَ الْأُمَمِ غَيْرِهِمْ، وَأَعْرِفُهُمْ أَنَّهُمْ يُؤْتَوْنَ كُتُبَهُمْ بِأَيْمَانِهِمْ، وَأَعْرِفُهُمْ بِسِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِمْ مِنْ أَثَرِ السُّجُودِ، وَأَعْرِفُهُمْ بِنُورِهِمُ الَّذِي بَيْنَ أَيْدِيهِمْ، وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ، وَعَنْ شَمَائِلِهِمْ"

“Mimi ndiye wa mwanzo atakayeruhusiwa kusujudu Siku ya Qiyaamah, na ndiye wa mwanzo atakayeruhusiwa kunyanyua kichwa chake.  Nitanyanyua kichwa changu na moja kwa moja nitaonyeshwa mbele yangu.  Hapo nitautambua umati wangu kati ya nyumati nyinginezo.  Mtu mmoja akauliza: Ee Rasuli wa Allaah!  Vipi utautambua umati wako katikati ya nyumati zinginezo?  Kipindi cha kati ya Nuwh hadi umati wako?  Akasema:  Watakuwa na nuru usoni mwao, mikononi na miguuni mwao kutokana na athari za wudhuu, na hatakuwa nayo yeyote katika nyumati nyinginezo isipokuwa wao tu.  Na nitawajua kwamba wao watapewa madaftari yao kwa upande wao wa kuume.  Na nitawajua kwa alama zao kwenye nyuso zao kutokana na athari ya sijdah.  Na nitawajua kwa nuru yao ambayo itakuwa mbele yao, kuliani mwao na kushotoni mwao”.   [Imekharijiwa na Ahmad. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

Waumini hawa watamwomba Allaah wakisema:  “Ee Rabbi wetu!  Tutimizie nuru yetu”.  Wataomba waendelee kuwa na nuru yao hiyo mpaka pale watakapofika Jannah Nyumba ya amani.  Na hii ni pale watakapoona nuru ya wanafiki imewazimikia, nao wataingia khofu nuru yao nayo isije kuzima.

 

Imenukuliwa toka kwa Adh-Dhwahhaak akisema:  “Hakuna yeyote isipokuwa atapewa nuru Siku ya Qiyaamah.  Watu watakapofika kwenye Swiraat, nuru ya wanafiki itazima.  Na Waumini wakiona hivyo, wataingia khofu ya kuzimikiwa nuru yao kama ilivyozimika nuru ya wanafiki hao”.

 

Halafu Waumini hao wataelezea sababu ya wao kuomba hilo wakisema: “Hakika Wewe juu ya kila kitu Ni Muweza”.

 

Kana kwamba wanasema:  “Ee Rabbi wetu!  Hatukukuomba hili isipokuwa tu kwamba sisi tunajua kuwa Wewe ni Muweza wa kila kitu.  Hakikushindi chochote, basi Tutimizie kheri hii na Ibakishe mpaka tufike kwenye Nyumba ya amani (Daarus Salaam) Uliyotuahidi”.

 

Na nuru hii ee ndugu yangu Muislamu, itakuwa kwa mujibu wa ‘amali zako hapa duniani.  Malipo ni kwa mujibu wa kazi.  Imesimuliwa toka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu) akiizungumzia aayah hii: “Watagaiwa nuru yao kwa mujibu wa ‘amali zao wakipita juu ya Swiraat.  Kati yao kuna ambaye nuru yake itakuwa mfano wa mlima, na wengineo kuna ambaye nuru yake mfano wa mtende.  Mwenye nuru ya chini zaidi ni yule itakayokuwa mfano wa kidole chake cha gumba; mara inazimwa, mara inawashwa”.

 

Na Muislamu anatakiwa amwombe Allaah Ta’aalaa Amtimizie nuru yake kamili hapa hapa duniani ili Amtimizie nuru kamili Siku ya Qiyaamah juu ya Swiraat. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Mola wake Tabaaraka wa Ta’alaa Amruzuku nuru kwenye sehemu zote za mwili wake mtukufu ili ikamilike kwake ‘ilmu, maarifa na uongofu.  Alikuwa akiomba:

 

 

"اللهُمَ اجعَل فِي قَلبِي نُوراً وفِي سَمعي نُوراً وعَن يَمينِي نُوراً وعن يَسارِي نُوراً وفَوقِي نُوراً وتَحتِي نُوراً وأَمامِي نُوراً وخَلفِي نُوراً وأَعظِم لِي نُوراً"

 

“Ee Allaah!  Jaalia ndani ya moyo wangu nuru, na kwenye masikio yangu nuru, na kuliani kwangu nuru, na kushotoni kwangu nuru, na juu yangu nuru, na chini yangu nuru, na mbele yangu nuru, na nyuma yangu nuru, na Nikuzie nuru yangu”.  [Al-Bukhaariy:  Kitaabu Ad Da’awaat, na Muslim:  Kitaabu Swalaatil Musaafiriyn wa Qaswrihaa. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

 

Du’aa hii ina faida zifuatazo:

 

 

1-  Kuna umuhimu mkubwa sana wa kumwomba Allaah du’aa hii, kwani ndani yake kuna maombi mawili yanayohusu dini, dunia na aakhirah:

 

 

(a)  Kutimiziwa nuru, yaani kuenezewa, ambapo kati ya athari zake ni ‘ilmu, uongofu na iymaan.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiiomba nuru wakati anapokwenda kwenye Swalah, wakati anaposujudu na wakati anaposimama usiku kwa ‘ibaadah.

 

 

(b)  Kumwomba Allaah maghfirah ya madhambi.  Ndani ya hili kuna kinga dhidi ya shari zote ambapo kubwa yake zaidi ni moto (Allaah Atulinde nao).

 

 

3-  Kutawassul kwa Jina la Allaah la “Al-Qadiyr” kunanasibiana na ombi lolote liwalo.

 

 

4-  Kwamba kati ya matunda makuu ya tawbah ya kweli iliyokamilisha masharti, ni kufaulu na kupata amani kwenye Nyumba ya Amani.

 

 

5-  Du’aa ina fadhla kubwa, na kwamba manufaa yake ya kidunia na kiaakhirah, yanarudi kwa mwombaji mwenyewe.  Haijalishi cheo chake wala nafasi yake.

 

 

Share