38-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Maghfirah Kwako, Wazazi Na Waumini

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

38- Maghfirah Kwako, Wazazi Na Waumini

 

 

 

"رَّبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِمَن دَخَلَ بَيْتِيَ مُؤْمِنًا وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا تَبَارًا"

 

Rabb wangu! N ighufurie mimi, na wazazi wangu wawili, na kila aliyeingia nyumbani mwangu akiwa Muumini, na Waumini wa kiume na Waumini wa kike, na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa”.  [Nuwh: (28)].

 

 

Hii ni du’aa miongoni mwa du’aa za Nabiy Nuwh (‘Alayhis Salaam). Imekusanya maombi ya dunia na aakhirah.  Amejiombea mwenyewe maghfirah, amewaombea wazazi wake, na amewaombea waumini wote walio hai na waliokufa kuanzia Aadam (‘Alayhis Salaam) mpaka kitakaposimama Qiyaamah. Aliiomba wakati alipojua kupitia Wahyi kwamba hakuna yeyote katika umati wake atakayeamini zaidi ya wale waliokwisha muamini.

 

 

Akaanza kujiombea mwenyewe maghfirah.  Hili linatakiwa kwa Muislamu ajianze yeye mwenyewe kabla ya mwingine yeyote.  Nafsi yake ina haki zaidi kwake kuliko mwingine yeyote.

 

 

Akawaombea pia maghfirah wazazi wake wawili kutokana na fadhla yao kubwa kwake.  Hili pia tumeamuriwa sisi tulifanye kwa wazazi wetu.

 

 

Halafu maghfirah hiyo hiyo akamwombea kila Muumini anayeingia nyumbani kwake.  Kwa kuwa kusuhubiana nao kuna usalama na uthabiti katika dini.  Na hili linatudokeza kuwa marafiki zetu ni lazima wawe watu wema ambao kama wataingia nyumbani kwako utahisi utulivu kwa kila jambo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

"لاَ تُصَاحِبْ إِلاَّ مُؤْمِنًا، وَلاَ يَأْكُلْ طَعَامَكَ إِلاَّ تَقِيٌّ"

 

 

“Usiandamane isipokuwa na Muumini, na asile chakula chako isipokuwa mchaji”.  [Abu Daawuwd: Kitaabul Adab]

 

 

Du’aa hii kwa hakika ina umuhimu mkubwa mno. Na hii ni kwa haya:

 

 

(a)  Ni kwamba du’aa za Manabii zinajibiwa.  Nasi tunatumai kwa yakini Allaah Atazijibu du’aa walizotuombea.

 

(b)  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa bishara njema ya kupata malipo makubwa kwa du’aa hii.  Amesema:

 

"مَنِ اسْتَغْفَرَ لِلْمُؤْمِنِيْنَ وَالْمُؤْمِنَاتِ، كَتَبَ اللهُ لَهُ بِكُلِّ مُؤْمِنٍ وَمُؤْمِنَهٍ حَسَنَةً"

 

“Mwenye kuwaombea maghfirah Waumini wa kiume na Waumini wa kike, Allaah Atamwandikia jema kwa kila Muumini wa kiume na Muumini wa kike”. [Musnad Ash-Shaamiyyiyn cha At-Twabaraaniy. Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan]

 

Hebu angalia ukubwa wa malipo haya!  Kila jema moja malipo ni kumi mfano wake hadi nyongeza nyingi maradufu kwa mabilioni ya Waumini wa tokea Aadam hadi Siku ya mwisho.  Na hii inaonyesha ukubwa wa Fadhla za Allaah kwa Waumini.

 

Kisha Nabiy Nuwh akaimalizia du’aa yake kwa kusema:  “Na wala Usiwazidishie madhalimu isipokuwa kuteketea kabisa”.   Du’aa hii inamjumuisha kila dhalimu tokea alipoiomba hadi Qiyaamah.  Na kwa vile du’aa za Manabii hujibiwa, basi kila dhalimu itampata tu.

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Kuna umuhimu mkubwa sana wa kumwomba Allaah Ta’aalaa maghfirah. Maghfirah ni katika sababu kubwa za kuingia Jannah.

 

 

2-  Mwombaji aombe la muhimu zaidi kisha linalofuatia kwa umuhimu.

 

 

3-  Kuna umuhimu mkubwa wa kuwaombea wazazi wawili maghfirah. Ni wema kwao wakiwa hai au maiti.

 

 

4-  Muislamu anatakiwa asiwasahau nduguze Waislamu katika du’aa zake pamoja na dhuria wake.

 

 

5-  Mwenye kukithirisha du’aa hii basi atajibiwa bila shaka kutokana na mambo mawili:

 

 

(a)  Ni du’aa ya Nabiy ambaye ni katika wale Watano (Ulul ‘Azm).

 

 

(b)  Ni du’aa ya siri, kwa kuwa anaowaombea wakiwa hawamjui wala yeye hawajui.

 

 

6-  Umuhimu wa kutawassal kwa Jina la Rabb.  Ni mwenendo wa Manabii na Mitume wote.

 

 

7-  Inajuzu kuwaombea mabaya madhalimu, na hasa madhara yao yanapowagusa watu.

 

 

8-  Inapendeza mwombaji aeleze sababu ya du’aa yake.

                                       

 

 

Share