Skip navigation.
Home kabah

Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha Baina Ya Watu Wachukiane) 2 - Sababu za Kufitinisha, Sifa Za Mfitinishaji

24 Rabiy'ul Aakhir  1428

Kufitinisha baina ya watu ni jambo ovu linalochukiza mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ambaye Ametuamrisha tuepukane nalo kama Anavyosema:

 

((وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ))

((Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui)) [Al-Maaidah :2]

 

Vile vile Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ))

 

((Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Allaah Hawapendi mafisadi)) [Al-Qaswas: 77]

 

Sababu zinazomfanya mtu afitinishe:

 

1.       Ujinga wa kutokujua makatazo yake katika Qur-aan na hatari yake na adhabu zake kutoka kwa Mola Muumba.

 

2.      Nafsi kuwa na chuki na uhasidi wa kuona ndugu wawili wanapendana na kushirikiana katika mambo yao. Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عن أبي هُريرةَ رضي اللهُ عنه قال: قال رسوُل الله صلى الله عليه وسلم : ((لا تَحَاسَدُوا، ولا تَنَاجَشُوا، ولا تَباغَضُوا، ولا تَدَابَرُوا،  ولا يَبعْ بَعْضُكُمْ على  بَيْعِ بَعْضٍ، وكُونُوا عِبادَ اللهِ إخْوَاناً، المُسْلمُ أَخُو المُسْلمِ: لا يَظْلِمُهُ، ولا يَكْذِبُهُ، ولا يَحْقِرُهُ، التَّقْوَى هاهُنا))  ويُشِيرُ إلى صَدْرِه ثَلاثَ مَرَّاتٍ – ((بِحَسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أن يَحْقِرَ أخاهُ المُسْلِمِ، كُلُّ المُسْلِمِ على الْمسْلِم حَرَامٌ: دَمُهُ ومالُهُ وعِرْضُهُ")) رَوَاهُ مُسْلِمٌ   

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema:  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msioneane choyo, wala msizidishiane bei (za vitu), wala msichukiane, wala msipigane mapande (msitengane), wala msishindane kwa kupunguza bei.  Lakini kuweni ndugu, enyi  waja wa Allaah, Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake, hamdhulumu wala hamvunji, hamwambii uongo wala hamdharau. Ucha Mungu  uko hapa (huku akiashiria kifuani kwa vidole vyake mara tatu) Ni uovu wa kutosha kwa mtu kumdharau ndugu yake Muislamu. Muislamu ameharamishiwa kwa Muislamu mwenzake: damu yake, mali yake na heshima yake [Yaani haramu kuchukua mali ya mwenzako, kumuua na kumdhalilisha] [Imesimuliwa na Muslim]  

 

3.     Kutaka kujikurubisha zaidi kwa mmoja wao aidha kwa kuona wivu kuwa wa kwanza hampendi kama anavyompenda wa pili.

 

4.     Kufuata maslahi yanayopatikana kwa mmoja wao ili afaidike naye baada ya kumfitinisha mwenzake.

 

Sifa za An-Nammaam (mwenye kufitinisha)

 

1.     Ni mwenye kupenda kuapa sana kwani hakuna mwenye kupenda kuapa sana isipokuwa mtu asiye mkweli.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ)) (( هَمَّازٍ مَّشَّاء بِنَمِيمٍ)) 

((Wala usimtii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa))

 

((Mtapitapi, apitaye akifitini)) [Al-Qalam: 10-11]

 

 

 

2.      Mwenye kupenda kusengenya na kuwatia aibu wenziwe aidha kwa kauli zake, au ishara wakiwa mbele yake au nyuma yake.

 

3.      Mwenye moyo mchafu usiopendelea kheri kwa wenzake.

 

4.      Huzidisha wema kwa wengine aonekane kuwa ni mwema, mwenye maneno mazuri. 

 

5.      Mwenye kupenda kulaumu bure bure almuradi tu akutie katika aibu kuwa una makosa japo atafute sababu yoyote imridhishe tu kuwa yeye ni mkweli na mwenziwe ni mkosa. 

 


 
 
*****