01-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Fadhila za Kumswalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

باب الأمر بالصلاة عَلَيْهِ وفضلها وبعض صيغها

01-Mlango Wa Fadhila za Kumswalia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Alhidaaya.com

 

قال الله تَعَالَى :

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake Wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini! Mswalieni na msalimieni kwa maamkizi ya amani. [Al-Ahzaab: 56]

 

Hadiyth – 1

وعن عبد الله بن عمرو بن العاص ، رضي الله عنهما : أنَّه سمع رسول الله صلى الله عليه وسلم ، يقول : (( مَنْ صَلَّى عَلَيَّ صَلاةً ، صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ بِهَا عَشْراً )) . رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa 'Abdillaah bin 'Amruw bin Al-'Aas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kuwa alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Mwenye kuniswalia mimi mara moja, Allaah humteremshia rehema Zake kwake mara kumi." [Muslim]

 

Hadiyth – 2

وعن ابن مسعود رضي الله عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( أَوْلَى النَّاسِ بِي يَومَ القِيَامَةِ أكْثَرُهُمْ عَلَيَّ صَلاَةً )) . رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن )) .

Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watakaopewa kipaumbele na kuwa karibu nami Siku ya Qiyaamah ni watu wanao niswalia mimi mara nyingi zaidi." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan]

 

Hadiyth – 3

وعن أوس بن أوس رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم: (( إنَّ مِنْ أفْضَلِ أيَّامِكُمْ يَومَ الجُمُعَةِ ، فَأكْثِرُوا عَلَيَّ مِنَ الصَّلاةِ فِيهِ ، فَإنَّ صَلاَتَكُمْ مَعْرُوضَةٌ عَلَيَّ )) . قَالَ : قالوا : يَا رسول الله ، وَكَيفَ تُعْرَضُ صَلاتُنَا عَلَيْكَ وَقَدْ أَرَمْتَ ؟! قَالَ : يقولُ بَلِيتَ . قَالَ : (( إنَّ اللهَ حَرَّمَ عَلَى الأرْضِ أَجْسَادَ الأَنْبِيَاءِ )) . رواه أَبُو داود بإسنادٍ صحيح .

Imepokewa kutoka kwa Aws bin Aws (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika siku iliyo bora kabisa kwenu ni siku ya Ijumaa. Hivyo, zidisheni kuniswalia kwayo, kwani Swalaah zenu zinafikishwa kwangu." Wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Na vipi Swalaah zetu zitakufikia wakati ambapo utakuwa umezikwa tayari na kuwa mchanga?" Akawajibu: "Hakika Allaah Ta'aalaa ameiharamisha ardhi kutoiharibu miili ya Manabiy." [Abu Daawuwd kwa Isnaad Swahiyh]

 

Hadiyth – 4

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( رَغِمَ أنْفُ رَجُلٍ ذُكِرْتُ عِنْدَهُ فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيَّ )) . رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن )) .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Ameangamia (amedhalilika) mtu ambaye nimetajwa mbele yake naye asiniswalie." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan]

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( لا تَجْعَلُوا قَبْرِي عِيداً ، وَصَلُّوا عَلَيَّ ، فَإنَّ صَلاَتَكُمْ تَبْلُغُنِي حَيْثُ كُنْتُمْ )) . رواه أَبُو داود بإسنادٍ صحيح .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Msilifanye kaburi langu sehemu ya kufanya sherehe, na muniswalie, kwani Swalaah zenu zinanifikia popote mulipo." [Abu Daawuwd kwa Isnaad iliyo Swahiyh]

 

Hadiyth – 6

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : (( مَا مِنْ أَحَدٍ يُسَلِّمُ عَلَيَّ إِلاَّ رَدَّ اللهُ عَلَيَّ رُوحِي حَتَّى أَرُدَّ عَلَيْهِ السَّلاَمَ )) . رواه أَبُو داود بإسنادٍ صحيح .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakuna yeyote anayenisalimia isipokuwa Allaah hunirudishia roho yangu mpaka nimuitikie salamu yake." [Abu Daawuwd kwa Isnaad iliyo Swahiyh]

 

Hadiyth – 7

وعن عليّ رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم : (( البَخِيلُ مَنْ ذُكِرْتُ عِنْدَهُ ، فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيَّ )) . رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Imepokewa kutoka kwa 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Bakhili ni yule ambaye ninatajwa mbele yake na hakuniswalia." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Hadiyth – 8

وعن فَضَالَةَ بنِ عُبَيْدٍ رضي الله عنه ، قَالَ : سَمِعَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم ، رَجُلاً يَدْعُو في صَلاَتِهِ لَمْ يُمَجِّدِ الله تَعَالَى ، وَلَمْ يُصَلِّ عَلَى النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم ، فَقَالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( عَجِلَ هَذَا )) ثُمَّ دَعَاهُ فَقَالَ لَهُ - أَوْ لِغَيْرِهِ - : (( إِذَا صَلَّى أَحَدُكُمْ فَلْيَبْدَأْ بِتَحْمِيدِ رَبِّهِ سُبْحَانَهُ ، وَالثَّنَاءِ عَلَيْهِ ، ثُمَّ يُصَلِّي عَلَى النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم ، ثُمَّ يَدْعُو بَعْدُ بِمَا شَاءَ )) . رواه أَبُو داود والترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Fadhalah bin 'Ubayd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimsikia mtu akiomba katika Swalaah yake bila ya kumsifu Allaah Ta'aalaa wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: "Huyu amefanya haraka." Kisha alimuita na kumwambia - au wengineo: "Anaposwali mmoja wenu basi aanze kwa kumtaja Rabb wake na kumtakasa na kumshukuru, kisha amswalie Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na baadae ndio aombe kwa dua anayotaka (kwa kitu chochote anachotaka)." [Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Hadiyth – 9

وعن أَبي محمدٍ كعبِ بن عُجْرَة رضي الله عنه ، قَالَ : خَرَجَ عَلَيْنَا النبيُّ صلى الله عليه وسلم ، فَقُلْنَا : يَا رَسُولَ اللهِ قَدْ عَلِمْنَا كَيْفَ نُسَلِّمُ عَلَيْكَ ، فَكَيْفَ نُصَلِّي عَلَيْكَ ؟ قَالَ : (( قُولُوا : اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ ، وعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ ، إنَّكَ حَمِيدٌ مَجيدٌ . اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ ، وعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ ، إنَّكَ حَمِيدٌ مَجْيدٌ )) . متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muhammad Ka'ab bin 'Ujrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitutembelea, nasi tukamuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Tumejua jinsi ya kukusalimu, vipi tukuswalie?" Akasema: Semeni "Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa Aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Aali Ibraahiyma Innaka Hamiydun Majiyd. Allaahumma Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa Aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Ibraahiyma Innaka Hamiydun Majiyd (Ee Mola wangu wa haki  Mrehemu Muhammad na jamaa za Muhammad kama ulivyo warehemu jamaa za Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwingi wa Kusifiwa na Uliye Mtukufu. Na Mbaarik Muhammad na jamaa zake kama ulivyo wabaarik jamaa za Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwingi wa Kusifiwa na Uliye Mtukufu)." [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

Hadiyth – 10

وعن أَبي مسعودٍ البدري رضي الله عنه ، قَالَ : أتَانَا رسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم ، وَنَحنُ في مَجْلِسِ سَعدِ بن عُبَادَةَ رضي الله عنه ، فَقَالَ لَهُ بَشْيرُ بْنُ سَعدٍ : أمَرَنَا الله تَعَالَى أنْ نُصَلِّي عَلَيْكَ يَا رَسُولَ اللهِ ، فَكَيْفَ نُصَلِّي عَلَيْكَ ؟ فَسَكَتَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم ، حَتَّى تَمَنَّيْنَا أنَّهُ لَمْ يَسْأَلْهُ ، ثُمَّ قَالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( قُولُوا : اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ ، وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ ، وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ ، كَمَا بَارَكْت عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ ، إنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ ، وَالسَّلاَمُ كَمَا قَدْ عَلِمْتُمْ )) . رواه مسلم .

Amesema Abu Mas'uwd Al-Badriy (Radhwiya Allaahu 'anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Alikuja kwetu tukiwa katika kikao cha Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhwiya Allaahu 'anhu), Akamuuliza Bwana Bashiyr bin Sa'ad (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Ee Rasuli wa Allaah! Allaah Ametuamuru tukuswalie, je tukuswalie vipi?" Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Alinyamaza, mpaka tukatamani kuwa hakumuuliza suala hilo. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Semeni: Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa Aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Aali Ibraahiyma, Wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa Aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Aali Ibraahiyma Innaaka Hamiidun Majiid (Ee Mola wangu wa haki Mrehemu Muhammad na jamaa zake kama ulivyo warehemu jamaa zake kama ulivyo warehemu jamaa za Ibraahiym. Na Mbaarik Muhammad na jamaa zake kama ulivyo wabaarik jamaa za Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwingi wa Kusifiwa na Uliyo Mtukufu). Na salamu tayari munaijua." [Muslim]

 

Hadiyth – 11

وعن أَبي حُمَيدٍ السَّاعِدِيِّ رضي الله عنه ، قَالَ : قالوا : يَا رسولَ الله كَيْفَ نُصَلِّي عَلَيْكَ ؟ قَالَ : (( قُولُوا : اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ ، وَعَلَى أَزْوَاجِهِ وَذُرِّيَّتِهِ ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ ، وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ ، وَعَلَى أزْوَاجِهِ وَذُرِّيَّتِهِ ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى آلِ إبْرَاهِيمَ إنَّكَ حَميدٌ مَجِيدٌ )) . متفقٌ عَلَيْهِ .

Amesema Abu Humayd As-Saa'idiy (Radhwiya Allaahu 'anhu): Swahaaba waliuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! vipi tutakuswalia?" Akasema: "Semeni: Allaahumma Swali 'alaa Muhammad wa 'alaa Azwaajihi wa Dhurriyyatihi kama Swallayta 'alaa Aali Ibraahiym. Wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa Azwaajihi wa Dhurriyyatihi kamaa Baarakta 'alaa Aali Ibraahiyma Innaka Hamiydun Majiyd (Ee Mola wangu wa haki Mrehemu Muhammad na wake zake na kizazi chake kama ulivyo warehemu jamaa za Ibraahiym. Na Mbaarik Muhammad na wake zake na kizazi chake kama ulivyo wabaariki jamaa za Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwingi wa Kusifiwa na Uliyo Mtukufu)." [Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik, Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

 

Share