03-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Katika Mas-ala ya Duaa

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

باب في مسائل من الدعاء

03-Mlango Wa Katika Mas-ala ya Duaa

 

Alhidaaya.com

 

Hadiyth – 1

وعن أسَامة بن زيد رضي الله عنهما ، قَالَ : قَالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( مَنْ صُنِعَ إِلَيْهِ مَعْرُوفٌ، فَقَالَ لِفاعِلهِ : جَزَاكَ اللهُ خَيراً ، فَقَدْ أبْلَغَ فِي الثَّنَاءِ )) . رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

Imepokewa kutoka kwa Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kufanyiwa wema akamwambia kwa aliyefanyia: 'Jazaaka Allaahu Khayran (Allaah akijazi kila la kheri)', hakika amefika kilele cha kumsifu na kumshukuru muhisani wake." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Hadiyth – 2

وعن جابر رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : (( لا تَدْعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ ؛ وَلاَ تَدعُوا عَلَى أوْلادِكُمْ ، وَلاَ تَدْعُوا عَلَى أموَالِكُمْ ، لا تُوافِقُوا مِنَ اللهِ سَاعَةً يُسألُ فِيهَا عَطَاءً فَيَسْتَجِيبَ لَكُمْ )) . رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Msijiombee dhidi ya nafsi zenu wala dhidi ya watoto wenu wala dhidi ya mali zenu, kwani inaweza kuafiki saa ambayo duaa hukubaliwa na Allaah, hivyo mkawa ni wenye kujibiwa." [Muslim]

 

Hadiyth – 3

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه : أنَّ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( أقْرَبُ مَا يكونُ العَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ ، فَأكْثِرُوا الدُّعَاءَ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mja anakuwa karibu sana na Rabb wake akiwa katika sijdah, hivyo jitahidini na ongezeni duaa (katika hali hiyo ya sijdah)." [Muslim]

 

Hadiyth – 4

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه : أنَّ رسُولَ الله صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( يُسْتَجَابُ لأَحَدِكُمْ مَا لَمْ يَعْجَلْ : يقُولُ : قَدْ دَعْوتُ رَبِّي ، فَلَمْ يسْتَجب لِي )) متفق عَلَيْهِ .

وفي روايةٍ لمسلمٍ : (( لا يَزالُ يُسْتَجَابُ لِلعَبْدِ مَا لَمْ يَدْعُ بإثْمٍ ، أَوْ قَطيعَةِ رحِمٍ ، مَا لَمْ يَسْتَعْجِلْ )) قيل : يَا رسولَ اللهِ مَا الاستعجال ؟ قَالَ : (( يقول : قَدْ دَعوْتُ ، وَقَدْ دَعَوْتُ ، فَلَمْ أرَ يسْتَجِبُ لي ، فَيَسْتحْسِرُ عِنْدَ ذَلِكَ وَيَدَعُ الدُّعَاءَ))

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraiyrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atajibiwa mmoja wenu kwa muda wa kutokuwa na haraka, kwa kusema: 'Nimemuomba Rabb wangu wala sikujibiwa." [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy]

Na ktika riwaayah ya Muslim: "Huendelea kujibiwa mja maadamu hataomba jambo la madhambi au kukata uhusiano wa kindugu na maadamu hatafanya haraka." Akaulizwa: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni nini maana ya kufanya haraka?" Akasema: "Ni kusema: Hakika nimeomba, hakika nimeomba, wala sioni kujibiwa. Hivyo, anakufa moyo na kuacha wakati huo kuomba duaa." 

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي أمامة رضي الله عنه قَالَ : قيل لِرسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم : أيُّ الدُّعاءِ أَسْمَعُ ؟ قَالَ : (( جَوْفَ اللَّيْلِ الآخِرِ ، وَدُبُرَ الصَّلَواتِ المَكْتُوباتِ )) . رواه الترمذي ،وقال : (( حديث حسن )) .

Amesema Abu Umamah (Radhwiya Allaahu 'anhu): Aliulizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ni duaa gani inayo sikilizwa (na kujibiwa)?" Akasema: "Ni ile inayoombwa usiku wa manane na baada ya kila Swalaah ya faradhi." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan]

 

Hadiyth – 6

وعن عُبَادَةَ بنِ الصامت رضي الله عنه : أنَّ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( مَا عَلَى الأرْضِ مُسْلِمٌ يَدْعُو الله تَعَالَى بِدَعْوَةٍ إِلاَّ آتَاهُ اللهُ إيَّاها ، أَوْ صَرفَ عَنْهُ مِنَ السُّوءِ مِثْلَهَا ، مَا لَمْ يَدْعُ بإثْمٍ ، أَوْ قَطِيعَةِ رَحِمٍ )) ، فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ القَومِ : إِذاً نُكْثِرُ قَالَ : (( اللهُ أكْثَرُ )) . رواه الترمذي ، وقال : (( حديث حسن صحيح )) .

ورواه الحاكم من روايةِ أَبي سعيدٍ وزاد فِيهِ : (( أَوْ يَدخِرَ لَهُ مِن الأَجْرِ مثْلَها )) .

Imepokewa kutoka kwa 'Ubadah bin Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hapana katika ardhi Muislamu ambaye anamuomba Allaah Ta'aalaa kwa ombi isipokuwa Allaah Humpatia au Humuondoshea jambo baya mfano wake maadamu hataomba jambo la madhambi au kukata undugu." Akasema mtu miongoni mwa waliokuwa katika kikao: "Basi, tuombe zaidi." Akasema: "Allaah, ni Mkarimu zaidi." [At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]

Na pia ameipokea Al-Haakim kutoka kwa riwaayah ya Abu Sa'iyd, na akaongeza ndani yake: "Au humukea malipo sawa na duaa yake mpaka Siku ya Malipo."

 

Hadiyth – 7

وعن ابنِ عباس رضي الله عنهما : أنَّ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم كَانَ يقولُ عِنْدَ الكَرْبِ : (( لا إلهَ إِلاَّ اللهُ العَظِيمُ الحَليمُ ، لا إلهَ إِلاَّ اللهُ رَبُّ العَرْشِ العَظيمِ ، لاَ إلهَ إِلاَّ اللهُ رَبُّ السَّمَاواتِ، وَرَبُّ الأَرْضِ، وَرَبُّ العَرْشِ الكَرِيمِ )) متفق عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa matatizo alikuwa anasema: "Laa ilaaha illaa Allaahul 'Adhwiymul Haliym. Laa ilaaha illaa Allaahu Rabbul 'Arshil 'Adhwiym. Laa ilaaha illaa Allaahu Rabbus Samaawaati wa Rabbul ardhi wa Rabbul 'Arshil Kariym (Hapana Mola wa kuabudiwa isipokuwa Allaah Aliye Mtukufu Mpole sana. Hapana Mola wa kuabudiwa isipokuwa Allaah Rabb wa kiti cha enzi kitukufu. Hapana Mola wa kuabudiwa isipokuwa Allaah Rabb wa mbingu na Rabb wa kiti cha enzi cha heshima)." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Share