04-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mkweli Mwaminifu

 

Alipokuwa akielekea nyumbani, Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anaikumbuka siku ilee jiwe jeusi lilipoanguka kutoka mahali pake baada ya kunyesha mvua kali, dhoruba na upepo na mafuriko makubwa, na sehemu kubwa ya msikiti kubomoka.

ma-Quraysh walikubaliana kuujenga upya msikiti huo, lakini mgogoro mkubwa ukazuka wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, kwani kila kabila lilitaka heshima ya kulirudisha jiwe hilo.

Akawa anakumbuka namna ma-Quraysh walivyokuwa tayari kupigana, pata shika panga mkononi, na mgogoro huo uliendelea muda wa siku tano bila kupatikana suluhisho, mpaka pale aliposimama Aba Umayya Ibn Al Mughira Al Makhzumy na kutoa shauri lake maarufu aliposema;

"Wa mwanzo kuingia msikitini kupitia mlango huu ndiye atakayehukumu baina yetu". 

ma-Quraysh wote kwa pamoja wakalikubali shauri hilo.

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anakumbuka namna gani ma-Quraysh walivyokaa kimya siku ile wakingoja na kusubiri kwa hamu kubwa nani atakayeingia mwanzo kupitia mlango ule atakayeweza kutoa hukumu itakayowatoa katika janga hilo la kuuwana na kumwaga damu.

Ghafla! Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatokeza baada ya kuingia kupitia mlango huo, na ma-Quraysh wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa furaha huku wakisema;

"Asw-Swaadiq Al-Amiyn" (Msema kweli Mwaminifu),  Sote tuko radhi juu ya uamuzi atakautoa Mkweli Muaminifu".

 

Akawa anaikumbuka miaka 40 alioishi naye akiwa sahibu yake mpenzi, Msema kweli, asiyepata kumsikia hata siku moja akitamka neno la uongo. Hata katika mzaha alikuwa akisema kweli tupu. Kisha akawa anajisemesha nafsini mwake;

"Leo mtu huyu aje aseme uongo, tena juu ya Mwenyezi Mungu? La, haiwezekani kabisa.

Wakati vijana wenzake walipokuwa wakenda ngomani na kuhudhuria sherehe mbali mbali, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwa akijishughulisha na mambo hayo, bali alikuwa akisema kuwa yeye hakuumbwa kwa ajili ya mchezo".

 

Share