Fadhila Za Mwezi Wa Muharam Na Siku Ya 'Aashuraa Na Bid'ah Zake
AlhamduliLLaah, Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha katika mwaka mpya wa Kiislamu. Leo Ijumaa ikiwa ni tarehe 3 Muharram 1429. Katika mwezi huu wa Muharram, kuna fadhila zake maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi mja anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho na aweze kujichumia thawabu tele. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Ashuraa, nategemea kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka wa nyuma)) [Muslim]
(soma maelezo chini kujua kwanini tufunge pia na tarehe 9 Muharram)
Jumla ya miezi mitukufu ni minne na mwezi huu wa Muharram ndio mwezi wa kwanza unaoanza kuhesabika
((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَق السَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ))
((Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Allaah ni miezi kumi na mbili katika ilimu ya Allaah (Mwenyewe tangu) siku Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajab, Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram) (kufanya) hivi ndiyo dini iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu (kwa kufanya maasi) katika (miezi) hiyo)) [At-Tawbah 9:36]
Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyotoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu):
(السنة اثنا عشر شهرا، منها أربعة حرم:ثلاث متواليات،ذو القعدة، وذو الحجة، والمحرم، ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان)) رواه البخاري ، ومسلم
((Mwaka una miezi kumi na mbili, minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab ambao uko baina ya (mwezi wa) Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ni neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutujuaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au masiku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine.
Kuhesabika Kwa Mwaka Mpya Wa Hijriyah
Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya kuhama (Hijrah) kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba kutoka Makkah kuhamia Madiynah. Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji ambao wataanza kutumia Sharia'h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana
Na mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama A.H kwa kirefu yenye maana 'After Hijrah', tarehe 1 Muharram A.H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622 C.E. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka mwezi wa Dhul-Hijjah ulipomalizika na mwezi wa Muharram ukaingia siku ambayo sawa na tarehe 9 Januari 2008.
Fadhila Za Mwezi Huu Khaswa
Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika aya ya juu ni mitukufu lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم
Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان " رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisubiri kufunga siku yoyote
Swawm ya 'Ashuraa imependezeshwa hata kwa watoto kuifunga
عن الرُّبيّع بنت معوذ رضي الله عنها قالت: "أرسل رسول الله صلى الله عليه وسلم غداة عاشوراء إلى قرى الأنصار "من أصبح مفطرا فليتم بقية يومه ومن أصبح صائما فليصم" ، قالت : فكنا نصومه بعد ونصوّمه صبياننا ... رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Ar-Rubay'i bint Mu'awwadh (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituma ujumbe Alfajiri ya siku ya 'Ashuraa katika vijiji vya Answaar "Aliyeamka akiwa amefuturu amalize siku yake (kwa kutokula) na aliyeamka amefunga afunge" Akasema (Ar-Rubay'i: 'Tulikuwa tukifunga baada yake na tukiwafungisha watoto wetu...' [Al-Bukhaariy na Muslim]
Sababu Ya Kufunga Siku Ya 'Ashuraa
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ" رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Ashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa Wana Wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy]
Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa kuongeza siku moja kabla.
روى عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قال : "حِينَ صَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ يَوْمٌ تُعَظِّمُهُ الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((فَإِذَا كَانَ الْعَامُ الْمُقْبِلُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ صُمْنَا الْيَوْمَ التَّاسِعَ)) قَالَ فَلَمْ يَأْتِ الْعَامُ الْمُقْبِلُ حَتَّى تُوُفِّيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ". رواه مسلم
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alipofunga Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya 'Ashuraa na akaamrisha ifungwe wakasema: Ewe Mtume wa Allaah, hii ni siku wanayoitukuza Mayahudi na Manaswara. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ikifika mwakani InshaAllaah tutafunga siku ya tisa pia)). Akasema (Ibn 'Abbaas) haukufika mwaka uliofuata ila alifariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Muslim]
Kwa hiyo ni bora kufunga siku ya tisa na kumi Muharram, na kama mtu hakujaaliwa kufunga siku ya tisa na kumi, basi afunge siku ya kumi na kumi na moja. Na
Kwa vile siku hii ni siku Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyomnusuru Muusa ('Alayhis-Salaam) na Wana Israili, na sisi pia tutakaofunga tuwe na tegemeo kuwa nasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatunusuru pia kutokana maadui wetu na mabaya
((إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ))
((Bila ya shaka Sisi Tunawanasuru Mitume Yetu na wale walioamini katika maisha ya dunia ya siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe)) [Ghaafir 40: 51]
Juu ya kwamba fadhila ya kufunga Swawm ni ibada Aipendayo kabisa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Ashuraa, nategemea kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka wa nyuma)) [Muslim]
Ndugu Waislam, hii ni fursa kubwa ya kujisafisha na dhambi na kuzidisha taqwa (ucha Mungu) ili kujibebea zawadi nyingi twende nazo Akhera kwa vile hatujui amali njema zipi zitakazokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na hatujijui kama tutakuwa na umri wa kuchuma zaidi.
Bid'ah Katika Siku Ya 'Ashuraa
Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa, tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu, kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu). Matendo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah Subhaanahu wa Ta'ala Amrehemu): "Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliharamisha kama ilivyo katika Hadiyth hii sahiyh:
عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية)) البخاري .
Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy]
Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo."
Ibn Rajab amesema: "Wanayoyafanya Ma-Rafidha (Mashia) katika siku hii kuwa ni siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema, wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya huzuni kwa wasio Mitume?"
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


