Skip navigation.
Home kabah

Qur-aan Na Usahihi Wake (The authenticity of the Qur-aan) -1

  (Prof.Dkt.Mustafa M. Azami, Uwaimir Anjum na S. Hussein)

 imefasiriwa na Shaibu H. Kifea

 
Misahafu Ya Yemen Na Tahakiki Ya Magharibi
 
 
‘Historia ya matini ya Qur’an’ ni mada iliyowasilishwa na M.M. Azami ukiwa ni uchambuzi wa kukosoa makala ya Toby Lester, “Qur’an ni nini?”
Makala hii ilichapishwa na jarida la January Atlantic Monthly mwaka 1999.
 
Kwa jinsi inavyoonekana, makala hii ilikusudiwa kuwayumbisha Waislamu ili wapoteze uhakika juu ya kuhifadhika kwa Qur’an na iwe habari njema kwa wasio-Waislamu ambao mara kwa mara, wamekuwa wakikerwa na imani isiyotetereka ya Waislamu juu ya Qur’an.
 
Makala yetu inalenga kuonesha udhaifu wa hoja za Lester na za watafiti wengine pamoja na maoni anayoyatoa ili kujenga hisia za shaka na kuleta mkanganyiko juu ya historia ya kukusanywa na kuhifadhiwa kwa Qur’an.
 
Kwa ufafanuzi wa wazi na kwa kadri iwezekanavyo, tutafanya hivyo kwa kutumia taaluma ya mada hii hasahasa ile iliyotolewa kwa mukhtasari  katika kitabu cha mwanazuoni mkubwa wa hivi leo, Profesa M.M. al-Azami.
 
Mhariri wa Jarida la Atlantic Monthly, Lester ametoa habari ya kugunduliwa kwa  baadhi ya vipande vya ngozi vya Qur’an vinavyoweza kukisiwa kuwa ni vya karne ya kwanza ya Uislamu (karne ya saba).
 
Habari hii ikafuatiwa na mukhtasari wa tafiti za magharibi ambazo zimejaribu kuthibitisha silsila ya Qur’an (historicity of the Qur’an) na kuonesha matumaini kuwa kukosolewa kwa matini ya Qur’an ambako, yadhaniwa, kunatokana na uvumbuzi mpya kama huu wa vipande vya ngozi uliofanywa na wasomi wa kisekula utasababisha mabadiliko makubwa ya kijamii na mageuzi ya fasihi ya Uislamu kwa misingi ya Ukristo.
 
Kama kawaida, makala hii iliwachokoza Waislamu, wale wasiofahamu fasihi ya Uislamu na nyenzo madhubuti na za hakika ambazo Qur’an imehifadhiwa na Allah kwazo, walichanganyikiwa na kuyumbishwa na habari hii ya uongo.
 
 
Na pia wale wenye elimu ya Qur’an na Hadith na wanaojua uongo wa madai hayo, nao walifadhaika kwa kruseidi hiyo ya kiakili dhidi ya imani yao. Lester anaonekana kufurahi kuwa ile tahakiki (criticism) iliyoibwaga Biblia hadi kuonekana kuwa ni kitabu cha kutungwa pia itaisibu Qur’an pasina kujua kuwa utafiti anaouonesha unakwenda kinyume na hivyo kabisa.
 
 
Kwa kunukuu maneno yake, anasema “jitihada kubwa ya kisekula katika kuipa tafsiri mpya Qur’an, iliyotegemea, kwa kiasi fulani, ushahidi wa matini kama ule uliotolewa na vipande vya Yemen inawakera na kuwaudhi Waislamu wengi kama vile jitihada za kutafsiri upya Biblia na maisha ya Yesu inavyowakera na kuwaudhi Wakristo wengi wahafidhina.
 
 
Hata hivyo, kuna wanazuoni, wakiwemo wa Kiislamu, ambao wanaona kuwa jitihada kama hiyo ambayo, kimsingi, inachangia kuiweka Qur’an katika historia, itachochea moto wa kufufua na kurejesha utamaduni wa zamani na kupiga hatua mbele kwa kuangalia nyuma. Hivyo, haitaishia tu katika mabishano ya wanazuoni bali fikra ya aina hii inaweza kuwa chagizo kubwa sana ambapo, kama zinavyoonesha historia za Mwamko (Renaissance) na Magauzi (Reformation), inaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya kijamii. Tangu hapo, kwa sasa, Qur’an ndicho kitabu chenye ushawishi mkubwa wa kiitikadi ulimwenguni kote.”
 
Lester anaendelea kutoa mfano wa Mtafiti mmoja wa sanaa ya uandishi ya Kiarabu (Arabic calligraphy), Mjerumani Gerd-R. Puin ambaye amekuwa akizihakiki hati 15,000 za ngozi ya Qur’an akishirikiana na mwenziwe Von Bothmer.
 
Puin katutobolea siri kuwa Serikali ya Yemen ilikuwa tayari kuficha siri ya hatua hii ya Mjerumani asiye Muislamu kuhakiki Qur’an ili kuepuka kuwachokoza Waislamu (ikidhaniwa kuwa Waislamu mara nyingi si watu wenye kutumia akili (irrational) na ni watu wa kuripuka (reactive) na hivyo wangeupinga mradi huo huru (objective) na wa kisomi (scholarly) pasina sababu ya maana.
 
Kwa maneno ya Puin, sababu ya hali hiyo ni kwamba, “Msimamo wa Waislamu ni kuwa chochote kinachotaka kusemwa juu ya historia ya Qur’an kilishasemwa miaka elfu moja iliyopita.”
 
Puin ambaye ni Mtafiti wa Sanaa ya Uandishi ya Kiarabu alizipiga picha ya filamu kurasa zote za Qur’an zilizopatikana na kwenda nazo Ujerumani ambako yeye na Wasomi wengine hatimaye watapata nafasi ya kuchunguza matini (texts) hizi na kuchapisha tafiti zao kwa uhuru kabisa
Puin anasema, “hatimaye tuweze kuthibitisha kuwa kama ilivyo Biblia, Qur’an nayo pia ni “historia” yaani ni kumbukumbu ya uzushi wa mwanadamu.” Lester anamnukuu Puin akisema, “Vipande hivi vya Sana’a (Yemen) vitatusaidia kufanya hili.”
 
Andrew Rippin, Profesa wa Canada ambaye ndiye anayedhaniwa kuwa ni “kinara wa tafiti za Qur’an hivi leo”, anasema kuwa usomaji  na mpangilio tofauti wa aya za Qur’an katika (ngozi za Yemen) vyote ni muhimu sana.
Kila mtu anakubaliana na hilo. Miswada hii inasema kuwa historia ya awali ya matini ya Qur’an ni suala lililo wazi zaidi kuliko vile ambavyo wengi wamekuwa wakidhani: matini ya Qur’an haikuwa madhubuti, na hivyo ilikuwa na chanzo dhaifu kuliko inavyodaiwa mara zote”.
 
Kisha Lester anatoa maelezo ya jitihada za karibuni za kuchimbua historia ya Qur’an zilizofanywa kijasiri licha ya hofu ya mlipuko wa Waislamu, akianza na Salman Rushdie na kuendelea na Yehuda Nevo wa Chuo Kikuu cha Jerusalem nchini Israil ambaye anasema kuwa hakukuwa na Wapagani Arabuni na hakukuwa na Wayahudi mjini Madina na ndiyo kusema kuwa Historia nzima ya Uislamu kama tuijuavyo si sahihi.
 
 
Patricia Crone, anadai kuwa Uislamu ambao  ni harakati za Kimasihi za Wayahudi, na Qur’an na Hadith  vyote vilikuwa ni uzushi tu ulioanzia karne ya tatu AH (Baada ya Hijiria), na hatimaye akaja kwa James Belley ambaye, kwa kudhani kuwa, Waislamu wanasuasua mno kufuata utamaduni wa Wayahudi na Wakristo wa “kusahihisha” maneno ya MwenyeziMungu, akajitutumua kutaja lukuki ya mabadiliko au masahihisho katika Qur’an.
 
 
Halafu makala hiyo ikatoa mfano wa jazba za Waislamu zilizochochewa na tafiti hizi za kufuru (ikionesha kuwa Waislamu hawana hoja dhidi ya wasomi majasiri na waadilifu wa Magharibi ila jazba tu).
 
Kisha inafuata simulizi ya msingi ya mwanzo wa Uislamu, kisha linafuata dai kuwa Khalifa Uthman (644-656), Kiongozi wa tatu wa dola ya Kiislamu baada ya Mtume Muhammad,” aliunda kamati ya Uhariri.
 
Kamati haikutaka kuhariri kila kitu, bali kukusanya Qur’an ambayo ilikusanya kwa uangalifu vipande mbalimbali vya Muswada ambao ulihifadhiwa au kuandikwa na Maswahaba wa Muhammad, Matokeo yakawa ni kupatikana kwa matini moja ya kuandikwa.”
 
Sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala ya Lester nayo pia ina makosa. Sehemu hii inachochea kuwa mbona Waislamu mbalimbali wenye mtazamo mamboleo kama Fazlur na Rahman, Nasr Abu Zayd nao pia wamehoji usahihi wa Qur’an. Hii si kweli kabisa.
 
Fazlur Rahman kwa kweli aliandika tahakiki ya kuvutia ambayo ilioesha dai la uwongo la Wansbrought kuwa Qur’an ilitungwa. Waislamu hawa mamboleo kweli walikuwa na mawazo na mtazamo ambao umekosolewa na Wanazuoni wengine wa Kiislamu lakini hawajahoji hata kidogo usahihi wa Qur’an.
 
Madai ya Lester katika makala hiyo, kwa kifupi, yaweza kuelezwa kwa nukta zifuatazo; (i)Kuvumbuliwa kwa ngozi za Yemen ni jambo muhimu na (ii) itawasaidia wanazuoni wa kisekula wasio na hiyana kuitafsiri ‘Qur’an’ bila hiyana, (iii) juhudi hiyo ya kisayansi itawaudhi Waislamu ‘wachaMungu’
 
                                                                                                                                                                  Inaendelea ..../2