Qur-aan Na Usahihi Wake (The authenticity of the Qur-aan) -2
(Prof.Dkt.Mustafa M. Azami, Uwaimir Anjum na S. Hussein)
imefasiriwa na Shaibu H. Kifea
MADAI ya Lester katika makala hiyo, kwa kifupi, yanaweza kuelezwa katika nukta zifuatazo:
- Kuvumbuliwa kwa vipande vya ngozi vya Yemen ni jambo muhimu, na;
- litawasaidia wasomi wa kisekula (wasio na hiyana) ‘kuifasiri upya’ Qur’an kwa uhuru;
- Jitihada hiyo ya kisayansi itawaudhi Waislamu ‘wachaMungu’ kwa sababu, kwa kipindi cha miaka elfu moja, Waislamu hawajasema au kuandika chochote kuhusiana na “historia” ya Qur’an;
- kila mtu anaukubali ukweli kuwa usomaji na mpangilio tofauti wa aya za Qur’an kama unavyobainishwa na ngozi hizi ni jambo muhimu, kwani linathibitisha kuwa matini ya Qur’an haikupangwa katika kipindi hicho (cha karne ya kwanza AH); hitilafu hizi “ndogo lakini tete” zitaleta mabadiliko ya kijamii yanayotakiwa katika Uislamu sawa na Mageuzi ya Kikristo;
- kwa mujibu wa simulizi moja ya Waislamu, Khalifa Uthman aliunda kamati ya Uhariri ambayo ndiyo iliyokusanya na kusanifu matini moja ya Qur’an
Kati ya nukta zote hizi, nukta ya mashambuzi zaidi ni kwamba matini ya Qur’an “haikuwa madhubuti” (‘unstable’) katika karne chache za mwanzo na haikuwa takatifu na ya mpango mmoja kama ilivyogeuzwa kimakosa hivi leo.
Hapa tunawasilisha hoja za Profesa M.M.Azami za kupinga nukta moja-moja hadi mwisho wa makala hiyo. Hebu kwanza tuanze kuangalia kwa undani zaidi kiini cha uvumbuzi wa ngozi za Yemen na utafiti wa Dkt. Puin
Uvumbuzi wa Ngozi za Yemen na Utafiti wa Dkt. Puin
Hebu tulikaribishe kwa muda mfupi tu swali gumu la kwanini Mustashirikina (orientalist) huyu wa Kijerumani amejipinda hadharani na bila haya kuonesha uzushi wa kihistoria na masahihisho ya Qur’an ambayo yalikaribishwa na Serikali ya Yemen ili kuzirejesha na kuzitunza ngozi hizi, kwa nini awe Mustashirikina na asiwe mwanazuoni miongoni mwa makumi kama si mamia ya wanazuoni wa Kiislamu ambao ni mabingwa wa herufi na sayansi ya uandishi wa herufi katika lugha (orthography) kama vile yeye mwenyewe Mustafa M. al-Azami.
Hao walioitwa wanazuoni ambao wanajifanya wako huru au makini hawana lolote bali lengo la jitihada zao ni kuonesha kuwa Qur’an ilitungwa. Ambalo Waislamu ulimwenguni kote wanaweza kulifanya ni kuonesha hisia zao juu ya hatua hizo za serikali ya Waislamu.
Halafu lipo swali la kwanini Jarida hilo, Atlantic Monthly, lilichapisha kazi hiyo potofu na changa ya uandishi. Profesa Jeffrey Lang, ambaye ni Muislamu anayekosoa makala hiyo, anabainisha kuwa ulikuwa ni uzembe na ukiukaji wa taaluma kwa Atlantic Monthly kumpa mradi huo mzito mwandishi mchanga na asiye na sifa. Toby Lester hana kabisa elimu ya masuala ya Uislamu.
Jarida hilo linataja tu miaka yake miwili katika Ujumbe wa Amani nchini Yemen (Peace Corps in Yemen) na miaka miwili kama Afisa wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wakimbizi (Refugee-affairs oficer for UN), hizi ndizo sifa pekee alizonazo.
Labda hii ni sawa na kumpa kazi ya kuandika makala ya Tahakiki ya Biblia mwanafunzi mgeni wa Kiislamu aliye ziarani nchini Marekani au Muhamiaji wa hivi karibuni ambaye hana kabisa ufahamu wa taaluma ya Ukristo. Hii ndiyo sababu kwa nini makala hiyo imekosa mzamo na maudhui na kwa nini mimi nina maoni machache sana juu ya makala hiyo.”
Huyo aliyeitwa mtaalamu wa utafiti, Dkt. Gerd-R Puin anajionesha mwenyewe kuwa mchanga na ana chuki. Lang anazidi kubainisha maneno yasiyo na mantiki ya Puin:
“Chanzo pekee cha maudhui ya Lester katika uvumbuzi huu na msingi mkuu ambao makala yake inautegemea ni Gerd-R Puin ambaye amekuwa akijihusisha na kazi ya kurejesha maandiko ya zamani.
Ingawaje Puin ni mtaalamu wa Sanaa ya Uandishi ya Kiarabu na Utunzaji wa matini, yeye si mwanazuoni wa Kiislamu. Puin anadhihirisha upinzani na ujinga wake juu ya Uislamu pale anapozungumzia kukataa kwa Waislamu kuoanisha tafsiri za Qur’an na Qur’an.
Msimamo wa Waislamu ni kwamba Qur’an ni ufunuo halisi uliopokewa na Mtume Muhammad katika Lugha yake ya kuzaliwa, Kiarabu na kwamba kuigeuza katika Lugha nyingine si Qur’an bali hiyo ni tafsiri tu ya Qur’an kwa sababu haifanani na wahai halisi na kwa sababu kuna mambo ambayo, katika tafsiri hupungua hata kama itafanywa vizuri kiasi gani.
Hata hivyo, tafsiri za Qur’an zimetolewa na wanazuoni wote wakubwa katika lugha nyingine kubwa. Katika kuchanganyikiwa kwake, anadai kuwa Waislamu wanakataa kutoa tafsiri za Qur’an katika lugha nyingine eti kwa sababu kitabu hicho hakieleweki na ndiyo kusema hakitafsiriki.
Puin anadhihirisha ujinga wake kwa kauli hii kwani wakati yeye akisema hivyo, Waislamu na hata Mustashirikina wengi watamwambia kinyume chake
Itaendelea..../3
»
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


