Qur-aan Na Usahihi Wake (The authenticity of the Qur-aan) - 3 -
UPUUZI wa fikra ya Puin unashangaza. Kwa upande mmoja, anasema kuwa Waislamu hawatoi tafsiri za Qur-aan katika lugha isiyokuwa ya Kiarabu (jambo ambalo si kweli) eti kwa sababu haieleweki, ilihali, yeye huyo huyo, kwa upande mwingine, anakiri kuwa Waislamu na Mustashirikina wengi wanaamini kuwa Qur-aan inaeleweka.
Kwa sababu hiyo, kwa kuizingatia mantiki ya Puin, tungehitimisha kuwa Waislamu wanakataa kuitafsiri Qur-aan kwa sababu ya kutoeleweka kwake kwamba wao wenyewe Waislamu hawaielewi kabisa. Hii ni sawa na kusema, Yohanna anakataa kuvuka barabara kwa sababu ya gari ambayo anaona haiji.
Kwa vile makala hiyo ya Toby Lester katika Jarida la Atlantic Monthly ni changa mno na inajikanganya kiasi ambacho haistahili maoni mengi ya kisomi, Dkt. Mustafa Azami anautazama utafiti uliochapishwa na Puin mwenyewe katika kitabu, Qur-aan as Text (S. Wild (ed.), Leiden, 1996).
Yafuatayo ni maelezo ya Dkt. Puin kuhusiana na ukusanyaji wa ngozi za Yemen ambao nguvu yote ya matumaini ya kulirudi chimbuko la Qur-aan imejengeka kwao:
- Hitilafu ya uandishi wa alif
- Mabadiliko katika utenganishaji wa aya katika aya kadha wa kadha
- Uvumbuzi mkubwa kabisa ni wa kipande ambacho tamati ya sura ya 26 inafuatiwa na Sura ya 37.
Puto la Toby Lester, kwa kiasi kikubwa, limetunishwa na hewa iliyotolewa na makala ya Puin lakini mhemko wa ziada unatokana na nadharia za Mustashirikina (wasomi wa Magharibi wanaousoma Uislamu) alizozitaja mwenyewe ambazo zinazungumzia uzushi wa Qur-aan.
Kwa kweli, majina anayoyataja ndiyo yenye hadhi miongoni wa Mustashirikina. Mashuhuri miongoni mwao ni Wansbrough na wanafunzi wake, Cook na Crone ambao wamesema kwa kiwewe cha jinamizi au hofu ya Uislamu, kuwa yale yote tunayoyajua kuwa ni maandiko na vitabu vya Kiislamu vilitungwa katika karne ya tatu AH/karne ya tisa CE na si katika kipindi cha uhai wa Mtume Muhammad (saw).
Kabla ya kulishughulikia, kiufundi, kila alilosema Puin, hebu tuitazame barua ya Kiarabu ambayo Dkt Puin aliandika kwa al-Qadi al-Akwa kule Yemen kutoa taarifa ya uchunguzi wake. Barua hiyo ilichapishwa katika gazeti la kila siku la ath-Thawra na kutafsiriwa na Dkt Azami kama ifuatavyo:
“Mabaki (ya Misahafu hii ya zamani), yamehakikishwa kisayansi, kuwa ni ya karne ya kwanza baada ya Hijiria! Kwa sababu ya kuwepo kwa miswada hii kule Sana’a,…(tuna) uthibitisho mmoja tu muhimu wa kukamilika kwa Qur-aan katika karne ya kwanza Hijiria na si kama wanavyodai wasomi wengi wasio-Waislamu kuwa ni kuanzia mwanzoni mwa karne ya tatu Hijiria!
Bila shaka, Waislamu wanaweza kuhoji nini kusudio la habari hiyo kutoka kwa mwanazuoni asiye Muislamu, ilihali Waislamu wana hakika kwamba Msahafu kamili ulikuwepo tangu wakati wa Khalifa wa tatu, Uthman bin Affan (yaani Waislamu kwa hakika wanaamini kuwa Qur-aan kwanza ilikusanywa na Abu Bakar, Khalifa wa kwanza).
Imani yao inashikiliwa kwa nia njema kwa kuwa hatuna nakala halisi ya Msahafu ulioandikwa chini ya usimamizi wa Uthman., wala hatuna hata nakala za baadae alizozituma katika nchi nyingine..” (uk. 314).
Barua hii ya Dkt Puin inadokeza jambo fulani muhimu sana-kwamba wale wote waliodai kuwa Qur-aan ilitungwa (na si kukusanywa) katika karne ya tatu Baada ya Hijira hawako sahihi kabisa. Ngozi za Qur-aan kuanzia karne ya kwanza zinapasua maputo yote ya wananadharia walioleta uzushi wa hivi karibuni.
Lakini ukweli huu ulio wazi sio anaotuambia Lester katika makala yake. Cha kushangaza yeye, katika makala hiyo, kataja nadharia zote za uzushi wa karne ya tatu kuwa ni utafiti wa Puin lakini hakukigusa hata kidogo kipengele cha wazi na chenye usahihi mkubwa katika uvumbuzi wa Puin-ambacho kinamalizia kwa kuzikanusha nadharia zote hizo!
Kinyume chake, Lester katumia maneno ya Puin kupenyeza shaka juu ya Qur-aan na vile vile katumia nadharia za uzushi ambazo Puin kazikosoa, likiwa ni jaribio la kuzidisha shaka! Je kuna uanahabari wa kishetani, uliokosa uadilifu na wa kifedhuli zaidi ya huo?
Fasihi ya Uislamu: Imehifadhiwa na kuthibitishwa na MwenyeziMungu
Hadi hapo, bado sijauzungumzia upande wa Uislamu juu ya habari hii ambayo imetafitiwa kikamilifu na kuwasilishwa kisomi katika kitabu cha Dkt Mustafa M. Azami.
Kwa kuirejea barua ya Puin katika gazeti la Kiarabu lililotajwa hapo juu, izingatiwe kuwa nayo haikuacha kuthubutu kupenyeza udanganyifu na upotoshaji. Inaielezea visivyo historia ya Uislamu, na inachochea kuwa Waislamu hawakuwa na chochote ila “imani tu” ya kuthibitisha dai lao la kuhifadhiwa kwa Qur-aan kabla ya kuvumbuliwa kwa ngozi za Yemen.
Ukweli ni kwamba Ngozi za Yemen haziongezi chochote kipya katika historia ya Uislamu, badala yake, zinaithibitisha tu.Tofauti kati ya Ngozi hizi na Msahafu sanifu uliokusanywa na Uthman (ra) ni ndogo mno na zinafahamika kwa wanazuoni wa Kiislamu.
Kwa kuwa fasihi ya Uislamu ni sahihi kabisa na ni ndefu, haitawezekana kuwasilisha maelezo yake yote katika makala hii. Mfano wa vitabu vya akina Azami ndivyo bora katika kufahamu elimu ya Uislamu juu ya Qur-aan. Mimi hapa nitatoa mukhtasari wa fasihi sanifu ya Uislamu kwa kifupi sana.
Ukurasa wa tano, wa sita na wa saba wa kitabu cha Dkt. Azami unatoa maelezo ya kisomi na yaliyoandikwa kiufundi juu ya kuandikwa, kupangwa na kukusanywa kwa Qur-aan.
Maelezo hayo yanafupishwa hapa. (Kwa maelezo zaidi soma vitabu hivi vya M.M. Azami Kuttab an-Nabi (Riyadh, 1981) na Studies in Early Hadith Literature (Indiana, American Trust Publications, 1978.)
Waandishi (Scribes) wa Mtume (saw) walikuwa wakiandika wahai pale pale alipowasomea. Kwa kuwa hakukuwa na karatasi, wahai ulikuwa ukiandikwa katika kitu kilichokuwepo kama vile ngozi za wanyama au bapa za mabega ya ngamia (Shoulder blades).
Kwa kuwa Mtume (saw) aliwahimiza kwa nguvu Waislamu kujifunza kuandika kama inavyobainishwa na Hadith nyingi Sahihi na Aya za Qur-aan, maswahaba wengi waliojua kusoma na kuandika waliandika nakala zao wenyewe za wahai wa Qur-aan pale pale uliposhuka.
Hata hivyo, Mtume (saw) hakukusanya nakala moja sanifu ya Qur-aan kwa sababu Qur-aan haikuwa imekoma kushuka hadi mwishoni mwa maisha yake. Lakini hilo halikuwa tatizo kwa mtu yeyote yule wa wakati huo kwani chanzo kikuu cha taarifa sahihi katika jamii hiyo kilikuwa ni fasihi simulizi (oral witness).
Utamaduni wa Warabu enzi hizo, kwa kiasi kikubwa, ulikuwa wa mdomo ambapo, kwa sababu za maana, watu walikuwa hawaliamini neno la kuandikwa bila uthibitisho wa shahidi au mwandishi.
Qur-aan ikahifadhiwa barabara katika nyoyo na vichwa vya maswahaba ingawaje si kila mmoja wao aliyehifadhi Qur-aan yote-sababu ni kuwa haikushuka kwa mfumo wa Kitabu kama ilivyo leo hii. Njia bora ya kuhifadhi Qur-aan ilikuwa ni hukumu yake ya kuisoma nyakati za Swala.
Kwa hakika, kwa mujibu wa Qur-aan yenyewe, Mtume (saw) alikuwa na wasiwasi juu ya kukihifadhi na kukikariri kile kilichokuwa kikifunuliwa kwake. Pale alipojaribu kurudia kusoma hali ya kuwa wahai ulikuwa bado unashushwa kwake na Malaika Jibril, MwenyeziMungu akamuhakikishia kuwa;
“Kwa hakika ni juu Yetu kuukusanya na kuusomesha. Wakati Tunapokusomea, basi fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu yetu kuubainisha”. (75:17-19).
Itaendelea …./4
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


