Qur-aan Na Usahihi Wake (The authenticity of the Qur-aan) - 4
(Prof.Dkt.Mustafa M. Azami, Uwaimir Anjum na S. Hussein)
imefasiriwa na Shaibu H. Kifea
Je Mtume (Sallallahu alayhi wasallam) aliyekuwa na wasiwasi juu ya kuhifadhi na kukariri kile kilichofunuliwa kwake, angewezaje basi kupuuzia kuiandika na kuihifadhi Qur’an?
Inaleta maana kamili, na historia inathibisha ukweli kuwa kama Mtume alikuwa na shaka namna hiyo kuhusu ufahamu sahihi na usomaji wa Qur’an katika maisha yake basi hangeweza kuacha chochote katika kuhakikisha kuwa inahifadhika kwa usalama baada ya kutawafu kwake.
Baada ya kutawafu kwa Mtume (sallallahu alayhi wasallam), Qur’an ikakusanywa katika muundo wa kitabu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kufuatia ushauri wa Umar kwa Abu Bakr.
Ni muhimu kuzingatia kwamba jambo hili lilikuwa na ubishani. Mwanzoni, Abu Bakr hakutaka kufanya jambo ambalo Mtume hakulifanya.
Halikadhalika Zayd ibn Thabit, bingwa wa mahafidh na mfasaha na mtu makini zaidi, mwanzoni na yeye hakutaka kuikusanya. Sababu ilikuwa kwamba wao walifikiri kuwa kuhifadhi na kuilinda Qur’an kulikwishafanywa na Umma wa Waislamu-kwa kule kuhifadhiwa kwake vifuani mwa mamia kwa maelfu ya waumini ambao walikuwa wamehifadhi sehemu kubwa za Qur’an na kuzisoma mchana na usiku.
Ukusanyaji kwa muundo wa kitabu ulionekana kama si jambo la lazima kwa kule kuwepo kwa mahafidhi. Hoja ya Umar yaonekana kujengeka kwa premisia mbili; (i) mahafidhi walikuwa wanatoweka duniani na hivyo hifadhi mbadala ya Qur’an ilikuwa ni ile ya kukusanya pamoja ngozi za Qur’an, na (ii) watu wengi walikuwa wameandika nakala zao za Qur’an na kwa vile yangeweza kuwepo makosa ya uandishi, basi itengenezwe nakala moja sanifu wakati wale mahafidhi wote bora wangali hai. Matukio haya yalitokea mwaka mmoja tu baada ya kutawafu Mtume na baada ya kukamilika kwa Qur’an.
Maelezo ya ukusanyaji huu wa Qur’an yameandikwa kwa kina katika fasihi ya Uislamu na yamewasilishwa vizuri katika kitabu cha Prof. Azami. Uandishi wa Masahafu katika kipindi cha Mtume ulikuwa makini, kama ambavyo mtu anaweza kuhisi ule wasiwasi aliokuwa nao Mtume juu ya Qur’an ambapo ushahidi wa jambo hili nao ni mwingi.
Zoezi la kukusanya Qur’an lilikuja kwa amri ya Abu Bakr mwaka mmoja baada ya kutawafu Mtume (sallallahu alayhi wasallam) na usanifishaji wa usomaji wake ulianzishwa na Khalifa Uthman, huu ulianza miaka kumi na minne baada ya kutawafu kwa Mtume (11AH).
Hatua zote hizo mbili ziliafikiwa na Maswahaba wote wa Mtume na zikasimamiwa kwa uangalifu mkubwa na wale waliokuwa na ilimu na uadilifu zaidi miongoni mwao. (Taz. Azami ch. 6).
Je ngozi za Yemen ndio uthibitisho pekee wa kukusanywa Qur’an katika Karne ya Kwanza?
Nguvu yote ya hoja ya Mustashirikina inajengeka kwa dhana kuwa hakuna nakala za awali za Qur’an zilizobakia na kwamba ngozi za Yemen ndizo nakala za kwanza kuvumbuliwa. Hili ni jambo lililombali kabisa na ukweli.
Kuna nakala nyingine nyingi za karne ya kwanza zilizobakia. Kwa bahati mbaya, Waislamu wengi hawana utashi wa kujibidiisha kusoma historia ya Kitabu chao na kutumia mbinu za kisayansi kuzichambua nyaraka hizi na ndiyo sababu mara nyingi, watafiti wenye hofu ya Uislamu (Islamophobic researchers) ndio wanaofanya kazi miaka baada ya miaka kutafuta angalau kielelezo kimoja tu ili kuvuruga imani ya Waislamu
Baadhi ya sababu za Waislamu kupuuzia jitihada za aina hii ni kwamba Qur’an, mara zote, imekuwa ikihifadhiwa nyoyoni na vichwani mwa Waislamu tangu pale ilipoanza kusomwa na Mtume, na muafaka wa Waislamu bilioni moja na wa vizazi vya Waislamu kwa karne kumi na nne ndivyo vinavyofanya Waislamu wasione haja ya kutetea imani yao inayotokana na vipande vidogo vya ngozi.
Hata hivyo, kwa vile taaluma ya Magharibi inataka kutumia kumbukumbu hizi ili kukosoa usahihi wake, ni jukumu la Waislamu sasa kuutia mikononi mwao utafiti wa historia yao na Kitabu chao.
Kwa utafiti uliofanywa na Mwanazuoni mwingine wa Kiislamu, K. Awwada ambaye mwaka 1982 alichapisha utafiti unaoorodhesha miswada ya awali kabisa ya Kiarabu ambapo kuna Misahafu mingi ya Qur’an ambayo ni kamili, na tarehe yake ni ya tangu karne ya Kwanza A.H” (uk. 316). Baadhi katika orodha ni:
1. Misahafu mitano inayonasibishwa na Khalifa Uthman bin Affan, hivi sasa ipo Istanbul.
2. Msahafu mmoja.wa karibu kurasa 1000, ulioandikwa baina ya mwaka 25 na 30 AH, upo al-Azhar, Cairo. (Zingatia kuwa mradi wa usanifishaji Qur’an wa Uthman ulianza mwaka 25 AH).
Mbali na hii, Azami kaorodhesha takribani Misahafu mingine ishirini ambayo inapatikana katika maktaba duniani kote, yote hii ni ya karne ya kwanza. Azami anaendelea kueleza kuwa: “ukusanyaji wa Turk ve Islam Eserleri Muzesi mjini Istanbul, ambao ndio wenye umuhimu mkubwa zaidi kuliko ngozi za Sana’a (Yemen), bado unawasubiri wanazuoni wakweli” (uk. 317).
Mpangilio tofauti wa Sura
Wanazuoni wanakubaliana kuwa aya zilipangiliwa katika sura kwa amri ya Mtume. Yaani, mpango wa aya uliamrishwa na MwenyeziMungu. Hata hivyo, kuna kuhitalifiana kuhusiana na iwapo mpangilio mzima wa sura uliamuliwa na Mtume (sallallahu alayhi wasallam).
Rai ya wengi ni kuwa mpango wa sura ulipangwa na Mtume, sallallahu alayhi wa sallam kama ilivyoagizwa na MwenyeziMungu. Rai za wachache miongoni mwa wanazuoni zimetofautiana na mtazamo huu.
As-Suyuti (d. 911 AH) kaziripoti rai hizi kama vile Sura zote zilipangwa na Mtume isipokuwa sura ya 9, at-Tawba, ambayo iliwekwa mahali ilipo na Uthman.
Ibn Atiyyah al-Andalusi (d. 546AH) yeye anashikilia kuwa baadhi ya Sura zilipangwa na Mtume na nyingine na Maswahaba. Sheikh Azami anasisitiza kwa mkazo mkubwa kuwa rai sahihi ni ile ya wengi ambayo kwa sasa ndiyo rai ya pamoja ya wanazuoni wa Kiislamu na ambayo inathibitishwa na ushahidi mwingi kama vile maamrisho ya wazi ya Mtume kwa waandishi wake kuziweka aya na sura katika mpangilio fulani (Taz. Hadith zilizoripotiwa katika Tirmidh 3086; Baihaqi ii:42; Ibn Hanbal 69; Abu Dawud i:29; Hakim i:221
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


