Skip navigation.
Home kabah

Jinsi Ya Kuyahimili Mambo Yasiyotarajiwa Katika Maisha Ya Ndoa




(Na Dk Salwa Rashad)

Imefasiriwa na Shaibu H. Kifea

Huwa unapata shida kuota ndoto za kumpata mwandani mwenye sifa unazozitaka. Lakini kinyume na ndoto zako yawezekana ukajikuta unaishi na mwenza ambaye halingani na ile picha iliyokuwa akilini mwako ambayo ulidumu nayo kwa miaka mingi.

   Ikiwa mwanandowa mwenzio ana upungufu kinyume na matarajio yako, si vizuri kumfanyia ukatili na kumfanya akose raha ya maisha ya ndoa au aone kuwa maisha ya ndoa ni machungu.

     Jaribu kurekebisha mambo kwa upole, uungwana na ucheshi kama ambavyo wewe ungependa wengine wakutendee pale unapokosea.

       Ni jambo jema zaidi kumpa majibu yako bila jazba. Jaribu kumuelimisha polepole, mueleze kwa utulivu na mpe heko pale mambo yanapokwenda sawa.

       Mara zote ukumbuke kuwa ni MwenyeziMungu Pekee Atakayekupa malipo unayostahiki kwa subira yako. Vyovyote mume atakavyostahamilia tabia mbaya ya mkewe atapewa malipo kama yale atakayoyapata Yaqub (as) na vyovyote mke atakavyovumilia tabia mbaya ya mumewe atapewa malipo sawa na yale ya Asia (mke mwema) wa Firauni.”  (al-Ghazal)

       Kuna stratejia kadhaa zinazoweza kukusaidia kupunguza pengo la tofauti kati yako na mwandani wako. Nazo ni:

    

              Kuweka Malengo na Mambo ya kipaumbele

      Isome vizuri  aina ya tabia ya mwandani wako, huenda ukabaini labda yale matarajio uliyokuwa nayo wewe ni ya juu mno kiasi kwamba hakuna mwanamke wa kibinadamu anayeweza kuyafikiya.

     Hebu sasa wewe mwenyewe jitahidi kuwa mkweli  katika kuyatathmini malengo yako na kuangalia yale mambo yenye umuhimu miongoni mwa yale unayoyataka.

      Kujenga tu matarajio kwa njozi zisizoweza kutekelezeka kwaweza kukuletea mfadhaiko. Mke kwa upande wake, anaweza kuishi bila kumtarajia mumewe kuwa tajiri au mtu wa mafanikio lakini bado akafurahi na familia yake.

     Wakati mwingine ni vigumu kufanikiwa kufanya jambo bila kujitowa muhanga ambao huigharimu familia. Kwa kutaka mke msomi au kwa ajili ya kuongeza kipato, mume huenda akamuhimiza mkewe atafute elimu au akafanye kazi nje ya nyumba yake.

   Lakini bado mume huyu anamtarajia mkewe afanye kazi kama mama wa nyumbani anayetumia muda wake wote na nguvu zake kwa ajili ya kazi za ndani ya nyumba.

    Changamoto halisi ni kuelewa mahitaji yako halisi na kuangalia mambo muhimu. Lazima utambuwe mambo ya kujitowa muhanga na mambo unayohitaji kuyafanyia marekebisho.

     Katika kuweka malengo na mambo ya kipaumbele, wandani lazima  watafakari na kujali mahitaji ya kila mmoja wao. Katika kufanya maamuzi ili kufikia malengo yao lazima watambuwe upungufu unaoweza kuwepo katika kipengele kimoja kwa ajili ya tija katika kipengele.

    Tufuwate ile kanuni ya uhifadhi wa nishati ambayo inasema kuwa tunatumia kiasi cha nishati katika shamba jipya kwa kuchukua kiasi sawa na hicho cha nishati kutoka shamba jingine.

    Unapoziendea shughuli zako lazima ukumbuke kuwa familia yako ndiyo kipaumbele nambari moja katika orodha ya mambo muhimu kwani wajibu wako kama baba au mzazi ni wako peke yako. Hakuna mtu yeyote duniani atakayekaa badala yako.

 

                     Stahamala na Ukarimu

   Pale hali fulani inapokuudhi, yumkini lawama na shutuma zisizo za haki huanza kukutoka, lazima uoneshe uvumilivu na ukarimu. Kumbuka usemi huu: “Muislamu wa kweli yuko kama ardhi: kila dhambi inatendwa juu yake lakini kile kilicho kizuri tu ndicho kinachotoka ardhini.”

   Mapenzi ya kweli sio kukasirika, sio kuona wivu, kutiliana shaka au kupagawa. Mambo haya ni ishara ya kutokuwepo kwa utulivu unaosababishwa na hali ya kudhaniana vibaya ambayo lazima ichukuliwe tahadhari. 

  Huwa ni rahisi sana kuona makosa ya watu wengine lakini ni vigumu kuyakubali yale yakwetu. Lakini tukiwa Waislamu wakweli lazima tujitahidi kujikosoa. 

    Mtume (saw) kasema; “Amebarikiwa yule anayejiangalia zaidi kasoro zake kiasi cha kutoona kasoro za wengine.

 

                             Pongezi na shukurani

   Ndivyo silika yetu ya kibinadamu ilivyo kushutumu mno udhaifu wa wandani wetu pale tunapopata fazaa, hasira au  tunapochanganyikiwa,  kwa sababu ya kutotimia kwa yale matarajio yetu.

      Unaposumbuliwa na hisia hizi mbaya, mkumbuke (mdhukuru Allah) na muombe akukinge na Shetani ambaye hulifanya jambo duchu sana liwe kubwa na kuleta mlipuko mkubwa kupita kiasi na kukufutia mema yako ambayo ulifaidika nayo hapo kabla.

     Kumbuka kuwa huyo mwenza wako ni neema kutoka kwa Allah ambayo lazima ushukuru kwayo. Kumbuka nasaha hizi za Mtume (saw) kwa waumini wakati wanapokuwa na hisia za kufadhaishwa na wandani wao.

   “Mwanamume aliyeamini asimchukie kabisa mwanamke aliyeamini; Iwapo anachukizwa na tabia moja ya mkewe basi ataona sifa nyingine ya kumfurahisha.” (Muslim).

      Kuoneshana upendo na kuishi kwa mapenzi

       Hata kama utakuwa unampenda mwandani wako kiasi gani, iwapo hutalionesha pendo lako, mwenzio hatahisi kama unampenda. Hata kama unafurahishwa vipi na mwandani wako, kama huoneshi kufurahishwa, yeye hatahisi kama anafurahiwa.

     Hakuna mume wala mke mkamilifu lakini wandani wanapooneshana mapenzi na furaha na kuishi kwa kufuata misingi ya Uislamu, siyo tu watapendana kwa mapenzi na heshima bali pia watapendwa na Allah.

    Magusano ya ziada huongeza zaidi uhusiano wenu wa ndoa na kukoleza huba ya kumfanya mwenza aongeze jitihada za kukuridhisha.

      Aidha zawadi ndogo ndogo ambazo zinaonesha jinsi unavyomjali hizi ni chachu za pendo, na zinasanbaza mawimbi ya mapenzi mwilini mwa kila mmoja

    Vilevile kula na kusali pamoja kwaimarisha mahusiano ya wanandoa. Usipuuze umuhimu wa chakula cha pamoja cha familia. Sufiyan ath-Thawri kasema; “Nimesikia kuwa MwenyeziMungu na Malaika Wake  huipa baraka familia inayokula pamoja.”

     Ni jambo la kupendeza kusali nyuma ya kiongozi wa familia na kufanya naye ibada pamoja. Hata hivyo mume-Imamu lazima azingatie mafundisho ya Mtume mwenyewe ambaye aliifanya sala ikidhi mahitaji na shida za jamaa iliyokuwa nyuma yake. 

      “Mimi husimama kusali kwa kisimamo kirefu lakini punde ninaposikia kilio cha mtoto naifupisha sala kwa kuchelea kuwa mama yake anaweza kudhikika”. (Bukhari na Muslim).

         Mbali na hayo, mambo mengine madogo sana kama haya yanaweza kukuleteeni kheri. Mtume (saw) kasema, “hata kumlisha mkeo tonge la chakula mdomoni ni sadaka” (Bukhari na Muslim).

 

      Hii inaonesha aina ya ukarimu unaotakiwa kuwepo katika ndoa ya Muislamu