Skip navigation.
Home kabah

Jinsi Ya Kujenga Maisha – Wito Kwa Wazazi

 

  

(Na Yasmin Mujaahid)

Imefasiriwa na Batul H. Kifea  (Ummu Ashraf)

 

“Miyaka miya moja, kuanzia sasa, haitakuwa na maana tena kuzungumzia akaunti yangu ya benki ilikuwaje, nyumba niliyoishi ilikuwa ya aina gani au gari langu lilikuwa la aina gani. Lakini ulimwengu unaweza kuwa mwingine kwa sababu nilikuwa mtu muhimu kwa maisha ya mwanangu au wanangu.”

 

Ubeti huo wa shairi unakumbushia jambo lile lile alilofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) miyaka 1400 iliyopita. Mtume wa Allah alisema, “Mwanadamu anapokufa, amali zake hukatika isipokuwa tatu; sadaka inayoendelea, elimu inayonufaisha wengine au mtoto mwema anayemuombea (Muslim na Ahmad).

Katika makaburi yetu, utajiri wetu hautakuwa na faida yoyote kwetu. Mafanikio yetu makazini, na viwango vyetu vya shahada za elimu, havitakuwa na thamani. Je tuliwaleaje watoto wetu? Hili ndilo jambo la maana

 Lakini bado muda wetu mwingi, elimu yetu nyingi na jitihada zetu nyingi zinatumika kwa ajili ya mambo hayo ya kupita.

Katika Hadiyth nyingine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kasema, “daraja la mja litanyanyuliwa, naye atasema: ‘ewe Mola wangu jambo hili limekuwaje kwangu?’ Mola amwambie: “Ni kutokana na watoto wanaokuombea maghfira nyuma yako”. (Ahmad na Ibn Majah).

Tukiondoka duniani, tutaacha nini nyuma yetu? Tutaacha alama gani? Nini tutakachopeleka huko twendako? Tutachukua nini? Watoto wetu watarithi maisha haya.

Katika mikono yao ndimo ilimo nusura yetu au ndimo yalimo maangamizi yetu. Mikononi mwao ndimo ilimo nusura ya Umma wetu au ndimo ilimo dhahama ya umma wetu.

Je jambo muhimu kama hilo halihitaji mazingatio yetu yote? Je hatupaswi kujitazama na kufanya juhudi zote kutimiza kazi hii muhimu ya malezi?

 

 

Usilazimishe Bali Pandikiza Mapenzi Mapema

Jaalia mtoto analelewa katika nyumba ambayo Uislamu haupo hata kwa maneno matupu. Wazazi hawana habari ya Swalah wala jambo lolote la Kiislamu, sasa chukulia mtoto huyo anafikia umri wa kubalekhe.

Kama ni msichana, ndio sasa anaambiwa avae Hijab na mvulana analazimishwa kuswali, je itashangaza kweli kama watoto hawa watagoma na kuwa waasi?

Lakini jaalia mtoto kalelewa akijuwa kusoma Qur’an, akiipenda dini yake, akienda msikitini na kusali pamoja na mzazi wake, je mtoto kama huyu atahitaji kushurutishwa kuswali au kuvaa Hijab? Si litakuwa jambo la kuendelea na mwenendo wa Kiislamu aliokwishakuwa nao.

Kwa hiyo, ni wajibu kwa mzazi kupandikiza na kukuza mapenzi ya mtoto kwa Allah, Mtume wake na dini yake mapema tangu anazaliwa

 

 

Chunga Televisheni Na Michezo Ya Video

Baadhi ya wazazi huchukua hadhari juu ya mambo ambayo watoto wao huyatazama katika televisheni lakini wazazi hao hawafanyi hivyo mara zote. Hata kama wazazi watasimamia vema utazamaji wa televisheni wa watoto wao bado kutakuwa na athari tu ya jambo hili kwa sababu kutazama TV ni mazoea ambayo mtoto hayaachi hadi ukubwani.

Kwanza, kwa upande wa programu, karibu programu zote hata zile zinaoonekana kuwa sio mbaya kwa mtoto kuangalia, si programu zilizoandaliwa kwa maslahi ya Uislamu.

Pili, zingatia muda mwingi unaoliwa na TV. Watoto huweza kushinda mchana kutwa au kukesha usiku kucha wakitazama TV na michezo ya video. Yazingatie maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) kuhusiana na umuhimu wa muda.

“Miguu ya mja haitaruhusiwa kuingia (Peponi) Siku ya Malipo mpaka aulizwe mambo manne: Uhai wake au maisha yake aliishije, ujana wake, aliutumiaje, mali yake aliichumaje na aliitumiaje na elimu yake nayo aliitumia vipi (at-Tirmidhiy).

La mwisho ni kwamba utafiti wa majumbani unaonesha kuwa watoto wanaopoteza muda mwingi kutazama TV na michezo ya video hupunguza hamasa ya kusoma, huchukia kutumwa, huwa hawapendi kazi zinazowakosesha wasaa wa kutazama “gemu”, akili yao muda mwingi hufikiria TV na kadhalika. Mtoto akiwa katika hali hii, ni wazi atachukia hata Swalah iwapo inaingiliana na muda anaotaka kutazama mchezo wake katika TV.

La muhimu kwa wazazi ni kuwa mbali na kuchunga mambo ambayo watoto huyatazama katika TV na Video ambapo wao lazima wafuatilie kila mkanda na ikiwezekana wao wenyewe waanze kuutazama ili kuona kama unafaa na kutowaacha watoto wajikodie tu mikanda na kuitazama peke yao, na kuhakikisha kuwa TV hailali chumbani kwa watoto, pia wapange ratiba mahususi ya utazamaji wa TV.

 

 

‘Waharibu’ Watoto Kwa Mapenzi

Moja ya semi mashuhuri inasema, “mapenzi ya kupita kiasi” huharibu watoto. Usemi huu hauko mbali na ukweli japo kwa kinyume chake. Watoto “wanaoharibiwa” kwa mapenzi na hali ya kuwajali huwa wakarimu mno, huwapenda na kuwapa vitu wenzao. Na wale waliokosa mapenzi haya mara nyingi huwa na nyoyo ngumu na wagumu wa kutoa.

Hakuna mtu aliyekuwa na huruma zaidi na aliyeonesha mapenzi makubwa kwa watoto kama al-Habib Mtume  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam). Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) aliwahi kutembelewa na Al-Aqra ibn Habis. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akamnyanyuwa Hassan na kumpakata mapajani na kisha akambusu (akamshumu). Al-Aqra akasema;

“Mimi nina watoto kumi lakini sijawahi kumbusu hata mmoja”. Jambo hili alilolizunguma kwa fahari, lilionesha kuwa, katika makuzi yake bwana huyo hakuwa na moyo laini, bali alikuwa na moyo mgumu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akamwambia;  Nikusaidieje ikiwa MwenyeziMungu ameondowa huruma moyoni mwako?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) akaendelea kusema; “na yeyote asiye na huruma hatapata rehema.” (al-Bukhaariy na Muslim)

Usiwape wala Usiwaahidi watoto zawadi kwa ajili ya matendo maalum ya Ibada

Usiwape malipo wanao kwa ajili ya kufunga au kuwaahidi zawadi nono ikiwa watasali. Badala yake pandikiza mapenzi kwa Allah nyoyoni mwao ambayo ndiyo yatakayowasukuma kusali na kufunga. Msukumo wa kufanya mambo haya lazima utuokee ndani ya nafsi na si nje.

Wanasaikolojia wa maisha ya jamii wameonesha kuwa watu wanapopewa bahashishi kwa sura ya nje au wanapopata msukumo wa nje kufanya jambo fulani, huhamasika kidogo sana kufanya jambo hilo kuliko wasipopewa malipo ya nje na badala yake wakapewa hamasa ya ndani ya nafsi.

 

 

Kuwa Karibu Na Wanao Tangu Mapema

Anza ulezi wa karibu mapema. Watoto wako wanapokuwa bado wadogo, waruhusu walale jirani nawe na uwabebe mara kwa mara. Utafiti unaonesha kuwa kufanya jambo hili hakuharibu watoto.

Lakini mzazi ahakikishe ukaribu huu na mtoto unaleta matokeo bora ukubwani mwake. Mbali ya kuwa ukaribu huu ndio chachu ya mafanikio  ya malezi ya mzazi kwa mwanawe au wanawe, pia ndiyo msingi bora wa da’awah ya mzazi kwa familia yake kwani bila ukaribu huo hawezi kupandikiza Uislamu kwa mtoto au watoto wake.

Lazima mzazi wa Kiislamu azingatie uhusiano wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na bintiye Fatima. Tangu mapema kabisa binti huyu alikuwa jirani mno na baba yake na hapo ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) alipofikisha ujumbe wa Allah Kwa mwanawe.

 

 

Ukaribu Ndio Hatuwa Ya Kwanza Ya Nidhamu

Iwapo utajengeka ukaribumwema mapema kati ya mzazi na mtoto, basi nidhamu itakuja kirahisi kabisa. Kama mzazi atadumisha ukaribu huu na mwanawe na kuonesha mapenzi na furaha basi mtoto ataepuka kufanya mambo ya kuhatarisha uhusiano huo.

Nidhamu sio mpaka ihitaji fimbo, bali inajengeka kimaumbile tu. Uhusiano wa mzazi na mtoto ukijengeka kwa mapenzi na heshima, mtoto hujawa na hamasa na hatimaye hujenga mazoea ya kudumisha heshima.

 

 

Wajengee Watoto Heshima

Hakikisha kuwa watato wanajuwa wao ni wabora kiasi gani. Pale inapowezekana wasifu kwa wema na unadhifu wao. Hakikisha kuwa wanao wanajuwa kuwa wao ni neema kubwa na ni watu muhimu sana.

Wafahamishe kwamba wao wana uwezo wa kuibadili jamii na dunia, na onesha tumaini na imani kubwa uliyonayo juu yao. Mtoto anayeambiwa mara kwa mara kuwa yeye ni hasara basi atakuwa hasara hivyo hivyo. Na mtoto anayeambiwa kuwa ataibadili dunia, basi atakuwa na fikra hiyo hiyo.