Zingatio: Waislamu Kwa Nabiy Wao

 

Zingatio: Waislamu Kwa Nabiy Wao

 

 Naaswir Haamid

 

 Alhidaaya.com

 

 

BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym. Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh.

 

Mwenye kumtii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi hakika amemtii Allaah, na mwenye kumuasi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakika amemuasi Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kwa masikitiko makubwa baadhi ya sisi Waislamu tunamtii Shaytwaan (Ibiliys) na hivyo kumuasi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Waislamu walio wengi hawana muda wa kutafuta habari au kujifunza juu ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa mkweli na katu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).  hajapatapo kusema uongo. Sisi tunafuata Sunnah ya Ibiliys kwa kusema uongo asubuhi na mchana. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa ni mwingi wa ibada za usiku na mchana.

 

Baadhi ya Waislamu leo Swalaah tano zinatushinda. Swalaah ina sharti na nguzo zake; walio wengi huziswali pasina mazingatio hayo na hivyo Swalah  hizo huwa hazipo yakinifu wala zenye uhakika. Matokeo yake Swalaah za aina hiyo  zinakiuka mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Swalaah za aina hiyo hazitupatii mema yaliyoahidiwa na Allaah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiamka usiku kuswali kwa khushu’u kubwa na huku akilia hadi mwili wake kuvimba na kupiga wekundu. Sisi binaadamu tunaangusha kilio kwa kukosa vyeo, mali na wanawake. Tupo tayari kupigana kwa kugombea vyeo, wanawake na siasa zisizokuwa na itikadi ya Kiislamu. Lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mbele ya mstari kwa kupigana na maovu na kuwaamrisha Waislamu kutendeana mema baina yao.

 

Yeye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na maovu ya aina yoyote kama vile ulevi, uzinifu, kamari, au mapumbao ya michezo kama karata, dhumna na kadhalika. Bali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye nguvu za kujiamini. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na chembe cha unafiki kama wengi wetu miongoni mwa sisi Waislamu wa leo tulivyo.

 

Waislamu katika miaka hii tumezongwa na maradhi ya ubakhili hali ya kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala) alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Toa! Allaah ndie Mpaji. Sisi binaadamu tunaogopa ufakiri; shughuli zetu za Kiislamu zimekosa muelekeo kwa kupungukiwa na fedha za kuendeshea kazi za da’awah na kazi za huduma katika jamii zetu.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahimiza Swahaba wake kujitahidi kufanya kazi na kuepukana na kuomba omba.  Leo mamia ya Waislamu hukaa njiani na vibarazani kunyooshea mikono wapitao bila ya haya wala aibu. Mafundisho sahihi ya Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tumeyatupa nyuma ya mgongo. Mafundisho sahihi ni kuwa ‘hayaa ndiyo Uislamu’.  Hayaa zetu zienee kwenye kuona aibu kutotenda mema na kuona aibu kutenda ma’asia.

 

Inasikitisha kuona kwamba viapo vya uongo vimekuwa ni vya kawaida kwa kumuapia Muumba. Viapo hivyo huenda katika kuwadhulumu hata mayatima bila ya aibu.  Hayaa na aibu zimetutoka hadi kufikia kumuapia Allaah tena kwa jambo la uongo hali ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekemea kwa ukemeo mkali sana kuapa kwa uongo.  Je haya ni mapenzi ya Allaah au Shaytwaan ?

 

Amri zake Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya wanawake zimewekwa chini ya nyayo na kutundikwa kwenye nguo zao. Imekuwa kama vile Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekuja kuwaamrisha wanawake kutembea bila ya nguo.  Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuja kuwaamrisha kuanzisha ngoma na kuicheza namna anavyotaka Ibiliys.  Imeruhusiwa sherehe katika harusi lakini sivyo wafanyavyo wengi katika wanawake. 

 

Ukiwaelekeza utapata jibu “kwani sherehe zimekatazwa?’ Jibu: ‘Je, hizo ngoma na ‘kitchen party’ ndiyo aliyotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?’ Yupo mbali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vitimbi hivyo vinavyoongozwa na Ibiliys. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanana na Qur-aan hali ya kuwa sisi tunasema kuwa Qur-aan haimtendei haki mwanamke.

 

Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi aalihi wa sallam) alikuwa mwalimu mwema kwa wanafunzi wake lakini sisi Waislamu tunakuwa ni walimu kwa midomo na waovu kwa vitendo. Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni kiongozi mwenye huruma kwa raiya wake ilhali viongozi wa Kiislam ndio wanaoongoza kwenye maasi na hata kufikia kuitwa madikteta. Na msiba zaidi, wengi wao wanashirikiana na makafiri katika kuupiga vita Uislam! Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hajifadhilishi na wenzake katika kivazi hali ya kuwa sisi Waislamu tunajifaharisha kwa kuvaa na kukiuka mipaka kwa kuendesha mashindano ya urembo.

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akijifidhalisha kwa chakula ilhali sisi Waislamu wa leo tupo tayari kukimwaga chakula kwa kumwonesha jirani kile kilichomo ndani ya tumbo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na nyumba wala vyombo vya kifakhari. Yupo mbali na anasa za dunia.  Ingawa haijakatazwa kulala pazuri wala kula vizuri, lakini sisi Waislamu tunalazimika kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuwa na vitu vya haja za lazima na wala siyo kujifaharisha. Sunnah yake isiwe mdomoni tu, bali iwekwe nyoyoni na kutekelezwa kwa vitendo.

 

Elimu aliyoileta Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu Waislamu iwe ndiyo dira na nuru; juhudi zichukuliwe kuigharimia elimu hiyo.  Ndugu Waislamu, tujipinde ili mambo yetu yasiwe tofauti na amri za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Juhudi zichukuliwe ili Uislamu wetu usiwe na mashaka katika uhai wote. Tujiepushe kujiingiza katika ukafiri na utovu wa nidhamu katika siku zote.  

 

Hadiyth ifuatayo ya Nabiy  Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iwe ni khitimisho ya makala hii na In shaa Allaah iwe ni nuru katika maisha yetu:

 

Imesimuliwa na Anas bin Maalik. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa  aalihi wa sallam):

 

"Naapa kwa Yule Aliyeimiliki nafsi yangu, Hatoamini mmoja wenu mpaka niwe (mimi Muhammad) kipenzi chake kuliko mwanawe na wazazi wake na kuliko watu wote waliobakia." [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].  

 

Share