Skip navigation.
Home kabah

Utabibu Na Utunzaji Wa Afya Katika Uislamu



(Na Hussein Haidi)

Imefasiriwa na Shaibu Kifea


Wakati nikiandaa makala hii, nilizingatia maonesho ya kuvutia yaliyoandaliwa na Maktaba moja ya Utabibu miaka michache iliyopita. Maktaba hii iliadhimisha mafanikio ya taaluma ya tiba katika jamii ya Kiislamu zaidi ya miaka 1000 iliyopita.

Pia ilionesha muswada wa tiba wa Kiarabu ulioandikwa na Daktari wa Kiislamu, Muhammad Z. ar-Razi (ambaye katika nchi za magharibi anaitwa ‘Rhazes’). Muswada huu wa Kihistoria ndiyo wa zamani zaidi katika maktaba yao..

Lakini tukio hilo ni moja tu kati ya mengi yanayohusiana na fani ya utabibu katika Uislamu. Mbali na makongomano na vitabu vinavyozungumzia suala hili, vituo vingi vya utafiti vilianzishwa ulimwenguni kwa lengo la kuendeleza zaidi fani hii. Hivi leo vituo hivyo vyaweza kuonekana Misri, Malaysia, Kuwait, Pakistan na Marekani.

Utabibu wa Waislamu, uliotumika katika vitabu vya tiba vya kihistoria vinavyohusu maendeleo ya elimu ya tiba, ulianzishwas na kuendelezwa katika zama zote zilizotawaliwa na utamaduni wa Kiislamu. Hata hivyo, fani hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko vile inavyodokeza historia.

Fani ya utabibu katika Uislamu inaoanisha mwili na roho. Kwani Uislamu hautenganishi sayansi na dini. Mafundisho yake mengi yanahusu magonjwa, afya, ustawi wa kisaikolojia, lishe, maradhi ya kuambukiza, ngono na kadhalika.

Katika Sunna ya Mtume sallallahu alaihi wa sallam, mtu anaweza kukuta mamia ya rejea zinazohusu masuala ya afya, tiba na maradhi. Mkusanyo wa Hadith hizi ndio ulioleta maendeleo ya fani nzima ijulikanayo kama at-Tibb an-Nabawi-Tiba ya Mtume.

Katika Hadith hizi, kuna kauli ya Mtume kuwa, “hakuna ugonjwa wowote isipokuwa MwenyeziMungu ameuumbia tiba (dawa) yake” (Bukhari). Hii ndiyo kauli iliyowapa changamoto wanazuoni wa Kiislamu kufanya tafiti za tiba.

Changamoto hii ya Uislamu ndiyo iliyofanya Waislamu wawe vinara katika  nyanja nyingi za tiba ambapo, kinyume na mtazamo wa wengi miongoni mwa wanahistoria, sio tu waliweza kutafsiri vitabu vikubwa vya elimu kutoka Ugiriki, Uislamu ulihimiza utafiti na taaluma, na ndio maana wanazuoni wa Kiislamu walikuwa matabibu na wakati huo huo walimu wa theolojia, sheria na sayansi.

Kwa ujumla, tiba katika Uislamu yaweza kuanishwa kama ni mfumo wa kanuni za afya na maadili unaowiana na Qur’an na Sunna. Huku Uislamu ukivikubali vipengele vya tiba ya kurejesha afya, pia unasisitiza kuwa uhai wenye afya unahitaji uwiano kati ya mwili, akili, roho na mazingira.

Uislamu hauutazami ugonjwa kuwa ni jambo baya. Bali ugonjwa hutazamwa kama ni mtihani kutoka kwa Allah, ikiwa ni njia ya kumtanabahisha mtu kumjua na kumtegemea MwenyeziMungu.

Ugonjwa pia unaweza kuonwa kama ni njia ya MwenyeziMungu ya kuhakikisha kuwa mtu anaupumzisha au kuutunza mwili wake kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Kwa mtazamo wa tiba wa Kiislamu, sababu za magonjwa zinatokana na maamuzi mabaya na uharibifu wa mwanadamu. Lakini uzima wa afya hupatikana kutokana na tiba sahihi na dua.

Mara zote tukumbuke kuwa hakuna kitu kinachoweza kufanya kazi bila amri na idhini ya MwenyeziMungu. Mara zote tuishi maisha yetu kwa kuizingatia na kuitekeleza Qur’an ambayo yenyewe pia inajieleza kuwa ni ponyo kwa wanadamu.

 

a.w.w.naam,makala ni

a.w.w.naam,makala ni nzuri,ila ingeboreshwa kwa kutoa mifano halisi ktk kipengele kilichogusia mchango wa sunna ktk tiba..yaani hadith,na maudhui yake,na insi gani ilivyo applicable....itatusaidia sisi wengine kutosumbuka kupata ref,hata hivyo wengine hatujazama ktk dini.....