Vipi Tumkaribishe Mgeni Wetu Mpenzi Na Mtukufu Ramadhwaan

Imekusanywa na: Abu Faatwimah

 

Shukrani zote ni Zake Muumba wa mbingu na ardhi Aliyezitukuza siku chache za mgeni wetu Ramadhaan kwa kujaalia mambo mengi ndani yake, Muumba Aliyemtunuku Ramadhaan zawadi tukufu ya kuwa ndio wakati aliouchagua wa kuyaleta/kuyashusha maneno Yake matukufu, ambayo ni uongozi na uongofu kwa viumbe wote, Qur-aan inasema:

 

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi…” Al-Baqarah aya ya 185.

 

Rehma na Amani za Allaah zimfikie Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na kila aliyejaaliwa kufuata na kushikamana na mafunzo yake swahiyhah, yeye Mtume (Salla AAllaahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasallam) amepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akisema kuwa: Allaah Amesema:

“Kila ‘amali anayoifanya mwanaadam huongezewa, jema moja kwa kumi mpaka mia saba, na halafu huongezwa kwa Atakavyo Allaah, isipokuwa Swawm (funga), hiyo (Swawm/funga) ni Yangu Mimi, na Mimi ndiye Mlipaji wake ….” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila za Swawm.

 

Ndugu zangu wapenzi katika imani, napenda kujiusia nafsi yangu kwanza na nasfi zenu kumcha Allaah na kumtii, kwa kutekeleza kila Aliloliamrisha kadiri ya uwezo wetu, na kujikataza na kila Alichokikataza mara moja.

 

Ndugu zangu katika imani, Ramadhaan ni mgeni aliyejenga uhusiano mzuri na wenye nguvu na Waislamu wa kila zama, kwa njia ya kuwatembelea katika nyumba zao kwa kukaa na kuishi nao kwa wakati wote wa kipindi cha mwezi mzima.  Mgeni huyu ndiye yule yule aliyewahi kuwatembelea na kukutana uso kwa uso mara karibu tisa na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), kipenzi chetu na kipenzi cha wote wenye kumtarajia Allaah na Siku ya Mwisho na wakamkumbuka Allaah sana.

Mgeni huyu aliwahi pia kuwatembelea Sahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) na Waislamu wote wa karne zilizopita, na ni huyu huyu atakayewatembelea insha Allaah kwa uwezo wake Mola Waislamu wa karne zitakazokuja baada yetu tutakapokuwa chini ya tani za udongo.

 

Twamuomba al-Hayyu al-Qayyuum Atusamehe makosa yetu na madhambi yetu makubwa na madogo, ya mwanzo na ya mwisho, tuliyoyafanya kwa dhahiri na kwa siri, na Aturuzukuku maghfirah na tawbah kabla ya kuiaga dunia hii yenye kutushughulisha karibu wengi wetu, na tukutane naye hali ya kuwa ni Waislamu waliosamehewa na waliokubalia tawbah zao insha Allaah, Aamiyn Aamiyn Aamiyn.

 

Ndugu zangu katika imani, ni miongoni mwa mambo yaliyozoeleka kuwaona Waislamu wa kila nchi, miji, vijiji na mitaa kujiwekea wakati wa kukumbushana na kuelezana namna ya kumpokea mgeni huyu mtukufu na namna ya kuishi nae, kama ni matayarisho na mapokezi yake. Hivyo utaona kwa mfano mihadhara kama sisi hapa leo kwa fadhila, rehma na uwezo wa Jabbaar tumekutana kwa hilo, au maandishi kwa wenye kutumia mtandao yenye kubeba anuani kama zifuatazo:

 

          Namna ya kuikaribisha Ramadhaan

          Vipi Tuikaribishe Ramdhan

Njia kumi za kuukaribisha vizuri Ramadhaan

          Mambo ya kuikaribisha Ramadhaan

         

 

Ndugu zangu katika imani, yote haya na mengine kama haya, huwa na lengo la kuwataka Waislamu kujiandaa na kujitayarisha kwa kujiweka tayari kumpokea mgeni wao mtukufu, kwa namna au njia itakayokubaliwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam).

 

Ndugu zangu katika imani, matayarisho ya kumpokea mgeni ni ya namna nyingi, hasa hasa kwa kuwa mgeni wenyewe ni ‘adhimu, na ni mwenye ku’adhimishwa na kila mwenye kuAamiyni Allaah na Siku ya Mwisho, kwani wao pekee ndio waliotajwa na kuainishwa katika Qur-aan, kuwa wamependekezewa mgeni afikie makwao, akae nao na kuishi nao, kwa kuchunga na kuhifadhi mipaka yake, wametajwa na kuainishwa kwa jina au sifa wanayoipenda wanasibishwe nayo, bali ndio kitambulisho (identity) chao katika uhai wao huu na ujao insha Allaah, kinachojitokeza hapa ni vipi sisi tutamkaribisha/tumkaribishe Mgeni huyu, mgeni ambae wenyeji wake ni watu maalum, kama inavyothibitisha Qur-aan, Allaah Anasema:

 

Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungual-Baqarah aya ya 183,

 

Ndugu zangu katika imani, muhadhara wenye anuani kama hii huwa na lengo la kutupelekea kuwa na hamu na shauku ya kujiweka tayari kwa at-Tawfiyq na uwezo wa Mola wa Ramadhaan kumpokea mgeni, lakini kwa kuwa wenyeji wake au waliopendekezwa wampokea mgeni, ni wale wenye kupenda kunasibishwa na sifa au kuainishwa kwa jina maalum (walioamini), jambo hili hupelekea tukawa na makundi ya watu yenye fikra na mawazo tofauti katika kumpokea mgeni Ramadhaan, hivyo kuwasili kwake kunawagawa Waislamu (sio waumini) katika makundi mengi yakiwemo yafuatayo:

1) Wanaompokea mgeni kwa moyo uliojaa furaha, kwa kuwa Allaah Amewapendekezea mgeni na Akawawafiqisha kuweza kukutana na mgeni wao Ramadhaan baada ya wengi miongoni mwao kuiaga dunia.

2) Wanaompokea mgeni kwa manung’uniko na masikitiko kwa kuwa mgeni huyu atawanyima starehe zao na atapekelea baadhi ya matamanio yao kutopatikanwa, bali ni maudhi na mateso tu, hakuna jipya, kwa nini watu wafunge na kujizuilia kula na kunywa! Bali hata hufikia kusema kuwa hivyo kweli Allaah Ameipendekeza Swawm kwa watu, jambo ambalo linapelekea kuingiliana katika mambo binafsi na uhuru na matakwa ya mtu.

3) Wanaompokea mgeni kwa michezo na kila lenye kupoteza wakati, (kupitisha masaa) kwao wao kuja kwa Ramadhaan ni jambo la kawaida na ni katika mila na desturi za jamii wanazoishi, lililo muhimu kwao ni kuonekana amefunga (hali, hanywi, aweza kufanya ayatakayo kama kawaida yake mradi atajichunga asionekane na ma-Ustaadh) hakuna jipya isipokuwa kushinda na njaa, kwani majumba mengi huwa hawapiki, kwa ufupi ni mwezi wa kushinda na njaa.

4) Wanaompokea mgeni kwa wasiwasi na shaka, huku wakijaribu kujitetea na kutaka kuonekanwa kuwa Waislamu poa (moderates), kwani wanachokifanya (funga) si jambo geni, wala hakuna tofauti na wengine, kwa kuwa linafanywa pia na wengine wenye dini (Manasara, Mayahudi, na kila mwenye kujidai kuwa ana siku katika dini yake za kufunga), hivyo hakuna jipya.

Je, mimi na wewe tumo katika kundi lipi? Tujipime kulingana na Ramadhaan tulizokutana nazo na ile ya karibu kabisa ni ya mwaka jana.  Je, mwaka huu mgeni ndio huyo yuko kizingitini, tunapenda tuwemo au kuingia katika kundi lipi? Lenye kupenda kunasibishwa na jina la waliotakiwa waishughulikie Ramadhaan, kwa kuchunga, kuheshimu na kuhifadhi mipaka yake, kulingana  na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), au makundi yasiyopenda kuainishwa na kunasibishwa na jina/sifa waliyonasibishwa nayo waliopendekezewa Ramadhaan?

Ndugu zangu katika imani, mgeni yeyote yule utaelewa hadhi yake na umuhimu wake kwa mwenyeji/wenyeji wake, kutokana na maandalizi na mapokezi yake, ndio sisi tukawa na anuani kama hii, Vipi tumkaribishe Ramadhaan,  na ili tuelewe namna gani anahitaji kupokewa na kukaribishwa huyo mgeni wetu Ramadhaan, ni vyema kwanza tumuelewe Ramadhaan mwenyewe ni nani? na baada ya hapo ndio upange, wewe na sio mimi, namna ya kumpokea na kumkaribisha, kwani si jambo la kawaida kuwa mgeni wako na atakuwa nyumbani kwako, bali atakuwa na wewe muda wa mwezi mzima katika masaa ishirini na nne (24) yako, ya kila siku yako, aje atokee mtu mwengine nje (kama mimi), akupangie namna ya kumkaribisha!, labda awe mtu wako wa karibu sana, kama vile rafiki yako na kadhalika.

Ndugu zangu katika imani, hata hivyo sisi leo hapa tuko katika kushauriana, kuwaidhiana, kupeana fikra, na mawazo, kupendekezeana juu ya jinsi ya kumkaribisha Ramadhaan, na mwisho wa hayo wewe ndiye muamuzi wa mwisho, hivyo suala ni hili, unamuelewa vyema mgeni wako? Kama kweli unamuelewa, basi vipi umepanga kumpokea? kama umejipangia, na kama bado, je, uko tayari kusikiliza mapendekezo yangu? Mapendekezo ambayo kwa kweli hayana uzuri wo wote kuliko yale utakayojiwekea wewe mwenyewe kwa hiari yako.

Ndugu zangu katika imani, Ramadhaan au mgeni wako (wetu) mpenzi yuko hivi kama alivyoelezwa na Mola wake, Allaah Anasema:

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru” Al-Baqarah: aya ya 185

Pia Mtume (Swalla AAllaahu 'Alayhi Wa ‘Alaaa Aalihi Wa Sallam) amesema kutokana na masimulizi ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu):

“Mwenye kufunga Ramadhaan (kama inavyotakiwa na sio kukaa na njaa) kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani.

Vilevile Mtume (Swalla AAllaahu 'Alayhi Wa ‘Alaaa Aalihi Wa Sallam) amesema kama ilivyosimuliwa na Abu Hurayrah kuwa:

"Inapoingia Ramadhaan, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya Moto hufungwa, na mashetani hufungwa …" Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila za mwezi wa Ramadhaan.

Ndugu zangu katika imani, miongoni mwa mambo yanayotupelekea kuwa na mihadhara kama hii itakayoweza kwa at-tawfiyq ya Mola kutupelekea kujiandaa vizuri, ni ile Hadiyth iliyothibiti ya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kuwa alisikiwa akisema Aamiyn Aamiyn Aamiyn mara tatu (3) huku alipanda Minbar, alipomaliza Sahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) walimuuliza kwa mshangao mkubwa, mbona umeitikia Aamiyn Aamiyn Aamiyn, mara tatu huku ukipanda vidaraja vya Minbar, jambo ambalo si kawaida yako, hukuomba du’aa, je kuna liilojiri?! Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) aliwajibu kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) na wengineo:

“Amenijia Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) na kuniambia kuwa: yuko mbali na Rehma za Allaah yule ambaye ametembelewa na Ramadhaan na akashindwa kutekeleza kitachopelekea kufutiwa madhambi yake, - nilinyamaza kimya, Jibriyl akanitaka niitikie kwa kusema: Aamiyn, nikasema: Aamiyn -akaendelea kusema: ‘Yuko mbali na Rahma za Allaah yule ambaye atasikia jina lako linatajwa, na akawa hana nafasi ya kukuswalia, - nilinyamaza kimya, Jibriyl akanitaka niitikie kwa kusema: Aamiyn, nikasema: Aamiyn -, akaendelea kusema: kuwa yuko mbali na Rehma za Allaah yule ambaye amejaaliwa kuwakuta wazazi wake wawili au mmoja wao na akashindwa kuingia peponi!, - nilinyamaza kimya, Jibriyl akanitaka niitikie kwa kusema Aamiyn nikasema Aamiyn”. Imepokelewa na Ibnu Khuzaymah, Kitabu cha Swawm, mlango wa inapendezwa (istihbaab) kujitahidi katika kufanya ibada ndani ya Ramadhaan.

Ndugu zangu katika imani, tujaribu kuwa na tabia ya kujiwekea mipango, malengo, njia na mbinu za kutekeleza mambo yetu, njia za kujitayarisha katika kuyatekeleza na kadhalika, tena tuwe wakweli na wawazi katika mipango yetu, kwa mfano na haya ndio hasa tunayoyapendekeza na kuyataka tuwe nayo katika kumpokea mgeni:

Azimia kuwa mgeni utampokea kwa kila aina ya ‘amali njema, na utajitahidi kiasi cha kumthibitishia mgeni, kuwa katika wageni wako wote wanaokutembelea nyumbani kwako na kuishi na wewe ni yeye Ramadhaan pekee ndiye unayempenda na kumthamini, kwa sababu kubwa moja, ni mgeni aliyekupendekezea Mlinzi wako na mlinzi wa waumini mote, Mlinzi Mwema na Msaidizi Mwema, amekupendekezea Ramadhaan awe mgeni wako ili kwa at-Tawfiyq Yake upate yale aliyoyaandaa na kuyatunuku ndani yake. Tafadhali angalia nini uliwafiqishwa mwaka jana na kile ulichoshindwa kukitekeleza, ukiwekee mikakati ya kukitekeleza mwaka huu, azimia kuwa mwezi wako huu uwe ndio mwezi bora utaoishi nao, na kutekeleza utachojaaliwa na kuwafiqishwa kutekeleza ukijilinganisha na miezi yote iliyopita ikiwemo Ramadhaan yako ya mwaka jana.

Weka mikakati na mipango yenye uhakika itakayokupelekea kuweza kuitekeleza, tena kwa ufanisi na bila uzito, wakati wote mgeni akiwa na wewe; kwa mfano:

Fufua au imarisha uhusiano wako na Mola wa Ramadhaan, kwa kumsikiliza na kumuitika, kwa kujizoesha kuwa karibu na maneno Yake ambayo Aliyachagulia mwezi wa Ramadhaan kuwa ndio wakati wa kuyateremsha. Jipangie wakati maalumu wa kuzungumza na As-Samiy’ul-Baswiyr, shauriana na ahli zako, rafiki zako, jirani, mnaofanya kazi pamoja, mnaocheza mpira pamoja, au wenzako mnaoswali pamoja, shauriana nao kuchagua wakati na pahala muwafaqa pasipohitaji taklifa, ambapo mutaweza kwa at-Tawfiyq yake Mola kukaa pamoja na kuzungumza na ar-Rahmaan, kwa mfano: kila baada ya Swalah fulani, nyumbani kwa fulani au msikiti fulani au klabu fulani.  Pia jiwekeeni wakati wa kuhifadhi maneno yake matukufu na kusikilizana hifdh yenu, jipangieni wakati wa kujielimisha na kuweza kufahamu maana yake, ili muweze kwa at-Tawfiyq yake Mola wa Ramadhaan kujiongezea na kujizidishia imani yenu na yaqini itakayokupelekeeni kuweza kutekeleza maamrisho Yake na kuacha makatazo Yake kama Atakavyo al-Wahiyd al-Qahhaar.

Fufua au imarisha uhusiano wako na Swalah tano, tumia diplomasia yako katika kisimamo chako cha Swalah tano kiijumuishe mahusiano na Swalah za usiku, fufua, imarisha Swalah zako kwa kuzipa uhai mpya, jaribu kutafuta utulivu na khushuu katika Swalah zako, refusha visimamo vya Swalah zako, refusha rukuu na sijdah za Swalah zako kwa kuzidisha vitajo vilivyothibiti ndani yake, fufua, imarisha au huisha Swalah za Sunnah zote zikiwemo zile za kabla hujalala witr au kabla Swalah ya Alfajiri au zile za usiku za Tahajjud.

Imarisha uhusiano wako na  jamaa zako, kwa kuwatembelea wazee wako au kuwasiliana nao, pia kwa kuwapa au kuwatengea sehemu katika kile alichokuruzuku Mola wa Ramadhaan kabla hujaiaga dunia.

Imarisha, fufua au anza kujifunza namna ya kuthamini wakati wako, chunga wakati wako katika shindano hili kubwa la mwaka lenye kushirikisha kila mwenye kuamini Allaah na Siku ya mwisho. Imarisha, fufua au jizoeshe na uzoeshe ulimi wako na moyo wako na ahli zako na wenzako katika baraza zako kumkumbuka na kumtaja kwa wingi Mola wa Ramadhaan na kumswalia/kumtakia Rahmah na Amani Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), aliyetufunza yote tunayoyahitaji katika uhai huu, yakiwemo tunayohitajia tuyafanye na tushikamane nayo wakati mgeni akiwa katika nyumba zetu, alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), yakimhuzunisha sana yanayotutaabisha; alikuwa akituhangaikia sana na kwa waliopendekezewa mgeni mtukufu –waumini- alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ni mpole na mwenye huruma sana, kama ilivyothibisha hayo Qur-an tukufu, Allaah Anasema:

“Hakika amekwishakujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayokutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma” at-Tawbah aya ya 128.

Imarisha, fufua au anzisha uhusiano mkubwa na wenye nguvu wa kumuomba mwenye kupenda kuombwa na aliyekupendekezea namna ya kumuomba, Allaah Anasema:

Na Allaah ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo… al-A’raaf aya ya 180; na wakati wa kumuomba pia, Allaah Anasema:

Na waja wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka al-Baqarah aya ya 186

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) katika kutuhangaikia ametupendekezea wakati wa kupeleka maombi yetu kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu):

“Allaah Anashuka katika mbingu za dunia kila usiku katika thuluthi ya mwisho na kusema; "Yuko mwenye kuniomba nimkubalie maombi yake?, Nani aniulizae nimpe?, Nani aniombae msamaha (Maghfirah) nimsamehe?." Imepokelewa na al-Bukhaariy, milango ya Tahajjud (kisimamo cha usiku), mlango wa du’aa na Swalah katika sehemu ya mwisho wa usiku.

Ndugu yangu katika imani, huisha na sisitiza kumtaka na kumuomba msamaha Mwenye kupenda kuombwa, kwani Yeye ni al-Ghaffaar, sisitiza kumuomba rehma Zake kwani Yeye ni Arhamur-Raahimiyn, sisitiza na shikilia kumuomba Akuepushe na Akulinde na moto kwani Yeye ni Qaadir wa kila kitu na ni Mwenye kufanya Alitakalo na wewe ni mja wake dhalili, muhitaji na ni mwenye kukiri madhambi na pungufu (taqswiyr) zako, na Yeye ni Msamehevu na Mwenye Rahma, Qur-aan inasema:

“Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu. Asaa Allaah akapokea toba zao. Hakika Allaah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu at-Tawbah aya ya 102.

Imarisha, fufua au huisha darasa yako, kama hakuna, basi pendekeza na shajiisha kuwepo kwa darasa, mihadhara, kufutarishana, kuwaidhiana, kukutana kwa ajili ya Allaah,  ambapo wewe na ahli zako utakuwa muhusika wa kwanza, mhudhuriaji wake na mtangazaji wake, na mhakikishaji kuwa haitapata pingamizi ya aina yo yote ile katika kuwepo kwake, iwe pingamizi ya pahala au malipo ya pahala, au hata vifuturishaji kama vitahitajika. Darsa, mihadhara, na mikusanyiko kama hii yenye kutajwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na waja wema ni pahala patakapokupelekea kuwa karibu na Allaah, kwani ni pahala unapokumbushwa na kushajiishwa kila lenye kukupelekea kuweza kwa at-Tawfiq Yake Mola kukufikisha kwenye lengo kuu lililosababisha Ramadhaan ipendekezwe na Mola Wake kuwa iwe mgeni wako. Katika masiku yake machache na matukufu, na hayo ni miongoni mwa chakula unachohitajia, ambacho ni adimu, chakula cha moyo wako, mwili wako unahitaji vyakula vya namna mbili; kimoja cha kukuza mwili na chengine cha kukuza imani yako ambacho utakipata tu ukiwa karibu na wenye kupenda kunasibishwa na Iymaan.

Fufua, imarisha au anzisha uhusiano wa kuwalingania watu kwa hikmah na mawaidha mema na mazuri kabisa na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora na  iliyo nzuri zaidi, kama inavyotupendekezea Qur-aan, Allaah Anasema:

“Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Anayemjua zaidi aliyeipotea Njia yake, na Yeye ndiye Anayewajua zaidi walioongoka.” An-Nahl aya ya 125,

Tumia diplomasia yako katika da’wah, wewe uko tayari kumkinaisha kila mtu kwa ulitakalo, kwa nini usitumie uwezo wako huo aliokupa na kukutunukia Mola wa Ramadhaan kuwakinaisha angalau Ahli zako, jamaa zako, rafiki zako, waswahili wenzako, kufikia kutekeleza maarisho ya Mola wako na hasa yatakayowapelekea kunufaika na kufaidika na Ramadhaan ambayo unaielewa vyema umuhimu wake katika maisha yako ya hapa duniani na kesho Akhera utakapokuwa chini ya udongo.

Orodhesha ‘amali njema ambazo utapenda kwa at-Tawfiyq ya Mola wa Ramadhaan uzitekeleze kwa ufanisi na ustadi wa hali ya juu kama alivyoagiza na kuonekanwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) akifanya katika mwezi huu, kwa mfano jipangie na jiwekee kusoma kitabu fulani; katika ‘Aqiydah – ‘Aqiydah ya Twahaawiyyah -, katika Swalah – Swalah kama alivyoiswali Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), Swawm na kadhalika.

Ndugu zangu katika imani, haya yote yanawezekana, na wewe na mimi tutayaweza kama tutaamua na kuchukua hatua moja muhimu; kabla ya kuichukua hatua hiyo, ni vyema tuelewe (mimi na wewe wenye kutaka kununua bidhaa ya Allaah), ni vyema tuelewe kuwa bidhaa tuitakayo imezungukwa na kila lisilopendwa na kuvutiwa na nyoyo zetu, na moto ambao hufungwa milango yake katika mwezi huu, umezungukwa na kila linalopendwa na kufurahiwa na nyoyo na nafsi zetu; hivyo basi simamisha bali vunja mawasiliano na uhusiano wako mzuri na wenye nguvu na wa karibu sana na shaytwaan, mwenye nafasi kubwa na ya pekee katika kila nyumba, tuliyemnunua kwa fedha Alizoturuzuku Mola wa Ramadhaan, nayo ni TV!

 

Mapendekezo kuhusiana na TV

 

Itumie kwa kuangalia yatakayokuletea kheri kama kuangalia mihadhara, mawaidha, iwe ndani ya mwezi wa Ramadhaan au miezi mengine, na kama huwezi kumkosa, basi jaribu kumsilimisha Shaytwaan wako huyo ili ufaidike na ugeni wa Ramadhaan katika nyumba yako.

 

Ndugu yangu katika imani, tukipata ushauri kwa wenzetu ushauri ulio mzuri basi tuwe tayari kuusikiliza na kuufikiria kuutekeleza kama tutauona una muelekeo mzuri na wenye kushikamana na mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na watu wema waliotutangulia, ambao katika uhai wao walishikamana na mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) bila ya kutia mawazo au fikra zao katika waliyoshikamana nayo.

Ndugu zangu katika imani, tujaribu kuishi wakati wetu huu na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ili tuangalie vipi yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) alikuwa akijitayarisha kumkaribisha na kumpokea Ramadhaan, na vipi alikuwa akiishi na Ramadhaan, yote haya kwa kuwa Yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ni Ma‘swuum, ambaye kwa maneno yake hupimwa maneno, na kwa matendo yake hupimwa vitendo, na kwa hali yake husahihishwa hali. 

Ndugu zangu katika imani, ni hakika isiyopingika kuwa mwenye kumfuata, na kuigiza mwenendo wake, na kuongoka kwa Siyrah yake Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ndie mwenye kheri nyingi na insha Allaah ndiye atakayefaulu na kufanikiwa katika hii dunia na kesho Akhera, na ni hasara kubwa isiyopimika na kuharibikiwa kusiko elezeka kwa yule asiyemfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) katika kila nyanja ya maisha yake ya kila siku hapa duniani na huko twendako kwa uhakika.

Ndugu zangu katika iman, Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) alikuwa akimpokea Ramadhaan kwa mapokezi yaliyojaa na kila aina ya furaha na maandalizi yenye kuonyesha na kuthibitisha kuwa, mja yuko tayari kuingia kwa at-Tawfiq ya Allaah katika masiku yenye fadhila na kila lenye kupendwa na Mola wa Rahmaan. Mja yu tayari kuingia katika mwezi ambao kwa at-Tawfiyq yake Rahmaan ukimalizika, awe katika walioghufuriliwa na kutolewa katika moto wa Jahannam. Mja yu tayari kukutana na kuishi msimu wa mavuno, mavuno atayoyahitajia bila ya shaka wala wasiwasi wa aina yoyote ile atakapokuwa chini ya udongo, mja yu tayari kukutana na msimu wa kheri, msimu wa Rahmah, msimu wa Maghfirah, msimu wa kutolewa watu katika moto wa Jahannam.

Ndugu zangu katika imani, leo tunashauriana juu ya namna ya kuukaribisha Ramadhaan, ningependelea mara nyengine kama tutajaaliwa kuwa hai na uzima kuelekea kuwa na tamaa ya kukutana tena na Ramadhaan, tuweke wiki ya mwanzo ya Sha‘abaan kuwa ndio wakati wa kushauriana namna ya kumpokea Ramadhaan, kwa kuwa matayarisho ya kumpokea mgeni mwenye nafasi kubwa katika nafsi za waumini hayawezi yakawa ya siku tatu au tano kabla ya kuwasili mgeni, hasa tukielewa kuwa bidhaa yake Mola wa Ramadhaan ambayo tunaitarajia kuinunua –kama tunacho cha kununulia- au kutunukiwa –kama tunazo sababu za kuthibitisha kuwa tunastahiki kutunukiwa- au kuiomba -kama maombi yetu yanatimiza masharti ya kukubaliwa-  tunaiomba tena kwa wingi katika masiku haya machache, bidhaa yake Mola wa Ramadhaan si rahisi, bidhaa yake anayoiuza ni ghali sana, bidhaa yake ni Jannah. 

Kisha tujipangie kuwa wiki ya mwisho ya Sha‘abaan kama leo, tuiweke au tuitumie kwa kutathmini maandalizi yetu tuliyojiwekea katika kuikaribisha Ramadhaan na kujiandaa kwa kukutana naye mgeni kwa kujikumbusha na kurejea sharia na hukumu za Swawm na yote yenye kufungamana na Swawm, nini cha kufanya ndani ya mwezi mzima wa Ramadhaan na kadhalika.

Ndugu zangu katika imani, hata hivyo tutashauriana na kujitahidi kutekeleza tutakayowafiqishwa, kwani kila kitu ni kwa at-Tawfiyq yake Mola wa Ramadhaan.  Ushauri au pendekezo langu ni kuwa kwa kuwa siku zilizobakia ni chache, basi tujitayarishe na tujiandae kwa kumpokea mgeni wetu kwa kila alilokuwa akilitekeleza Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kwani kama ilivyothibitisha Qur-aan kuwa yeye ndie wa kufuatwa na kuigwa kama tunataka kuongoka na kutengenewa mambo yetu, Allaah Anasema:

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allaah kwa anaye mtaraji Allaah na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allaah sana al-Ahzaab  aya ya 21

Ndugu zangu katika imani, imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) katika kujiandaa kwake kumpokea Ramadhaan, alikuwa akifunga sana katika mwezi wa Sha‘abaan, mpaka ikafika wakati Sahaba (Radhiya AAllaahu ‘Anhum) wakawa hawaelewi lini Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ameamka amefunga na lini ameamka hajafunga kama anavyosimulia mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha):

Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) akifunga mwezi mzima kama isipokuwa Ramadhaan, na sijamuona akifunga sana –katika siku alizokuwa akifunga- kama alivyokuwa akifunga katika mwezi wa Sha‘abaan.” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa Swawm za Sha‘abaan.

Ndugu zangu katika imani, Mtume (Salla Allaahu 'Alayhi Wa’ala Aalihi Wasalla) alikuwa akifunga sana katika mwezi wa Sha‘abaan kama ilivyothibiti, na sisi leo tumebakiwa na siku chache sana za mwezi, hivyo hilo hatukufanikiwa kulipata kwa baadhi yetu. 

Ndugu zangu katika imani, Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) alikuwa akifanya yote haya kama ni matayarisho ya kukutana na mgeni mtukufu Ramadhaan, ili iwe wepesi kwake kutekeleza yote atakayowafiqishwa kutekeleza kwa at-Tawfiyq ya Rabbu wa Ramadhaan ndani ya masiku machache na matukufu ya Ramadhaan, na haya kikweli yanatuhusu sisi (mimi na wewe), kwani yeye hana tatizo katika kutekeleza ‘amali njema, haoni uzito, na vipi ataona uzito hali amejaaliwa kuwa kipoza macho yake ni katika Swalah!, lakini kwa kuwa ameletwa awe kigezo kwa viumbe ndio akawa anafanya ayafanyayo kwa kuwa tupate kumuiga na sio vyengivyo AAllaahu A‘lam.

Ndugu zangu katika imani, Mgeni wetu ndio yuko milangoni mwetu (anahodisha), na baada ya siku chache ataingia ndani na kuwa nasi, suala la kujiuuliza ni vipi tutaishi naye katika kipindi hicho cha mwezi mmoja?

 

Hili (namna ya kuishi na Ramadhaan) ni somo lenye kujitegea, na wengi wetu kwa uhaba wa elimu zetu, na shindikizo la tamaduni zetu zisizokubalika katika Uislamu tunahitaji kuelewa jambo hili, hivyo tukipata wasaa tutawaomba ma-Ustaadh wetu - Allaah Awape kila la kheri - watuandalie na kutueleza namna ya kuishi na Mgeni mtukufu, kwani Mgeni huyu aliyewahi kuwa Mgeni wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na Sahaba zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum), bila shaka atakuwa anakuja na mbinu na namna ya kuishi nasi, nini anapenda sisi tukipate kutoka kwake, nini hapendi sisi tufanye, nini afanyiwe ili tufaidike na ugeni wake, vipi asemezwe ili tupate fadhila zake, na kadhalika.

 

Ndugu Waislamu, mgeni wetu anakuja kwa lengo la kututayarisha sisi kuweza kufikia lengo lililowekwa na Muumba wetu, lengo ambalo bila ya kuelewa namna ya kuishi nae itakuwa ni vigumu kulifikia.

 

Ndugu Waislamu, Ramadhaan inakuja kwa lengo la kutusafisha, kutufunza heshima, utii na kadhalika, tuwe wavumilivu katika kupata mafundisho yake na tuwe wastahalimivu katika kukabiliana na mitihani inayotukuta kila siku. 

 

Ndugu Waislamu, Ramadhaan haiwi Ramadhaan kama hatutokuwa tayari kusameheyana, kukumbushana, kuwaidhiana, kuusiana na kuamrishana mema na kukatazana maovu katika shughuli zetu zote za kila siku, kurekebishana kwa namna itakayoheshimu kila mmoja utu wake.

Ndugu zangu katika imani, ningependa kwa at-Tawfiyq yake Mola wa Ramadhaan kuhitimisha kwa kujaalia miongoni mwa ya kumkaribisha mgeni Ramadhaan ni kubainisha/kuainisha au kutaja baadhi ya habarí (Hadiyth dhaifu au si sahihi) zilizo mashuhuri katika ndimi zetu ukiwemo wangu, haya ni kwa kuwa tunatakiwa kumpokea mgeni kwa kutumia Hadiyth sio habari, miongoni mwa hizo habari ni:

 

  • “Lau wangeelewa waja yaliyomo katika Ramadhaan wangelitamani umma wangu iwe Ramadhaan mwaka mzima, hakika pepo hupambwa kwa ajili ya Ramadhaan ...” ni habari ndefu.

 

  • “Enyi watu, umekufikieni/umekufunikeni mwezi mtukufu, mwezi ndani yake umo usiku ambao ni bora kuliko miezi alfu, Amejaalia Allaah funga yake ni fardh na kisimamo cha usiku wake kuwa ni tattawu’ -Sunnah sio fardh-,  mwenye kujikurubisha ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo lolote la kheri, huwa ni kama aliyetekeleza fardh katika mwezi usiokuwa Ramadhaan, ...  na ni mwezi ambao mwanzo wake ni rahmah, katikati yake ni maghfirah, na mwisho wake ni kuachwa huru na Moto .....” ni habari ndefu pia.

 

  • “Fungeni mtapata afya”

 

  • “Mwenye kula siku moja katika Ramadhaan bila ya udhuru wowote ule wala maradhi, haitalipika siku aliyoiacha kwa kufunga dahri kama atafunga

 

  • “Kila kitu kina mlango, na mlango wa ‘Ibaadah ni Swawm

 

  • “Usingizi wa mwenye kufunga ni ‘Ibaadah”

 

  • “Mambo matano humfunguza mwenye kufunga: kusema uongo; kusengenya; kuchochea/kutia fitina; kula yamini ya uongo; na kutazama kwa matamanio”

 

  • “Wanawake wawili walifunga wakati wa  Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), wakawa kazi yao ni kuwasengenya watu... alisema Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) hawa wawili wamefunga/wamejizuia na waliyohalalishiwa na Allaah, na wamefungua na yale waliyoharamishiwa na Allaah

 

Ndugu zangu katika imani, habari hizi na nyengine kama hizo, ambazo sikuwafiqishwa kuzitaja hapa ni zenye kueleweka kwa wahusika wake, na sio Hadiyth na kama Hadiyth basi ni dhaifu mno, hivyo ni vyema kutozitumia kwani sio Hadiyth sahihi, na kutumia kama ni Hadiyth baada ya kuthibiti kuwa sio, ni kumzulia uongo Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), na vipi utakuwa mwenye kujitayarisha kumpokea Ramadhaan! Huku unamzulia aliyekuwa yakimuhuzunisha sana yanayotutaabisha; aliyekuwa akituhangaikia sana na kwa mimi na wewe -na waumini wote- kama hatumzulia uongo ni mpole na mwenye huruma sana.

Ndugu zangu katika imani, kilichothibitishwa na waliotunukiwa na kuruzukiwa macho ya kuona ndani ya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kuwa sio sahihi au ni dhaifu, ni vyema kwa kila anayepata nafasi ya kutuwa‘idhi, asitumie habari kama hizi, hata kama maneno/matamshi yake yanaonekana au yana harufu ya yote yenye muelekeo na Uislam, lakini sio Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), na kama Hadiyth basi sio sahihi, na kuzitumia kama ni Hadiyth kwa kusema: “Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam):...” hayo, baada ya kuthibiti kuwa sio sahihi, ni kumzulia uongo Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), na makemeo ya kuzua uongo tunayaelewa vyema, wachilia mbali kumzulia uongo aliyeletwa kwa lengo la kuigwa nae ni Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam).

 

Ndugu Waislamu, tumuombe ar-Rahmaan Atuwafikishe katika kuikaribisha na kumpokea mgeni wetu Ramadhaan, tumuombe Atuwafikishe katika kuishi na kukaa na Ramadhaan kwa kuifunga, kutekeleza Ayatakayo Muumba, na kuachana na makatazo Yake, pia twamuomba Muumba Atupe uwezo wa kufikisha amana kama alivyoifikisha Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), Atutie mapenzi baina yetu, mapenzi yatayotupelekea kuwa tayari kusameheyana, kuhurumiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kukosoana na kurekebishana kwa njia na namna alivyokuwa akiwarekebisha Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum).

 

 

Share