Zingatio La Wiki -Wakati Ni Huu Wa Ramadhaan
‘Abdun-Naaswir Hikmany
Nani mwenye hakika ya kuishi hadi Ramadhaan kumalizika? Nani mbabe wa kujinasibu kwamba ataishuhudia Ramadhaan ijayo? Yeyote mwenye kusema atafikisha tamati ya Ramadhaan hii na ataishuhudia Ramadhaan ijayo si chochote ila ni mpungufu wa akili. Na haitokuwa ni kosa kumuita Mjinga. Kwani elimu ya Ghayb yote ni yake Mola Muweza.
Huu ni wakati wa kuthibitisha utiifu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
{{“Na Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu Mimi.”}} [Adh-Dhaariyaat: 56].
Umefikia wakati wa kudhihirisha khofu kwa Mola wetu Mtukufu. Haitokuwa na maana
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Swalah tano, na Ijumaa mpaka Ijumaa, na Ramadhaan mpaka Ramadhaan, zitamfidia baina yake madamu atakua ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa" (Imepokewa na Muslim)
Huu ni wakati wa kuurekebisha ulimi kuwa ni wenye kusema kweli, kuacha fitna na kuacha kusengenya katika maisha yote yaliyobaki. {{“Na wale ambao ni wenye kujitenga na upuuzi”}} [Suratul-Muuminuun: 3]
Funga ya kweli kweli ni ile ambayo ulimi pamoja na viungo vyote vinafunga na kuacha maasi
{{“Je anapenda mmoja wenu kula nyama ya ndugu yake akiwa maiti, mkamchukia?! Na mcheni Allaah hakika Allaah ni mwingi wa kusamehe na mwenye kurehemu.”}} [Suratul-Hurujuraat: 12]
Katu mwenye kufunga hatakiwi kupoteza wakati wake hata kidogo kwa mambo ya michezo. Huu ni wakati wa kutembelea wagonjwa ili kujionea tofauti ya uzima na ugonjwa. Ni wakati wa kulisha masikini ili kuondosha pazia baina ya tajiri na masikini. Ramadhaan ni wakati wa kuwa na uchu wa kukumbilia mema na kuwa na wivu nao namna sawa anavyoona wivu kwa mkewe. Bila ya kusahau kusoma mno Qur-aan, kuswali kwa wingi, kukaa I’tikaaf pamoja na kuhudhuria darsa tofauti.
Basi tusikae tukawa na hiari katika amri za Mola wetu. Kwani Analotuamrisha Mwenyezi Mungu lina kheri kwetu. Hekima za Swawm Anazijua zaidi Yeye Mtunga Sheria kwani hatukupewa katika elimu ila kidogo. {{“Hamkupewa katika elimu isipokuwa kidogo.”}} [Suratul-Israa: 85]
Bila ya kusahau kwamba fadhila za kufunga Ramadhaan zitalipwa kikamilifu na Mola Siku ya Qiyaama.
{{{“Bila shaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ni haki; basi yasikudanganyeni maisha ya (hii) dunia, wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Iblisi) katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu.”}} [Suratu-Luqmaan: 33]
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


