Mimi Ni Ramadhwaan

Imekusanywa na: Abu Faatwimah

 

Ametukuka Muumba wa viumbe vyote Anayestahiki kuabudiwa pekee kwa haki, Muumba Aliyehalalisha usiku katika masiku yangu kuwa ndio wakati wa kuruhusiwa kuingiliana na wake zenu na kula na kunywa mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku,

 

Mmehalalishiwa usiku wa Asw-Swiyaam kujamiiana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah Anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkizihini nafsi zenu hivyo Akapokea tawbah yenu na Akakusameheni. Basi sasa changanyikeni nao (waingilieni) na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Na kuleni na kunyweni mpaka ibainike kwenu weupe (wa Afajiri) kutokana na weusi (wa usiku) al- Baqarah aya ya 187

 

Na ni wakati huu (usiku) ambao umehalalishiwa uliyoharamishiwa mchana wangu, ndio wakati wa pekee wa kujikurubisha kwa Mola kwa kutekeleza nafli, kwani mwenye kujikurubisha na kujipendekeza kwa Allaah kwa kutekeleza amali zisizokuwa faradhi/wajibu (ambazo ni nawaafil) Allaah Humpenda, kama ilivyothibiti katika, katika hadithi Qudsy, amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam):

“Amesema Allaah mwenye kumfanyia uadui - kumuudhi - walii Wangu basi mtu huyo amejitangazia vita na Mimi, na hutojipendekeza Kwangu mja Wangu kwa amali yoyote ile Niipendayo katika niliyomfaradhishia na atapobakia mja Wangu anajipendekeza Kwangu kwa nawaafil mpaka Nitampenda, na Nitapompenda basi Nitakuwa masikio yake, macho yake mkono wake na mguu wake, na pindi Akiniomba/akiniuliza basi Nitampa…” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha ar-Riqaaq, mlango wa tawaadhu’u.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, mwenye kupendwa na Allaah kama tulivyoona mambo yake yote yako katika usimamizi Wake, hana haja ya kutafuta wengine wa kumpenda!

 

Ndugu zangu ktika Iymaan, wakati huu wa usiku ndio wakati uliokuwa ukitumiwa na waja wema dhalili kujikurubisha kwa Mola wao wanaempenda, huutumia wakati huu (wengi wetu huwa tumelala) kwa kuzungumza na Subhaanah wanayempenda sana kwa khushuu, shauku na utulivu; kumsikiliza kwa heshima na taadhima na kwa utulivu kabisa Anavyowasemesha, kumkumbuka, kumshukuru, kumuomba msamaha, kumuomba Awatoe katika Jahannam, kuwaruzuku ladhatun-nadhwar ilaa Wajhih - kuwaruzuku shauku ya kukutana Naye, kuwaruzuku ridhaa katika waliyopewa na Yeye, na kumuomba  Awatunuku Jannah Yake kwa rehmah na fadhila Zake na kupeleka maombi yao mengine.

 

“Hakika wenye taqwa (watakuwa) katika Jannaat na chemchemu.  Wenye kuchukua yale Atakayowapa Rabb (Mola) wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wenye kufanya ihsaan.  Walikuwa wakilala kidogo katika usiku (wakifanya ‘ibaadah).  Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah.” adh-Dhaariyaat aya ya 15-18.

 

Naye Ndiye Aliyejaalia mchana kuwa ni wakati wa kujizuilia na kila kitachopelekea kuharibika kwangu (mimi Swawm)

 

Kisha timizeni Asw-Swiyaam mpaka usiku.Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf  Misikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Allaah Anavyobainisha Aayaat (na hukmu) Zake kwa watu wapate kuwa na taqwa.” al-Baqarah aya ya 187

 

Na ndiye Yeye Subhaanah Aliyejaalia jua kuwa na mwangaza na kuupimia mwezi vituo ili viumbe waweze kuelewe idadi ya miaka kwa kuja kwa mwezi mpya na kumalizika kwake; Qur-aan inasema:

 

Yeye Ndiye Aliyejaalia jua kuwa ni mwanga na mwezi kuwa ni nuru; na Akaukadiria vituo ili mjue idadi ya miaka na hesabu (nyingine).  Allaah Hakuumba hivyo ila kwa haki. Anafasili Aayaat kwa watu wanaojua.” Yuwnus aya ya 5.

 

Muumba wangu na wako Amejaalia kuwasili kwangu kunatakikana kuthibitishwe kwa kuonekana na kushuhudiwa kwa mwezi au kukamilika kwa siku 30 za mwezi wa Shaaban - kama mlivyojaaliwa mwaka huu - kwani mimi hupendeza na ndio hasa ninavyotakiwa nipokelewe kwa uyakini na uhakika na sio dhana, shaka wala wasiwasi wa kuingia na kuwasili kwangu au kutumia hesabu au kujaribi kunitegea katika kuingia kwangu kwa kufunga siku au masiku kabla, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) anasema:

“Asiitangulie mmoja wenu Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili isipokuwa kwa mtu aliyekuwa akifunga Swawm yake, basi huyo aendelee na Swawm yake.” Imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango asiitangulie mmoja wenu Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili.

Rehma na Amani za Allaah zimfikie Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na kila aliyejaaliwa kufuata na kushikamana na mafunzo yake swahiyhah, yeye Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) amepokelewa akisema :

“Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni kwa kuonekana kwake” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango kuwajibika Swawm ya Ramadhaan kwa kuonekana mwezi.

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili kwa rehma na fadhila Zake Muumba, nimewasili katika siku aliyoitaka na kuichagua Yeye Subhanah Fa’aalul Limaa Yuriyd (Mfanyaji Alitakalo) na Asiyeulizwa kwa Alifanyalo, Amenijaalia mwaka huu kwa fadhila Zake kuwa niwasili katika siku aliyokuwa akipenda Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kuwa nami (kuifunga), Allaah Amejaalia Alkhamiys kuwa ndio iwe siku yangu ya kwanza kuwa mgeni wenu, bila ya taklifa ya aina yoyote ile.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, kwa kuwa nilikuwa na wewe mwaka uliopita, nimeonelea ni vyema nianze na shughuli ya kutathmini, na huku kutathmini ni miongoni mwa mambo au kawaida anayotakiwa awe nayo kila Muislam, unatakiwa ujihesabu kabla hujahesabiwa, jihukumu kabla hujahukumiwa, uswali kabla hujaswaliwa, hivyo tathmini ugeni wangu wa mwaka jana (Ramadhaan yako iliyopita), tathmini itayokuwa na ukweli na yenye kukufikisha kuelewa kama kweli ulifaidika na ugeni wangu au hukufaidika, tathmini ambayo itakupelekea kuweka mikakati na kuamua nini cha kufanya.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, tathmini yako ni kwa faida yako, na tathmini yangu ni siri ya hali ya juu, katika tathmini yangu kubwa nilitafutalo ni kutaka kufika pahala na kuelewa kama ulifaidika na ugeni wangu au ulikuwa ukishinda na njaa tu, na kukesha bure? Nitapenda kuelewa nini hasa kilikuwa chenye faida kwako katika yangu, na nini hukufaidika nacho? Nitapenda kuelewa pia nini ulipendezewa katika yale yote niliyotunukiwa katika mapambo yangu na vivutio vyangu, kwani mimi huwa nakuja na mengi, na nini uliwafikishwa kutekeleza na nini hukujaaliwa.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, tulipokutana kwa uwezo wake Mola mwaka uliopita nilikupendekezea mambo mengi na ilikuwa hamu yangu kuwa utaweza kwa tawfiki Yake Mola kushikamana nayo, kwani nilihakikisha kuwa kila jema na zuri nilikupendekezea, kwa namna, njia na mbinu mbali mbali zenye kuvutia na kukupelekea kuingiwa na hamu na shauku itayokupelekea kuona raha katika kushikamana nayo. 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, nilikupendekezea tena kwa kukushikilia na kukusisitiza kushikamana na Swalah tano katika jama‘ah tena msikitini na kujaribu kwenda mapema, pia Ijumaa kwenda katika saa za mwanzo mwanzo.  Nilikupendekezea Qiyaamul-Layl (kusimama Usiku kwa kuswali) na kukutaka uhakikishe kuwa unamaliza Swalah anapomaliza Imaam. Nilikupendekezea kuisoma Qur-aan sana na kujifunza tafsiri yake na kujaribu kutekeleza maamrisho yake na kujikataza na makatazo yake.

 

Na pia nakukumbushia kuhusu Qiyaamul-Layl hapa ikiwa umesahau:

 

Fadhila Za Qiyaamul-Layl - 1 (Kusimama Kuswali Usiku)

 

Fadhila za Qiyaamul-Layl -2 (Kusimama Kuswali Usiku)

 

Ndugu yangu katika Iymaan, nilikupendekezea utoe sadaka na kuwapa wahitaji, na nilikupendekezee tena kwa kukushikilia na kukusisitiza kuunga udugu kwa kuwashughulikia wazazi wako; kuwafanyia wema na ihsaan na jamaa zako.  Nilikupendekezea kujaribu kumfuturisha aliyefunga, nilikupendekezea kujaribu kukaa I’tikaaf katika kumi la mwisho Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhaan au kujaribu kutumia wakati wako mwingi msikitini. Nilikupendekezea wakati wa kula daku na kuutumia wakati wa mwisho wa usiku kuzungumza na ar-Rahmaan na kumuomba uyatakayo na ya mwanzo katika hayo na ya mwisho na ndio lakuomba ni kumuomba Akutoe katika Moto wewe na wazee wako, mkeo/mumeo na watoto wako na dhurriyah wako, walimu wako na Waislamu wenzako na kumuomba Akuruzukuni kwa pamoja al-Jannah kwa rehma na fadhila Zake na Yeye ni Muweza wa hayo yote.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, yote haya na mengine mengi tulikubaliana tujitahidi kuyatekeleza katika masiku yangu machache na kuzidisha juhudi na hima katika siku kumi zangu za mwisho hasa hasa nyakati za usiku kwani huenda ukajaaliwa kuupata usiku wenye cheo ambao ni muhimu sana kwetu Laylatul-Qadr- Vipi Tunaweza Kuupata Usiku Huu?.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, msema kweli ni kipenzi cha Mola, nini ulitekeleza katika hayo na mengine mengi? Tafadhali usijidanganye nafsi yako kwani wewe ndiye mwenye kuelewa undani wako na sio mwengine.  Hata hivyo nitapenda uelewe kuwa nimewasili na kuikuta hali kama hii; wengi katika wenyeji wangu niliopendekezewa kuwa mgeni wao mwaka uliopita, ambao walikuwa na tamaa kama wewe ya kukutana nami tena mwaka huu wameshaiaga dunia; wengine nimewakuta wamejichotea, wajikumbia na kujikusanyia mijidhambi tele, juu ya kuishi na kukaa na mimi (kuwasafisha na kuwakosha) mwaka uliopita; wengine wameweza kwa tawfiki Yake Mola kujichumia mema na kujidundulizia katika benki isiyofilisika huku wakiwa na khofu na tamaa ya kukubalika ugeni wangu kwao.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kufarijika kwa kukutana na wenyeji wangu wapenzi waliokuwa wakibubujikwa na machozi kama mvua za masika wakati nipokuwa nikiwaaga mwaka uliopita wakichelea kuwa hututokutana tena; nimewasili na kufurahi sana mwaka huu kwa kukutana na wenyeji wengine ambao nilipokuwa nikiwaaga mwaka uliopita walikuwa na furaha sana kwa kuondoka kwangu, kama ilivyothibiti katika sherehe zao za kimaajabu za kusheherekea siku ya ‘Iyd, lakini baada ya kuondoka kwangu kwa tawfiki yake Mola walibahatika kufanya urafiki na kukaa katika mabaraza ya watu wema na wazuri, hivyo walifaidika na urafiki wao huo, kwani waliweza kwa tawfiki yake Mola katika kuwepo kwao na usuhuba huu mzuri, kusikia na kufuata yaliyo mazuri katika waliyoyasikia, hivyo walijaaliwa kuhudhuria baadhi ya mihadhara na kusikia Aliyoyaandaa Mola na kuwaahidi waja wake wema, jambo ambalo liliwapelekea kuwa na shauku na hamu ya kuwa miongoni mwa hao waja wema kwa yale walioahidiwa, hivyo walijuta majuto yasiyoelezeka kwanini walifurahia kuondoka kwangu mwaka uliopita! Jambo liliwapelekea kuamua kurudi kwa Mola wao kabla kuwasili kwangu kwa kumuomba msamaha na kutubia kwake, tawbah ya wenye kuelewa kutubia kama inavyotufundisha Qur-aan kwa kusema:

 

“Na (pia Allaah Akapokea tawbah) ya wale watatu waliobaki nyuma (kutokwenda vita vya Tabuwk; wakajuta mno) mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana na zikadhikika nafsi zao, na wakatambua kwamba hakuna pa kumkimbia Allaah isipokuwa (kuelekea) Kwake; kisha (Allaah) Akapokea tawbah yao, ili watubie. Hakika Allaah Yeye Ndiye Tawwaabur-Rahiym (Mwingi wa kupokea tawbah – Mwenye kurehemu).” at-Tawbah aya ya 118.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, wenyeji wangu waliofurahi kuondoka kwangu mwaka uliopita, mwaka huu wamelia sana kwa kuwasili kwangu jambo lililowashangaza wengi nikiwemo mimi, kilio kinachothibitisha kuwa sasa wameweza kwa tawfiki Yake Mola kunielewa, kunithamini, kuelewa umuhimu wangu, nafasi yangu katika nyoyo za waumini na kazi yangu itakayopelekea kufikia lengo walilopendekezea ugeni wangu.  Pia nimefurahi kukutana kwa mara nyengine na rafiki zangu wasionipenda hawana raha wala furaha bali huanza kubadilika kila wakisikia kukaribia kuja kwangu, na kuwasili kwangu huwa kama janga limewashukia, huwa mgeni asiyetakiwa ugeni wake, hivyo hufanyiwa kila chenye kuthibitisha kuwa yeye hatakiwi wala hana nafasi katika nyumba zao wachilia mbali nasfi zao, huku nikiwausia kunienzi, kuniheshimu kwa kunipa haki za mgeni na kuwatakia mema na kheri kwa kuhakikisha kuwa mengi ya maasi hayapatikanwi katika haya masiku yangu machache na matukufu.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kuanza kumuwaidhi rafiki yangu ulimi kwa kumwambia, habiby unahitaji kufunga, funga ya mama wa ‘Iysa bin Maryam, usizungumze na mtu wala usiseme ila kheri, hivyo funga na kusema uongo, funga na kusengenya, funga na kuchochea, funga na kuzua, funga na kuzungumza yasiyo ya kheri, funga na kupenda kusema (kufurahisha jamaa) ili uonekane kuwa na wewe umesema kitu, funga na kumdhalilisha mkeo na watoto wako kwa kumwambia kuwa atangaze kuwa hamuko pamoja. Funga na kuzungumza sana katika simu. 

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kuyawaidhi macho, ewe rafiki yangu mzuri macho funga!  Funga na kutazama yasiyo halali kwako, funga na kuangalia mambo yasiyozidishia Iymaan wala yaqini, funga na kuwabeza ndugu zako.

 

Nimewasili na kuyawaidhi masikio, tafadhali sikiliza yatayokuletea manufaa na kheri, tafadhali funga na kusikiliza muziki, funga ewe masikio na kusikiliza yasiyokuhusu.

 

Nimewasili na kuyawaidhi mikono, funga na kuchukua riba, funga na kuchukua au kutoa rushwa, funga na kunyang’anya watu haki zao, funga na kupiga watu, funga na kuua watu..

 

Nimewasili na kuyawaidhi migumu, tafadhali funga na kwenda katika yanayomkasirisha na kumghadhibisha Jabbaar, funga na kwenda katika maasi, funga na kwenda katika kila lililokatazwa na Uislam. 

 

Nimewasili na kuliwaidhi tumbo, habiby tumbo wewe unajifanya unahitaji sana kula, na kila ukila hushibi, hivyo habiby tumbo, funga na kula visivyo halali, funga na kula mali ya mayatima na mali za watu bila ya haki, funga na kula mali za haramu, funga na kula jasho la watu wakati unao uwezo wa kula cha jasho lako.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, jitahidi kadiri ya uwezo wako na hili unaliweza, jitahidi viungo vyako viwe na mimi katika masiku yangu yote, jitahidi kujikumbusha siku utaofungwa mdomo na kupewa uhuru viungo kusema, si wewe unasoma Yaasiyn kila ukiwa na lako, akizaa jamaa unasoma, akifa unaisoma, akiumwa unaisoma, na kadhalika jambo ambalo huna ushahidi nalo, je katika kuisoma kwako Yaasiyn hujasoma ndani yake hili!

 

Leo Tunapiga mhuri (Tunaviziba, hawatoweza kuvifunuwa na wala kusema chochote) vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. Yaasiyn aya ya 65 pia Qur-aan inasema :

 

“Na Siku watakayokusanya maadui wa Allaah kwenye Moto, nao wanapangwa safusafu. Mpaka watakapoujia (huo Moto), yatawashuhudia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale (yote) waliyokuwa wakiyatenda. Na watasema (kuziambia) ngozi zao: “Mbona mnashuhudia dhidi yetu?” (Ngozi zao) Zitasema: “Ametutamkisha Allaah Ambaye Anatamkisha kila kitu, Naye (Ndiye) Aliyekuumbeni mara ya kwanza na Kwake mtarejeshwa.  “Na hamkuwa mkijisitiri (duniani) hata yasishuhudie masikio yenu, na wala macho yenu, na wala ngozi zenu; lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda. “Na hivyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Rabb (Mola) wenu (ndio) imekuangamizeni, mkapambaukiwa kuwa miongoni mwa waliokhasirika.” Na Tuliwawekea quranaa (marafiki wandani ambao ni mashaytwaan) wakawapambia yale yaliyo mbele yao na ya nyuma yao (ya madhambi), na ikawathibitikia kauli (ya adhabu wawe) katika umati nyingi zilizokwishapita kabla yao miongoni mwa majini na wanadamu; kwamba wao wamekuwa wenye kukhasirika. Fusswilat (Haa Mim Sajdah) aya ya 19-24

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kufurahi kwa kuleta habari njema kuwa baadhi ya walioishi na kukaa nami mwaka uliopita kama walivyoagizwa na ar-Rahmaan wako Barzakh huku wakineemeka kwa kukubaliwa ugeni wangu kwao.  Hawa walikuwa wakifurahi na kujifakharisha kwa ugeni wangu kwao, na leo najifakharisha kwa kuwa niliwahi kuwa mgeni wao na upande mwengine nasikitika kuwakosa wenyeji kama wao.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kufanya tathmini ya mwanzo kuhusu wenyeji wangu na kufikia kuwa inafurahisha na inanitia tamaa kwa kuona kuwa wengi wenu mwaka huu muko tayari kunipokea na kuingia katika masiku yangu machache na matukufu kwa shime, juhudi, uchangamfu na nguvu mpya.  Nimewasili baada ya wengi wenu kuamua tena kikweli kweli kufungua ukurasa mpya katika maisha yenu, baada ya kufaidika na ugeni wangu uliopita, kwani nimegundua kuwa kuna maendekeo na ufanisi fulani katika utendaji na utekelezaji wa ibada zenu.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kujiweka tayari kwa ajili yako kukuenga enga, kukusukuma sukuma na kukushajiisha kwa tawfiki yake Mola uingie katika kila amali njema na za kheri ambazo ni nyingi katika masiku yangu haya machache na matukufu, na hasa hasa zile amali ambazo ulikuwa mzito mwaka uliopita, au hukufanikiwa kuzitekeleza au hukuzielewa umuhimu na nafasi yake wakati nikiwa mgeni wako au umezielewa lakini ufahamu wako si sahihi.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, naelewa kuwa unasoma Qur-aan, lakini huna kawaida ya kuisoma kama walivyokuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na Sahaba zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum), hivyo napenda uelewe kuwa Qur-aan na mimi ni chanda na pete, si hilo tu bali imeteremshwa katika masiku yangu, na yawezekana kwa hilo ikawa sababu tosha ya kupendekezwa ugeni wangu kwako, Allaah anasema:

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na al-Furqaan (pambanuo la haki na ubatilifu). al-Baqarah aya ya 185.

Ndugu zangu katika Iymaan, kubwa ni hili ambalo hasa ndio nakupendekezea uwe nalo mwaka huu kwa tawfiki yake Mola, nalo ni kuwa Allaah alikuwa akimleta Jibriyl (‘Alayhis Slaam) nyakati za usiku kuja kusoma Qur-aan, kusikilizana na kuipitia kama mutwala’ na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kama ilivyothibiti:

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ajwad (mbora, mwenye matendo mazuri, mwema, karim) wa watu, na alikuwa mbora zaidi (huzidi) katika Ramadhaan wakati anapokutana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam), alikuwa akikutana naye kila usiku wa Ramadhaan, wanapokutana huwa anamdurusisha Qur-aan” Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ni mbora (ajwad) katika Ramadhaan .

Ndugu yangu katika Iymaan, jaribu na wewe kuisoma Qur-aan nyakati za usiku.  Isome Qur-aan kwa utulivu na huku ukijaribu kusita sita na kupumzika kila penye kuhitaji kusita sita au kupumzika, jaribu kila penye kutajwa Moto umuombe Allaah Akuepushe nao, penye kutajwa Pepo muombe Akuingize, penye kutajwa Rahmah na Maghfirah muombe na uwaombee wazazi wako na wako wote waliotangulia mbele ya haki.  Soma Qur-aan nyakati za usiku uwaige Sahaba wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), soma Qur-aan usiku Malaika (‘Alayhimus Salaam) washuke kuisikiliza na kukufunika na mbawa zao, soma Qur-aan umkimbize Shaytwaan katika nyumba yako, soma Qur-aan ikuongoe na kukushika mkono mpaka iweze kukufikisha kwenye yaliyonyooka, Qur-aan inasema:

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa, na inawabashiria Waumini wanaotenda mazuri kwamba watapata ujira mkubwa”. Al-Israa aya ya 9.

Soma Qur-aan ipate kuja siku ya Qiyaamah na kukusimamia kwa kukuombea shufaa kwa Mola Wako, soma Qur-aan utafanikiwa, soma Qur-aan utahifadhika, soma Qur-aan utaburudika, soma Qur-aan utapata utulivu, soma Qur-aan uitie nyumba yako nuur, soma Qur-aan utafarijika, soma Qur-aan na wewe angalau katika uhai wako ulijaaliwa kutekeleza amri aliyoamrishwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na Allaah kuitekeleza miongoni mwa aliyotakiwa ayatekeleze, Qur-aan inasema:

“(Sema ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika nimeamrishwa nimwabudu Rabb (Mola) wa huu mji (Makkah) Ambaye Ameufanya mtukufu. Na ni Vyake Pekee kila kitu. Na nimeamrishwa kwamba niwe miongoni mwa Waislamu. “Na kwamba nisome Qur-aan.” Hivyo anayeongoka, basi hakika anaongoka kwa ajili ya (manufaa ya) nafsi yake. Na anayepotoka, basi sema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.”  Na sema: “AlhamduliLLaahi (Sifa njema zote ni za Allaah); Atakuonyesheni Aayaat (ishara, dalili) Zake na mtazitambua.” Na Rabb (Mola) wako si Mwenye kughafilika kutokana na yale (yote) wanayoyatenda. An-Naml aya ya 91-93  

Soma Qur-aan kwani imefanya iwe nyepesi kufahamika kama ilivyotibisha Qur-aan kwa kusema:

“Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote (yule) anayekumbuka? al-Qamar aya ya 17.

Soma Qur-aan kwani Mfundishaji wake ni ar-Rahmaan, soma Qur-aan umsikilize Muumba wako anayotaka, soma Qur-aan ujichumie na kujidundulizia kwa tawfiki yake Mola thawabu, kwani kila herufi uisomayo malipo yake ni thawabu kumi, soma Qur-aan kwa rehma na fadhila Zake Mola siku ya Qiyaamah utaambiwa, soma kama ulivyokuwa ukisoma katika uhai wako na makaazi yako yapo katika aya ya mwisho utayojaaliwa kuisoma, soma Qur-aan kwa rehma, fadhila na tawfiki Yake Mola itakuingiza Peponi.

Ndugu zangu katika Iymaan, nimewasili na kukuomba tena kwa kukushikilia na kukusisitiza utege sikio lako ili nikunong’oneze baadhi ya mambo ambayo tunayahitaji katika kila amali yetu tuitekelezayo kubwa na ndogo, tunahitaji mambo makubwa matatu: Ikhlaas, Ukweli (Swidq) na Namna ya kutekeleza hiyo amali yenyewe (Mutaaba’ah).

 

Ndugu yangu katika Iymaan, mambo haya matatu ni muhimu kwa kila aliyeamini, umuhimu wa maji katika maisha ya viumbe, kwani haya matatu pekee Allaahu A‘lam ndiyo yanayopelekea amali ikubaliwe au ikataliwe, hivyo mimi (funga) ugeni wangu kwako usiwe kama ni desturi na mila au jambo la kawaida katika jamii yako, bali ugeni wangu kwako ni lazima uhakikishe kuwa umenipokea kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu) pekee na kutarajia Aakhirah, huna haja ya kumfurahisha kiumbe, huna haja ya kumridhisha kiumbe, huna haja ya kutaka kusifiwa au kutajwa, huna haja ya kutaka kuonekanwa kwa amali yako, kwani wewe katika amali yako hiyo nikiwemo mimi (funga) huwa unamtarajiya Allaah na unategemea malipo kutoka Kwake Jabbaar, Mkwasi, Anajitosha, na Msifiwa na sio kiumbe, kwa rehma na fadhila Zake huku ukichelea ghadhabu na adhabu Zake na hii ndio inayofahamika kama ndio Ikhlaas.

Ndugu yangu katika Iymaan, jambo la pili muhimu ni kuchunga na kushikilia katika utekelezaji wa amali zako zote kuwa unamuigiza na kumfuata aliyeletwa kwa lengo la kuigwa nae ni Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), tekeleza kila amali kadiri ya utekelezaji wake kama ulivyothibiti au kadiri ya maagizo yake au maamrisho au ushauri wake ulivyopokewa katika Sunnah sahihi. Usimuabudu (ibada ni tamshi lenye kukusanya kutekeleza - iwe kwa ulimi, vitendo, matamshi na kadhalika - kila Aliyoamrisha na Kuyaridhia Allaah na kujiepusha na kila Aliyoyakataza) Allaah isipokuwa kwa kile Alichokipendekeza kwako tena iwe kwa namna alivyoagiza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam).

Ndugu yangu katika Iymaan, jambo la mwisho ni Swidq, uwe mkweli katika utekelezaji wako wa amri zote za Allaah kwako, utekeleze kadiri ya uwezo wako baada ya kuzisoma, kujifunza na kuelewa namna ya kutekelezwa, pia ujiepushe na kujikataza makatazo yote aliyokukataza Allah mara moja, na kujitayarisha na kukutana Nae, na kuachana na uvivu na ajizi katika kumtii Allaah. Hivyo tekeleza amri kadiri ya uwezo wako na sio kuondosha njiani au kuripuwa ripuwa kama wanavyoripuwa Waislamu wengi katika ugeni wangu pambo langu la Swalah ya Taaraawiyh, pambo ambalo huenda likapelekea mja kufutiwa majidhambi yake kama atalitekeleza kwa kuambatana na mambo hayo matatu na kuongezeka Iymaan na kumtaraji Allaah, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) amesema:

“Mwenye kusimama Ramadhaan (kisimamo cha usiku, kama inavyotakiwa na sio kuripuwa ripuwa na kutaka lazima umalize Qur-aan, mpaka ikawa haijulikanwi panasomwa nini, hapajulikani rukuu, kisimamo wala sijdah, wala vitajo vyake) kwa Iymaani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan kwa Iymaani,

Ndugu yangu katika Iymaan, tega sikio lako ili nikunong’oneze jambo litalokupelekea kwa tawfiki Yake Mola kuingiwa na hamu na shauku zitazokupelekea kuwa mchangamfu, mwenye hima, jitihada na nguvu mpya katika masiku yangu haya machache na matukufu.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, toka kuwasili kwangu milango yote ya Pepo (Jannah) Habiby kwa rehma na fadhila zake Mola wangu na wako imeachwa wazi!!! Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) amesema kama ilivyosimuliwa na Abu Hurayrah kuwa:

"Inapoingia Ramadhaan, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya Moto hufungwa, na mashetani hufungwa …" Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila za mwezi wa Ramadhaan.

Milango yote ya Pepo imeachwa wazi, Habiby kuachwa milango ya Pepo wazi, tena yote kunaashiria jambo, Allaahu A’alam, jambo jepesi la kudhania na kufikiria mimi na wewe mwenyeji wangu, ni kuwa Habiby, unatakiwa uingie Peponi kwa hali yoyote ile ndani ya masiku yangu haya machache kwa rehma na fadhila zake Muumba na utolewe/utoke katika Moto. Habiby unatakiwa na unaombwa kwa heshima na tadhima ufanye ulitakalo na uliwezalo kwa rehma na fadhila zake Mola na tawfiki yake lakini hakikisha kuwa litakupelekea kuingia Peponi, upate kuneemeka na yaliyomo ndani yake yaliyoandaliwa na kuahidiwa watu wake, Habiby chagua mlango wa kukuingiza na kuingilia Peponi, kwani milango yake yote iko wazi!  

 

Ndugu zangu katika Iymaan, fanya ulitakalo ili uingie Peponi tena kwa kuchagua mlango uutakao wewe kwa rehma na fadhila zake Mola na kwa tawfiki yake, Habiby chagua na ufanye ulipendalo miongoni mwa yaliyokusanyika katika masiku yangu machache ambayo kwa ujumla yote ni miongoni mwa sababu itayokupelekea kwa rehma na fadhila za Mola kuwa miongoni mwa waliofaulu kikweli kweli kwa kusukumwa na kuepushwa na Moto, kwani atakayeepushwa na Moto siku hiyo ndio kweli aliyefaulu kama inavyothibitisha Qur-aan kwa kusema:

 

“Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na Moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu. Al-‘Imraan aya 185.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, masiku yangu yamekusanya mambo mengi lakini mambo matatu ndio yanayojitokeza kwa wepesi na kuonekanwa, bali kupendwa kutekelezwa na kila mja, mambo ambayo ni miongoni mwa yanayopelekea mja kupata Pepo kwa rehma Zake Mola na kwa tawfiki Zake, masiku yangu yamekusanya; Swawm, Qiyaam na Itw’aam (kulisha watu). Swawm ambayo ndio mimi unanielewa sifa zangu kama alivyonisifu Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kwa kusema:

“Mwenye kufunga Ramadhaan (kama inavyotakiwa na sio kukaa na njaa) kwa Iymaan na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan kwa Iymaan, pia aliulizwa na mtu kuhusu nini cha kufanya apate Pepo akamjibu funga kama ilivyothibiti. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kwa kusema:

Amesema Abu Umaamah (Radhiya Allahu ‘Anhu) kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Aalaa Aalihi Wa Sallam), “Ewe Mtume wa Allaah Niamrishe/nielekeze amali itayonifaa mbele ya Allaah”. Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), akamwambia “Shikamana na Swawm (funga) kwa hakika hakuna mfano wake" Imepokelewa na lbn Hibbaan, kitabu cha Swawm, fadhila za Swawm.

Ndugu zangu katika Iymaan, kisimamo cha usiku (Qiyaamul-Layl) kinapatikanwa siku zote, ila tu katika ugeni wangu wa masiku yangu machache kwako huwa kinasisitizwa sana na aliyeletwa umuigize, kama ilivyothibi, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kasema:

 

Mwenye kusimama Ramadhaan (kisimamo cha usiku, kama inavyotakiwa na sio kuripuwa ripuwa na kutaka lazima umalize Qur-aan, mpaka ikawa haijulikanwi panasomwa nini, hapajulikani rukuu, kisimamo wala sijdah, wala vitajo vyake) kwa Iymaani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia” Imepokelewa na al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan kwa Iymaan.

Yeye aliyeletwa ili aigwe alikuwa akisimama katika maisha yake yote mpaka wakawa wanamhurumia kama ilivyothibiti katika Sunnah, kama anavyosimulia mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhu):

 

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) akisimama usiku hadi miguu yake huvimba, nikamwambia: Kwanini unafanya hivi (unajitesa namna hii) ewe Mjumbe wa Allaah, hali ya kuwa ushasamehewa (ushaghufuriliwa) madhambi yako yaliyotangulia na yatayokuja (yatakayofuatia)? Akasema Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam  " Base nisiwe hata mja mwenye kushukuru?!” Imepokelewa na Al-Bukhaariy, milango ya Tahajjud, mlango wa kisimamo cha Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam).

 

Ndugu zangu katika Iymaan, kisimamo cha usiku kwa rehma na fadhila zake Mola kinawaingiza marafiki zake wanaokishughulikiwa katika Pepo au ni sababu katika sababu moja ya mja kupata Pepo kwa rehma Zake Mola, kama inavyofahamika katika aya za Qur-aan, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

“Hakika wenye taqwa (watakuwa) katika Jannaat na chemchemu.  Wenye kuchukua yale Atakayowapa Rabb (Mola) wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wenye kufanya ihsaan.  Walikuwa wakilala kidogo katika usiku (wakifanya ‘ibaadah).” Adh-Dhaariyaat aya ya 15-17, pia Anasema:

“Mbavu zao ziinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb (Mola) wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa. Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. as-Sajdah 16-17, pia Anasema:

“Na waja wa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah) ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu, na majahili wanapowasemesha, wao husema (maneno ya) salama. Na wale wanaopitisha (baadhi ya nyakati za) usiku kwa ajili ya Rabb (Mola) wao wakisujudu na kusimama. al-Furqaan aya ya 63-64.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, kumlisha mwenye kuhitaji kulishwa kwa sababu zinazokubalika na sio kwa ujanja wa kusema ametengana katika hali ya kawaida, ni amali iliyosisitizwa sana na Uislam, muhitaji huyo awe katika mafakiri asiyeweza kazi, au mayatima, au wafungwa wasiomiliki kitu, amali hii huwa na daraja ya namna yake ikiwa Mlishaji anakipenda hicho anachokitoa kuwalisha wahitaji, na anakihitaji. Amali hii Itw’aam (kulisha) chakula ni amali iliyopendekezwa sana na Qur-aan na kusisitizwa kutekelezwa katika kafara nyingi zilizowekwa na Uislam, jambo linalopelekea kuelewa kuwa kumlisha muhitaji ni miongoni mwa amali nzuri na njema anazopendekezewa mwenye kuamini Allaah na siku ya Qiyaamah kuzitekeleza.

 

Ndugu zangu katika Iymaan, katika huku kulisha, nitapenda tuangalie nani wa kumlisha, kwani mara nyingi Qur-aan inapotaja kulisha huwa inataja watu maalum, kama Maskini, Mafakiri, na kadhalika na sio kila mtu kama wanavyofanya wengi katika wenyeji watu.  Wengi wa wenyeji wangu huwa na sadaka ya kulisha na huwalisha wasiostahiki kulishwa kwa uhakika, hivyo hujikosesha yaliyoandaliwa wenye kuwalisha wahitaji, basi mwenye kutaka malipo ya kulisha kwanza aelewe kuwa wa kulishwa sio kila mtu. Ama katika kufutarisha hakukutajwa watu maalum wa kuwafutarisha zaidi ya aliyefunga (Mfungaji), kama ilivyothibiti katika Sunnah, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kasema:

 

“Atakayemfuturisha aliyefunga, huandikiwa ujira mfano wa ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga” Imepokelewa na ad-Daarimy, kitabu cha Swawm, mlango wa fadhila za mwenye kumfutarisha mwenye kufunga.

Ndugu zangu katika Iymaan, ujira upo kwa kumfutarisha aliyefunga, na kama huyo aliyefunga atakuwa katika wale wanaoainishwa na Qur-aan kila inapotaja Itw’aam (kulisha) Allaahu A’lam ukimfutarisha huyu aliyetajwa kuwa ndie anaestahiki kulisha bila shaka ni bora zaidi.  Kulisha ni amali nyengine nzuri na njema uliyopendekezewa katika masiku yangu na inayopelekea kwa Rahmah Zake Mola kukuingiza Peponi kama inavyoonyesha na kujitokeza katika aya nyingi za Qur-aan, Allaah Anasema:

 

“Na wanalisha chakula juu ya mapenzi yao (kwa hicho wanacholisha) masikini na mayatima na mateka. “Hakika sisi tunakulisheni kwa (ajili ya) Wajihi wa Allaah, hatutaki kwenu jazaa na wala shukurani. “Hakika sisi tunakhofu kwa Rabb (Mola) wetu siku inayokunjisha uso ngumu nzito. Basi Allaah Atawakinga na shari ya siku hiyo, na Atawakutanisha na mng’ao na furaha.al-Insaan aya ya: 8-12.

 

Ndugu Waislamu, tumuombe ar-Rahmaan tumuombe kwa kuyatumia Majina Yake Matukufu kama Alivyotuagiza, tumuombe Allaah al-Waahyd al-Ahad as-Swamad Asiyezaa wala Asiyezaliwa na Asiyefanana na chochote kile, tumuombe aturuzuku Ikhlaas, Iymaan, Yaqini, kumfuata na kumuigiza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na Aturuzuku utekelezaji wa aliyotufunza kwani Yeye ni Qaadir wa kila kitu. Tumuombe Jabbaar Atutoe katika Moto na Aturuzuku Pepo kwa Rahmah na fadhila Zake, Aturehemee wazee wetu na Waislamu wenzetu waliotutangulia mbele ya haki, Atughufurilie madhambi yetu, Aamiyn Aamiyn Aamiyn.

 

 

Share