Zingatio La Wiki - Tukirimu Ramadhaan
‘Abdun-Naaswir Hikmany
Ni juu yetu kuelewa kwamba wakati haupo nasi, kila sekunde inayokatika hakika itakuwa imeandikwa. Andiko litakaloangukia kuwa ni thawabu au dhambi. Tunamuomba Allaah Atughufirie madhambi yetu kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhaan.
Ramadhaan ni mgeni mwema,
Mazuri kwake yametuwama,
Ni sisi kujitahidi kuyachuma,
Kwa nguvu, bidii na hima.
Wangapi wamepita kabla yetu na kushuhudia Ramadhaan zikija na kuondoka hali ya kuwa ni wenye kukhasirika? Lakini wapo wema waliopita ambao walielewa kuwa bidhaa ya Ramadhaan ni ghali kuinunua, bei yake inayouzwa si rahisi hata kidogo, nayo si bidhaa nyengine ila ni Jannah. Hao ndio wa kuwaiga mwendo wao. Na hakuna mwengine aliye bora wa mfano ila Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tufuate Sunnah zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ramadhaan amejaa fadhila kede kede, na moja wapo ni kuachiwa huru na moto. Ni sawa na mfano wa Raisi anapowaachia huru wafungwa kadhaa kwa mnasaba wa kuadhimisha sherehe za taifa. Ndivyo ilivyo kwa Allaah kwa mwezi huu wa Ramadhaan. Wala hatuna haja ya kufichana kwamba yawezekana kabisa kuwa sisi ni miongoni mwa watu wa Motoni. Allaah Atuepushe na adhabu ya Jahannam! Tujipinde kwenye mwezi huu mtukufu ili tuachiwe huru na moto kama anavyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakika ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: " Swawm ni kinga, itamukoa mja kutokana na moto (siku ya Qiyaamah) [Imepokewa na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Uthmaan bin Abil ‘Aas]
Hivyo tuishi naye kwa vizuri kwani hana siku nyingi kwetu sisi, tumtayarishie yale mazuri ayapendayo sio tu kwenye maakulati bali kuanzia kwa Qiyaamul-Layl, tabia njema, ibada sahihi, hadi futari ya halali. Tusiwe ni wenye kumkasirisha Mola Subhaanah kwa kutoitumikia Ramadhaan kwani abadan Ramadhaan hajajia mabaya. Ramadhaan katu hajafika kututilia rangi vikao vya karata wala kuwaweka kitako wanawake kufanya ibada ya kupika tu mchana na usiku. Basi tumfanyie mema ili tufaidike na ugeni wake.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


