Skip navigation.
Home kabah

Mimi Ni Siku Za Mwisho Za Ramadhaan

   

Abu Faatwimah

Sifa njema zote ni Zake Allaah, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Al-Kibriyaau ni Chake Yeye pekee, mbinguni na ardhini, na Yeye pekee Ndiye Mungu mbinguni, na Ndiye Mungu katika ardhi, Mwenye kumiliki funguo za mbingu na ardhi, Mwenye hikima, Mjuzi wa ghayb na shahaada, na ni Yeye pekee Atae hukumu baina ya waja Wake katika yale waliyokhitalifiana.

Tumshukuru Mola kwa kutupendezea Iymaan na Akaipamba katika nyoyo zetu, na tumshukuru Mola kwa Kutuchukizia ukafiri, upotofu, na uasi kwa fadhila Zake na neema Zake na ni Yeye pekee ndio tarajio la mwenyeji wangu aliyenienzi, niheshimu  na kukesha kwa ajili ya Mola wake Mlezi kwa kusujudu, kusimama, kusoma Qur-aan na kadhalika.

 

Rehma na Amani za Allaah zimfikie Al-Habiyb Mustwafa (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na kila aliyejaaliwa kufuata na kushikamana na mafunzo yake swahiyhah, yeye al-Habiyb Mustwafa (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) alitakiwa na Mola wangu na wako katika mwisho wa amali aliyopewa ya kufikisha ujumbe ashikamane na Tasbiyh na Istighfaar, Qur-aan inasema:

“Itakapokuja nusura ya Allaah na ushindi. Na ukaona watu wanaingia katika Dini ya Allaah kwa makundi, Zitakase sifa za Mola wako Mlezi, na umwombe msamaha; hakika Yeye ndiye Anayepokea toba.”  an-Naswr aya ya 1-3.

 

 

Ndugu zangu katika Iymaan, siku hizi umefunikwa na siku zangu za mwisho za ugeni wangu kwako, (ugeni wangu umebakia siku moja au mbili), siku ambazo ameridhiwa na Subhaanah kila aliyenipokea na kunikirimu kwa kunienzi, kuniheshimu, kunishughulikia, kunitunza, kuishi na kukaa na mimi kama alivyoagizwa na kuelekezwa na al-Habiyb Mustwafa (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), siku ambazo husamehewa na kufutiwa madhambi kila aliyesimama kwa Iymaan na kutarajia malipo kwa Allaah, siku ambazo ndani yake milango yote ya Pepo huwekwa na kuachwa wazi! Siku ambazo pumzi za wenyeji wangu ni zenye thamani kubwa isiyonunulika, kwani harufu zake mbele ya Mola zashinda harufu ya misk!  Siku ambazo huwatoa kwa rehma na fadhila zake al-Jabbaaru al-Ahadu al-Waahid asw-Swamadu katika kila usiku wa masiku yake Motoni watu waliothibiti kuuingia! Siku ambazo Amezijaalia al-Khaaliqu kuwa ni fungamano (uhusiano) lenye nguvu kabisa baina Yake na waja Wake kwa ujumla, na hasa hasa wale waja Wake wenye makosa.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, ugeni wangu kwako umefikia khitamu yake, ugeni wangu kwako utakuwa Shahidi wako kwa yale yote uliyojaaliwa kwa tawfiki Yake Mola kuyatekeleza na kuyatimiza, basi kama ulijitahidi na kujilazimisha kadiri ya uwezo aliokujaalia Mola katika masiku yangu haya machache yanayomalizika, basi mshukuru Allaah. Mshukuru Allaah kwa kukuwezesha na kukufanyia wepesi ukafanikiwa kutekeleza na kuyakamilisha Aliyokujaalia, mshukuru Allaah kwa kukuwezesha kukesha kwa ajili Yake, mshukuru Allaah kwa kukuwezesha kusujudu na kusimama, mshukuru Allaah kwa kukuwezesha kuyakhitimisha Maneno Yale - Qur-aan - mara ulizojaliwa (mara chache kwa mtu mvivu kama mimi ni mara tatu, kiasi cha kukhitimisha mara moja kila siku kumi), hivyo tegemea malipo kutoka Kwake, kwani hakika Yeye Hapotezi kazi ya mfanyakazi, akiwa mwanamume au mwanamke, Qur-aan inasema:

“Mola Mlezi wao, Akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanyakazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi…, kwa yakini Mimi Nitawafutia makosa yao, na kwa yakini Nitawaingiza katika Mabustani yanayopita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayotoka kwa Allaah. Na Allaah Kwake yapo malipo mema kabisa” al-‘Imraan aya ya 195.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, tegemea malipo kutoka kwa Mlipaji Asiyesahau wala kughafilika, tegemea malipo kutoka kwa Mwenye cha kulipa na ukaridhika, tegemea malipo kwa Aliyekupendekezea ugeni wangu kwako, tegemea malipo watayotunukiwa waja wa ar-Rahmaan, Qur-aan inasema:

“Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi Tunamwandikia.” Al-Anbiyaa aya ya 94, pia Qur-aan inasema:

 

 “Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu.” Twaahaa aya 75, pia Qur-aan inasema:

 

“Na anayefanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende.” an-Nisaa aya ya 124.

 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, ugeni wangu kwako pia unaweza ukageuka na kuwa Shahidi dhidi yako, kwa namna ulivyonipokea kama ulivyotaka wewe na sio kama alivyokupendekezea al-Habiyb Mustwafa (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kutonijali, kutokuwa na shauku wala hamu ya yale yote niliyotunukiwa na ar-Rahmaan, ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kutokubali kufuata na kusikiliza nasaha wala mawaidha ya wenye kukupendelea kila jema (nikiwemo mimi), ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kutenda na kuendelea bali kujifakharisha na kuwa mbunifu katika maasi, Qur-aan inasema:

“Hakika atayemjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu, basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi” Twaahaa aya ya 74.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kutokuwa tayari kuchukua hatua yoyote ile itayoweza kukubalisha na kukufikisha kuwa katika waja wema au wenye kupenda kukaa na kuwasikilia na kuwaiga waja wa ar-Rahmaan, ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kutoheshimu mipaka yangu na kumkejeli kila aliyejaaliwa kunipenda, kuniheshimu, kuchunga mipaka yangu na kunienzi, Qur-aan inasema:

“Kisha timizeni Swawm mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Allaah, basi msiikaribie. Namna hivi Allaah Anabainisha Ishara Zake kwa watu ili wapate kumcha” al-Baqarah aya 187, pia Qur-aan inasema:

 

“Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka Yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha” an-Nisaa aya ya 14.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, ugeni wangu utakuwa shahidi dhidi yako kwa kila ulichotenda chenye kwenda kinyume na mafundisho ya ar-Rahmaan kiwe kikubwa au kidogo.

 

Ndugu yangu katika Iymaan, basi kama ulijisahau kwa ujinga wako na kupendezwa na maneno na mbinu za wenye kujidanganya nafsi zao na kupelekea ukadanganyika, Qur-aan inakunasihi na kukuwaidhi:

 

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Allaah ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Allaah mdanganyifu” Luqmaan aya ya 33.

 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, kama uliwafikishwa kutekeleza yaliyowahi kutekelezwa na waja wa ar-Rahmaan katika ugeni wangu, basi usighurike na amali yako wala usijione kuwa umeikamilisha kama inavyotakiwa na kuwa ugeni wangu kwako umekubaliwa bila ya wasiwasi wo wote, usilale miguu juu na kusahau kuwa si kila amali na si kila mwenye kutenda amali hukubaliwa, ni katika kawaida na desturi za waja wema baada ya kutekeleza amali njema kujitahidi kuomba na kushikilia kumuomba Allaah Awakubalie amali yao hiyo, kwani wao wanaelewa kuwa Allaah Huwakubalia watu wenye sifa fulani na kushikamana nayo kila walipo, Qur-aan inasema:

 

“Hakika Allaah Huwapokelea – Huwakubalia- wacha Mungu.” al-Maaidah aya ya 27.

 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, kama unahisi na kuwa na tamaa (tunatakiwa tuwe na khofu na tamaa kwa kila amali tuitekelezayo) ya kukubaliwa ugeni wangu kwako, bali ushauri wa Qur-aan kwako ni ushauri ule ule kwa waja wa ar-Rahmaan baada ya kila amali njema kushikamana na Istighfaar, kama walivyoshauriwa Mahujaji baada ya kumaliza shughuli zao za Hijja, Qur-aan inawashauri:

 

“Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu Mlezi. Na mtakapo miminika kutoka ‘Arafaat mtajeni Allaah penye Masha'ril Haraam. Na mkumbukeni kama Alivyokuongoeni, ijapokuwa zamani mlikuwa miongoni mwa waliopotea” al-Baqarah aya ya 198.

 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, kama ulifadhilisha kucheza, kupoteza wakati, kuangalia TV, kucheza karata na starehe nyengine za kidunia, kila waja wa ar-Rahmaan wakielekea kwenye mawaidha, madarsa na visimamo, wewe huwa huna nafasi kwa kuwa ni virefu au kwa sababu zako za kimaajabu, basi ndugu yangu katika Iymaan, tafadhali tena sana tumia fursa hii isiyokuwa na mithili kwa kutumia masiku yangu ya mwisho haya – siku hizi zilizobakia kabla sijakuaga - kwa kurudi kwa Mola wako, kwa namna mbali mbali ikiwemo kuleta tawbah kuomba msamaha na kadhalika, Qur-aan inakunasihi kwa kukwambia:

 

“Na anayetenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghfira kwa Allaah, atamkuta Allaah ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu. an-Nisaa aya ya 110

 

 

Ndugu yangu katika Iymaan, lini atatubia asiyetubia katika masiku yangu haya machache na matukufu! Lini atarudi kwa Mwenye kumiliki vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, kama hakurudi katika masiku yangu haya matukufu! Lini atajihisabu na kutathmini amali zake kama hukufanya haya katika masiku yangu haya ya mwisho! Lini utakaa chini na kukumbuka kuwa wewe umeumbwa na utakufa na kufufuliwa na kuhukumiwa na aliye Mkwasi na Mwenye kusifiwa!

 

Mwenyeji wangu mpenzi na ndugu yangu katika Iymaan, kabla hatujaagana napenda kuiusia nafsi yangu na kukuusia wewe na wenyeji wangu wengine kuwa tutumie siku hizi zilizobakia kunyanyua sana mikono yetu na nyoyo zetu kwa kumuomba Mwenye kupenda kuombwa huenda Akatughufirilia mijizambi yetu na insha Allaah Atatukubalia maombi yetu kwani Ameahidi kufanya hivyo, Qur-aan inasema:

“Na waja wangu watakapokuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.” al-Baqarah aya 186

 

 

Mwenyeji wangu mpenzi na ndugu yangu katika Iymaan, kabla hatujaagana napenda kukupa nasaha hizi, baada ya kunipokea na kukubali ugeni wangu kwako na kwa uwezo wa Rabbuka kukufundisha na kukuelekeza mengi, ni tegemeo langu kuwa hutojitosa katika madhambi baada ya kufutiwa insha Allaah kwa kuwepo kwangu kwako, ni tegemeo langu kuwa utaendelea kushikamana na masomo na mafunzo yote uliyo yapata katika chuo cha Ramadhaan, ni tegemeo langu kuwa utaendelea kusoma Qur-aan, ni tegemeo langu kuwa utaendelea kusimama usiku, ni tegemeo langu kuwa utaendelea kuishi na mimi, na ni tegemeo langu kuwa kama nitajaaliwa kuja na kukutana na wewe tena nitakukuta ukiwa katika hali yenye kutazamika na kuridhisha.  

 

Twamuomba al-Hayyu al-Qayyuum al Mutakabbiru al-Khaaliq al-Qaadiru al-Qudduus al-Maaliku al-Mannaan al-Ahadu asw-Swamadu Asiye na mwana Atughufirilie makosa yetu, Atutoe katika moto wa Jahannamu, Atuepushe na adhabu Zake, Atuonyeshe njia za ibada yetu, Atujaalie juu ya upungufu wetu tuwe miongoni mwa Aliowatakabalia na kukubaliwa Swawm zao, ‘amali zao, visimamo vyao, vitajo vyao, visomo vyao, du’aa zao, sadaqa zao na kadhalika, kwani Yeye ni Khayrul Ghaafiriyna, Tawwabur Rahiym, As Samiy’ul-‘Aliym (Msikizi Mjuzi) na ni Arhamur Raahimiyna, twamuomba Atuwafikishe katika yote Anayoyapenda na kuyaridhia.

Tuitikie maombi yetu kama ulivyotuahidi Yaa Rabb Yaa Mujiyb Ya Qariyb Ya Allaah.

 

Aamiyn … Aamiyn … Aamiyn

 

Wassalaamu 'alaykum WarahmatuLlaahi Wabarakaatuh