Skip navigation.
Home kabah

Tathmini Baada Ya Ramadhaan

   

Ummu Naaswrah

 

Shukurani zote kwa Allaah سبحانه وتعالى Ambaye Ametufikisha kukaribia kuukamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhaan kwa salama, afya na kwa nguvu zote. Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atukabalie Swawm zetu, sala zetu visomo vyetu visimamo vyetu na du’aa zetu inshaAllaah, Aamiyn.

 

Ni vigumu kwa mtu kumudu kuendeleza mazuri yote ambayo akiyatenda wakati wa Ramadhaan pindi itapomalizika, inakuwa kama mwanamke alieukata uzi wake vipande vipande baada ya kuusokota kuwa mgumu (an-Nahl 16:92). Huko ni kupoteza nguvu bure. Ramadhaan tunafunga, tunasoma Qur-aan, tunatoa sadaka, tunasimama usiku kwa du’aa, jee tutaendelea kuwa hivyo baada ya kumalizika Ramadhaan au tutafuata njia nyengine ya Shaytwaan kufanya makosa na kuingilia mipaka (makatazo) ya Allaah سبحانه وتعالى?

 

Kama Muislam ataendelea kuwa na subira ya kuendeleza mazuri baada ya Ramadhaan basi hiyo ni ishara ya kukubaliwa Swawm yake na Allaah سبحانه وتعالى na ni rehma kutoka kwa Mola wake. Na kama atashindwa kuyaendeleza mazuri na badala yake kumuasi Allaah kwa kuwa Ramadhaan imemalizika ni aibu kwake na kujishushia hadhi mwenyewe mbele ya Allaah سبحانه وتعالى, na ambaye Allaah Amemfedhehesha basi hakuna atakayempa heshima [al-Hajj 22:18].

Ni mazoea ya wengi kufanya mazuri katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan, mara tu mwezi unapomalizika, binaadamu anabadilika kabisa na kujenga uhusiano mbaya na mola wake. Utaona sala zinapuuzwa, mashungi huvuliwa, sala za usiku hazipo tena, huyaacha mazuri yote na kuyakimbilia maovu ya kila aina na kujiweka mbali na twaa ya Allaah سبحانه وتعالى.

 

Ni ubaya ulioje mbele ya Allaah kwa mtu kumtambua kipindi cha Ramadhaan tu.

 

Muislam aijenge Ramadhaan kuwa ni bahati na ni fursa ya kufungua ukurasa mpya wa uhusiano mzuri na Mola wake, kuendeleza kumuabudu Allaah na kumtii. Jua kwamba Allaah Anakumurika kila dakika. Hivyo baada ya Ramadhaan ni kuendeleza mazuri, kumcha Allaah na kuepukana na kila baya na ovu. Hii itakupelekea kuwa karibu na Allaah. Ukiendelea kufanya mema, maovu huondoka [Huud 11:114]

 

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّـيِّئَاتِ ذَلِكَ ذِكْرَى لِلذَّاكِرِينَ


{{Hakika mema huondoa maovu huu ni ukumbusho kwa anayekumbuka}}


Yeyote atakayejitahidi kuendeleza mazuri hata baada ya Ramadhaan Allaah Naye Humuongoza kwa hayo duniani na akhera, Allaah Anatueleza [Ibraahiym 14:27]

 

يُثَبِّتُ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ

{{Mwenyezi Mungu Huwathubutisha wale walioamini kwa kauli thaabit katika maisha ya dunia na akhera}}

 


Tuombe msamaha sana katika mwezi wa Ramadhaan na kuazimia kutorudia tena makosa yetu, kwani toba inayokubaliwa ni pale mtu anapofanya kosa kwa kutokujua na kutubia haraka anapotambua, sio kurumbikiza makosa na kusubiri mauti ndio atake msamaha. Allaah
سبحانه وتعالى Anatueleza [An-Nisaa 4:17 -18]

إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللّهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوَءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُوْلَـئِكَ يَتُوبُ اللّهُ عَلَيْهِمْ وَكَانَ اللّهُ عَلِيماً حَكِيماً

{{Toba inayopokelewa na Allaah ni yale waliofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi, hao ndio Mwenyezi Mungu Huipokea toba yao, na Allaah ni Mjuzi na Mwenye hekima}}

 

وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّى إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ

{{Hawana toba wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, akasema: hakika mimi sasa nimetubu}}






Mara nyingi ikimalizika Ramadhaan, utawakuta watu wapo makundi mbali mbali. Yaliyo maarufu ni haya:

 

1.       Kuna wale ambao wakati wa Ramadhaan ulikuwa ni mgumu kwao, huwaoni kusali wala kusoma Qur-aan au kujishughulisha na ibada yoyote, huona kama wamo kifungoni. Ikimalizika Ramadhaani tu huwa kama wamefunguliwa na kulipiza yale yote waliojizuia nayo kipindi cha Ramadhaan.

 

  1. Kuna wengine baada ya kujizuilia na kila lenye kufungulisha na kuutumia muda wao kwa kufanya kila aina ya ibada ikimalizika Ramadhaan tu huyaacha yote na kutojishughulisha na kheri yoyote.  Huyarudia yale yale waliokuwa wakiyafanya. Hawa ni wale wanaomtambua Allaah katika wakati maalum tu.

 

  1. Aina nyengine ni wale ambao huwa na huzuni kwa kumalizika kwa Ramadhaan kwa sababu  wamepata utamu wa kusamehewa makosa yao na kujikurubisha zaidi kwa Mola wao. Wamefunga kwa Iymaan na kutaraji malipo kwa Mola wao, wakiwa na khofu ya kukubaliwa matendo yao na tamaa kubwa ya malipo mazuri kutoka kwa Mola wao.  Hao huwa na masikitiko sana kwani hawajui kama wataipata tena fursa hii.

 

Bila ya shaka aina zote hizo zina mtazamo tofauti mbele ya Allaah سبحانه وتعالى   Jiulize ndugu yangu katika Iymaan katika aina hizi tatu ni ipi uliyopo wewe.   Kila mmoja anaijua nafi yake vilivyo hata kama atatafuta nyudhuru tofauti.

 

Ndugu zangu katika imani, baraka tuliopata katika kipindi cha Ramadhaan tusiiache ikatutoka hivi hivi. Kumbuka wakati wako ulioutumia kwa kukesha, kufunga, duaa zisizorejeshwa na mengi mazuri, yatunze usiyaache mazuri hayo yakayayuka bure kwa kufanya maasi baada ya Ramadhaan.  Binaadamu makosa hayatuepuki, basi angalau tujitahidini na madhambi makubwa ili Allaah Naye Atusamehe madogo, na hiyo ni ahadi kutoka kwake. [al-Nisaa 4:31]

إِن تَجْتَنِبُواْ كَبَآئِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ

{{Kama mtajiepusha na maovu makubwa mnayokatazwa tutakufutieni makosa yenu madogo}}

 

Tumuombe Allaah Atukubalie funga zetu, ibada zetu na Atujaalie izidi Iymaan yetu kwake na Kututia nguvu ya kuendelea mazuri na kuwa na msimamo nayo inshaAllaah.

 

 

WabiLlaahi at-Tawfiyq