Kujitupa Kwa Mwenyezi Mungu (Ta’alluq Billah)
Imetayarishwa na Shaibu H.Kifea
Waadhi wa kwanza kabisa uliotolewa na Mitume wote, Makhalifa waongofu na WachaMungu miongoni mwa Umma wa Kiislamu ulikuwa ni ule wa kujenga hofu juu ya Allaah, kupandikiza mapenzi Kwake katika moyo wa mtu na kuzidisha ukaribu na Allaah.
Imani juu ya Allaah ndiyo kipengele muhimu zaidi kuliko vipengele vingine vyote. Kwa hiyo makurubiyano ya moyo wa mtu na dhati ya Allaah ndiyo muhimu zaidi katika Ibada za mja.
UchaMungu lazima utawale maadili ya mtu na kutafuta radhi za Allaah ndiyo liwe jambo la mbele kabisa katika mambo yote anayoyafanya mtu.
Kwa kifupi mwenendo mzima wa maisha yetu ujengeke kwa msingi wa kupata radhi za Allaah na hili ndilo ndilo jambo la kuwekwa mbele katika jitihada na harakati zetu.
Hasa hasa hili jukumu zito tulilonalo sisi ambalo kwalo sote twaungana kama jamaa moja ya Kiislamu au kama kundi moja la wanaharakati.
Kundi hili laweza kufanikiwa kwa chachu ya ukaribu wetu na Allaah. Litakuwa na nguvu au dhaifu kutegemeana na ukaribu wetu na Allaah.
Ni ukweli unaokubalika kuwa jambo lolote analoliendea mwanadamu liwe la kutafuta dunia au Akhera, msukumo mkubwa nyuma ya jambo hilo unatokana na lile lengo ambalo mtu anataka kulifikiya ambapo juhudi huweza tu kushitadi iwapo ana utashi na hamasa ya kufikia lengo hilo.
Mtu atafutaye maslahi binafsi hawezi kufaulu bila kuwa na ubinafsi. Ule ukubwa wa kupenda kujinufaisha yeye binafsi ndio unaompelekea kufanya kazi ya kuinufaisha nafsi yake.
Mtu anayefanya kazi kwa ajili ya familiya yake, hufanya hivyo kwa sababu ya mapenzi aliyonayo kwa watoto wake, huwa tayari kujituma kwa kila hali na tena kwa furaha ili kuwapatiya hali bora wanawe.
Naye mtu anayefanya kazi kwa ajili ya Taifa lake ni mateka wa mapenzi ya Taifa lake na kwa sababu ya mapenzi haya huwa tayari hata kupata hasara ya fedha na kupata magumu na machungu mengine ya kuwekwa kizuizini na kufungwa jela.
Mtu huyu anafanya kazi usiku na mchana na kukubali hata kufa kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi yake, kuilinda na kuipatiya maendeleo.
Sasa basi na sisi tunafanya harakati za kujenga utaratibu wa maisha wa Kiislamu na si kwa ajili ya malengo yetu binafsi; na wala si kwa maslahi ya familia na wala si kwa maslahi ya Taifa bali kwa tamaa tu ya kumridhisha Mola wetu.
Na kama tumeingia katika kazi hii kwa kuamini kuwa Hii ni kazi Yake basi mwaweza kutambua kuwa kazi hii haiwezi kwenda isipokuwa mpaka ukaribu wetu na Allaah uwe wa kweli na wa ndani kabisa ya nyoyo zetu.
Jitihada katika Kazi hii hudumu iwapo tu nyendo zetu zote zitaelekezwa katika harakati za kueneza Neno la Allaah. Kwa wale wote waliojiunga na harakati hizi haitoshi kwao kusema kuwa “na wao pia” wamejikurubisha kwa Allaah bali ukaribu huo uwe wa dhati.
Kwa maneno mengine, usiwe alimuradi uhusiano tu bali uwe uhusiano wa kweli kabisa. Mara zote tuwe hadhiri kuwa ukaribu wetu na Allaah haupungui badala yake unaongezeka na kuwa mkubwa na mkubwa zaidi kadri muda unavyokwenda
Kujitupa kwa Allaah ndiyo chachu kubwa ya kuendesha harakati zetu. Alhamdulillah, hakuna mwanaharakati wa Jumuiya yetu asiyeuzingatia ukweli huu na asiyejua umuhimu wake.
Lakini bado wengi hawaelewi sawasawa nini hasa maana ya hili neno Ta’aluq Billaah. Ni ipi njiya ya kuipandikiza na kuidumisha na ni kwa vipi mtu atajuwa kuwa yeye ana ukaribu na Allaah au la, na ni kwa kiwango gani.
Mara nyingi kumekuwa na ile hali ya watu kutoelewa mambo haya. Watu hawaelewi wako mahali gani na wapi wanakwenda na ni umbali gani ambao hawajaufikia.
Matokeo yake baadhi ya wanaharakati huangukia katika mambo yenye utatanishi na baadhi huelekea katika njia na mambo ambayo kamwe hayawezi kuwafikisha kule waendako. Wengine hushindwa kutofautisha kati ya mambo ya kumkurubisha mtu kwa Allaah na yale ya kumsukuma mbali Naye.
Maana ya Ta’aluq Billah
Maana yake kwa mujibu wa Qur-aan ni kuwa mtu aishi na kufa kwa ajili ya Allaah ambapo mambo yake yote yafanywe kuwa ibada kwa ajili ya Allaah
((Hakika Swalah yangu na ibada (zangu nyingine zote) na uzima wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya MwenyeziMungu, Muumba wa walimwengu, Muumba wa Walimwengu wote)) (6:162).
Mtu hana budi kuelekeza utii wote kwa Allaah pekee. Qur-aan inasema;
((Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu MwenyeziMungu kwa kumtakasia dini, wawache dini za upotofu, na wasimamishe Swalah na kutowa Zakaah-hiyo ndiyo dini iliyo sawa)). (98:5)
Mtume wa Allaah, kwa nyakati tofauti alifafanua maana ya kujitupa kwa Allaah kwa maneno ya wazi kabisa. Hakuna utata wowote ulioachwa katika maana na madhumuni yake.
Inadhihirika katika kauli zifuatazo kwamba, kuwa karibu na Allaah ni
Kutegemea Uweza wa Allaah badala ya nguvu zake (al-Bayhaqiy).
Mtu awe tayari kuzikabili ghadhabu za watu ili kupata radhi za Allaah na kamwe asiwe tayari kufanya kinyume chake. Na pindi ukaribu na Allaah unapofikia mahala ambapo mapenzi, uadui, kutoa na kunyima vyote hufanywa kwa ajili ya Allaah, pasipo msukumo mwingine wowote basi hiyo maana yake ni kuwa mtu amefikia ule ukaribu na Allaah.
Mtume (SwallaLlaahu ‘alayhi wa sallam) kasema; ((Yeyote aliyependa kwa ajili ya Allaah, aliyechukiya kwa ajili ya Allaah, aliyetowa kwa ajili ya Allaah na aliyenyima kwa ajili ya Allaah, huyo amekamilisha imani yake)) (al-Bukhaariy).
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
