Mirungi Ni Haraam? Vipi Mtu Aweze Kuacha Kutumia?

SWALI:  

Naimani wewe ni mzima wa afya na mimi ni mzima nashukuru Allah kwa kunipatia Pumzi siku ya leo.  

swali langu ni je mirungi ni haramu? Na je nifanyeje ili ndugu yangu aache kutumia? Wabillah tawfiq. 

 


JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu mirungi. Mwanzo kabisa ni kuwa mirungi ni haramu katika Dini yetu ya Kiislamu kwa madhara yake maovu sana katika nyanja tofauti. Miongoni mwazo ni: Kufuja pesa kwa kitu kisichokuwa na manufaa, kuharibu afya ya mlaji pamoja na magonjwa na madhara mengi ambayo yanatokana nayo kama kuvunja nyumba kwa kuleta talaka baina ya wanandoa, kuleta uhalifu na wizi na maovu mengine mengi.

 

Allaah Aliyetukuka Anatueleza: " Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Allaah Huwapenda wafanyao wema" (2: 195).  

Uislamu umekuja kuyathibiti maslahi ya wanaadamu wote na kitu chochote ambacho kina madhara basi huwa kimekatazwa kwa kuchunga ule msingi wa kuihifadhi nafsi 'Hifdhun-Nafs'. Na kwa madhara yote hayo basi sheria imejitokeza moja kwa moja kukataza ulaji wa mirungi. Taabu na tatizo linatokea kwa ma-Shaykh ambao ima kwa maslahi yao kwa sababu ya uhaba wa elimu wanahalalisha lakini kufanya hivyo kwao hakuwezi kufanya jambo haramu kuwa halali. 

 

Ama kumtoa ndugu yako katika ulaji wa majani hayo inategemea anakula kiasi gani. Je, yeye ni mlaji wa starehe tu au ni yule ambaye ni lazima apate kila siku? Katika hali zote inatakiwa juhudi za juu kwa upande wako ili umwokoe na maafa makubwa yanayomkumba. Ushauri wetu ni kuwa ufuate mfumo ufuatao nasi twakuombea tawfiki katika hilo

 

1- Kumfahamisha uharamu wake: Mara nyingi Waislamu hufanya kitu cha haramu kwa kutojua uharamu wake. Hivyo, ni juu yako kumfahamisha hilo. Uharamu wake umetajwa na Shaykh al-Amiyn Mazrui katika Qurani Tukufu, juzuu ya kwanza. Pia zipo kaseti za wataalamu wa Kiislamu katika nyanja ya sayansi na udaktari ambao wametoa madhara yake.

 

 

 

 

2- Umauti: Zungumza naye kuhusu suala hilo la kuwa sote tutakuwa ni wenye kuaga dunia na kwenda kuhukumiwa na Aliye Muadilifu. Je, sisi tumejiandaa vipi kwa suala hilo? Tupo tayari kukutana na Allaah Aliyetukuka? Mweleze umuhimu wa kuweza kuihesabu nafsi yake kwa yote ambayo nafsi inafanya mazuri na maovu na ajaribu kuyapima yepi ni mengi. Hilo linaweza kumsaidia.

 

3- Kielelezo Chema: Jaribu kumpatia mawaidha kutumia ruwaza njema za watangu wema na jinsi gani walikuwa na ari ya kuitafuta haki na kufanya juhudi kuifuata pindi wanapoipata. Mueleze jinsi gani Maswahaba (Radhiya Allaahu 'Anhum) walivyokuwa ni wanywaji vileo (ulevi) kwa kupindukia lakini pindi Allaah Aliyetukuka Alipoteremsha Aayah ya 90 hadi 91 katika Suratul Maaidah walivyoacha papo hapo bila kusita. Tafuta vitabu vya maisha ya watu wema vilivyo sahihi na ujaribu kumuelimisha katika hayo.

 

4- Marafiki: Urafiki na uchaguzi wa rafiki au marafiki ni muhimu sana. Mara nyingi utakuta mtu ameingia katika wema au uovu kwa sababu ya urafiki. Ndio kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyh iliyonukuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim akafananisha urafiki mwema na muuzaji manukato ambayo anaweza ima akakupa hadiya au akakupaka na rafiki muovu ni kama kusuhubiana na mfua chuma. Huyu ima ataunguza nguo yako au utatoka kwake na harufu mbaya. Hivyo, jaribu wewe kama ndugu mwema kusuhubiana naye na kumtoa katika magenge na mabaraza ambayo hayafaidishi. 

 

Mbali na yote hayo itategemea yeye mwenyewe ataka kuwaje. Je, anataka kubadilisha maisha yake au anataka kubaki kama alivyo? Lakini letu sisi ni kufikisha ujumbe kama ulivyo na kutia juhudi pamoja na kupanga mikakati na kumwachia mengine Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Anatueleza: "Hakika Allaah Habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao" (). 

 

Makala

Kokeni, Hiroini, Bangi, Mirungi - Haramu

Mirungi - 1

Mirungi - 2 (Historia, Madhara Na Mikasa)

Mirungi - 3 (Mwisho) - Fataawa Za Wanachuoni

Mirungi Ni Jamii Moja Na Bangi

Mirungi - Majani ya Mashetani

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share