Skip navigation.
Home kabah

Sanda ya Mwanaume na Mwanamke Inavyotayarishwa

   

SWALI:

 

asalaam aleikum,

Allaah swt awajazieni kulla la heri kwa kazi yenu aali mnayoitekekeleza inshaAllaah.WAllaahi ningependa mnifafanulie kwa kutumia picha namna ya kushona sanda ya maiti,taratibu zote zinazofuatwa katika ushonaji,yaani vipande vingapi kwa mwanamke na vingapi kwa mwanamume,tofauti ya ushonaji kati ya sanda ya mwanamume na mwanamke, pamoja na mihimili ya kauli za Mtume  wa Mwenyezi Mungu,saw.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Kabla hatukutoa maelezo ya ushonaji sanda, ni vizuri kusoma yafuatayo:

Jifunze kujua mambo anayopaswa kufanyiwa mtu akifariki

Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti

Kumkafini na kumpamba maiti

Yampasayo Maiti

 

Kafan (Sanda) ya Maiti

Maiti hukafiniwa baada ya kuoshwa kama utakavyopata maelezo katika makala hizo za juu. Sanda inapendekezeka iwe ni kitambaa cheupe kisichokuwa cha thamani kubwa kwani israaf ni jambo lililokatazwa katika Dini yetu, hivyo maiti ni muhimu kumuepusha nalo. Haipasi sanda kuwa ni ya Hariri wala yenye marembo ya dhahabu au aina yoyote.

Kafan Ya Mwanamume:

Vitambaa vitatu kutokana na dalili ifuatayo:

وعن عائشة رضي الله عنها قالت : "كفن رسول الله صلى الله عليه وسلم في ثلاثة أثواب بيض سحولية من كرسف، ليس فيها قميص ولا عمامة"  متفق عليه.

Kutoka kwa Mama Wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikafiniwa na nguo tatu nyeupe, hakuna katika hizo kanzu wala kilemba" [Al-Bukhaariy na Muslim]

Saizi ya kafani iwe kama ifuatavyo na maelezo ya wazi yako katika picha tulizozitayarisha kwa ajili ya wepesi wa kufahamu. Tazama Picha Namba 1

 

Ziwe ni saizi ya futi 7 kwa futi 7, ziwe safi na kubwa za kumtosha kumfunikia maiti mwili wake mzima. Maiti akafiniwe baada ya kupakwa manukato mazuri na udi.

Tumia kamba 4 kila moja ikiwa ni futi 7 urefu. 

Baada ya kuoshwa afunikwe kwa shuka na alazwe chali katika ubao wa kumkafini.

Apakwe manukato khaswa katika sehemu za kusujudia; kipaji cha uso, pua, mikono, magoti na miguu

Mpangilio wa kumkafini Mwanamume:

  1. Tandaza shuka za kumviringishia maiti moja juu ya nyingine.
  2. Utaanza kumfunika maiti kwa upande wa shuka kuanzia kulia kwenda kushoto, kisha upande wa kushoto kwenda kulia.
  3. Shuka ya pili aviringishiwe hivyo hivyo.
  4. Shuka ya tatu nayo aviringishiwe hivyo hivyo.
  5. Mwisho zitumiwe kamba hizo kwa kumfunga maiti kama unavyofunga fundo ili mwili wake uthibitike katika shuka asilegee; ya kwanza kichwani, ya pili miguuni na mbili afungwe katikati ya mwili wake.

 

Kafan ya Mwanamke

Maelezo Katika picha Namba 2 yanajielezea zaidi vizuri.

 

Sifa ya vitambaa iwe vile vile kama tulivyotaja ya mwanamume, yaani nyeupe isiyokuwa ya gharama na isiyo na mapambo n.k.

Vitambaa viwe vikubwa vya kumtosheleza kumfunika vizuri maiti asitirike sehemu zote zake za mwili isipokuwa uso. 

Kamba zitumiwe vile vile kama anavyofungwa maiti mwanamume.

Idadi ya Kafan ya mwanamke iwe ni vitambaa vitano ikiwezekana, kama ifuatavyo:

 

  1. Shuka ya Kumviringishia mwisho
  2. Shuka ya kumviringishia baada ya kumvalisha kanzu
  3. Kanzu iwe ndefu ya kumfunika hadi miguuni
  4. Izzaar - Shuka inayotokea kiunoni hadi miguuni kumstiri sehemu zake za siri.
  5. Khimaar – Ushungi utakaomfunika kichwa chake hadi kwenye kifua (ambao unafunika kichwa na uso).

 

Baada ya kuoshwa awe amefunikwa na kulazwa chali juu ya ubao wa kumkafini.

Anaweza kupakwa manukato khaswa katika sehemu za kusujudia; kipaji cha uso, pua, mikono, magoti na miguu

 

Mpangilio wa kumkafini Maiti Mwanamke:

1.                 Shuka mbili za kumviringishia za saizi ya futi 7 kwa futi 7 zitandazwe juu ya ubao wa kukafini maiti.

2.                 Kanzu ya kumvisha ikiwa ni saizi ya ya futi 14 (ambayo itakapokunjwa na kuvishwa nayo maiti, itakuwa ni sawa na futi 7 mara 2), kwa futi 3 1/2 iliyopasuliwa shingoni kama ionekanavyo katika picha kwa ajili ya kukipitisha kichwa bila ya tabu; itandazwe.

3.                   Izaar (shuka) iliyo saizi ya futi 6 x futi 3 1/2.

4.                 Khimaar ikiwa ni saizi ya futi 4 x futi 4

 

Mpangilio wa kumvisha:

  1. Anza kumvisha izaar (shuka) kuanzia kiunoni.
  2. Kisha fautilia na kanzu.
  3. Mvishe Khimaar ifunike kichwa hadi kifua chake.
  4. Aviringishwe vizuri na shuka ya kwanza iliyokwishatandazwa chini yake.
  5. Aviringishwe na shuka ya pili.
  6. Mwisho zitumiwe kamba hizo kwa kumfunga maiti kama unavyofunga fundo ili athibitike katika shuka asilegee; ya kwanza kichwani, ya pili miguuni na mbili afungwe katikati ya mwili wake.

 

Na Allaah Anajua zaidi