Skip navigation.
Home kabah

Kuomba Msaada Kwa Wasio Waislamu Kwa Ajili Ya Jumuiya

 

SWALI:

ASSALAAM ALAYKUM,

SISI NI WAISLAMU WENYE NIA YA KUANZISHA JUMUIYA YA KUSAIDIANA KATIKA MAMBO MBALI MBALI YA KIMAISHA. ILI KUTIMIZA LENGO HILO TUNANIA YA KUANZISHA MIRADI HALALI YA KIISLAMU. HATA HIVYO KWA KUWA HATUJAKUWA NA MSINGI WA KUTOSHA TUNA NIA YA KUWAANDIKIA VIONGOZI TOFAUTI ILI KUOMBA MISAADA.

1) JE, UISLAMU UNASEMAJE KATIKA HILO?

2) JE, TUNAWEZA KUOMBA KWA VIONGOZI WASIOWAISLAMU?

NDUGU YENU KATIKA KHERI.



  JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo zuri na lipo hasa katika ulimwengu wa sasa.

Ni muhimu sana kwanza mkitaka kuanzisha miradi mwanzo mtazame nyinyi kama waanzilishi mnaweza kujitolea vipi katika hilo. Hakika ni kuwa hasa mashirika ya kikafiri huwa hayatoi usaidizi wa miradi hivi hivi. Wao huwa wanataka kujua nyinyi wenyewe mumeweza kujimudu kuchanga kiasi gani katika hazina ya miradi. Ni wazi kuwa kwa sababu ya kutekeleza malengo yao makubwa huwa wanafadhili miradi hata yetu, Waislamu kwa lengo la kupunguza chuki zetu kwao au kutuvutia katika Dini zao au kujipenyeza kwa nia ya kuingiza sumu zao. Asiyekuwa Muislamu hawezi kabisa kusaidia Waislamu ili waweze kuinuka kiiktisadi au kibiashara.

Uislamu unakubali usaidizi wa wasiokuwa Waislamu katika kusaidia miradi ya Waislamu ikiwa hakutakuwa na masharti yoyote kwa usaidizi huo. Mfano ni kujenga Msikiti au mradi mwingine wowote. Usaidizi halisi unatakiwa utoke kwa Waislamu lakini ikiwa haufiki kima kilichowekwa Waislamu wanaweza kuchukua usaidizi kwa makafiri. Lau utasibu kuwa makafiri wenye kutoa msaada wataweka masharti yao kwa mfano watataka kusaidia kujenga Msikiti, shule au kufadhili mradi fulani lakini watataka wahusishwe katika uongozi au usimamizi au uendeshaji wa shughuli hiyo au hata kutekeleza jambo ambalo ni kinyume na Uislamu, hapa unatumiwa msingi wa Fiqhi unaosema: “Dhara lililo dogo (lenye nafuu) zaidi”, yaani kuangalia kwa mchango au ufadhili wao huo kutakuwa na madhara gani na faida gani.

Kwa hali ilivyo sasa, wasiokuwa Waislamu wamejengea mazingira ya kuweza kufadhili Waislamu na miradi yao kwa mikakati yao na malengo yao makubwa. Leo imekuwa mpaka watu kama Freemason wanafadhili miradi katika maeneo ya Waislamu. Ni dhahiri kuwa taasisi nyingi za Kiislamu za kimataifa zimefungiwa katika nchi nyingi za Waislamu kwa kisingizio kwamba zinasaidia ugaidi na magaidi. Hivyo, kumefanya taasisi na mashirika ya kanisa pekee yakifanya kazi hata katika maeneo ya Waislamu. 

Tukichukua msingi ulio juu, “Dhara lililo dogo zaidi”, tutapata ya kwamba kufadhiliwa mafano na Marekani kunapatikana dhara kubwa zaidi kuliko faida. Mwanzo jambo hili haliingii akili kuwa Marekani inawatakia kheri Waislamu wa Afghanistan, Iraaq, Kenya, Tanzania, Zanzibar, Uganda na nchi nyingine. Ilhali hapo hapo wanawaua ndugu zetu katika nchi kama Afghanistan, Iraaq, Palestina na kumsaidia Israili katika kuwaua ndugu zetu Palestina na hata kuwaadhibu na kuwafunga ndugu zetu wengi katika nchi ya Kenya.

Hivi tunavyozungumza ni kwamba, kwa shinikizo la Marekani, serikali ya Kenya imewashika hata watoto wadogo, mama zao, na hata wanawake waja wazito. Watoto walio chini ya miaka 5 kadhaa wameshikwa baada ya uvamizi wao katika nchi ya Somalia na kuwatoa mamlakani Mahakama za Kiislamu ambazo ziliweza kwa muda wa miezi sita kurudisha amani na utulivu katika nchi hiyo. Hili ni jambo ambalo haliingii akili mwa mtu yeyote mwenye akili japokuwa chache. Vipi taasisi hizi zinakwenda kusaidia katika nchi hizo hasa Afghanistan na Iraaq na ilhali huko wanataka kubadilisha mifumo ya Dini kwa kuua Madrasah na kubadilisha mitaala (Syllabus) za masomo na kusaidia kueneza Biblia nyingi sana katika nchi hizo!  

Kwa taarifa, hivi sasa nchi za kiarabu mbalimbali kama Kuwait, Oman na nyinginezo zimeshaanza kubadilisha na kuondosha zile Aayah zote za Jihaad na zile zenye kuwazungumzia Mayahudi n.k. kwenye vitabu vya masomo ya shule!! Yote hayo ni kuwaridhisha hao makafiri wa kiamerika.

Kwa kawaida sisi tunapopata msaada kutoka nchi hizo, taasisi na mashirika yao huwa ni wenye kufurahi lakini hicho ni chambo cha kututoa sisi katika Dini yetu pole pole. Uadui wao upo wazi kwetu sisi kwani Allaah Aliyetukuka Anatueleza: “Hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila zao” (2: 120).

Uadui wa Mayahudi kwetu unashinda hata ya washirikina kama alivyosema Aliyetukuka: Hakika utawakuta walio wakali kuliko watu wote katika uadui kwa walioamini ni Mayahudi na washirikina (5: 82).

Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha mikakati katika usaidizi wao: “Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia (watu wasipate kuamini) njia ya Allaah. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa” (8: 36).

Hii ndio hakika ambayo kila mmoja wetu anaiona. Kwa minajili hiyo ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akatutahadharisha: “Enyi Mlioamini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa marafiki (wa kuwapa siri zenu); wao kwa wao ni marafiki. Na miongoni mwenu atakayefanya urafiki huo nao, basi huyo atakuwa pamoja nao. Hakika Allaah Hawaongozi watu madhalimu” (5: 51).

Kwa hali ilivyo na itakavyoendelea kuwa ni bora zaidi Waislamu kuepuka misaada yao. Hakika ni kuwa ikiwa tutakuwa na Imani thabiti Allaah Atatutolea njia iliyo bora kuliko hiyo na hilo litakuwa kheri kwetu. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atufanikishie mambo yetu, Atuauni katika jumuiya zetu kwa kutusahilishia mambo yetu bila kuomba misaada kutoka kwa makafiri, Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi