Isbaal: Hukmu Ya Nguo Inayovuka Mafundo Ya Miguu Ya Mwanaume

 

SWALI:

 

Napenda kufahamu ukweli kusuhu kuvaa nguo inayopita vifundo viwili vya miguu.

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa suala lako hilo kuhusu isbaal (kuburuza) nguo kwa wanaume. Isbaal ni jambo ambalo limekatazwa na sheria na ikiwa jambo hilo litafanywa kwa kiburi basi dhambi lake ni kubwa zaidi. Nadhani Hadiyth chache kuhusu jambo hilo litaliweka wazi na utata wote kuondoka.

 

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Kilicho chini ya fundo mbili katika vazi kitakuwa motoni” [Al-Bukhaariy na an-Nasaa’iy]. Akikusudiwa mvaaji wa lile vazi kuingia motoni na si vazi lenyewe.

 

 

Na imepokewa tena kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Allaah Hamuangalii mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi [Al-Bukhaariy, Muslim na Maalik].

 

 

Na imepokewa katika riwaya nyingine kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hatazungumza na watu aina tatu Siku ya Qiyaama wala Hatawaangalia na wala Hatawatakasa na watakuwa na adhabu iumizayo”. Akasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikariri kauli hii mara tatu”. Akasema Abu Dharr: “Watu hao wamehasirika, ni kina nani ewe Mtume wa Allaah?” Akasema: “Mwenye kuburuza nguo kwa kiburi; na mwenye kujionyesha kwa fadhila aliyomfanyia mtu mwengine; na mwenye kuuza mali duni kwa kiapo cha uongo” [Muslim].  Na katika riwaya nyengine: “Mwenye kuburuza kikoi chake kwa kiburi". 

 

 

Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Allaah Hatawaangalia wale watu walioburuza nguo zao kama kikoi na kanzu na kilemba kwa kiburi[Abu Daawuud na an-Nasaaiy kwa Isnadi iliyo sahihi].

 

 

Tunatumai Hadiyth hizo chache zitaingiza nuru katika nyoyo zetu hivyo kuweza kuvaa nguo kama ilivyoamrishwa kutoka kwenye Sunnah. Hivyo, kuvaa nguo yenye kupita mafundo mawili za miguu ni kujitakia adhabu iumizayo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na pia kutotazamwa siku ya Qiyaamah na kutotakaswa. Kwa hiyo, ni juu yetu kutahadhari kwa kiasi kikubwa ili tusiingie katika maangamivu hayo. Allaah Aliyetukuka Atuepushe na hayo.

 

 

Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura) - 1

 

Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura) - 2  

 

Nini Maana ya Kibri Iliyotajwa Katika Mas-ala Ya Isbaal?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share