Skip navigation.
Home kabah

Umuhimu Wa Zakaah - 2: Masharti Yanayomuwajibikia Mwenye Kutoa Zakaah

 

Abu 'Ammaar

 

MASHARTI YANAYOMUWAJIBIKIA MWENYE KUTOA ZAKAAH

 

Zakaah ni ibadah iliyo na masharti ambayo kila mwenye kutaka kutoa atatakiwa ahakikishe ameyatimiza.

 

Zakaah ni wajibu kwa:

1       Muislamu

Zakaah ni ibadah na nguzo ya tatu katika uislamu. Humuwajibikia Muislamu tu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu Wata’ala):

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo. [At-Tawbah: 103]

Amri hii imekuja kwa waumini tu hivyo kisheria si wajibu kuchukua au kutoa Zakaah kwa wasiokuwa waislamu.

 

2       Baleghe na mwenye akili timamu

Haya ni masharti ya kimsingi katika jambo lolote la ibadah. Mukallaf ni anaewajibika na hukumu za kisheria. Hata hivyo kuna rai mbili katika hili:

Rai ya kwanza:

Baleghe na kuwa na akili timamu si miongoni mwa masharti ya Zakaah kwani  hii ni haki ya mali na si haki ya kimwili kama zilivyo ibadah nyengine kama Sala na Funga. Hii ni kwa mujibu wa Jamhuur Ulamaa (makubaliano ya wanazuoni) wakiwemo Ash-Shaafi’iy, Maalik na Hanbal kwa dalili ya kauli ya Mtume (Salla Allaahu ’Alayhi Wasallam) kwa Mu’aadh bin Jabal, Allaah (Amuwie radhi), alipomtuma Yemen na kumwambia:

‏(‏أعْلِمْهُم أن اللّه افترض عليهم في أموالهم صدقة تؤخذ من أغنيائهم وترد على فقرائهم‏.‏‏)‏ أخرجه الجماعة

“Waelimishe kwamba Allaah Amewafaradhishia sadaqa katika mali zao huchukuliwa kutoka kwa matajiri na kurudishwa kwa mafakiri” Imetolewa na Jama’ah

Maelezo haya hayakupambanua kati ya mtoto na asiye na akili bali yametaja matajiri tu kwa ujumla bila ya kujali hali zao.

Rai ya Pili:

Abu Haniyfah anaona kwamba si wajibu kwa mtoto na asiye na akili kutoa Zakaah kwani hii ni ibadah na kila ibadah huhitajia nia wakati wa kuitekeleza. Na hawa si Mukallaf hivyo hawana nia.

Rai yenye nguvu na tunayoipendekeza ni rai ya kwanza kwamba Zakaah hutolewa kwa niaba yao kwa wanaowasimamia mambo yao.

 

3       Kumiliki mali yenye kupita kiwango (Nisaab)

Nisaab ni kiwango cha mwanzo kilichowekwa na sheria kinachompa mwenye kutoa Zakaah uwezo wa kuitekeleza nguzo hii. Viwango vinatofautiana kulingana na aina ya mali inayopaswa kutolewa.

Ni wajibu kwa mwenye kutoa Zakaah kuhakikisha kwanza anamiliki mali kikamilifu. Nayo ni kwamba mali hii haifungamani na haki za wengine kama deni, amana, dhamana, wakfu, haijapatikana katika njia za haramu (rushwa, riba, wizi, kughushi na kadhalika)

Mwenye kuimiliki mali anakuwa na uwezo wa kutasarraf na mali yake atakavyo bila ya kujifunga na haki nyengine. Na hili limethibitishwa ndani ya Qur-aan:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo. [At-Tawbah: 103]

Mali ikifikia tu kiwango cha mwanzo, chochote cha ziada huingia katika hesabu yake.

 

4       Iwe Ziada ya mahitaji ya lazima

Mahitaji ya lazima kisheria ni mahitaji yote ya kimsingi kama chakula, mavazi na makaazi. Pia vitendea kazi kama usafiri, mashine, vitabu na kadhalika. Deni linalodaiwa hujumuishwa katika mahitaji ya lazima wakati wa kuangalia kama mali iliyopo inastahiki kutolewa Zakaah. Kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam kama ilivyosimuliwa na Abu Hurayrah, Allaahu amuwie radhi:

ليس على المسلم في عبده ولا فرسه صدقة   روى البخاري ومسلم وغيرهما

Muislamu hapaswi kutoa Zakaah kwa mtumwa wake wala farasi wake. [Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo]

 

5       Imepitiwa na mwaka mzima wa Kiislamu (Hawl)

Hawl ni neno la kitaalamu katika Zakaah likimaanisha kukamilika kwa mwaka wa Kiislamu ikiwa ni mojawapo ya masharti ya kukamilishwa kabla Zakaah kutolewa kwa mali iliyotimia Nisaab. Kinachotakiwa ni mali hii iwe chini ya milki ya mwenye kutoa Zakaah na tayari imeshavuka kiwango cha mwanzo kutolewa kwa mwaka mzima. Mali yoyote ya ziada itakayopatikana ndani ya Hawl itajumuishwa pamoja hata kama iliongezeka ndani ya Hawl.

Endapo mali itapungua chini ya Nisaab basi Hawl yake itaanza pale kiwango cha mwanzo kitakapofikiwa tena.

Tanbihi: Shurti hili halitumiki katika Zakaah ya matunda na nafaka kisheria wakati wa kutolewa kwake ni pale yatakapovunwa bila ya kujali kama yametimia Hawl, kupungua au kupitiza. Kwa mujibu wa aya ya Suuratul-An’aam

وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. [Al-An’aam: 141]

 

Mchoro 1.1

 

Katika mfano huu kiwango kimevuka katika mwezi wa Ramadhaan


(Pauni 3000.00) na ndani ya mwaka kilipungua lakini hakikuvuka chini ya Nisaab (Pauni 2000.00) na mwishoni mwa mwaka kiliongezeka. Kufikia Pauni 6000.00. Zakaah itawajibika kwa mali yote iliyopo mwisho wa mwaka wa Zakaah.

 

Mchoro 1.2

 

 

Katika mfano huu kiwango kimevuka katika mwezi wa Ramadhaan (Pauni 3000.00) kilipungua kidogo na kisha kuongezeka kufikia Pauni 5,000.00 katikati ya Hawl. Na mwishoni mwa mwaka wa Zakaah kikapungua kufikia 4,000.00. Zakaah itawajibika kwa kiwango kilichopo Pauni 4,000.00 mwisho wa mwaka wa Zakaah (Ramadhaan) bila ya kujali ongezeko lililopatikana katikati ya Hawl.

 

Mchoro1.3

 

Katika mfano huu Kiwango kilifikia na kupita katika Ramadhaan kisha mali kupungua chini ya Nisaab Shawwaal na Dhul Hijjah kupanda tena. Ilipofika Safar ikapungua tena chini ya Nisaab na kuanzia hapo ikaanza kupanda tena kupita Nisaab hadi Ramadhaan ya mwaka ujao. Kwa kuwa mali ilipungua chini ya Nisaab, Hawl yake haitoanza Ramadhaan bali itaanzia Rabiy’u Thaani na hivyo kutolewa Zakaah Rabiy’u Thaani ya mwaka utakaofuatia.

(Tanbihi – Hawl haitoanzia Dhul Qa’adah ingawa mali ilivuka Nisaab kwa sababu ilipungua tena ilipofikia Safar)

Ikiwa Zakaah itatolewa kwa mwaka usiokuwa wa kiislamu ni wajibu kwa mwenye kuitoa kuangalia tofauti ya siku katika miaka (Wa Kiislamu ni siku 354 na wa kikristo ni 365) na hivyo kuongeza asilimia kidogo kufidia siku za ziada.

 

UTARATIBU WA KUTOA ZAKAAH

Ikifika wakati wa kutolewa mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:

1       Nia

Ni lazima itakapotolewa iambatanishwe na nia. Nako ni kunuia ndani ya nafsi kuitoa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wata’ala) huku akitaraji thawabu. Pia kuazimia ndani ya moyo kwamba anayoitoa ni Zakaah iliyo wajibu kwa mujibu wa sheria. Nia pahala pake ni moyoni kwani ni moja katika amali za nyoyo.

2       Hutolewa 2.5% (asilimia mbili na nusu ya mali iliyofika au kupita Nisaab)

Hiki ndicho kiwango cha Zakaah kinachotolewa yaani asilimia mbili na nusu ya mali iliyofikia Nisaab. Hii ni robo ya fungu la kumi au 1/40

Kiwango hiki kimepatikana kutokana na ufahamu wa Maulamaa kwa Hadiyth ya Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam) iliyosimuliwa na ‘Aliy bin Abi Twaalib, (Allaah Amuwie radhi),

إذا كانت لك مائتا درهم وحال عليهما الحول ففيها خمسة دراهم وليس عليك شيء حتى يكون لك عشرون ديناراً وحال عليها الحول ففيها نصف دينار فما زاد فبحساب ذلك، وليس في مال زكاة حتى يحول عليه الحول " وهو حسن كما قال الحافظ ابن حجر في بلوغ المرام

Ikiwa una Dirham mia mbili na kupitiwa na mwaka hutolewa Dirham tano na hutopaswa kutoa kitu mpaka uwe na Dinari ishirini na kupitiwa na mwaka na hutolewa nusu Dinari na kitakachozidi huingizwa katika hesabu yake. Na mali ya Zakaah haipaswi kutolewa mpaka ipitilize mwaka (Hawl). Abu Daawuud na Ibn Hajr anasema ni Hasan katika Buluughul Maraam.

Dirham tano inayotolewa katika mia mbili ni 1/40 kama ilivyo nusu Dinari katika Dinari ishirini ambayo ni sawa na robo ya fungu la kumi.

Kama mfano mali inayopaswa kutolewa Zakaah ni £2460.00

£ 2460 × 2.5 = £61.5  

Baadhi ya aina Zakaah huwa na taratibu tofauti kama zilivyo Zakaah ya matunda na nafaka na Zakaah za wanyama.

 

3       Hutolewa mara tu muda wake ukitimia

Ni wajibu kwa kila mwenye kuitekeleza nguzo hii kuhakikisha anaitoa haraka iwezekanavyo pale ikitimia muda wake. Ni haramu kuichelewesha isipokuwa kwa dharura zinazokubalika kisheria. Kisheria baada ya wakati huo mali hii si milki yake na si haki yake kubaki nayo na hivyo kufanya hima katika kujiepusha nayo na kuwapa wenye kustahiki kuimiliki kwa wakati uliowekwa kwa mujibu wa sheria. 

 

TOFAUTI KATI YA ZAKAAH NA SADAQAH

Hizi ni ibadah mbili zinazofanana na pia kutofautiana. Zakaah kilugha ni kuongezeka na kutoharika na Sadaqa linatokana na neno Sidq – Ukweli- kwani mwenye kutoa anathibitisha kikweli kweli imani yake kwa Allaah (Subhaanahu Wata’ala).

 

 

ZAKAAH

SADAQAH

1

Ni ibadah inayomuwajibikia kila mwenye uwezo kutoa na kuwapa wanaostahiki

Ni ibadah isiyolazimishwa na sheria ya kutoa mali kwa ajili ya kujikurubisha kwa mola

2

Ina vitu maalum ambavyo hupaswa kutolewa na kwa utaratibu maalum

Haina vitu maalum wala haina utaratibu wa kutoa

3

Ina masharti ambayo lazima yatimizwe kabla ya kutekelezwa kama kupitiwa na mwaka,kutimia kiwango n.k.

Haina masharti hutolewa wakati wowote na kitu chochote

4

Hupewa watu maalum ambao wametajwa katika Qur-aan

Hupewa waliotajwa na wengineo kwani haikuwekewa masharti katika utoaji wake

5

Mwenye kukataa kutoa huadhibiwa kisheria

Hakuna adhabu isipotolewa

6

Hawapewi wake/waume, wazazi au watoto

Hupewa mtu yeyote

7

Hawapewi wanaojiweza na wenye uwezo

Hupewa

8

Haipaswi kusafirishwa katika mji iliyotolewa isipokuwa kwa dharura. Wanaostahiki ni wanaoishi katika mji/nchi ilipotolewa

Inatolewa sehemu yoyote

9

Ni wajibu kumilikishwa mpewa yaani kukabidhiwa rasmi ili ikamilishe utaratibu

Hupendeza kama ikitolewa kwa siri na si lazima ifikishwe kwa mlengwa ,inaweza kutolewa katika taasisi za kusaidia Waislamu

10

Hupewa Waislamu tu (na katika hali ya nadra kwa wale wanazoezwa nyoyo zao)

Hupewa Waislamu na wasiokuwa Waislamu

 

 

TOFAUTI KATI YA ZAKAAH NA KODI (TAX)

Zakaah na kodi zinaweza kufanana katika baadhi ya vipengele kwani zote zinamuwajibikia kuzitoa kwa wanaohusika. Kodi hutolewa kwa vyombo vya dola wakati Zakaah hupelekwa Baytul Maal kama ipo na kama haipo ni wajibu mwenye kuitoa kuifikisha kwa wanaostahiki. Hata hivyo si kigezo kwamba mwenye kulipa kodi hawajibiki kutoa Zakaah au mwenye kutoa Zakaah si wajibu wake tena kulipa kodi.

Katika baadhi ya nchi za Waislamu kama Malaysia wameweka utaratibu mzuri wa kuchagua kutoa moja katika haya. Kama Muislamu akitoa Zakaah hawajibiki kulipa kodi. Na akilipa kodi na kama ni Muislamu bado wajibu wa kutoa Zakaah uko pale pale ingawa dola haitomlazimisha wala haijaweka sheria ya adhabu dhidi ya asiyetoa.

 

 

ZAKAAH

KODI

1

Ni ibadah na moja katika nguzo za Kiislamu

Ni wajibu wa raia katika kuchangia pato la taifa

2

Viwango vyake vimewekwa na sheria na havibadiliki

Viwango huwekwa na Serikali na vinabadilika kwa kuongezwa, kupunguzwa au kufutwa

3

Ni mafungamano kati ya mja na Mola wake na huwajibika kuitoa hata kama hajaombwa au kutakiwa kufanya hivyo

Ni mafungamano ya mtu na nchi yake na mara nyingi huchukuliwa hata kama mtu hayuko radhi nayo

4

Ina malengo ya kiroho, kimaadili na kiutu kwani ni ibadah na hapo hapo ni aina ya kodi

Ina malengo ya kidunia tu kama kujenga miundo mbinu ya taifa  hospitali, mashule, barabara huduma za jamii na kadhalika

5

Haijali ongezeko la mali katika kutoa kwa na viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria

Huangalia uwezo na mali ya mtoaji kila mali ikiwa nyingi na kodi inakuwa kubwa.

6

Hupewa wanaostahiki kwa mujibu wa sheria

Hutumika katika shughuli za maendeleo ya nchi.

 

Hivyo ni wajibu kwa kila Muislamu aliyekamilisha masharti yote anayopaswa kutoa Zakaah kufanya hivyo kwani Zakaah haitoporomoka au kusamehewa kwa sababu tu ya kutokujua hukumu zake au kwa sababu ya kuihitaji mali kwa malengo mengine. Kwani hata Muislamu akiwa ni mgonjwa lakini ametimiza masharti, bado Zakaah itamuwajibikia.

Pia itampasa mwenye kutoa Zakaah kuhakikisha amekamilisha masharti yote yaliyotajwa. Kukamilisha baadhi tu ya masharti, Zakaah haitokuwa wajibu kwake. Kama aliefikisha Nisaab lakini mali bado kupitiwa na Hawl. Au mali kupita Hawl na kupita Nisaab lakini si milki yake.

 

Inaendelea InshaAllaah…

 

 

 

ZAKA NA SADAKA Najilinda kwa

ZAKA NA SADAKA

Najilinda kwa Mwenyeezi Mungu kutokana na shetani mlaanifu. Naanza kwa jina la Mwenyeezi Mungu mwenye kurahamu na ni mwingi wa kurehemu, amesema:-

“Ametukuka Yule ambae mikononi mwake umo ufalme wote nae ni mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambae ameumba mauti na uhai ili akujaribuni (kwa mitihani) ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi”.
Al-mulk 1-2 .

Mtihani mkubwa kuliko yote aliyotupa Mola wetu ni mali na pesa, ambavyo tunatakiwa tuvitolee zaka na sadaka ili tuwe miongoni mwa waliofaulu, vyenginevyo tutafeli na tutakua ni wenye kula hasara na kujuta baada ya kuondoka duniani. Ametufahamisha Allah Subhaanahu Wataala namna ya kuwafikia wema waliofaulu:-

“Bali wema khasa ni wale wanaomuamini Mwenyeezi Mungu na siku ya mwisho, na malaika, na kitabu (Qur-an), na manabii, na juu ya kua wanazipenda mali zao wanawapa sadaka na zaka jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri walioharibikiwa”. Al-baqrah 177.

Hapo hapo Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu akatufahamisha namna ya kutoa sadaka na ubora wake, kwa kusema:-

“Sadaka iliyobora ni ile unayoitoa wakati una afya yako, unaogopa ufakiri na unataka kuwa tajiri. Usicheleweshe mpaka kifo kimekukaribia, halafu useme hiki na hiki apewe fulani, na hiki apewe fulani”. Imepokelewa na Imam Bukhari.

Na tukafahamishwa hayo hayo tena ndani ya Qur-ani kwa kuambiwa:-

“Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavovipenda. Na chochote mtakachokitoa, basi hakika Mwenyeezi Mungu anakijua”. Aali-imraan 92.

Kwa maana hiyo kila anaetaka kua mwema basi naafanye vitendo vya kheri ili awe miongoni mwa waja wa peponi, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyeezi Mungu:-

“Na kheri yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu, Mtaikuta kwa Mwenyeezi Mungu imekua bora zaidi na ina thawabu kubwa zaidi”. Al-muzzammil 20.

Kile tulichokitoa, kwa hakika hakijapotea bali tumejiwekea akiba ya akhera, ndio maana Mweyeezi Mungu anatuhimiza sana katika kutoa zaka na sadaka, kwani faida tutaiona wenyewe, na wala Mwenyeezi Mungu hanufaiki na tunachokitoa, kwa mujibu wa kauli yake mwenyewe:-

“Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mweneezi Mungu, ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba, na katika kila shuke pana punje mia, na Mwenyeezi Mungu humzidishia amtakae (zaidi kuliko hivi), na Mweyeezi Mungu ni mwenye wasaa mkubwa na ni mweye kujua”. Al-baqrah 261.

Mtume Sallallahu Alayhi Wassallam ametupa mfano wa watu watakaoingia peponi na namna ya malipo yao yatakavyokua kama:-

“Mwanamke mwenye kutoa sadaka chakula cha nyumbani kwake, atapata thawabu kwa chakula hicho, na mumewe atapata thawabu kwa vile amekichuma, na aliekihifadhi pia atapata thawabu. Thawabu za mmoja hazitopungua kwa sababu ya thawabu za mwenziwe”. Imepokelewa na Imam Bukhari.

Mola wetu Mtukufu ametupa siri ya watu wema ili kila anayetaka kuwa mtu wa peponi basi naafanye kama aya hii inavyosema:-

“Na huwalisha chakula masikini, mayatima na wafungwa. Ilhali yakuwa wao wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Nafsini mwao husema) Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyeezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani. Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na tabu. Basi Mwnyeezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na neema na furaha”. Ad-dahr 8-11.

Kwa hakika kutoa zaka na sadaka ni uwamuzi wa yule ambae anataka kheri na baraka zimshukie, kinyume chake ni kujitafutia maapizo ya buree, kwa ushahidi wa kauli ya Mtume Sallallahu Alayhi Wassallam:-

“Kila siku malaika wawili huja duniani, mmoja husema; Yaa Rabbi mpe malipo ya kheri kila anaetumia mali yake kwa ajili yako. Na mwengine husema; Yaa Rabbi muangamize kila bakhili na asietoa”. Imepokelewa na Imam Bukhari.

Inatubidi tufahamu kwamba Mweyeezi Mungu ametupa jukumu la kuwatazama masikini na mayatima, kwa njia yoyote ile mradi iwe ya halali, mradi riziki zao zipo mikonomni mwetu, mfano mzuri ni:-

“Na katika kugawanya mali za urithi wakihudhuria jamaa, yatima na masikini, wapeni kitu katika mali hizo, na waambieni kauli njema”. An-nisaa 8.

Na hii zaka na sadaka sio kama tunawagaia bali ni haki yao ambayo Allah Subhaanau Wataala ameiweka itoke kwetu:-

“Basi mpe jamaa haki yake na masikini na msafiri alieharibikiwa. Hayo ni bora kwa wale wanaotaka radhi za Mwenyeezi Mungu, na hao ndio Watakaofuzu”. Ar-ruum 38.

Yeyote yule ambae hatoi zaka na sadaka basi atakua amemdhulumu masikini na yatima, hata kama hakuombwa au aliombwa, kwa mujibu wa kauli ya Mtume Sallallahu Alayhi Wassallam:-

“Tahadhari na mwenye kudhulumiwa na mwenye kunyanyaswa, kwani dua na maapizo yao, hapana kizuwizi cha kufika kwa Mwenyeezi Mungu”. Imepokelewa na Imam Bukhari.

Kwa maana hiyo adui wa yatima na masikini ni yule anaezuia zaka na sadaka, ndio maana Mwenyeezi Mungu akasema:-

“Je, umemuona Yule anaeikadhibisha dini? Huyo ni Yule anaemsukuma yatima kwa kutokumsaidia. Wala hajihimizi kulisha masikini, wala hahimizi wenziwe (kusaidia masikini na yatima)”. Al-ma’un 1-3.

Hawa wasiotoa zaka na sadaka huwa hawafikirii kuwa Mola wao anaweza kuziondoa mali na pesa walizonazo mara moja halafu wakabaki na matafrani, kama inavosema aya hii:-

“Na (Mwenyeezi Mungu) anapomfanyia mtihani (mja wake) akampunguzia riziki yake, husema Mola wangu amenidhalilisha. Sivyo hivyo, bali nyinyi hamuwatazami mayatima kwa jicho la huruma. Wala hamujihimizi kulisha masikini”. Al-fajr 16-18.

Binaadamu tumeghafilika na kupata kilicho kingi pasina ya kumtazama masikini wala yatima, hatuiyoni hatima yetu wala wala hatujitengenezei akhera yetu, basi inatupasa tuitafakari sura hii:-

“Kumekughafilisheni Kutafuta wingi wa mali na watoto. Hata mumeingia makaburini hamjafanya kheri yoyote. Hasha! kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema mlizopewa mlizitumiaje”. At-takaathur 1,2&8.

Kwa kila ambae anao uwezo wa kutoa zaka na sadaka na akaizuia mikono yake kwa heasabu zake kali alizonazo, basi adhabu kali kali ametayarishiwa:-

“Ambae amekusanya mali na kuzihesabu bila ya kuzitumia kwa njia za kheri. Anadhani kuwa mali yake itambakisha milele? Hasha! Bila ya shaka atavurumishwa katika moto uitwao hutwama”. Al-humazah 2-4.

Kwa mujibu wa Qur-an, kila asietoa zaka na sadaka ni mtu mbaya, na kila aliembaya, bora ajirekebishe leo kabla ya kesho, ili isije ikamkuta aya hii inayosema:-

“Juu ya watu wabaya (waambiwe). Ni kipi kilichokupelekeni motoni? Waseme,hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakiswali. Wala hatukuwa tukilisha masikini. Na tulikua tukizama pamoja na waliokuwa wakizama (katika maasi)”. Al-muddath’thir 41-45.

Zaka imemuwajibikia kila mwenye uwezo, kutoa mbili na nusu katika kila mia moja (2.5%), na kama atatoa zaidi ni bora kwa faida yake mwenyewe. Ama sadaka ni kutoa kwa mujibu wa tartibu zako na uwezo wako, mradi usiache kutoa lakini usijifilisi. Kwa yule ambae atamuweka masikini au yatima ndani ya nyumba yake, na akamtazama kwa jicho la huruma, basi huyu inshaallah ni miongoni mwa minal faaizin, na inshaallah hatokua miongoni mwa wenye kujuta siku ya kiama.

Kumpa kitu masikini na yatima halafu ukamdharau au kumsimbulia, basi jua kwamba huna kheri yoyote utakayoipata kutoka kwa Mola wako, bali unatafuta shari na Mola wako. Masikini na yatima hakuchagua kuwa hivyo bali ni majaaliwa kutoka kwa Allah Subhaanahu Wataala, na kila mwenye uwezo amepewa mtihani mgumu na Allah Subhaanahu Wataala.

Inshaallah atuwafikishe kusikia yaliyo ya kheri, na kuifuata njia ya peponi.
AMIN