Mwenyeezi Mungu Yuko Wapi?
Imekusanywa na
Muhammad Shaykh 'Umar na Muhammad Baawazir
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
I. Dalili kutokana na Qur’an
Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi. Tena akazielekea mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu (2:29) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi (kabla Hajakuumbeni ili mkute kila kitu tayari) tena Akakusudia kuumba mbingu; na Akazifanya mbingu saba Naye ndiye Ajuaye kila kitu. (2:29) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu Aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha Akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazotumika kwa amri Yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni Zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. (7:54) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu Aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha Akatawala juu ya ‘Arshi Yake. Huufunika usiku kwa mchana, uufuatao upesi upesi, (na Huufunika mchana kwa usiku uufuatao upesi upesi). Na (Ameliumba) jua na mwezi na nyota. (Na vyote) vimetiishwa kwa amri Yake (Mwenyezi Mungu viwe vya manufaa makubwa nanyi). Fahamuni: kuumba (ni Kwake tu Mwenyewe Mwenyezi Mungu). Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote. (7:54) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye Ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, na Ametawala kwenye ufalme Wake, Anaendesha mambo yote. Hapana mwombezi ila baada ya idhini Yake. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki? (10:3) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Bila shaka Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye Ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, kisha Akatawala juu ya ‘Arshi (Yake). Yeye ndiye Anayepitisha mambo yote. Hakuna muombezi illa baada ya idhini Yake (Mungu). Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki (kuwa hayo mlio nayo sio mambo ya haki)? (10:3) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Mwenyezi Mungu Aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona, Ametawala kwenye Ufalme wake, na Amefanya jua na mwezi Zimtii, kila kimoja kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na Anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi. (13:2) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Mwenyezi Mungu Aliyeziinua mbingu bila ya nguzo: mnaziona hivi Kisha Akatawala juu ya ‘Arshi (Yake). Na Akalitiisha (kwenu) juu na mwezi (akavifanya vitii). Kila kimoja kinaendelea mpaka muda uliowekwa. Yeye ndiye Anayeliendesha (kila) jambo. Anzipambanua aya hivi ili mupate yakini ya kukutana na Mola wenu. (13:2) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Ar-rahmaan, Mwingi wa Rehema, Aliyetawala juu ya Kiti cha Enzi. (20:5) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Ndiye Mungu Mwenye rehema Aliyetawala juu ya Kiti (Chake) cha Enzi. (20:5) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Ambaye Ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha Akatawala juu ya ‘Arshi, Ar-rahmaan, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari Zake kwa wamjuaye. (25:59) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Ambaye aliziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake; (Ameviumba) katika siku, (nyakati) sita, kisha Akatawala juu ya ‘Arshi (Yake), (na hali ya kuwa ni ) Mungu Mwenye huruma; uliza habari Zake kwa ajuaye. (25:59) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Mwenyezi Mungu ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa siku sita, na Akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki? (32:4) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, katika nyakati sita (anazozijua Mwenyewe Mwenyezi Mungu); na Akatawala katika ‘Arshi Yake. Nyinyi hamna mlinzi wala muombezi isipokuwa Yeye tu, je, hamufikiri? (32:4) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Kisha Akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, Akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni watiifu. (41:11) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Kisha Akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, basi, Akaziambia (mbingu) na ardhi: “Njooni, mkipenda msipende.” Vyote viwili vikasema: “Tumekuja, hali ya kuwa wenye utiifu.” (41:11) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Yeye ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha Akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda. (57:4) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Yeye ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita; kisha Akakaa katika Enzi (Yake). Anayajua yanaoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda humo; Naye Yu pamoja nanyi popote mulipo. Na Mwenyezi Mungu anaona mnayoyatenda (yote) (57:4) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Pale Mwenyezi Mungu Aliposema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua Kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkikhitalifiana. (3:55) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
(Kumbukeni) Mwenyezi Mungu Aliposema: Ewe Isa! Mimi nitakutimizia muda wako wa kuishi (hawatakuua hao maadui). Na Nitakuleta Kwangu, na Nitakutakasa na wale waliokufuru, (hawataweza kukudhuru) na Nitaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Kiama. Kisha marejeo yenu yatakuwa Kwangu, Nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkikhitalifiana. (3:55) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Naye Ndiye Mwenye nguvu juu ya waja Wake, na Ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari zote. (6:18) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Naye ni Mshindaji (amewatawala) waja Wake (wote); Naye ndiye Mwenye hikima (na) Mwenye khabari zote. (6:18) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Vinamkhofu Mola wao Mlezi Aliye juu yao, na vinafanya vinavyoamrishwa. (16:50) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Wanamuogopa Mola wao Aliye juu yao, na wanatenda wanayoamrishwa. (16:50) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda neno zuri, na amali njema Yeye Huitukuza. Na wanaopanga vitimbi vya maovu watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu. (35:10) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Anayetaka ukubwa (naamtii Mwenyezi Mungu) kwani ukubwa wote ni wa Mwenyezi Mungu tu. Kwake hupanda maneno mazuri; na kitendo kizuri huyapandisha (hayo maneno mazuri. Maneno mazuri peke yake hayana maana kubwa). Na wale wanaofanya hila ya maovu, hao watapata adhabu kali. Na hila za hao zitaangamia (zitaondoka patupu). (35:10) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.
Malaika na Roho hupanda kwendea Kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu! (70:3-4) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu mkubwa.
Malaika na Roho hupanda katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu khamsini. (siku moja hiyo ya kuhisabiwa huko Kiyama; kwa vishindo vyake wataiona kama miaka khamsini elfu). (70:3-4) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika! (67:16) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Je! Mnadhani mko salama kwa (Mwenyezi Mungu) Ambaye uko mbiguni (ufalme Wake mkubwa) ya kuwa Yeye hatakudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inataharaki (na nyinyi, inakudidimizeni chini kama walivyodidimizwa hao wa zamani)? (67:16) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye Hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu? (67:17) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Au mnadhani mko salama kwa (Mwenyezi Mungu) Ambaye Yuko mbinguni (ufalme Wake mkubwa), yakuwa yeye hatakuleteeni kimbunga chenye changarawe (zikuangamizeni changarawe hizo)? Mtajua vipi maonyo Yangu. (67:17) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walioamini, na kuwa ni uongofu, na ni bishara kwa Waislamu. (16:102) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Sema: “Roho Takatifu (yaani Jibrili) ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwathubutisha wale walioamini, na kuwa uongofu na khabari njema kwa waliosilimu. (16:102) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Litakase jina la Mola wako Mlezi aliye juu kabisa, (87:1) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Litukuze Jina la Mola wako aliye Mtukufu, (87:1) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Aya hizi zinatubainishia kwa uwazi kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Ndiye Muumba nasi ni viumbe vyake.
Sifa mbili hizi zinatofautiana na hazitangamani pamoja. Kusema Allaah “Yupo kila mahali” kunadharurisha kuwa Muumba na viumbe ni kitu kimoja.
Cha nyongeza na hakika ni kwamba, ayah hizi zinaoonyesha Allaah kuwa ni Mjuzi wa kila jambo na kuwa Yeye Ndiye mwenye kuendesha mambo yote. Yuko juu ya enzi na hili hakulikanusha. Na mfano mzuri ni kuwa, daima utasikia watu wakisema, “Wanamcha Mola wao Aliye juu yao” na wala hawasemi “Wanamcha mola wao Aliye chini yao,” au “Aliyewazunguka,” au “Aliye ndani yao.”
Inatubanikia kwa uwazi kwamba kukaririwa kwa ayah hizi kwenye Qur’an kuwa hili ni jambo muhimu na la kuzingatiwa. Na kwa hakika huu ndio ujumbe waliokuja nao Mitume wote.
Ushahidi wake unapatikana katika ayah zifuatazo:
Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia. Njia za mbinguni ili nikamuone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyopambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. (40:36-37) [Tarjama ya Ali Muhsin Al-Barwani]
Na Firauni akasema: “Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia. Njia za mbinguni ili nikamuone Mungu wa Musa; na kwa yakini ninamjua kuwa ni muongo tu (huyo Musa, lakini nataka kukuonyesheni na nyinyi).” Na hivi ndivyo Firauni alivyopambiwa ubaya wa vitendo vyake na akazuiliwa njia (ya haki); lakini vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. (40:36-37) [Tarjama ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy]
Ukweli wa mambo ni kuwa, ni jambo la kuhuzunisha kuwa kiumbe kiovu kilichowahi kuishi katika dunia hii na juu ya ukafiri wake lakini alikuwa na fahamu ya kisawa sawa kuhusu wapi alipo Mola wetu kuliko baadhi ya waislam katika jamii yetu.
II. Dalili kutokana na Sunnah
1. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Makundi mawili ya Malaika yanakujieni, kundi moja linakujieni usiku na lingine linakujieni wakati wa mchana, yanakutana wakati wa Alfajiri na Alasiri. Kundi lilokesha usiku Larejea juu kwa Allaah na Kisha Allaah Huwauliza na hali kwamba anazo habari kamili, “Ni katika hali gani umemuacha Mja wangu.” Kisha Malaika watajibu, “Tuliwakuta walikuwa wakiswali tulipowaendea na tumewaacha hali ya kuwa wanaswali.” (Humaam bin Munabih katika ‘Sahiyfah as-Saadiqah’ (uk.89), Ahmad katika ‘Musnad yake’, Ibn Khuzaimah katika ‘Kitaab at-Tawhiyd’ (uk.78) ‘Uthmaan Daarimiy katika ‘Radd Alal-Jahmiyyah’ (uk.30))
2. Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) amesema imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu), ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba: Allaah Atasema, “Kwa sababu ya nguvu Zangu, wako wapi wale watu waliokuwa wakipendana, leo Nitawapatia kivuli cha Kiti Changu cha Enzi. Siku ambayo hatopata kuwa na kivuli ispokuwa kivuli Changu.” (Hadithi hii imekuja kwa mapokezi mengi).
Hadithi hii inatuthibitishia kuwepo kwa Kiti cha Enzi na wala si jambo la kimajazi (metaphorical) tu.
3. Imepokewa kutoka kwa ‘Abdullah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kueni marahimu kwa wale walioko juu ya ardhi, ili yule Aliyoko juu mbiguni Awe ni Rahimu kwenu” (Al Bukhaariy na Muslim).
4. Zaynab (Radhiya Allaahu ‘anha), mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa akidai ubora juu ya wenziwe kwa kuwaambia “Ni wazazi wenu waliowatoeni nyinyi muolewe na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) , hali kuwa ni Allaah Ndiye Aliyeniozesha kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka juu ya mbingu saba. (Al Bukhaariy).
5. Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema, “Allaah Ameigawa rehema yake katika sehemu mia moja na Akijibakizia sehemu tisini na tisa na Akaiteremsha chini (ardhini) sehemu moja ya rehema Yake, na kwa sababu ya hiyo sehemu moja, viumbe Vyake vinahurumiana, kiasi kwamba farasi hunyanyua kwato lake kwa kuchelea asimkanyage mwanawe hata akadhurika” (Al Bukhaariy).
6. Amesema Jabir ibn ‘Abdullah, (Radhiya Allaahu ‘anhu) “Mtume wa Mwenyezi Mungu (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika khutba yake siku ya Arafah, “Je nimekufikishieni ujumbe? ‘Wakamjibu ndiyo, ‘Hali ya kuwa akiashiria kidole chake mbinguni kisha akakielekeza kwa Maswahaba, akisema: “Ewe Mola wangu! Kuwa Shahidi.’” [ Muslim]
7. Abu Sa’iyd (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema ya kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Je, hamuniamini hali ya kuwa naaminiwa na aliyeko juu mbinguni? Wahyi unaletwa kwangu usiku na mchana” (Al Bukhaariy na Muslim)
8. Imepokelewa kutoka kwa Abu Musa al-Ash’ariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Allaah Halali na wala Haimpasi kulala. Huiteremsha Qist (uadilifu) na kuipaza juu. Vitendo vya usiku vinapazwa Kwake kabla ya siku. Pazia yake ni nuru, kama akikashifu pazia hiyo, nuru ya uso Wake utaunguza vitu vyote vitakavodhihirikiwa na nuru hiyo” (Muslim).
9. 'Abdullah Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) Amesema: Bwana mmoja kutoka Ansari miongoni mwa Maswahaba wake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinihadithia ya kuwa: Tulipokuwa tumekaa usiku pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilichomoza nuru kali ya nyota iangukayo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Mlikuwa mkisema nini kabla ya Uisilamu kuja wakati mkiona nyota hiyo (kimondo)? Wakajibu: Allaah na Mtume wake ndiyo wajuzi, lakini tulikuwa tukisema usiku wa leo amezaliwa mtu ambaye atakuwa maarufu na mtu maarufu amefariki, hali ya kuwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hizi nyota ziangukazo (vimondo) sio lengo la kuuawa kwa mtu yeyote wala kuzaliwa kwa mtu yeyote. Allaah Mtukufu Aliyetakasika Hutoa amri pindi Atakapoamua kutenda jambo. Kisha Malaika wabebao Kiti Cha Enzi humtukuza, na wale Malaika wa karibu yao katika wakazi wa mbiguni wakimtukuza mpaka kutukuza huko kutawafikia Malaika wa mbingu za ardhi yetu. Kisha wale Malaika walio karibu na wabebaji wa Kiti cha Enzi watawauliza hao wabebaji, amesema nini Mola wenu? Kisha watawapa khabari kama ilivyoelezwa kwao. Kisha wakazi wa mbiguni watatafuta khabari hadi zitafika katika mbingu za duiniani. Katika kupashana habari huku (majini wanategea kusikia khabari yoyote ile), chochote atakachopata kusikia atawapelekea habari hizo marafiki zake. Na pindi Malaika wamuonapo Jini wanawashambulia kwa vimondo. Na wakisimulia watakayobahatika kusikia katika habari za kweli watazichanganya na uongo wao na kujazilia ya ziada ndani ya ukweli huo. (Muslim)
10. Imepokelewa na Salmaan al-Faarisiy (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Amesema: “Mola wenu ni Mkarimu mno na Anaona haya kurudisha patupu pindi mja wake anyanyuapo juu mikono yake. (Abu Dawud).
11.Mu'awiyah as-Sahmi (Radhiya Allaahu ‘anhu) Amesema: “Nilikuwa na kondoo niliomuachia mtumwa wa kike awachunge, baina ya Uhud na Juwaniyyah nikaendea siku moja kuwakagua nikagundua kuwa mmoja ameliwa na mbwa mwitu Mimi ni kama binadamu yeyote yule (ghadhabu ilinishika) nikampiga yule binti. Kisha baadaye nikamuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea kisa hicho. Alinishtusha kwa uzito wa kosa nililofanya, nikamwambia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimuache huru (iwe kama kafara ya dhambi nililotenda)? Akasema, ‘kamuite’. Nilipomuita, alimuuliza, “Yuko wapi Allaah?” Akajibu, juu ya mbingu. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza. “Mimi ni nani?”. Akajibu, ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Basi hapo ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniamrisha nimuache huru mtumwa huyo kwani ni Muumini” (Muslim, Abu Dawud, na wengineo).
Vilevile hadithi hii inaoonyesha kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amethibitisha imani ya kweli kwa binti huyu kwa kujibu maswali haya tu. Hii ni kwa sababu imethibitika pasi na shaka yoyote ya kuwa fikra ya tawhidi ilikuwa ni ya kisawasawa na ni kinyume na tawhidi ya Waarabu kabla ya Uislamu.
III. Dalili kutokana na Swahabah
1. Katika khutba yake mara tu baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Yeyote yule aliyekuwa akimuabudu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mjulisheni ya kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki na yule aliyekuwa akimuabudu Allaah Mjulisheni ya kuwa Allaah Yuko juu za mbingu Ana uzima wa milele, na Hana sifa ya kufa. (Al Bukhaariy).
2. Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) amesema, imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbass (Radhiya Allaahu ‘anhuma), “Kabla ya kuumbwa kitu chochote, Allaah Alikuwa juu ya kiti Chake Cha Enzi. Kisha Akaumba Kalamu na ikaandika kila kitu kitakachotendeka mpaka itakapofika siku ya kiama” (Al Bayhaqiy, ‘Asmaa Was-Swifaat’).
IV. Dalili kutokana na Madhehebu Manne
1. Imamu Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) aliulizwa, ‘Allaah Yuko juu ya mbingu saba, na juu ya kiti Chake Cha Enzi, na Uwezo na Elimu yake ipo kila mahali? Na akajibu, ‘Ndiyo, Yuko juu ya Kiti Cha Enzi Uwezo na Elimu Yake ipo kila mahali’ (‘Sharh Uswuul I'itiqaad Ahlus Sunnah’ ya al-Laalikaiy (T.414AH)).
2. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema: “Allaah Yuko juu ya mbingu, na Elimu Yake imeenea kila mahali, hakuna kinachofichika Kwake.” (‘Sharh Uswuul I'tiqaad Ahlus Sunnah’ ya al-Laalikaiy (T.414AH)).
3. Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) amesema, alipoulizwa juu ya rai yake kuhusu yule asemaye, ‘Sijui kuwa kama Allaah Yuko juu ya mbingu au juu ya ardhi,’- “Amekufuru, kwa sababu Allaah Amesema: “Ar-Rahmaan, Mwingi wa Rehema, Ametawala juu ya Kiti cha Enzi” na Kiti Chake cha Enzi kipo juu ya mbingu zake saba.’ Kisha akaulizwa, ‘Vipi mtu akisema Allaah Yuko juu ya Kiti Chake Cha enzi lakini hajui Kiti Cha Enzi kipo mbinguni au ardhini? Akajibu, atakua amekufuru, kwa sababu atakuwa amekanusha kuwa yupo juu ya mbingu na yeyote yule atakayekanusha kuwepo kwake juu ya mbingu atakuwa amekufuru” (‘Sharh Uswuul I'itiqaad Ahlus Sunnah’ ya al-Laalikaaiy (T.414AH), ‘al-Uluww’ ya adh- Dhahabiy, vilevile ‘Sharh Aqiydah at-Tahaawiyyah’ ya ibn Abi al-Izz al-Hanafiy).
4. Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) amesema: “Na Allaah Aliyetukuka Husifiwa kwa sifa za juu na wala si sifa za chini kwa sababu chini si sifa ya Rububiyah (Uola) wala Uluuhiyah (Uungu) katika chochote kile” (al-Fiqh ul-Asbat).
5. Mwanamke alimuuliza Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) “Yuko wapi Mola unayemuabudu” Kisha akamjibu, “Ama kwa hakika Allaah Aliyetakasika Yuko juu ya mbingu (fis-samaa`), wala si ardhini.” Kisha mtu akasema, ‘Je, umeiona kauli ya Allaah Aliyetakasika “Naye yu pamoja nanyi popote mlipo.”? (57: 4) Akasema, “Yuko na wewe kama vile unavyomuandikia mtu ukisema, “Ama kwa hakika niko pamoja na wewe, hali ya kuwa yule mtu hayuko na wewe” (al-Asmaa was-Swifaat).
6. Na Abu Nu’aym amepokea kutoka kwa Ja’afar Ibn ‘Abdullaah ambaye amesema: ‘Tulikuwa na Maalik Ibn Anas, (Rahimahu Allaah) akaingia mtu, kisha akasema “Ewe Abaa ‘Abdillaah! “Ar-rahmaan, Mwingi wa Rehema, Ametawala juu ya Kiti cha Enzi”. (20:5). Ni vipi kutawala juu huko? Ghadhabu ikamshika Maalik haijawahi kushuhudiwa akatazama ardhini na huku akikwaruza ardhi na fimbo aliyokuwa nayo mkononi, akafuta jasho kwenye bapa lake, akaitupa fimbo ile akasema, Sampuli (kayf) akili ya mwanadamu haiwezi kuifikiria na al-istawaa (kutawala) hakujulikani na ni wajibu kuamini na kuuliza swali juu ya hilo ni uzushi, na akaamrisha huyo bwana aondoke.” Amesema Ibn Hajar katika Fat-hul Baariy (Tafsiri ya Sahih al-Al Bukhaariy 13/406- 407) na isnadi (orodha ya wapokezi) ni hasan (nzuri). Na imesahihishwa na adh-Dhahabiy katika al-Uluww (uk. 103).
Watu wengi wanachanganyikiwa kwa kuwepo madhehebu manne au Wanavyuooni waliotofautiana rai. Ama kwa hakika wanavyouni hawa walitofautiana kwenye masuala ya sheria ya Kiislamu (fiqh). Kwa mfano mwanachuoni mmoja ataitakidi ya kuwa wakati wa kusujudu utangulize magoti kabla ya mikono na mwingine atasema utangulize mikono kabla ya magoti au Mmoja atakuwa na rai ya kuwa mwanamke anaweza kuingia msikitini wakati wa ada yake na mwengine akasema hawezi.
Jambo la kusikitisha watu wengi hudhania madhehebu ya Maimamu wanne hawa wanatofautiana katika masuala ya ‘aqiydah. Kwa mfano Masuala ya kuwa Allaah Yuko wapi, Adhabu ya Kaburi na masuala yote ya ghaibu na kadhalika Maimamu wanne walikuwa na ‘aqiydah sawa sawa. Na wala hapana upenyo wa kuweza kuwepo kwa tofauti katika suala la ‘aqiydah. Ama kwa hakika imenukuliwa mara nyingi ya kuwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikasirishwa na mambo ya watu kujihusisha na ‘aqiydah isiyokuwa sahihi. Imedhihirika wazi kama vile baadhi ya watu walipoomba baraka kutokana na mti (Dhaat Anwaat) au pale mtu alipomwambia, “Kile akitakacho Allaah na wewe”, ndipo Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomkemea kwa kumwambia, “Hivi umenifanya kuwa ni mshirika wa Mwenyezi Mungu?!”
Tukichukua nukta hii hata kama walitofautiana ki-‘aqiydah, ni lazima tutafute ukweli wa jambo lolote lile kutokana na Qur’an na Sunnah, na dalili kwayo haya tumeshatangulia kuyataja humu.
La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye Wewe ndiye muamuzi katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa. (4:65)
V. Dalili Kutokana Na Wanavyuoni
1. Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) amesema: “Yeyote utakayemuuliza, “Yuko wapi Allaah? Jibu la haraka na halisi litakuwa yuko juu mbiguni. Kuna nukta mbili katika hii hadithi, ya kwanza ni Muislamu kuuliza, yuko wapi Allaah? Na ya pili jibu la aliyeulizwa, atasema, “Juu mbinguni.” Yeyote atakayekanusha nukta mbili hizi atakuwa amemkanusha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)” (‘Kitaab al-Uluww’ (Uk.101)).
2. Imaam adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) amepokea kutoka kwa ‘Abdullah ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma), “Allaah Ameviumba vitu vinne kwa mikono yake, Kiti Cha Enzi, Kalamu, Adam na Pepo, viumbe vyote vilivyobakia alisema, “kua” na Vikawa” (Ibn Jariyr katika ‘Tafsiri’ yake (23/185), Ad-Daarimiy kwenye ‘radd Alal Maarisy’ (uk.90), Al-Bayhaaqiy kwenye ‘Asmaa Was-Swifaat’ (uk.233)).
3. Imaam Abu Sa’iyd Uthmaan Ad-Daarimiy (Rahimahu Allaah) Amesema, “Wanavyuoni wote kabla yetu na baada yetu wameafikiana ya kuwa pindi tutakapo msaada kutoka kwa Allaah au tuombapo du’aa, huwa twainua mikono yetu juu na muelekeo wetu twatazama juu. Hatumuombi yeye hali ya kua twatazama chini ardhini, nyuma yetu au mbele yetu, kuliani au kushotoni kwetu. Wote tunadhamiria, na kuelekea juu mbiguni, kwa sababu kila mmoja wetu anajua Allaah yuko juu yetu, kila mtu anayeswali wakati wa kusujudu husema “Sifa zote Anastahiki Allaah Aliyetukuka” (Radd ‘Alal Jahmiyyah’ (uk.20)).
4. Sufyaan Ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu aya isemayo, “Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.” (57:4), Akajibu, ‘Elimu yake’. (Al Bukhaariy, ‘Khalq Af’aal al ‘ibaad’).
5. Muhammad bin Yuusuf (Rahimahu Allaah) amesema, (Mmoja wa waalimu wa Imam Al Bukhaariy) ‘Yeyote asemaye ya kuwa Allaah Hayupo juu ya Kiti Chake Cha Enzi ni kafiri na yeyote anayedhania Allaah Hakuzungumza na Nabii Musa (‘alayhi as-salaam) ni kafiri’. (Al Bukhaariy, ‘Khalq ul Af’aal al ‘ibaad’).
6. Qataada (Rahimahu Allaah) (mwanafunzi maarufu wa Ibn ‘Abbaas radhi ya Mwenyeezi Mungu ziwe kwao) amesema kuhusu usemi wake Mwenyeezi Mungu: “Na ni Allaah Mbinguni na Ardhini” kuwa “Ni yeye pekee Apasa aabudiwe mbinguni na ardhini”. (Al Bukhaariy, ‘Khalq ul Af’aal al ‘ibaad’).
7. Imam ibn Khuzaymah (Rahimahu Allaah) amesema, “Yeyote asiyekubali ya kuwa Allaah Yuko juu ya Arshi yake, juu ya mbingu Zake saba na ametengana na viumbe Vyake, ni kafiri. Mtu huyu ni lazima atubie na akanushe hiyo imani yake la sivyo akatwe kichwa na atupwe kwenye jaa la taka ili Ahlul-Qiblah (Waislamu) na Ahlu dh-Dhimmah (Wasiokuwa Waislamu waishio katika ardhi ya Waislamu) wasije wakaudhiwa na harufu mbaya ya mzoga wa mtu huyo”.
VI. Kutofahamu aya za Qur’an
Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema, “Yeyote atakaye yatazama maneno ya Maimamu mashuhuri wa kisalaf (vizazi vitatu vya kwanza vya Kiislamu) kuhusu suala hili, atakuja kujua ya kuwa walikuwa ni watu wenye maarifa zaidi juu ya suala hili, kutokana na vitabu sahihi na akili isiyo na ghushi. Ataona yote wayasemayo yamethibitishwa kwenye vitabu na akili. Kutokana na hili, waliungana, wala hawakutofautiana, wakawa imara, pasi na kasoro. Wale wapingao Masalafi na Maimamu hawakuufahamu ukweli wa maelezo yao. Hivyo hawakufahamu ukweli wa vitabu na akili, hatimaye wakanza kushika muelekeo tofauti wakaanza kutofautiana kuhusu kitabu, hivyo wakawa wapinzani wa kitabu. Ama kwa hakika Allaah Aliyetakasika Amesema: “Na wale waliokhitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki” (2:176). (Dar-ut Ta'arudhul-Aql wan-Naql (2/301)).
Wakati wowote tunapotafsiri ayah ya Qur’an ni lazima tuangalie aya zingine za Qur’an zimeeleza vipi juu ya ayah hiyo, kisha tutazame Sunnah (Kwani Sunnah ni maneno yanayoelezea Qur’an) kisha tunaangalia Maswahaba, kisha kizazi cha kwanza cha Uislamu tuone namna walivyozifasiri ayah hizi. Tumeteremshiwa Uislam tuufuate, wala sio kuuzulia vitu kama walivyofanya wakristo, sasa tazama uelewaji wa kimakosa kwenye baadhi ya ayah hizi:-
“Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake”. (50:16)
Kwa ayah hii watu wanasema ya kuwa Allaah Yupo kila mahali, vinginevyo Asingekuwa karibu nasi kuliko mshipa wa shingoni. Hili linakanushwa kwa uwazi kama utasoma ayah yote kamili,
“Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayompitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake”. (50:16) Hapa Allaah ((Subhaanahu Wa Ta’ala)) Ameikanusha kutokana na ayah yenyewe ya kuwa ukaribu wake ni wa kielimu.
Aya ifuatayo inafanana,
“Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye Huwa ni wanne wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye Yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama Atawaambia waliyoyatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu”. (58:7)
Ama kwa hakika ayah hii vilevile yataka isomwe kikamilifu:
“Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu Anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye Huwa ni wanne wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama Atawaambia waliyoyatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu”. (58:7)
Inatubainikia kuwa aya hizi si dalili ya kuwa Allaah Yuko kila mahali kwa dhati yake, bali ni dalili ya kinyume na hilo kwa wenye kusema hivyo, kwa sababu aya hizi zaonyesha kwa uwazi ya kuwa ‘Yu pamoja nasi’ kwa elimu Yake.
Aya nyingine itajwayo kama dalili:
”Wa Huwa-Allaahu fis-samawati wa fil-ardh”.
“Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini”. (6:3)
Neno Allaahu lamaanisha, Anayeabudiwa. Kwa hiyo aya inamaanisha yule ambaye Anaabudiwa mbinguni na Anayeabudiwa ardhini. Kwa lugha ya Kiarabu ayah inaanza, “wa Huwa Allaah” ikitumia kiwakilishi ‘Huwa’ (Yeye). Khaswa itakuwa, “Yeye (Huwa) ambaye (al) anabudiwa (llahu) [sifa inayoashiria kiwakilishi Yeye].” Kudai kwamba ayah hii ni dalili ya kuwa Allaah Yupo kila mahali katika viumbe Wake, inatakiwa uifasiri kama ifuatavyo: “Allaah ni Allaah mbinguni na ardhini” ili ilete maana unayoitaka, na hiyo ni sentensi ambayo ni makosa kwani hafasiri hivyo ila mtu mwenye elimu ndogo ya sarufi ya lugha ya kiarabu.
Qataada (Rahimahu Allaah) (mwanafunzi maarufu wa Ibn Abbaas radhi ya Mwenyeezi Mungu ziwe kwao) aliifasiri ayah hii: “Yeye ambaye anaabudiwa mbinguni na ardhini”. Imamu al-Aajurriy pia amesema, “Al-illaah ni anayeabudiwa. Yeye ambaye anaabudiwa mbinguni na anayeabudiwa ardhini.”
Pia ayah hii ni lazima ifahamike kwa kuzitazama ayah nyingine zenye maana sawa:
“Na Yeye Ndiye Mungu mbinguni, na Ndiye Mungu katika ardhi. Naye Ndiye Mwenye hekima, Mwenye ujuzi”. (43:84)
“Na Yeye Ndiye Anayeanzisha uumbaji, kisha Ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi Kwake. Naye Ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.” (30:27)
Vilevile kama zilivyo ayah nyingine, ayah hii ni dalili kinyume na wasemao kuwa Allaah Yupo kila mahali. Aya kamili inasomeka hivi,
“Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na ya nje yenu. Na Anajua mnayoyachuma.” (6:3)
Ayah nyingine ifahamikayo kimakosa ni,
“Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnakoelekea, kuna wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.” (2:115)
Ayah hii ni lazima iangaliwe kwa mnasaba ulioteremshiwa:
Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema, “Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalah za Sunnah (nafl) hali ya kuwa juu ya ngamia, bila kujali anakoelekea, wakati wakitoka Makkah kwenda Madina” Kisha Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) akasoma ayah hii “Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnakoelekea, kuna wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi. (2:115)
Ibn ‘Umar amesema (Radhiya Allaahu ‘anhuma), “Ni juu ya jambo hili Aayah hii iliteremshwa” (Imepokelewa na at-Tirmidhiy, 2883 amesema, hadithi hii ni sahihi hasan).
Mwanachuoni mkuu maarufu Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) ameelezea ayah hii,
"Faaynama tuwalluw fathama wajhu-Llah". (2:115)
kama ifuatavyo:
“Kisha baadhi ya salaf (vizazi vitatu vya kwanza vya Kiislamu) waliifasiri muelekeo (Uso) unamaanisha ‘Qiblah’ cha Mwenyeezi Mungu. Kwa hiyo hii tafsiri inakubalika kwenye ayah hii. Je, hivi ni sawa tukitumia tafsiri hii kwenye ayah zingine zenye kutaja Uso? Ikiwa ni hivyo, basi ni manufaa gani yatapatikana kwenye ayah za Mwenyeezi Mungu zifuatazo:
"Kullu man 'alayha faan. Wayabqaa wajhu Rabbika dhul-Jalaali wal-ikraam" (55:26-27)
Na “Ila-btighaa wajhi Rabbihil-a'alaa.” (92:20)
Na “Innama nutw'imukum liwajhi-Llaahi La nuriydu minkum jaza-aw wala shukuura” (76:9)?
Tafsiri ya sawa kuhusu ayah ya Mwenyeezi Mungu isemayo, “Basi kokote mnakoelekea, kuna wajihi wa Mwenyezi Mungu.” Ni sawa na maelezo ya Allaah katika ayah zote zilizotaja uso. Katika sehemu zote kwenye Qur’an na Sunnah neno Uso litajwapo limenasibishwa na Allaah kwa namna moja na kwa maana moja. Haina maana mbili tofauti zenye kupingana. Lakini kuna dharura katika ayah iliyopo katika Surat Al-Baqarah. Kwenye aya hii, maelezo yake yanaashiria Qiblah (muelekeo) na wala si tafsiri pekee. Inaweza kufasiriwa kuwa Uso wa Allaah kwa dhati yake (haqiyqatan). Na hii kwa sababu aya hii iliteremshwa kwa ajili ya safari. Kwani mtu akiswali na hakuweza kupata kuelekea Qiblah basi popote atakapoelekea atakuwa ameelekea kwa Mola wake. Na Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, ”Mja akisimama kuswali, Allaah huwa Yupo mbele yake” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Hii ni kwa sababu Yuko juu ya viumbe vyake Ametawala juu ya Kiti Chake Cha Enzi na Amevidhibiti viumbe Vyake vyote. Kwa hiyo popote mja atakapoelekea atampata Mola wake.
Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Hakika Allaah Amewaamrisha mswali, na pindi mnaposwali msigeuke [kuangalia kushoto na kulia) kwani Allaah Anauelekeza Uso wake kumuelekea mja wake kwa kadiri ya mja wake asimamapo pasi kutazama kwengineko." (Ahmad na at-Tirmidhiy, Hasan-Sahiyh).
Pia Mtume wa Mwenyeezi Mungu (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Mja akishika wudhuu kikamilifu kisha akasimama kuswali, Allaah Humuelelekezea Uso Wake” (Ibn Maajah, wapokezi wote ni thiqah [wenye kuaaminika]).
Kwa hiyo ni juu ya huyo asemaye kuwa aya hii ina tafsiri tofauti na hiyo hapo juu kutupa ushahidi kutoka kwenye Qura’n na Sunnah.
Aya hizi zifuatazo ni dalili nyingine zinazodhihirisha ya kuwa Allaah Yu pamoja nasi kwa Elimu Yake na wala sio kwa dhati Yake Mwenyewe.
Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na Ninaona. (20:46)
Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi Nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka. (2:186)
Anajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwenye kusamehe. (34:2)
Na Mwenyezi Mungu Amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha Akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala hazai, ila kwa ilimu Yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu. (35:11)
Na ziko Kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye Anajua kilichoko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila Analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha. (6:59)
Anajua vilivyomo katika mbingu na ardhi, na Anajua mnayoyaficha na mnayoyatangaza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliomo vifuani. (64:4)
MWENYEZI MUNGU Amekwishasikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. (58:1)
Ambaye Anakuona unaposimama, Na mageuko yako kati ya wanaosujudu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. (26:218-220)
Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'an, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi. (10:61)
VII. Hatari ya kusema Mwenyeezi Mungu ‘Yupo kila mahali'
Imaam Ahmad ibn Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema: “Allaah Amejisifu kwa yale aliyojinasibisha nayo yeye mwenyewe au Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomsifu kwayo. Hakuna la ziada lapaswa kusemwa baada ya Qur’an na Hadiyth”
Jambo la kwanza la hatari ilo wazi kuhusu suala hili, ni kumpachika Allaah na jambo ambalo sio yeye wala Mtume wake (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemsifu nalo. Hakuna ayah hata moja wala hadiyth isemayo kuwa “Allaah Yupo kila mahali” (fiy kuli makaan). Hakuna hadiyth hata moja Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema Allaah Yuko kila mahali. Mtu awezaje kusema kumhusu Allaah hali hakuna hata chembe ya dalili juu ya hilo?
Ibn 'Abdul-Barr amepokea kutoka kwa Yuunus Ibn 'Abdul-A'laa ambaye amesema ‘Nilimsikia Imaam Ash-Shaafi’i (Rahimahu Allaah) akisema, “Ukimuona mtu akimtajia jina (Allaah) ambalo haliambatani naye, au kitu kisichokua kitu. Ni lazima ushuhudie upotofu wa huyu mtu” (katika Al-Inqitaa' (uk. 79), na Majmu'ul-Fataawaa (6/187).
Na nani dhaalimu zaidi kuliko anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu, na akazikanusha Ishara Zake? Hakika madhaalimu hawafanikiwi. (6:21)
Basi ni nani aliye dhaalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu na Akazikanusha Ishara Zake? Hakika hawafanikiwi wakosefu. (10:17)
Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anayekumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyotangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi Tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uongofu hawakubali kabisa kuongoka. (18:57)
Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu au anayekanusha Haki inapomjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri? (29:68)
Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi Tutajilipiza kwa wakosefu. (32:22)
BASI NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliyemsingizia uongo Mwenyezi Mungu na kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makaazi ya hao makafiri? (39:32)
Kusema ya kuwa Allaah Yuko kila mahali ina madhara yake mbali ya kuukataa ukweli. Kusema Allaah Yupo kila ‘mahali’ kunajuzisha ya kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Yupo ndani ya viumbe vyake. Hii inamaanisha ya kuwa tunatembea ndani ya Allaah, sehemu ya Allaah ipo ndani ya bafu, jaa la taka,ndani ya sanamu na moto wa Jahanam (na'udhubillah)!! Watu kama hawa wasemao haya maneno ndio wanaohalalisha kuabudu asiye mungu na kuabudu makaburi, sababu isemekane ya kuwa wanamuabudu Allaah kwa kuwa Allaah yupo ndani ya miungu isokuwa yeye na makaburi (na'udhubillah)! Huku pia ni kumaanisha hapana tena tofauti kati ya Muumba na viumbe, sababu Allaah Yupo kila mahali, kwa hiyo, viwili hivi vinakuwa sawa!! Na ndiyo sababu hii, Imaam Abu Haniyfah alimkemea vibaya yule mtu aliyesema maneno haya na kumtuhumu kuwa ni kafiri.
Baadhi ya madhehebu potofu wanatumia huja hii kama dalili ya kuwa “mashekhe” wao wanaweza kuabudiwa, sababu wamekuwa “kitu kimoja na Allaah.” Wanasema kuwa Allaah Alikuwa kila mahali. Allaah Alikuwa ndani yao na kwa hiyo walikuwa Allaah (na’udhubillah)!
Baadhi ya watu wanasema kusema Allaah Yupo juu ya Kiti Chake Cha Enzi ni kuweka mpaka juu uwezo Wake. Lakini ukizingatia hili, Allaah Kuwepo juu ya Kiti Chake cha Enzi ni namna pekee ya kutoweza kumuwekea mipaka. Hii ni kwa sababu ukisema “Allaah Yuko kila mahali”, utakuwa unamfungamanisha Allaah na viumbe Vyake.
Watu wengine husema ya kuwa Allaah Aliye juu ya Kiti Chake Cha Enzi ni kimajazi au kiistiari (isti'ara) [metaphorical or allegorical], nayo ni hatari. Sisi Tunachukua maana ya ayah hizi kama zijielezavyo. Wala hatujaribu kuzieleza sifa za Allaah zikoje. Na wala hatuzikanushi, wala hatuzifananishi na viumbe vyake au kuzielezea zikoje.
Allaah Amesema Yuko juu ya Kiti Chake Cha Enzi. Kwa hiyo sisi tunalithibitisha hilo. Hatusemi Ameketi juu ya Kiti Chake Cha Enzi kama akaavyo Mwanadamu kitini - huku kutakuwa ni kumfananisha na viumbe Vyake. Wala hatusemi ya kuwa kuwepo Kwake juu ya Kiti Chake Cha Enzi ni 'majazi' (metaphor) yenye kumaanisha ushindi wake dhidi ya viumbe vyake kama wasemavyo baadhi ya watu. Na kama ingelikuwa hivi, basi viumbe vilikuwa kwenye milki ya nani kabla Allaah?? Wala hatuwezi kukataa kuwepo Kwake juu ya Kiti Chake Cha Enzi, wala hatujaribu kusema kuwepo kwake juu ya Kiti Chake Cha Enzi kunamaanisha jambo lingine.
Na kama tukiifasiri kuwa hiyo si maana yake halisi, huku kutakuwa ni kumtuhumu Allaah ya kuwa ni muongo. Na hata kama hii si dhamiri yetu, lakini ndio hatima yake. Allaah Amesema Yuko Juu ya Kiti Chake Cha Enzi, sisi ni nani wa kulikanusha hilo?
Kwa kusema Allaah Yuko kila mahali ni kuwa watu hawa wanasema maneno ya Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayaendani na akili zao, kwa hiyo ni lazima yawe ni uongo. Labda huu ni ugonjwa ndani ya mioyo yao, kwa sababu wanamfananisha Allaah na viumbe Vyake pindi mtu atajapo ayah hizi, ilhali ya kuwa Allaah Ameshatubainishia Aliposema,
Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. (42:11).
Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah (Rahimahu Allaah) amesema katika Aqiydatul Waasitiyyah, “Na ni katika imani kuwa na imani juu Allaah kwa Alichojielezea nacho mwenyewe katika Kitabu Chake na kile Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichomuelezea nacho, bila ya kuibadilisha maana yake halisi [ya hayo maelezo] (Tahriyf), bila ya kukanusha sifa za Allaah (Ta’atwiyl) bila kuuliza namna Yake halisi (takyiif) na bila ya kufananisha sifa Zake na zile za viumbe Vyake (Tamthiyl).”
Shaykh Swaalih al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) amelezea juu ya hili kwa kusema, “Baada ya mtunzi (Rahimahu Allaah) kutaja kwa ujumla, misingi ya sharia, kuwa na imani ni lazima, anavielezea kwa undani na kufafanua zaidi. Anaanza na msingi wa kwanza nao ni kuwa na imani juu ya Allaah Aliyetukuka. Anasema nguzo hii inajumuisha kuwa na imani kwa sifa Zake Alizojisifu nazo katika Kitabu Chake au kwa yale aliyosifiwa na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Sunnah yake. Hii inaweza kupatikana tu kama tutathibitisha na kutilia mkazo sifa za Allaah kama ilivyokuja kwenye Kitabu Chake na Sunnah kwa kutumia maneno yenyewe na maana ilyokusudiwa, bila ya kubadilisha maneno yaliyotumika katika sifa hizo, kukanusha maana yake, au kufananisha na zile sifa ya viumbe Vyake na kuuliza namna yake halisi. Hili litapatikana tu kama mategemeo yetu yatakuwa kwenye Kitabu na Sunnah. Hatutatumia tafsiri zaidi ya Qur’an na Hadiyth kwani vinazuia (utumikaji usio juu ya vitu viwili hivi kama vile akili na vinginevyo).
Maana ya (tahriyf) ni kuleta mabadiliko au kufanya marekebisho (taghyiir) na pia ni kugeuza kitu kutoka pahala pake pa sawasawa (imaalah). Inasemekana: Ametoka kwenye njia ya sawasawa (inharafa) kwenye jambo fulani pindi atakapoenda nje ya maudhui na akayapa mgongo.
Tahriyf ni za namna mbili:
Namna ya kwanza: Ni kulibadilisha neno. Huku ni kujizuia na (kulikubali) neno kama lilivyo na badala yake kuchukua neno jingine ima kwa kuongeza au kupunguza herufi ya ziada au neno au kwa kubadilisha nukta ya irabu. Mfano ni kama usemi wa wale wapotofu kuhusu kauli ya Allaah:
"Ar-Rahmaanu ‘alal-‘Arshi-stawaa" (20:5)
"Ar-Rahmaan, Mwingi wa Rehema, Ametawala (istawaa) juu ya Kiti cha Enzi". (20:5)
Wanasema: istawalaa, ambayo ina pia maana ya ushindi, hivyo wameongeza herufi ambayo haipo kwenye ayah. Pia kuhusu kauli ya Allaah:
Na akaja (ja-a) Mola wako Mlezi na Malaika safu safu. (89:22)
Wanasema: ‘Amri ya Mola wako’, wakimaanisha amri ya Mola wako ikija. Hivyo hapa wameongeza neno. Pia kwenye usemi wao juu ya Kauli ya Allaah:
"Wa kallama-Llahu Muusa takliyma" (4:164)
"Na Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa kwa maneno". (4:164)
Wamebadilisha nukta ya irabu kwenye neno Allaah, wakalifanya badala ya Allahu kuwa Allaha na kuipa maana isio ya sawa, nayo inaleta maana hii: ‘na Kwa Allaah Musa akazungumza nae moja kwa moja’. Hivyo wamebadilisha nukta ya irabu kutoka dhamma hadi fat-ha ili maana ipate kubadilika.
Namna ya pili: Kubadilisha maana: Hii ina maana ya kujizuia (kukubali) yale (yaliyokwisha thibitishwa na dalili) maana (ya neno lenye kukusudiwa) kama yalivyo, kukataa ukweli wake na kuipa maana inayomaanisha neno jingine. Mfano ni ule usemi wa wazushi: Maana ya neno rehema (rahmah) ni: Haja ya kukidhi hisani na ile maana ya hasira (ghadhab) ni: Haja ya kulipa kisasi.
Maana ya Ta'atwiyl kilugha ni kuacha na kuihama (al-ikhlaa’). Husemwa aliipuzia, aliiacha (‘atwalahu) ikimaanisha kaihama (akhla’ahu). Maana inayokusudiwa hapa ni ukanushaji wa sifa za Allaah, Ametakasika Yeye na upungufu, Mtukufu, Tofauti kati ya tahriyf na ta’atwiyl ni kuwa tahriyf ni kukataa maana iliyo sahihi, iliyokwisha thibitishwa na kunukuliwa (kwenye Kitabu na Sunnah) na kubadilisha maana nyingine iliyo potofu.
Ta’atwiyl ni kule kukataa kilchokwisha thibitishwa na dalili bila kubadilisha maana nyingine, na hii ndio njia ya Mufawwidah. Kwa hiyo yeyote anayebadilisha maana ya neno (Muharrif) pia atakuwa yule ambaye anayekataa maana sahihi iliyothibitishwa na dalili (mu’attwil) lakini yule ambaye anayekataa maana ya neno kama linavyojieleza hatakuwa amebadilisha maana iliyothibitishwa na dalili.
Maana ya (takyiif) ni kufafanua kwa uwazi kwa maana iliyokwisha thibitishwa juu ya sifa. Husemwa: Amekipa kitu umbile au sura (kayyafa) pale aifanyapo kuwa ni sifa ijulikanayo. Kunasibisha takyiif na sifa za Allaah ni kuelezea maumbile makhsusi, hali au sababu na sura au umbile. Jambo hili ni muhali kwa mwanaadamu kwani elimu hii ni kati ya elimu ambazo Allaah Anazozijua Mwenyewe pekee. Hivyo hakuna namna yoyote ile makhsusi ya kufahamu sifa za umbile lake kwa sababu sifa hufuata dhati (dhaat) yake. Kama vile ambavyo si sawa kwa mtu kumjua Allaah kwa dhati Yake mwenyewe.
Udhahiri Wake haujulikani katu. Kwa sababu hii ndio Imaam Maalik pale alipoulizwa kuhusu ayah isemayo:
Ar-Rahmaan, Mwingi wa Rehema, (istawaa) juu ya Kiti cha Enzi. (20:5)
Ni vipi kulingana (istawaa) huko? Akajibu, “Kutawala ni maarufu na namna yake hakujulikani na ni wajibu kuamini na kuuliza swali juu ya hilo ni uzushi.”
Na hivi ndivyo isemwavyo kwenye sifa zote za Allaah.
Maana ya (tamthiyl) ni kufanana (tashbiyh) na inatumika pale isemekanapo ya kuwa sifa za Allaah ni kama sifa za viumbe Vyake. Kwa mfano, mikono ya Allaah ni kama mikono yetu na usikiaji Wake ni kama tusikiavyo. Ametukuka Allaah na sifa hizi. Allaah amesema:
Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. (42:11)
Hivyo hatuwezi kusema ya kuwa sifa za Allaah ni kama zetu au zinafanana na za kwetu. Kama ambavyo hatuwezi kusema Dhati ya Allaah ni kama yetu au inafanana na yetu.
Mwenye kuamini anayempwekesha ni yule anayethibitisha na kukaririsha sifa Zake zote kwa namna ipasavyo na inavyomstahiki Allaah Mwenye Enzi na Utukufu. Mu'attwil hukataa sifa zake zote au baadhi yake na Mushabbih ambaye ni Mumathil (yule ambaye anayefananisha na kushabihisha na viumbe) huzikaririsha sifa kwa namna isiyomstahiki Allaah bali ni kwa namna inayowastahiki viumbe vyake.
Kama kufasiri kimajazi (metaphorical interpretations) ndio kusudio, basi tungeamrishwa na Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tutumie tafsiri ya kama hizo, bali hayakuthubutu katu ndani ya Qur’an wala Sunnah.
Nyongeza, hii inatufungulia mlango kutumia njia hii kufasiri aya zote za Qur’an. Mtu aweza kuja akasema “Unajua zinaa haikukatazwa ni majazi tu inamaanisha jambo jengine!!”
Njia hii ya kutoa hoja inaenda dhidi ya Uislam kuonyesha kuwa si dini ya vitendo na haiendi sambamba na wakati wote pahala popote. Hupelekea watu kudhania Qur‘an imejaa mafumbo, ikimaanisha ni watu wachache tu wenye uwezo wa kuifasiri sawasawa” (mwisho wa kumnukuu Shaykh al-Fawzaan).
Muhammad bin Abdul-‘Aliym Abul-Hammaam wa Jaami’atul-Azhar amesema baada ya kuhutubia suala la kudai ya kuwa istiwaa (Aliyetawala) kunamaanisha istawlaa (Ameshinda):
“…..na kutokana na hatari ya ta’awiyl [ya kuwa, inadharurisha mtazamo wa kuwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wamesema uongo].”
Na Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) anaelezea ya kuwa [ta’awiyl] ni mbaya zaidi kuliko ta’atwiyl ambayo ina “Kanusha sifa za Uungu na kukataa kuthibitisha dhati ya Allaah Aliyetukuka” kwa sababu [ta’atwiyl] inajumuisha vyote; tashbihi na ta’atwiyl, na inachezea na kukadhibisha Kitabu pamoja na kuwa na rai potofu juu yake. Mu’attwil (Mkanushaji wa Sifa) na Mu’awwil (mwenye kugeuza maana) wameshirikiana [baina yao] katika kukanusha uhakika wa Majina na Sifa. Lakini Mu’awwil amepituka mpaka kwa kukadhibisha Kitabu na kuwa na rai potofu juu yake. Na pia kamfungamanisha yule azungumzae nae – ya kuwa azungumza maana yake ya dhahiri na kuwa amepotoka na amewapotosha wenzake.
Hivyo wamechanganya na kujitwesha [kutumbukia] kwenye hatari zifuatazo:-
[1] Imani yao ya kuwa yale yaliyobainika na kudhihiri katika maneno ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni muhali na uongo - hivyo wameelewa ya kuwa ni tashbihi (Wamezipa sifa za ki-binadamu) kutoka mwanzo.
[2] Wamekanusha uhakika wa maana halisi ya kuwa kuzifahamu sifa zake hakuwastahiki wala haimstahiki Mwenyezi Mungu – Aliyetukuka.
[3] Kumnasibisha Mzungumzaji – Aliyekamilika na maarifa na uelezaji (bayaan) na Aliyekamilika katika kutoa uongofu - naye ni Allaah, Aliyetukuka – kinyume cha maelezo (bayaan), uongofu (hudaa) na kutoa muelekeo (irshaad). Huku [kutumia ta’awiyl] kunawapa dharura ya kuwa ni wenye elimu kumshinda, na ufasaha na uwazi [katika maneno] kuliko Yeye na kuwa wao ni bora katika kuwapa wanadamu wenzao muongozo.
[4] Kukejeli maandiko (ya Vitabu na Sunnah) na kuondosha utukufu na heshima ya viwili hivi.
[5] Ya kuwa hii ta’awiyl - kama Allaah Alijitakia – basi Angeamrisha kwenye Kitabu Chake au kwenye ulimi wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha ta’awiyl ya sifa za Allaah – Aliyetukuka - ingekuwa wajibu na sehemu muhimu katika dini yetu - kuiacha kungelikatazwa na yeyote atakayeepukana nayo atapata madhambi. Na hii juu ya kuwa Allaah – Aliyetukuka - Hakutupa ruhusa basi kulifanya itakuwa ni kosa na tabia iliyokatazwa na atalaumiwa mwenye kulitenda - kwani tendo hili linamaanisha [ya kuwa] ni jinsi ya kumkosoa na kumweka sawa Allaah – Aliyetukuka - na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
[6] Huyu Mu’awwil wa sifa za Allaah - kwa kuepuka kwake kumshabihisha (kwa sifa za ki-binadamu) na kuchelea kwake – amekuwa katika wale majaahil wakuu wa uhakika ya kuwa ni muhali kupatikana kwa sifa zenye kufanana kati ya Allaah - Aliyetukuka na zile sifa za viumbe Vyake, kwani hakuna kifananacho katu baina ya sifa za Muumba na viumbe Vyake abadan. Na hili linatokana na kwamba Allaah Ameshatufahamisha ya kuwa Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona, na ya kuwa ni Mpweke (Ahad) na hakuna kinachofanana Naye. Na huyu Mu’awwil [katika kutumia ta’awiyl] anakua muongo (kaadhib) kwani uhakika haufanani kabisa na anachokisema na ni mkanushaji (mukadhdhib) kwa sababu amemkataa Allaah kutokana na Usemi Wake:
Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. (42:11)
[7] Huyu Mu’awil wa sifa za Allaah – Aliyetukuka - kwa kujiepusha kwake na kumshabihisha na kuchelea hilo - tofauti kubwa kati ya sifa za Muumba Mtakatifu Aliye Tukuka - na sifa za viumbe dhaifu wasiojiweza zimefichikana Kwake.
[8] Na ta’awiyl kunafanya maandiko (ya Kitabu na Sunnah) kupoteza umaalumu wake wa kiibada na fahari yake, kwani hii ta’awiyl haijategemea vitabu sahihi vya sharia na wala hakuna hata mwanachuoni mmoja wa kisalafi aliyelizungumzia hilo.
[9] Na vile vile hii ta’awiyl inapingana na hakika ya kuwa dini ya Kiislamu ni ya kimatendo yanayaoendana na kuafikiana sambamba na kila wakati na kila zama. Na vilevile inapingana na Allaah Aliyetukuka - Ameelezea Qur’an ya kuwa ni mahubiri (bayan), na ufafanuzi (tibyaan) kwa kila kitu na ni ukumbusho ulio rahisi - na ndani ya ayah zake mnatakiwa kutafakari na kuzingatia. Na kwa sababu hiyo Abul-Qaasim bin Mandah amesema katika kitabu chake “Ar-radd ‘alal-Jahmiyyah’: ‘kwa watu wa hadiyth – ta’awiyl ni namna upingaji (takdhiyb)” (mwisho wa kumnukuu Abul-Hammaam).
Yeye ndiye Aliyekuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili. (3:7)
Kutumia haya maneno yenye maana ya kimajazi ni kufanya ilhaad (kupindua) majina ya Allaah na hili limekaripiwa sana kwenye Qur’an.
Na Mwenyezi Mungu Ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina Yake.. (7:180)
Imam Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) ameelezea: “Kufanya ilhaad na Majina Ya Allaah kunamaanisha kuyapa mgongo maana sahihi ya Majina Yake ambayo yamekwisha thubutu. Neno Lahd limetokana na ilhaad likimaanisha khitilafu mtu anapojikuta amepotoka na Firqah (Pote). Usemi ‘Mulhid fiyd Diyn’ pia linatokana nalo, ikimaanisha yule ambaye amepotoka na Ukweli na amezua ndani ya Dini vitu ambavyo havina uhusiano wowote ndani yake. Ilhaad kutokana na Majina na ayah za Allaah hupatikana ama kwa kuyakataa kwa ujumla au kuyakanusha maana yake, au Tahriyf (kubadilisha neno au maana) juu ya ukweli wake au kwa kutumia Ta’awiyl (Kugeuza maana) ya kimakosa na kuipotosha maana yake halisi, au inaweza kupatikana kwa kubuni maana ya hayo Majina.
Mafundisho:-
Hapana CHOCHOTE mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. (42:11)
Wala Hana anaye fanana Naye hata mmoja. ( 4:112)
Wa Allaahu A’alam
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


