Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (1)

 

 

 

(Na Prof. Dkt. Shaykh 'Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea

 

Al-Amash Asimulia Jinsi Alivyokutana na Jini

Kumekuwa na utata juu ya maumbile na maisha ya viumbe wenzetu wanaoitwa majini. Watu wengi katika jamii mbalimbali wamekuwa wakisikia habari za viumbe hawa lakini bado uhalisia wao haufahamiki kwa wengi.

Pengine hii ni mada tete kwa mtafiti kuiendea lakini kwa hakika ni mada inayoweza kuvuta hisia za wengi ambao wanataka kujuwa hasa hawa majini ni viumbe gani, wakoje kimaumbile, wanakula chakula gani, je wanazaa watoto, je na wao wanakufa kama binadamu?.... na maswali mengine mengi.

Kama kuna mtafiti ambaye amefanya utafiti wa aina yake basi ni Dk Umar Suleiman al-Ashqar, Profesa wa Shariah katika Chuo Kikuu cha Jordan. Profesa huyu ameandika kitabu chenye kurasa 243 kuhusiyana na Majini.

Lakini jambo la muhimu ni watu kusoma na kuelewa yale aliyoyaandika mtafiti ambayo, kwa kiasi kikubwa, yametokana na ushahidi wa Qur’an na Hadith za Mtume (saw).

Makala haya yanaanza kwa kuwatambulisha wasomaji majina ya Majini:

                            Majina ya Majini kwa Kiarabu

 Kwa mujibu wa wanazuoni wa Masuala ya Lugha ya Kiarabu, kuna aina mbalimbali za Majini:

1.      Iwapo mtu anazungumzia majini tu peke yao basi  

          wanaitwa hivyo hivyo “Majini”.

2.   Iwapo mtu anazungumzia Majini wanaoishi na wanadamu, basi hao wanaitwa “aamar” au kwa jina la wingi “amaar”.

3.   Ikiwa mtu anazungumzia Majini wanaowafanyia uwaduwi vijana, basi hao wanaitwa “arwaah”

4.      Ikiwa mtu anazungumzia Majini wanaowafanyia uwadui wanadamu wote, basi hao wanaitwa Mashetani

5.      Kama wanaleta madhara makubwa na kuwa na nguvu zaidi wanaitwa “afriit”

 

                                                Aina za Majini

Mtume (saw) kasema, “kuna aina tatu za Majini, aina ya kwanza ni yule anayeruka angani, aina ya pili ni mbwa na nyoka, na aina ya tatu ni yule anayekaa kwenye makazi na anayesafiri huku na kule”.

                     Hakuna hoja ya kukanusha kuwepo kwa majini

Wapo watu wachache wanaokanusha kuwepo kwa kiumbe anayeitwa Jini. Baadhi ya washirikina walidai kuwa maana ya jini ni roho za sayari. Baadhi ya wanafalsafa nao wanadai kuwa majini ni nguvu za uwovu katika roho za wanadamu kama ambavyo Malaika ni nguvu za wema katika roho za wanadamu.

Baadhi ya watu wa hivi leo wanadai kuwa majini ni bakteria na vijidudu ambavyo sayansi ya leo imevigunduwa hivi karibuni.

Katika sherehe yake ya Surati al-Jinn ya Qur’an, Muhammad al-Bahi anasema kuwa majini ni Malaika. Kwa mtazamo wake, majini na malaika kiumbe mmoja, hakuna tofauti kati yao. Ushahidi anaoutoa ni kwamba malaika nao pia hawawezi kuonekana kwa macho ya wanadamu.

Kutokuwa na elimu ya kuwajuwa majini si ushahidi wa kutokuwepo kwao

Zaidi wanachoweza kukisema wakanushaji hawa ni kuwa wao hawana elimu inayohusu maisha ya majini. Lakini kutokuwa na elimu hiyo si ushahidi kuwa majini hawapo

                                                      Ukweli wa mambo

Hoja sahihi ni kuwa majini ni aina ya tatu ya viumbe mbali ya malaika na wanadamu. Ni viumbe wenye akili na ufahamu. Si vijidudu wala si nguvu za uovu zinazodhaniwa na wanafalsafa.

Majini ni viumbe wanaowajibika kwa vitendo vyao na wameamrishwa na MwenyeziMungu kufanya baadhi ya mambo na kuzuiwa kufanya mengine. Ushahidi wa hoja hii ya kuwepo kwa majini umetolewa na makundi mbalimbali ya watu.

Katika kitabu chake, Majmul al-Fatawa, Imam Ibn Taymiya anasema: Makundi ya Waislamu hayajahitilafiana juu ya kuwepo kwa majini, na wala hayajatofautina juu ya ukweli kuwa Muhammad (saw) aliletwa kuwa Mtume wa Majini piya.

Na hata watu wa kitabu miongoni mwa Wayahudi na Wakristo pia wanakubali kuwepo kwa majini vile vile kama wanavyoamini Waislamu, ingawaje mtu anaweza kukuta watu miongoni wakikanusha kuwepo kwao, kama ambavyo mtu anaweza kukuta watu miongoni mwa Waislamu wakikanusha kuwepo kwao kama vile Jahamiyya na Mutazila.

Lakini madhehebu mengi na wanazuoni wao wanakubali majini wapo. Hii ni kwa sababu simulizi juu ya maisha ya majini zimekuja kwa njia ya mutawaatir kutoka kwa Mitume jambo ambalo lina elimu yenye ushahidi wa hakika na moja kwa moja.

Ni jambo la hakika kuwa wanaishi, wanafikiri na wanatenda mambo kwa hiyari. Wameamrishwa kufanya mambo fulani na kukatazwa kufanya mambo mengine. Majini si sifa wala khulka za wanadamu au viumbe wengine kama wanavyodai baadhi ya washirikina.

Kwa kuwa suala hili la majini limesimuliwa kwa njia ya mutawaatir kutoka kwa Mitume, wanazuoni na umma unawajuwa na hakuna kundi linalojinasibisha na Mtume linaliweza kuwakana.

Aidha katika ukurasa wa 13, Ibn Taimiya kaandika: makundi yote ya waislamu yanakubali kuwepo kwa majini kama wanavyokubali watu wa kitabu, washirikina miongoni mwa Waarabu na wengine waliotokana na kizazi cha Ham (mtoto wa Nuhu).

            Ushahidi wa Qur’an na Hadith

Kuna aya nyingi za Qur’an na kuna Hadith nyingi zinazothibitisha kuwepo kwa majini. Mathalani MwenyeziMungu anasema katika Qur’an:

   Sema, “imefunuliwa kwangu kuwa kundi moja la majini lilisikiliza Qur’an ........ (72:1)”.

  “Na kwa hakika kulikuwa na wanaume miongoni mwa wanadamu wakijikinga kwa wanaume miongoni mwa majini, kwa wakawazidishia takhlifu... (72:6).”

Kwa kweli kuna aya nyingi za Qur’an zinazowahusu majini ambazo tutazinukuu huko mbele InshaAllah.

                                      Simulizi za kuwaona majini kwa macho

Kuna watu wengi wa zama hizi, hizi zetu na wengine wa zama zilizopita ambao wameona jambo la majini, japokuwa  watu wengi kati yao waliowaona au kuwasikia majini hawakutambuwa kuwa hao waliowaona au kuwasikia walikuwa ni majini.

Huwenda baadhi yao walidhani ilikuwa ni mizuka, mapepo, vivuli, viumbe wa angani na kadhalika. Watu wengi wa kuamika katika zama hizi na zama zilizopita wamusimulia mikasa inayohusu majini

Mwanazuoni mashuhuri wa Hadith, al-Amash kasimulia mkasa huu, “jini lilijitokeza miongoni mwetu. Mimi mwenyewe nikamuuliza, ‘ni chakula gani unachokipenda?’ Akajibu, ‘Wali’. Sisi tukamletea kiasi cha chakula hicho na (kwa macho yangu) nikaona kijiko kikienda juu na chini lakini mwenyewe sikumuona. Nikamuuliza, ‘hivi na nyie mnao watu wa matamanio (na bidaa) kama tulionao sisi?’ Akajibu ‘ndiyo’.

Baada ya kunukuu kisa hicho, Ibn Kathir kaandika hivi: “niliwasilisha isnadi ya kisa hiki kwa mwalimu wetu Imam Abu al-Hajjaj al-Mizi, akasema: ‘hiyo ni isnadi ya hakika kutoka kwa al-Amash.’ Kisha akasema, ‘hata Ibn Asaakiir alinukuu maelezo ya al-Abbas ibn Ahmad al-Dimishqi kwamba kasema, “niliwasikia baadhi ya majini wakighani hivi: “nyoyo hudhikika mpaka zikurubiane na yule zinaempenda na ziko pamoja naye mahali popote pale, Magharibi au Mashariki, zimejawa na mapenzi juu ya allah, na Allah ndiye Mola wao, nazo zinajikurubisha kwa Allah tu na si kwa kiumbe chake. 

Dk Ashqar, mwandishi wa makala haya, anaongeza hapa kusema: “watu wengi wa kuaminika wamenisimulia jinsi walivyosemeshana na majini na wengine kuwaona kabisa. InshaAllah mikasa hii tutaisimulia pale tutakapozungumzi uwezo wa majini wa kujitokeza kwa sura tofauti.’

 

Itaendelea...