Skip navigation.
Home kabah

Bado Mali Haijaisha…Endelea Kuitafuta!

 

 ‘Abdun-Naaswir Hikmany

 

Nafasi ya kumuabudia Mola wetu Mlezi tumeiondosha na kuifanya mali ndio bendera yetu ya iymaan. Hali ya kuwa hiyo mali si kitu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Je, hatuoni namna mali inavyokimbia? ukiipata inakuwa mtihani na kuikosa halikadhalika. Matumizi hayeshi ila wakati unakwisha.

 

Yareti Waislamu wote wangeliitikia wito wa Qawl ya Mola Aliposema: ‘Iqraa’ pamoja na mahimizo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuitafuta elimu, tusingelifikia hali ya kuwa sawa na wendawazimu katika kuitafuta mali. Tuipitie pamoja Hadiyth ifuatayo:

 

Kutokana na Mahmuud bin Lubayd (Radhiya Allaahu ‘Anhu), amesema kwamba, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Mambo mawili binaadamu anayachukia: anachukia mauti na mauti ni kheri kwake kutokana na fitnah, anachukia uchache wa mali, na uchache wa mali ni uchache wa hisabu” (Imepokewa na Ahmad)

 

Tuelewe ya kwamba vyote tunavyovichuma hapa duniani tutaenda kuulizwa mbele ya Muumba, na ndio sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia kuwa uchache wa mali ni uchache wa hisabu. Tukumbuke kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakwenda kutuuliza juu ya kila neema Aliyotupatia kwa Qawl Yake:

 

{{Kisha kwa hakika mtaulizwa Siku hiyo juu ya neema (mlizopewa mlizitumiaje.}} [Suratut-Takaathur: 8]

 

Tunadhani ya kwamba nafsi itakinai mbele ya mali? Na haikuwa nafsi ila ni yenye kuamrisha maovu. Kila kukicha tunaendelea kuwa na uchu wa mali hali ya kuwa hiyo mali haina mwisho abadan! Ni vyema tukaelewa kwamba Allaah Hana haja ya kuangalia wingi wa mali wa mtu wala sura yake. Anachokiangalia ni a’maal ambazo wingi wetu tumeacha kutekeleza. Kama tunategemea mali kuwa ni muokozi wetu hapa duniani, tujiweke tayari na Moto unaoitwa Hut   wamah ambao hakuna miongoni mwetu anayeweza kuuvumilia. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

{{Ambaye amekusanya mali na kuyahisabu (tu bila ya kuyatumia katika njia za kheri). Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele. Hasha! Bila shaka atavurumizwa katika (Moto unaoitwa) Hutwamah.}} [Suratul-Humazah: 2-4]

 

Na ukoje huo moto uitwao Hutwamah? Huo ni moto uliowashwa ukawa mkali usio na mfano wa moto wowote unaoufahamu hapa duniani. Na moto huo utamchoma mtu nje na ndani ya mwili wake ukapita na kuingia hadi kwenye moyo na wakiwa wamefungwa kwa magogo marefu mrefu pasiwe na upenyo wa kutokea.

 

Hakuna masikhara mbele ya Mola Mtukufu, kwani kubwa litaingizwa kwenye mizani na dogo halitatoka. Yote yatakuwa na hisabu yake kamili, wala hakuna ambaye uvumbuzi wake wa teknolojia utayafanya matendo yake yasiwekwe katika Miyzaan. Mali haina mwisho hadi Qiyaama, ila tambua ya kuwa rizki ya kila mmoja imeshaandikwa!