Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (2)



 (Na Prof. Dkt. Sheikh 'Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea



Binadamu Hatuwaoni Majini Lakini Punda, Mbwa Wanawaona.

Wanadamu hatuwaoni majini kwa macho yetu japo tuko nao, tunapishana nao lakini wao wenzetu wanatuona. Wakati sisi wanadamu hatuwaoni majini, baadhi ya  wanyama kama Punda kihongwe na Mbwa wanaofugwa majumbani huwaona Majini.

Katika vitabu vya Hadith vya Musnad Ahmad na Sunan Abu Dawud imenakiliwa Hadith yenye isinadi sahihi kutoka kwa Jabir kwamba Mtume (saw) kasema:

“Mkisikia mlio wa kubweka wa mbwa au mlio wa punda vihongwe wakati wa usiku, basi ombeni ulinzi kwa MwenyeziMungu kujikinga na Shetani kwani wanyama hao huona kile msichokiona nyinyi.”

Kisayansi, jambo hili si geni kwani wanasayansi wengi wamethibitisha kuwa wanyama wanaweza kufanya mambo mengi ambayo wanadamu hawayawezi. Kwa mfano, nyuki huweza kuona mionzi isiyoonekana kwa macho ya binadamu na pia huweza kuliona jua katika mchana uliogubikwa na wingu zito. Na bundi naye huweza kumuona panya usiku wa manane kwenye rundo la makorokoro au magunia ya nafaka yaliyoshonana.

                                              Ibilisi na Jini

Ibilisi ambaye MwenyeziMungu kamtaja mara nyingi ndani ya Qur’an, anatokea katika ulimwengu wa Majini. Mwanzoni alipoumbwa, Ibilisi alikuwa akimuabudu MwenyeziMungu. Katika maisha yake ya awali aliishi pamoja na Malaika mbinguni. Akaingia mpaka Peponi.

Lakini baada ya hapo akamuasi Mungu pale alipokataa kumsujudia Adam kutokana na majivuno, kiburi na husuda. Kwa sababu hiyo, MwenyeziMungu akamfukuzilia mbali kabisa na Rehema Zake.

Kwa lugha ya Kiarabu, Ibilisi ni jina la jumla kwa muasi yeyote aliyetakabari. Jina hili hutumika zaidi kwa yule ibililisi mwenyewe kwa sababu yeye ndiye aliyetakari na kumuasi Mungu. Katika Surati Nisaa ya Qur’an, aya ya 76, Ibilisi katajwa kwa jina la Twaghuuti. Kwa mujibu wa kitabu kiitwacho “Ibilisi” kilichoandikwa na Bw. Aqad, Twaqhuut ndilo jina mashuhuri kwa watu wengi duniani.

Kiumbe huyu aliyeasi kaitwa jina hili kwa sababu amechupa mipaka kwa kumuasi Mungu na kudiriki kujikweza kama mungu wa kuabudiwa. Kiumbe huyu amekata tamaa ya kupata Rehema za MwenyeziMungu ndio maana Mungu kamwita Ibilisi (ibliis).

 Neno Alabalas la Kiarabu maana yake ni yule asiye na kheri kwa nafsi yake. Na neno ublis maana ni aliyekata tamaa na aliyepotea. Wanazuoni wengi wa awali wamesema kuwa kabla ya kumuasi Mungu, kiumbe huyu alikuwa anaitwa azaaziil. Mungu ndiye ajuaye kama hilo ndilo jina sahihi.

                                     Ibilisi ni kiumbe

 Mtu anayesoma Qur’an na Hadith za Mtume (saw), anajua kuwa Ibilisi ni mmoja wa viumbe vya MwenyeziMungu ambaye ana akili, ana uwezo wa kuelewa mambo na kadhalika. Hayuko kama wasemavyo baadhi ya watu wasiomjuwa kuwa ni “nguvu ya uovu inayochukua sura ya silika mbaya katika sehemu ya unyama ya mwanadamu, nguvu ambayo humuongoza mtu pale inapokaa mahali pa silika njema ya roho moyoni mwa mtu huyo.” (Taz. Dairat al-Maarif al-Haditha, uk. 357).

                                     Asili ya Ibilisi

Tayari tumekwishasema kuwa Ibilisi ni jini. Baadhi ya waandishi wa zamani na wa hivi leo wamepinga jambo hili. Wao wanatoa ushahidi wa tamko la Mungu kwa jamii ya Malaika kuwa wamsujudie Adam:

 "Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri" [2:34]

Wanadai kuwa waliotakiwa kusujudu hapa ni malaika kwa sababu jina lililotumika kwa ujumla wao ni “malaikati”, kama kulikuwa na kiumbe mwingine asiyekuwa malaika basi tamko hilo halikumuhusu, kwa hiyo amri ya kusujudu isingemuhusu isipokuwa labda na yeye angetajwa kwa jina lake. Na kama amri ilimuhusu, basi na yeye alikuwa Malaika na huu ndio utaratibu wa kusemeshana.

Katika vitabu vingi vya tafsiri ya Qur’an na vitabu vya historia tunakuta maelezo haya haya kuwa ibilisi alikuwa ni wa jamii ya malaika na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mtunzaji wa Pepo au wa mbingu ya chini kabisa. Alikuwa Malaika bora na wa kuheshimika na kadhalika. Katika sherehe yake ya Qur’an, Ibn Kathir kasema hivi: 

Visa hivi vimepokewa kwa simulizi kutoka kwa wanazuoni wengi wa zamani. Visa vingi kati ya hivyo vimetokana na Hadith za Kiisraliati (ngano za Wayahudi na Wakristo) ambavyo lazima vichunguzwe kwa undani.

MwenyeziMungu tu ndiye Ajuaye usahihi wa simulizi za aina hii. Vingi ni vya uongo uliodhahiri kwani vinapingana na ukweli tulionao mikononi (Qur’an na Hadith za Mtume). Chochote kilichomo ndani ya Qur’an kinajitosheleza na hatuhitaji kutegemea visa hivyo vya watu wa kale.

 Simulizi zao hazikusalimika na mabadiliko, nyongeza na upungufu. Watu hawa wametiya maneno mengi ya uongo katika simulizi zao. Hakukuwa na watu waadilifu miongoni mwao kama wale ilionao jamii ya Waislamu ambao wangeweza kulinda maandiko yao na simulizi zao zisiharibiwe na wakorofi.

 Jamii ya Waislamu imekuwa na wanazuoni, wataalamu, Maimamu, Mahafidhi, na watu wachaMungu wa kuweza kuthibisha vipi kati ya hivyo ni zipi simulizi sahihi, ni zipi za kukubaliwa, ni zipi dhaifu, ni zipi za kutupiliwa mbali, ni zipi za kutunga na za uongo.

 Waislamu walifahamu ni akina nani wazushi na ni nani waliosimulia visa hivyo bila wao wenyewe kujulikana ambao hawapaswi kuaminiwa kabisa. Hii ni kutokana na nafasi ya Mtume Muhammad na kwamba yeye ndiye muhuri wa Mitume na kiongozi wa walimwengu.

 Kwa sababu hiyo, mambo ya kughushi na ya kupotosha hayakuweza kubambikizwa kwake na kukubaliwa na Wanazuoni.

                         

                                                       Inaendelea ......

 

 

Asalaam Alaikum.mimi mohamed

Asalaam Alaikum.mimi mohamed mtambo.je tunaweze kusikiliza haya maelezo ya majini?ombi lingine tuna weza kusikiliza mhadhara wa Mazinge au yeyote yule aina yake?sisi tuliombali na huko tuna mtihani mkubwa na maswali kutoka kwa wagalatia.

Alhidaaya.com Wa 'alaykumus

Alhidaaya.com

Wa 'alaykumus Salaam wa RahamtuLLahi wa Barakaatuh,



Tumepokea maoni yako na tunapenda kukujulisha kwamba unaweza kusikiliza mada hizo kuhusu majini na mashyatwaan katika viungo vifuatavyo:



http://www.alhidaaya.com/swahili/iframe/videos/AbdulLatwiyf.html

 



http://www.alhidaaya.com/swahili/iframe/videos/NaaswirBachu.html



Ama kuhusu mihadhara ya Mazinge hatuweki kwenye tovuti yetu japokuwa ina faida upande mwengine, ila lugha wanayotumia mara nyingi si ya kistaarabu na pia kuna baadhi ya mambo ambayo wanayaunga mkono, huwa hayakubaliani na mafunzo sahihi ya Sunnah ya bwana wetu Mtukufu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Tunasikitika kuwa hatukuweza kutekeleza maombi yako hayo, ila tunaamini kuwa utafaidika na mengi mengine kwenye tovuti yako hii inshaAllaah.

Tunakuombea kheri nyingi na At-Tawfiyq kwenye mambo yako na juhudi zako za kutafuta elimu. Allaah Akuruzuku elimu yenye manufaa na fahamu pana.



Ndugu zako

AL HIDAAYA