Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (3)

 

 

 (Na Prof. Dkt. Sheikh 'Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea

 Je, Majini Huoa Na Kuzaa? Je, Wanaweza Kuoana na Binadamu?

 

 

Kuhusiana na ushahidi wao kuwa MwenyeziMungu alimtowa Ibilisi katika jamii ya Malaika, huu si ushahidi wa hakika. Maelezo hayo yanaweza kuwa ya mkumbo au jumla-jumla tu yaani kwa vile fulani na fulani wameyakubali.

 Katika Qur’an, MwenyeziMungu ameeleza bayana kuwa Ibili alikuwa ni mmoja wa majini.: “Na (kumbukeni) tulipowaambia Malaika, msujudieni Adamu. Basi wakasujudu isipokuwa Ibilisi, yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake...” (18:50)

 Aidha imethibitika katika Hadith sahihi kwamba majini hawafanani na malaika wala binadamu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kasema: "Malaika wameumbwa kwa Nuru, majini wameumbwa kwa moto na Adam aliumbwa kwa udongo.” (Taz.sahih Muslim)

 Al-Hassan al-Basri kasema: Ibilisi hakutokana na malaika hata kwa (nukta ya) kubwenza jicho (hata kidogo). (Taz. Ibn Kathiir, al-bidaaya wa al-Nihaaya Juz. 1, uk.79)

 Naye Ibn Taimiya kasema, “Kwa kweli, Ibilisi alikuwa na haiba ya Malaika alipotoka kwa malaika lakini hakuwa na asili ya malaika na wala hakuwa na umbile sawa na malaika. (Taz. Majmu al-Fatawa, Juz. 4, uk. 235 na 346).

 

                      Je Ibilisi ndiye chimbuko la majini wote?

 Hatuna matini yenye maelezo ya wazi kuwa Ibilisi ndiye mzazi wa majini wote. Rai ya Ibn Taimiya ni kwamba Ibilisi ndiye mzazi wa majini wote kama ambavyo Adamu ni mzazi wa wanadamu wote. (Taz.Majmu al-Fatawa, Juz.4, uk. 235 na 346).

 

                            Chakula na Kinywaji cha Majini

 Majini ambao miongoni mwao wamo mashetani hula na kunywa. Katika Sahihi Bukhari, imenakiliwa Hadith kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alimwambia (yeye Abu huraira) amletee mawe kadhaa ili asitanjie baada ya haja kubwa.

 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamwambia Abu Huraira “usiniletee mifupa au mavumba”. Abu Huraira akamuuliza Mtume kwanini kasema asiletewe vitu hivyo huku akivitaja kwa majina.

 Mtume akamwambia: “hivyo ni vyakula vya majini. Ulinijia ujumbe (wa majini) kutoka Nasiib. Hawa walikuwa ni majini wazuri kabisa ambao waliniuliza kuhusu vyakula vyao. Nikawaombea kwa Allaah kuwa wasiyapite mavumba au wasiipite mifupa ila wakute kitoweo katika vitu hivyo.”

 Na imenakiliwa Hadith yenye isinadi sahihi katika Kitabu cha Sunan at-Tirmithi kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kasema: “msisitanjie mavumba au mifupa kwani hivyo ni vyakula vya ndugu zenu majini”. (Taz. Sahih al-Jaami, Juz. 2, uk. 154).

 Pia katika kitabu cha Hadith cha Sahihi Muslim imenakiliwa Hadith kutoka kwa Ibn Masud kuwa mjumbe mmoja kutoka jamii ya majini alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakaondoka wote. Huko Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akawasomea (majini) baadhi ya Aya za Qur’an. Mtume (aliporejea),  akawaonesha watu mabaki ya vijinga vya moto vya majini hao. Watu wakamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kuhusu chakula chao, naye akawaambia; “Kila mfupa ambao umesomewa jina la Allaah ukiwa  na nyama juu yake ni kwa ajili yenu. Na mavumba ni chakula cha wanyama wenu. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akasema, “msisitanjie vitu hivyo kwani ni vyakula vya ndugu zenu” (majini).

 Aidha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)ametuambia kuwa mashetani wa jamii ya majini hulia mkono wa shoto, na akatutaka sisi tulie mkono tofauti na huo. Katika kitabu chake i cha Hadith mashuhuru kwa jina la Sahih, Bw.Muslim amenakili amenakili Hadith kutoka kwa Ibn Umar kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kasema:

 “Ikiwa mmoja wenu anakula, basi alie mkono wa kulia. Na anapokunywa anywe kwa mkono wa kulia. Kwa hakika, Shetani hula kwa mkono wa kushoto na hunywa kwa mkono huo wa kushoto.”

 Katika kitabu cha Musnad Ahmad, imenakiliwa Hadith ifuatayo:

 “Yeyote anayekula kwa mkono wa kushoto, Shetani hula pamoja naye. Na yeyote anayekunywa kwa mkono wa kushoto, shetani hunywa naye.”

 Hadith ifuatayo pia imenakiliwa katika kitabu hicho Musnad Ahmad:

 “Mtu akilitaja jina la Allaah (Bismillah) pale aingiapo nyumbani mwake na akala chakula humo ndani, Shetani husema, “Hamna pa kulala wala chakula kwangu humu (ndani)’.

 Lakini mtu akiingia nyumbani mwake na kupuuzia kulitaja jina la Allaah pale aingiapo, Shetani husema, “nimepata pa kulala kwako.” Na asipolitaja jina la Allaah (asiposema Bismillah) anapokula chakula, Shetani husema: “nimepata pa kulala na na chakula.”  Hadith hii pia imenakiliwa na Muslim. Hadith hizi zipo katika matini sahihi zikithibitisha kuwa mashetani hula na kunywa.

 Halikadhalika ni haramu kwa binadamu kula nyama yoyote ambayo haikusopmewa jina la Allaah. Mtume wa Allaah kawaruhusu majini walioamini kula mfupa wowote uliosomewa jina la Allaah. Hawaruhusiwi kula nyama isiyosomewa jina la Allaah. Vitu vyote vinavyoliwa bila kutaja jina la Allaah huwapatia chakula majini yasiyoamini ambao ndio mashetani.

 Kwa maneno mengine mashetani hujihalalishia vyakula vyote ambavyo havikusomewa jina la Allaah. Ndiyo maana wanazuoni wengi wakatoa rai kuwa mizoga ya wanyama waliojifia ni chakula cha cha mashetani.

 Akisherehesha Aya hii, “Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi ulevi na kamari na kuabudiwa asiyekuwa MwenyeziMungu na kutazamia kwa mishare ya kupiga ramli ni uchafu na ni kazi ya shetani. Basi jiepusheni ili mpate kufaulu.”(5;90), Ibn Qayyim kasemahivi:

 “vinywaji vya kulevya ni vinywaji vya mashetani. Ulevi ndicho kinywani ambacho shatani huwataka washirika wake wanywe, naye hushiriki nao katika kunywa kinywaji hicho, kuchuma dhambi ya kitendo hicho na hatimaye kuadhibiwa.

 Ni  dhahiri kuwa majini wana maingiliano ya kijinsia. Kuthibitisha hili, baadhi ya wanazuoni hurejea maelezo ya Qur’an kuhusu wanawake wa peponi.  MwenyeziMungu anawazungumzia wanawake hao hivi:

 “watakuwamo humo wanawake watulizao macho yao, hajawagusa, hapo kabla, binadamu wala jini yeyote.” (55:56)

 Mwandishi wa Kitabu kiitwacho Lawaami al-Anwaar al-Bahiya kataja Hadith ambayo isinadi yake inahitaji kutazamwa kwa makini kama ni sahihi au la. Hadith hiyo inasema:

 “Majini wana watoto kama binadamu walivyo na watoto lakini watoto wa majini ni wengi zaidi. Riwaya hii ilisimuliwa na Abu Haatim pamoja na Abu al-Shaikh ikiwa imepokewa kutoka kwa Qataada.”

 *Kwa jinsi riwaya hii inavyorejewa, yaonekana kuwa inatoka katika riwaya za Mursal za Qataada. Riwaya hizi husadikiwa kuwa ni dhaifu ila tu labda zihakikishwe kupitia vyanzo vingine. Yasikitisha kuwa  toleo jipya la Tafsiri ya Ibn Haatim halikuiendea kwa mapana na marefu Surati Rahman (sura ya 55) ili kuihakiki isinadi nzima.

 Baadhi ya watu hudai kuwa majini hawali, hawanywi wala hawajamiiani lakini dai hili halina ukweli kwani tumekwishaonesha ushahidi wa wazi kutoka ndani ya Qur’an na Hadith.

 Baadhi ya wanazuoni wana rai yao kuwa wapo majini wa aina mbalimbali ambao baadhi yao hula au kunywa ilihali wengine hawali wala kunywa. Bw. Wahb ibn Munabih kasema, “wapo majini wa aina mbalimbali. Aina ya kwanza ni jini twaharifu ambalo liko kama upepo, jini huyu hali, hanywi, hafi wala hazai watoto.

 Na ipo jamii nyingine ya majini ambao hula, hunywa, hujamiiana, huzaana na hufa. Na hawa ndio wale mashetani wa kike, mashetani wa jangwani na kadhalika.” Hii ilinakiliwa na Ibn Jarir at Tabari. (Taz. Lawaami al-Anwaar, Juz. 2, uk. 222)

 Lakini hayo aliyoyasema Bw. Wahb nayo pia yanahitaji dalili hivyo hayawezi kuwa ushahidi unaojitehemea.

 Wanazuoni wengi wamedadisi namna majini wanavyokula; je ni sawa na walavyo binadamu, je nao humeza chakula au wao hupitishia chakula  puani na kadhalika? Ni makosa na haiswihi kudadisi mambo haya wala hatuhitajiki kuyajua mambo haya. Hakutujuza mambo haya MwenyeziMungu wala Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).