Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (4)

 

 (Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea

Ndoa Ya Jini Na Binaadamu


WATU wamepata kusikia kuwa mwanaume fulani kaowa Jini au mwanamke fulani kaolewa na Jini au mwanamke fulani kachumbiwa na Jini.  Al-Suyuut kataja mikasa mingi ya aina hiyo iliyosimuliwa na watu wa jamii za awali.

Aidha wanazuoni nao wamebainisha kuwa zipo ndowa baina ya binadamu na majini. Mwanazuoni mashuhuri Ibn Taimiyya kasema, “Binadamu na Majini wamepata kufunga ndowa na kupata watoto. Jambo hili limetokea mara nyingi na linafahamika kabisa.” (Taz. Majmuu Fatawa, Juz. 19, uk. 39)

Izingatiwe kuwa hakuna rejea ya moja kwa moja ya jambo hili. Mtume (saw) hakuwahi kabisa kuzungumzia jambo hili. Simulizi zinazohusu mikasa hiyo kutoka kwa Maulamaa waliokuja katika zama za baadae, haziwezi kusadikika kama dalili za jambo hili.

Isitoshe hailekei kama kuna ushahidi wa kuwepo kwa watoto wenye ubadhi wa sifa za kibinadamu na ubadhi wa sifa za kijini (chotara wa jini na binadamu). Hivi leo katika falme za Kiarabu kuna ukoo unaodai kuwa umetokana na mwanamke wa kijini. Hata hivyo, maumbile ya watu hao hayatofautiani na binadamu wengine. Hivyo, ni vigumu kuthibitisha dai hili.

Hata ikijaaliwa kuwa zipo ndowa hizo lakini wanazuoni wengi wameonesha kutozipendelea. Wanazuoni kama vile al-Hassan, Qataada, al-Hukum na Ishaaq wao wamefahamika kuwa hawakulipendelea jambo hilo.

Imam Malik pamoja na kwamba hakuweza kupata aya ya kuharamisha ndowa hiyo lakini yeye binafsi hakupendelea itokee  na alitoa hoja hii: “sipendelei kwani litakuwa tatizo tukimuona mwanamke mjamzito na kumuuliza, “mume wako nani?” Naye atajibu ‘jini moja hivi.’ Uovu mwingi utatokea kwa jambo hili. (Kwamba wanawake watazini na wakipata mimba, wasingizie majini).

Kundi fulani la watu linatowa rai kuwa hairuhusiwi kuoana na majini. Kwa Rehema Zake, MwenyeziMungu Katuumbia wake wa jinsi yetu ya kibinadamu. Anasema katika Qur’an:

“Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu.” (32:21).

Iwapo kungetokea ndoa hiyo, ingekuwa vigumu kupata utulivu na mapenzi hayo baina ya wanandowa kutokana na tofauti ya jinsi zao. Lengo na hekima ya ndowa haingeweza kufikiwa kwani utulivu na mapenzi yaliyotajwa na MwenyeziMungu hayangewezekana.

Vyovyote iwavyo, ijapokuwa watu wanadai kuwa ndowa hizo zinatokea hata hivi sasa na zimetokea zamani lakini kutokea kwake ni jambo la nadra na ni kioja. Isitoshe mtu anayefunga ndoa hiyo lazima atafute hukumu ya Uislamu kuhusiana na ndoa hiyo. Labda lingekuwa shauri jingine kama yule anayefunga ndowa hiyo, kwa kujitambua, katenzwa nguvu na hana namna ya kuliepuka jambo hilo.

Kinachoipa uwezekano ndoa ya Jini na Binadamu ni kule kutajwa kwa wanawake wa peponi katika Qur’an. MwenyeziMngu Anawaelezea wanawake hao hivi 

“watakuwamo humo wanawake watulizao macho yao; hajawagusa binadamu wala jini yeyote kabla (ya hao waume wao). (55:56).

Aya hiyo inabainisha kuwa viumbe wote wawili Binadamu na Majini  wanastahili kuozwa wanawake hao.

                                            Je mashetani nao hufa?

Hapana shaka kuwa majini na mashetani nao hufa. Aya ifuwatayo ya Qur’an inawahusu wote:

“Kila kilichoko juu (ya ardhi na mbingu) kitatoweka. Inabaki Dhati ya Mola wako Mwenye utukufu na hishima. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha?” (55:26-28).

Katika Sahihi Bukhari imenakiliwa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas kuwa Mtume[Salallahu alaihi wasalam] alikuwa akisema: “najikinga kwa Utukufu Wako ewe Mpweke ambaye hakuna mungu mwingine ila Wewe Mmoja usiyekufa ambapo majini na wanadamu hufa.”

 Kuhusiana na kitambo cha maisha yao, sisi hatujuwi mengi isipokuwa yale aliyotuambia MwenyeziMungu kuhusiana na Ibilisi aliyelaaniwa ambaye amepewa muda na uhai hadi Siku ya Hesabu. MwenyeziMungu Anasema:

Na hakika Tulikuumbeni kisha Tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika” ‘Msujudieni Adamu.” Basi wakasujudu isipokuwa Ibilisi hakuwa miongoni mwa waliosujudu. MwenyeziMungu Akasema: “Nini kilichokuzuiya kumsujudia nilipokuamrisha?’ Akasema, “Mimi ni bora kuliko yeye. (Mimi) umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo”. Akasema (MwenyeziMungu), “Basi shuka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. (Haya) toka; hakika wewe ni miongoni mwa wadhalilifu.” Akasema: “Nipe muda (nisife) mpaka siku watakapofufuliwa viumbe” (MwenyeziMungu) Akasema: “Utakuwa miongoni mwa waliopewa muda.” (7:11-15) 

Kuhusiana na majini au mashetani wengine, hatujuwi muda wao wa kuishi. Ila tunajuwa kuwa muda wao wa kuishi ni mrefu zaidi kuliko ule wa wanadamu

Ushahidi zaidi kuwa viumbe hawa hufa ni kwamba Khaalid ibn Waliid alimuua shetani wa al-uza (mti ambao Waarabu walikuwa wakiuabudiya) na hapo Sahaba huyo akamuua Jini aliyejitokeza kwa sura ya nyoka kama itakavyokuja kuelezwa huko mbele.

 

      Makazi ya majini, mahali na muda wanaoweza kukutikana

Majini wanaishi hapahapa duniani wanapoishi binadamu. Wengi miongoni mwao huweza kukutikana kwenye magofu na maeneo makongwe, na pia hukutikana mahali palipo na najisi nyingi kama vile chooni. Pia wanakutikana kwenye maficho ya bangi, kwenye mazizi ya ngamia na Makaburini.

Ndiyo sababu Mwanazuoni Ibn Taimiyya kasema kuwa wale waliokaribu na Ibilisi mara nyingi hukaa kwenye maeneo hayo. Kuna Hadith zisemazo kuwa mtu asisalie chooni kwa sababu ya najisi iliyomo humo na kwa sababu hayo ni makazi ya shetani na asisalie makaburini kwani jambo hili hupelekea kwenye ushirikina na pia makaburini ni makazi ya Mashetani.

Aidha Mashetani wengi wa kijini wapo kwenye maeneo yenye maasi kama vile sokoni. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alimpa Sahaba mmoja nasaha hizi:

“Ukiweza, basi usiwe mtu wa kwanza kuingia sokoni. Na usiwe mtu wa mwisho kuondoka sokoni. Kwani hayo ni makazi ya Ibilisi na humo ndimo anamosimamisha bendera yake.” Hadith hii imenakiliwa katika Sahih Muslim.

Mashetani pia huishi ndani ya majumba wanayoishi watu. Mtu anaweza kuwazuwia wasiingie ndani ya nyumba au anaweza kuwafukuza ndani kwa kulitaja Jina la MwenyeziMungu (Bismillah), kumdhukuru au kumtaja Allah, kusoma Qur’an hasa hasa “Ayatu Qursiyu ya Surati Baqara (ambayo ni aya ya 255 ya sura hiyo).

Mtume (swalallahu alaihi wasalam] kasema kuwa mashetani huzagaa na kurandaranda kwa wingi pale giza linapoanza kuingia. Kwa sababu hii, amewanasihi Waislamu kuwarudisha ndani watoto wao katika muda huo. Haya yamesemwa katika Hadith iliyonakiliwa na Bukhari na Muslim.

Mashetani huikimbia Adhana na hushindwa kustahamili kuisikiliza. Katika Mwezi wa Ramadhani Mashetani hufungwa minyororo (pingu).

     Mahali wanapopenda kukaa au kukusanyika Mashetani

Mashetani hupendelea kukaa baina ya kivulini na juani (katikati ya kivuli na mwanga wa jua. Kwa sababu hiyo Mtume(swalallahu alaihi wasalam] kawakataza Waislamu kukaa sehemu hizo. Hadith hii sahihi imenakiliwa katika vitabu vya Sunan na vitabu vingine.

                                              Wanyama wa Majini

Katika Hadith ya Ibn Masud iliyonakiliwa katika Sahih Muslim, Majini walimuuliza Mtume (swalallahu alaihi wasalam] kuhusu chakula chao. Akawaambia, “kila mfupa uliosomewa Jina la Allah ni chakula chenu. Muda uleule mfupa utakapofika mikononi mwenu utavikwa nyama. Na kinyesi cha (ngamia) ni chakula cha wanyama wenu.” Hivyo, Mtume (swalallahu alaihi wasalam) katujuza kuwa majini wanao wanyama wao ambao chakula chao ni kinyesi cha wanyama wa binadamu.

Wanyama maalum ambao mashetani huandamana nao

 Mashetani huandamana na wanyama kadha wa kadha kama vile ngamia. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema:

 

 “Kwa hakika ngamia kaumbwa kutokana na mashetani. Na nyuma ya kila ngamia yupo shetani.” (Hadith hii ilinakiliwa na Said ibn Mansuur katika kitabu chake Sunan ikiwa na isinadi ya Mursal hasan. Taz. Sahih al-Jaami, Juz. 2, uk. 25.)

Kwa sababu hiyo, Mtume (swalallahu alaihi wasalam) katukataza kusalia kwenye mazizi ya ngamiya. Imenakiliwa Hadith katika Vitabu vya Musnad Ahmad na Sunan Abu Dawud kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema:

“Msisalie katika mazizi ya ngamia, kwani wanatokana na mashetani. Ila salieni kwenye machungio ya kondoo kwani wana bar-ka”. (Mfasiri hakukuta kauli hizi mbili kwa pamoja katika matini. Bali Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kama alivyonukuliwa katika vitabu vilivyorejewa, aliulizwa swali juu ya kusalia kwenye mazizi ya ngamia na katika machungio ya kondoo na akajibu kila swali kwa nyakati tofauti. Allah ndiye Mjuzi wa yote.)

katika Kitabu chake, Sunan, Ibn Majah kanakili Hadith yenye isinadi sahihi kuwa Mtume kasema:

 “Msisalie mahali wanapopumzikia ngamia (yaani pale waendapo baada ya kunyweshwa maji, kwani wao wameumbwa kutokana na mashetani.” Hadith hii inakanusha madai ya wale wanaosema kuwa sababu ya kukatazwa kusalia kwenye mazizi ya ngamia ni kuwa mkojo na kinyesi chao ni najisi. Ukweli ni kuwa mkojo na kinyesi cha mnyama yeyote yule anayesadikika kuwa ni halali kuliwa hakihesabiwi kuwa ni najisi.

 

Inaendelea ..../5