Mfululizo Wa Mada Ya Majini (5)
(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)
imefasiriwa na Shaibu H.Kifea
Wajihi Wa Shetani unatisha! Ana Pembe!
Shetani ana wajihi wa kuchukiza sana. Hili ni jambo linalokubalika kabisa akilini. MwenyeziMungu Anavifananisha vichwa vya Mashetani na matawi ya Mzaqqum (mti wa Motoni). Anasema:
“Je, karibisho la namna hii silo bora au kupata mti wa zakkum? (Mti mchungu kabisa watakaolishwa watu wa Motoni). Kwa yakini sisi tumeufanya ni adhabu ya madhalimu. Hakika huo ni mti (unaoota) katikati ya Jahanamu. (Panda za) Matunda yake (zinatisha) kama kwamba ni vichwa vya mashetani”. (37:62-65).
Wakristo wa zama za kati walikuwa wakimchora shetani kwa picha ya mtu mweusi mwenye ndevu moja ya mshale, nyusi za wima, mdomo unaotoa miale ya moto, mapembe, kwato na mkiya. (Taz. Dairat al-Maarif al-Haditha, uk. 357).
Shetani ana mapembe mawili
Katika Sahihi Muslim, imenakiliwa Hadith kutoka kwa Ibn Umar kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema: “Msipendelee kusali wakati jua linapochomoza au wakati linapozama. Kwa hakika linachomozea (na kuzamia) katikati ya mapembe mawili ya shetani”. Pia imenakiliwa Hadith katika Bukhari na Muslim kwamba Mtume [Salallahu alaihi wasalam) kasema:
“Iwapo juwa linazama basi acha kusali hadi litoweke kabisa. Na msikawize sala zenu hadi jua linapochomoza au linapozama. Kwani kwa hakika linazamia na kuchomozea katikati ya mapembe mawili ya shetani”.
Hadith hizi zinawarudi washirikina miongoni mwa Waarabu ambao walikuwa na kawaida ya kuliabudia jua na wakawa wanalisujudia pale lilipokuwa linachomoza au kuzama. Kwa sababu hiyo, shetani hujiimarisha katika njia hiyo ili ibada yao ielekee kwake.
Mtume (Salallahu alaihi wasalam) ametukataza kusali nyakati hizo. Kwa kweli, rai sahihi ni kwamba sala, katika nyakati hizo, inaruhusiwa iwapo kuna sababu fulani ya kufanya hivyo, kama vile sala ya kuingilia msikitini. Lakini hairuhusiwi ikiwa hakuna sababu hiyo ya kusali Sala hiyo ya Sunna.
Maana ya maneno haya ya Mtume (Salallahu alaihi wasalam) ni kuwa mtu asikusudie kusali katika nyakati hizo.
Na miongoni mwa riwaya nyingine ambazo zinataja pembe la shetani ni hii ambayo imenakiliwa katika Sahih ya Bukhari: Ibn Umar kasimulia kuwa alimuona Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akinyoosha kidole mashariki na kusema:
“Kwa hakika fitna itakuja kutoka huku, maangamizi yatatokea huku ambako pembe la shetani huchomozea”.
Uwezo na Nguvu za Jini
MwenyeziMungu Amewajaalia majini uwezo na kipawa ambacho Hakuwapa wanadamu. Allah ametufahamisha baadhi ya vipawa vyao ikiwa ni pamoja na kasi ya mwendo.
Mmoja wa majini alimuahidi nabii Suleiman kuwa angeweza kukileta Jerusalem kiti cha Malkia wa Sheba kwa muda mfupi mno hata kabla mtu hajaweza kuinuka mahala alipokaa. Lakini yule aliyepewa ilimu ya Kitabu akasema, “Mimi nitakileta hata kabla hujabwenza jicho”.
MwenyeziMungu amelielezea tukio hili katika aya zifuwatazo:
“Mjasiri mmoja wa majini akasema, Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahali pako hapo na mimi bila shaka ninazo nguvu za hayo (na) ni mwaminifu.” Akasema yule aliyekuwa na ilimu (kwelikweli) ya Kitabu (cha MwenyeziMungu): “Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako (kufumba na kufumbua).” Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, alinena: “hayo ni kwa fadhila za Mola wangu, ili anijaribu nitashukuru au nitakuwa mwizi wa fadhila; Na anayeshukuru, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake, na anayekufuru, kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi (si muhitaji) na Karimu.” (27:39-40).
Majini waliwatangulia wanadamu kwenda angani
Majini walikuwa na kawaida ya kupaa hadi mbingu ya chini kusikilizia kwa wakaazi wa huko (Malaika) kama kuna fununu juu ya mambo yatakayotokea wakati ujao. Pale alipotumwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) na ujumbe wake, ulinzi ukaimarishwa mbinguni. Idadi ya walinzi ikaongezeka.
Katika Qur’an, MwenyeziMungu Anawanukuu majini wakisema:
“Nasi tulizigusa mbingu (tulikwenda mbinguni) tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na nyota (zing’arazo). Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anayetaka kusikiliza atakuta kimondo (kijinga cha moto) kinamvizia.” (72:8-9).
Halikadhalika Mtume (Salallahu alaihi wasalam) naye kaelezea jinsi majini walivyojaribu kuiba aya mbinguni. Abu Huraira kasimulia kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alimwambia hivi: “MwenyeziMungu Anapoamuru jambo mbinguni, malaika hutikingishika mbawa kutii kauli yake.
Wanapoondolewa woga nyoyoni husemezana, “Mola wenu kasemaje?” na hupata jibu kuwa alichokisema ni haki, Naye ndiye Aliye juu na Mkuu’. Hapo ndipo wale wanaosikiliza kwa wizi (Majini) nao husikia kauli hii.
Wao wanakuwa hivi: baadhi yao huwa juu ya wengine. Kisha yule anayesikia neno hulipeleka kwa wa chini yake, naye hulipeleka kwa wa chini yake na inakuwa hivyo hivyo hadi pale mmoja wao atakapolipitisha mdomoni mwa mtabiri au mwaguzi.
Mara nyingi kimondo huwa kinampata huyu kabla ya kulifikisha neno hilo (kwa mtabiri) ambaye naye hulichanganya na maneno mia ya uwongo. Hapo watu huuliza, “jamani, fulani si aliwahi kusema neno fulani tarehe fulani (si aliwahi kutabiri)? Mtabiri huyu huaminika kwa sababu ya neno hilo lililosikiwa (na majini) mbinguni”. (Imenakiliwa na Bukhari katika Sahih).
Imani za ushirikina katika zama za ujahili
Kwa kuijuwa sababu kwa majini walipopolewa na vimwondo, ikakomeshwa ile imani ya kishirikina waliyokuwa wakiieneza watu wa zama za ujahili. Ibn Abbas kasimulia Hadith iliyotoka kwa sahaba wa Mtume (saw) miongoni mwa Ansar ambaye kasema kuwa usiku mmoja walikuwa pamoja na Mtume (Salallahu alaihi wasalam) na wakaona nyota ya kimondo.
Mtume akawauliza, “mlikuwa mkisemaje kuhusiana na nyota ya kimwondo kama ile katika zama za ujahili?” Wakasema, “MwenyeziMungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi. Tulikuwa tukisema kuwa usiku huo (wa nyota ya kimwondo) huzaliwa mtu muhimu au hufa mtu muhimu.
Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akasema “(nyota hiyo ya kimondo) haitokei kwa sababu ya kufa na kuzaliwa kwa mtu yeyote yule. Bali MwenyeziMungu Anapoamua jambo, Malaika wanaobeba Kiti cha Enzi huimba kumtukuza kwa Sifa Zake na wale wa mbingu inayofuata nao hufanya hivyo hivyo na wengine halikadhalika hufanya hivyo hivyo hadi mbingu ya chini kabisa.
Kisha wale walio karibu na malaika wanaobeba Kiti cha Enzi huwauliza hao wanaobeba Kiti hicho, “kasema nini Mola wenu?” Hapo huambiwa kile ambacho ameamrisha MwenyeziMungu.
Kisha na wao hupeleka habari hiyo mbingu inayofuata na mlolongo huwa hivyo hivyo hadi habari hiyo ifike mbingu ya chini kabisa. Hapo sasa majini nao huisikiliza na kuipeleka kwa watumwa wao. Malaika wanapowafuma, huwashambulia kwa vimondo.
Laiti Majini wangelikuwa wanasimulia vile vile habari nzima waliyoisikia, basi wangelikuwa wakweli. Lakini, kinyume chake, wao huichanganya na kuitia chumvi. (Hadith imenakiliwa katika Sahih Muslim)
Majini wana ujuzi wa kujenga majengo na wanajua ufundi mwingine
MwenyeziMungu Ametufahamisha kuwa majini waliokuwa wametiishwa katika ufalme wa Suleiman walifanya mambo mengi ya ajabu ambayo ni uthibitisho wa uwezo wao wa kimwili, akili na maarifa yao. Katika Qur’an, MwenyeziMungu Anasema:
“Na katika majini (kulikuwa na wale) waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na kila anayejitenga na amri Yetu miongoni mwao Tunamuonjesha adhabu ya Moto uwakao. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama ngome na masanamu na mabunguu (madaste) makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa sana yasiyoondolewa mahala pake (34:12-13)
Huenda majini pia walikuwa na mawasiliano ya masafa na masafa mithili ya Radio na Televisheni. Ibn Taymia kaeleza kuwa, mmoja wa Masheikh waliopata kuwasiliana na majini alimfahamisha kuwa majini waliwaonesha wao kitu kilichokuwa kinameta-meta kama maji au kioo. Na ndani ya chombo hicho waliwaonesha kila walichokitaka kuhusiana na habari.
Mtu aliyemsimulia jambo hili Ibn Taimiya kasema kuwa majini hao wakaweza kuyaleta maelezo ya yule aliyekuwa anaomba msaada wangu, nami nikamjibu ambapo maelezo yangu wakayanasa kuyarejesha kwake.” (Taz. Majmu Fatawa, Juz. 11, uk. 309)
Pengine-labda majini waliweza kuvumbua teknolojia ya Radio na Televisheni muda mrefu huko nyuma.
Uwezo wao wa kujitokeza kwa maumbile mbalimbali
Majini wana uwezo wa kujitokeza kwa maumbile ya wanadamu au wanyama. Katika Vita ya Badri, shetani wa kijini aliwatokea washirikina kwa umbile la Suraaqa ibn Malik na kuwaahidi msaada na ushindi katika vita hiyo.
MwenyeziMungu aliteremsha wahayi kuhusiana na tukio hili:
“Na (kumbukeni) Shetani alipowapambia vitendo vyao na kusema: “Leo hakuna watu wa kukushindeni na mimi ni mlinzi wenu,” (8:48).
Lakini pale majeshi yalipokutana na yeye shetani kuona malaika wakiteremka kutoka mbinguni, akatimua mbio. Aya hiyo inaendelea: “Lakini yalipoonana (yalipokutana) majeshi mawili, (Shetani) alirudi nyuma na kusema: “Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msioyaona nyinyi, mimi ninamuogopa MwenyezziMungu; na MwenyeziMungu ni Mkali wa kuadhibu.”
Inaendelea …./6
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
