Mfululizo Wa Mada Ya Majini (6)
(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)
imefasiriwa na Shaibu H.Kifea
Jini huweza kujitokea kwa maumbile mbali mbali
Abu Huraira kasimulia mkasa ufuatao ambao umenakiliwa katika Sahihi Bukhar na vitabu vingine. Swahaba huyu kasema kuwa Mtume (swalallahu alaihi wasalam) aliwahi kumpa kazi ya kusimamia usalama wa mali ya zaka iliyotolewa katika mwezi wa Ramadhani.
Kwa maneno yake Abu Huraira anasimulia, “akanijia mtu mmoja na kuanza kuchukua mafungu ya chakula. Mimi nikamkamata na kumwambia kuwa nitampeleka kwa Mtume wa Allah. Mtu huyo akalalama, “Nina dhiki kubwa na nina watoto wanaonitegemea.”
Kwa kutoa sababu hii, basi mimi nikamwachia aende zake. Asubuhi ya kesho yake Mtume (swalallahu alaihi wasalam) akaniuliza, “vipi yule mtu uliyemkamata usiku Abu Huraira?” Mimi nikajibu, ‘Ewe Mtume wa Allah mtu yule alinililia kwa dhiki kubwa aliyonayo na kwa watoto wanaomtegemea, kwa hiyo nikamuonea huruma na kumwacha aende zake.’
Mtume (swalallahu alaihi wasalam) akasema, “kakudanganya huyo na atarudi tena.’ Kwa hiyo nikajuwa tu mtu huyo atarudi maadam Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema hivyo. Nikakaa kumsubiri. Alipokuja, akaanza tena kusombelea mizigo ya chakula.
Nikamkamata tena na kumwambia kuwa nakupeleka kwa Mtume. Lakini aliponisihi, “niachie niende, nina dhiki na watoto wanaonitegemea mie’, nikamuonea tena huruma. Asubuhi Mtume (saw) akaniuliza tena, ‘Abu Huraira vipi yule mtu wako uliyemkamata usiku?’
Nikajibu, ‘ewe Mtume wa Allah, kanilalamikia juu ya dhiki kubwa aliyonayo na watoto wanaomtegemea, nami nikamuachia tena aende zake.’ Mtume (swalallahu alaihi wasalam) akasema, “kakudanganya huyo na atarudi tena’. Kwa mara nyingine tena nikamsubiria na akaja na kuanza kusomba mizigo ya chakula.
Sasa nikamwambia ‘bwana wee, safari hii nakupeleka kabisa kwa Mtume wa Allah. Hii ni mara ya tatu sasa unatenda kitendo hiki.’ Akaniambia, ‘ukiniachia niende, nitakufunza maneno ambayo Mungu atakunufaisha sana kwayo! “Upandapo kitandani mwako kulala, soma Ayatu Qursiyu kuanzia pale, ‘MwenyeiMungu, hakuna mola ila Yeye Mwenye uhai wa Milele’ hadi mwisho wa aya.
Ukifanya hivi, atakujia mlinzi kutoka kwa Allah kukukinga na mashetani mpaka asubuhi.’ Basi mimi tena nikaamua nimuache tu mtu huyo aende zake. Asubuhi Mtume akaniuliza kwa mara nyingine tena, ‘’vipi yule mtu wako uliyemkamata usiku?’
Mimi nikajibu, ‘alijidai kunifunza maneno ambayo yangeninufaisha mno”. Mtume (swalallahu alaihi wasalam) akasema, ‘kasema kweli ingawaje ni muongo. Je wewe unamjua mtu yule ambaye umekuwa ukiongea naye nyakati za usiku mara tatu?’
Mimi nikajibu, hapana. Mtume (swalallahu alaihi wasalam] akasema, “alikuwa shetani yule”. Kwa hadith hii, ni dhahiri kuwa shetani huyu wa kijini alijitokeza kwa umbile la kibinadamu.
Majini pia huweza kujitokeza kwa umbile la wanyama kadha wa kadha, mathalani ngamia, punda kihongwe, ng’ombe, mbwa au paka. Lakini hasa hasa, majini hujitokeza kwa umbile la mbwa mweusi.
Mtume (swalallahu alaihi wasalam] kasema kuwa mbwa mweusi alipata kuingilia kati sala yake na akaeleza kuwa mbwa huyo alikuwa ni shetani. Mwanazuoni wa kuaminika Ibn Taimiya naye kasema, “mbwa mweusi ndiye shetani wa mbwa.
Na mara nyingi majini hujitokeza kwa umbile lake. Vile vile majini hujitokeza kwa umbile la paka mweusi (hata hivyo hakuna ushahidi wa Qur’an au Hadith kuwa ni sahihi kusema kuwa majini hujitokeza kwa umbile la paka mweusi. Kauli kama hizi huhitaji kuthibitishwa kwa dailili zilizosahihi).
Rangi nyeusi ndiyo yenye nguvu mno kwa mashetani kushinda rangi nyinginezo, ndani yake kuna nishati ya joto-joto”
Majini ndani ya majumba ya wanadamu
Majini hujitokeza kwa maumbile ya nyoka machoni mwa wanadamu. Ndiyo sababu Mtume (swalallahu alaihi wasalam) amekataza uuwaji holela wa nyoka wanaoonekana ndani ya majumba kwa sababu ya kuchelea kwamba wanaweza kuwa majini waliosilimu.
Katika Sahih bukhari imenakiliwa Hadith kutoka kwa Abu Sa’id al-Khudhri kuwa Mtume (swalallahu alaihi wasalam) kasema, “jamii moja ya majini imesilimu mjini Madina. Kwa hiyo yeyote amuonaye mmoja wa majini hao, ampe tahadhari mara tatu. Kama atajitokeza tena baada ya hapo, basi auwawe kwani huyo lazima atakuwa ni shetani.”
Swahaba mmoja wa Mtume (swalallahu alaihi wasalam] aliua nyoka mmoja nyumbani mwake ambapo kitendo hiki kikamletea maafa. Katika kitabu chake, Sahih, Muslim amenakili Hadith kuwa Abu al-Saib alikwenda nyumbani kwa Abu Saiid ambako alimkuta anaswali. Akaa kumsubiri amalize kuswali.
Mara akasikia chakara-chakara kwenye rundo la kuni ambazo zilikuwa pembezoni mwa nyumba. Alipotazama, akaona nyoka. Ilikuwa bado kidogo tu amuue nyoka huyo pale Abu Said alipomuashiria akae chini.
Baada ya kumaliza kuswali, Abu Said akakinyooshea kidole chumba kimoja na kusema, ‘unakiona chumba hiki?’ al-Saib akajibu, ‘ndiyo’. Abu Saiid akasema, “basi aliwahi kuwepo mtu mmoja ambaye alikuwa kwenye fungate la harusi, mtu huyu tukaenda kushiriki naye katika vita vya Handaki tukiwa pamoja na Mtume (swalallahu alaihi wasalam]
Bwana huyu alikuwa na kawaida ya kumuomba ruhusa Mtume[swalallahu alaihi wasalam] kwenda kumuona mkewe. akamuhadharisha kuwa aende huko na silaha zake kwani alikuwa akichelea (mashambuzi) ya BanuQuraidha (kutokea upande wa nyuma)
Basi bwana huyo akabeba silaha zake na aliporejea kwa mkewe, akamkuta amesimama baina ya milango miwili ya nyumba. Bwana huyo akapandwa na ghadhabu za wivu na akamjeruhi mkewe kwa mkuki wake.
Mkewe akamwambia aweke kando mishale na kisha aingie ndani aone mwenyewe kile kilichomfanya yeye atoke nje ya nyumba. Bwana huyo akaingia ndani na kukuta bonge la joka kitandani.
Akalichoma mkuki na kulitoboa. Alikikilisana nalo kulitoa nje lakini joka hilo lilikuwa na nguvu kubwa na kumuuma bwana huyo. Hakuna mtu aliyejua ni nani aliyeanza kufa kutokana na purukushani hiyo ya mtu na nyoka.
Watu wakamsimulia Mtume (swalallahu alaihi wasalam] mkasa huu na kumuomba amuombe MwenyeziMungu amuhuishe mtu huyo. Lakini akasema, “Muombeeni maghfira mwenzetu. Hapa Madina kuna majini ambao wamesilimu. Yeyote kati yenu akimuona mmoja wao (ambaye ni nyoka) basi ampe tahadhari ya siku tatu. Ikiwa atatokea tena baada ya hapo basi auwawe kwa sababu ni shetani huyo.”
Mambo ya kuzingatia hapa
1. Kanuni hii inayokataza uuaji wa wanyama inahusu nyoka tu na si wanyama wengine.
2. Kanuni hii haijuzu kwa kila nyoka isipokuwa wale tu wanaokutwa ndani ya nyumba. Wale wanaokuwa nje wanaweza kuuliwa.
3. Iwapo mtu atamuona nyoka ndani ya nyumba amsihi kwa maneno sawa na haya, “Nakupia kwa jina la Allah uondoke nyumba hii na uipeleke shari yako mbali nasisi, usipofanya hivyo, tutakuua.” Iwapo utamuona tena nyoka huyo baada ya siku tatu, muuwe.
4. Sababu ya nyoka kuuliwa baada ya siku tatu ni hatua ya tahadhari ili kuhakikisha kuwa mtu hamuuwi jini ambaye amesilimu. Kama ni jini huyo basi ataondoka katika nyumba hiyo. Na asipoondoka basi auliwe, kwani, kwa hali hiyo, huyo ni jini-asi ambaye anastahili kuuliwa kutokana na madhara anayoweza kuyaleta kwa wakaazi wa nyumba hiyo.
5. Kuna aina moja ya nyoka waonekanao majumbani ambao, ruhusa maalum imetolewa kuwauwa bila kuwasihi waondoke. Katika Sahihi Bukhari, imenakiliwa Hadith kutoka kwa abu Lubaba kuwa Mtume (swalallahu alaihi wasalam) kasema:
“Msiue jini isipokuwa yule mmoja mwenye mistari miwili mgongoni kwani hawa husababisha uzazi wa mtoto njiti na hufifiliza uoni wa macho. Hivyo, wauweni”.
Je hukumu hii kuwa nyoka ni majini, ina maana kuwa kila nyoka ni jini au baadhi yao tu?
Mtume (swalallahu alaihi wasalam) kasema, “Nyoka ni aina ya mabadiliko ya umbile la jini kama vile walivyogeuzwa nyani na nguruwe bani-Israili (wana wa Israili).” (Hadith hii ilinakiliwa na at-Tabaraani na Abu ash-Shaikh katika Udhma ikiwa na isinadi sahihi. Taz. Muhammad Nasir al-Din albani, Silsilaat al-Ahadith al-Sahiha, Juz. 3 uk. 103. (Hiyo ndiyo rejea iliyotolewa katika matini ya Kiarabu. Kwa usahihi ni Juz. 4, uk. 439. Aidha al-Albani anaelezea nukta hii muhimu ifuatayo katika uk. 440:
“Juweni kuwa Hadith hii haina maana kuwa nyoka waliopo hivi leo wametokana na umbile la jini, bali, hii ina maana kuwa baadhi ya majini waligeuzwa kuwa nyoka, ni sawa na ilivyotokea kwa wale mayahudi walivyogeuzwa kuwa nyani na nguruwe. Hata hivyo hawakuzaliana kama inavyoelezwa katika Hadith sahihi, ‘kwa hakika Allah hakuwafanyia kizazi viumbe waliogeuzwa maumbile. Kwa hakika nyani na nguruwe walishakuwepo kabla ya hilo.”
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
