Mfululizo Wa Mada Ya Majini (7)
(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)
imefasiriwa na Shaibu H.Kifea
Shetani humtembea Mwanadamu mithili ya damu itembeavyo kwenye mishipa
Katika Sahih Bukhari na Sahih Muslim imenakiliwa Hadith kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema:
“Kwa hakika, Shetani humtembea mwanadamu kama inavyotembea damu.” Pia imenakiliwa Hadith katika Sahih hizo mbili kuwa Safiyya bint Hayy, mke wa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema, “Mtume wa Allah alikuwa akifanya Itiqaf msikitini na nikamletea kikoi usiku. Nikaongea naye kisha nikainuka kuondoka. Mtume naye akainuka kuongozana nami. Nilikuwa naishi katika nyumba ya Usama ibn Zaid. Wanaume wawili wa Ansar wakatupita. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alipowaona, akawaendea haraka na kusema,’Yule ni Safiyya bint Hayy.’ Wakasema, “Subhana-Allah, ewe Mtume wa Allah (sisi hatukuwa na hisia mbaya juu yako).’ Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akawaambia, “Ibilisi humtembea mtu kama inavyotembea damu. Nilichelea kwamba angepenyeza tuhuma mbaya katika nafsi zenu.”’
Udhaifu na upungufu wa majini
Katika baadhi ya mambo, majini na mashetani wana uwezo lakini katika mambo mengine nao wana udhaifu. MwenyeziMungu anasema;
“Hakika hila za Shetani ni dhaifu.” (4:76).
Hapa tutataja baadhi ya mambo ambayo MwenyeziMungu na Mtume (Salallahu alaihi wasalam) wametufahamisha.
Meshetani wa kijini hawana uwezo mbele ya Wachamungu
MwenyeziMungu hakumpa Ibilisi uwezo wa kuwashurutisha wanadamu kuuendea upotofu na ukafiri. Katika Qur’an MwenyeziMungu anasema:
“Hakika waja wangu huna mamlaka juu yao. Na Mola wako anatosha kuwa Mlinzi (wao).” (17:65).
Aidha MwenyeziMungu anasema:
“Na bila shaka Ibilisi alisadikisha dhana yake juu yao, nao wakamfuata isipokuwa kundi la walioamini (kwelikweli). Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa sababu Tudhihirishe nani mwenye kuamini Akhera na nani anayetilia shaka..” (34:20-21).
Maanake ni kwamba Shetani hana namna ya kuwahadaa ima kwa njia ya ishara au kwa nguvu yoyote ile. Hata Ibilisi mwenyewe analitambua hili kama inavyosema aya hii ya Qur’an:
“(Ibilisi) akasema, ‘Mola wangu! Kwa sababu umenihukumu kupotea basi nitawapambia (upotofu) katika ardhi na nitawapoteza wote isipokuwa wale waja wako waliosafika kweli kweli.” (15:39-40).
Nguvu yake ya ushawishi huwahadaa wale watu na majini wanaoridhia mambo yake na wale wanaohiari wenyewe kumtii na kumfuata. MwenyeziMungu anasema:
“hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao isipokuwa wale wenye kukufuata (kwa hiyari yao) katika hao wapotevu.” (15:42).
Siku ya kufufuliwa viumbe, Ibilisi atawaambia wale waliomfuata katika upotevu na ufisadi;
“Na Shetani atasema itakapokatwa hukumu (ya wema kwenda Peponi na wabaya kwenda Motoni; atawaambia wale waasi watakaomng’ang’ania): ‘MwenyeziMungu alikuahidini ahadi ya kweli (na leo ameitimiza) nami nilikuahidini; lakini sikukutimizieni. Wala sikuwa na mamlaka juu yenu (ya kukulazimisheni kunifuata) isipokuwa nilikuiteni tu, nanyi mkaniitika. Basi msinilaumu bali jilaumuni wenyewe; siwezi kukusaidieni, wala nyinyi hamuwezi kunisaidia....” (14:22).
Aya nyingine ya Qur’an inasema
Nguvu zake (shetani) ni juu ya wale wanaomfanya rafiki (na kumfuata), na juu ya wale wanaomshirikisha MwenyeziMungu” (16:100).
Nguvu za shetani ni uchochezi na upotoshaji. Huwachochea na kuwazuzua hadi kuwapeleka kwenye ukafiri na ushirikina. Anawaandama mpaka waingie huko. Na katu hawaachii. MwenyeziMungu anasema:
“Je! Huoni ya kwamba Tumewatuma mashetani juu ya makafiri wanawachochea (kufanya mabaya)? (19:83).
Uwezo alionao shetani juu ya watu na majini wanaomfuata si wa ishara wala hoja bali kwa sababu tu mambo anayowaitia yanaendana na matashi na matamanio yao. Watu hawa wamehujumu wenyewe nafsi zao kwa kumruhusu adui yao mkubwa, Shetani awe rafiki yao na bwana mkubwa wao.
Yote haya ni kwa sababu wanakubaliana na yale anayoyataka kwao. Wanapomnyooshea mikono, huwa wafungwa wake, hii ikiwa ni aina ya adhabu kwa matendo yao wenyewe.
MwenyeziMungu hakumpa Ibilisi mamlaka juu ya mja wake yeyote yule hadi pale mja mwenyewe alipomfungulia njia shetani kwa kumtii na kumshirikisha na MwenyeziMungu. Hapo ndipo MwenyeiMungu anapoacha Shetani amtawale mja na kuwa na mamlaka juu ya yake.
Shetani huwa na nguvu kwa waumini wanaotenda dhambi
Hadith moja inasema, “MwenyeziMungu huwa pamoja na hakimu maadam tu hafanyi dhuluma. Akifanya dhuluma, MwenyeziMungu hujitenga naye na kumuweka shetani pamoja naye.” (Hadith hii imenakiliwa na al-Hakim na al-Baihaqi kwa isinadi ya hasan. Taz al-Albani, sahih al-Jaami, juz. 2 uk. 130)
Abu al-Faraj ibn al-Jauzi amesimulia kisa cha aina yake kutoka kwa Al-Hassan al-Basri. Kisa hiki, kutegemeana na usahihi wake, kinaonesha uwezo alionao binadamu kumshinda shetani pale anapokuwa mkweli kwa MwenyeziMungu na anapokuwa na Ikhilasi katika dini yake. Pia Hadith hii inaonesha kuwa shetani hupata nafasi pale mtu anapopotoka.
Al-Hasan al-Basri kasimulia kuwa, kulikuwa na mti mmoja uliokuwa ukiabudiwa badala ya MwenyeziMungu. Bwana mmoja akaamua aukate mti huo. Pale alipokuwa njiani kwenda kuukata mti huo kwa ghadhabu za kutafuta radhi za Allah, akakutana na Ibilisi akiwa katika umbile la binadamu.
Ibilisi akamuuliza mtu huyo, “”Kitu gani unachopanga kufanya?” Bwana huyo akajibu, “nakwenda kuukata ule mti unaoabudiwa badala ya MwenyeziMungu.” Ibilisi akasema, “ Kama wewe huuabudii, unakudhuru nini wengine wanapomuabudia?”
Mtu huyo akajibu, “mimi nitaukata tu”. Ibilisi akamwambia, “Je unataka kitu kizuri zaidi ya hicho? Usiukate mti huo, utapata dinari mbili kila asubuhi chini ya mto wako wa kulalia.” Mtu huyo akauliza, “ zitatoka wapi (hizo dinari)?”
Ibilisi akasema, “mimi nitakupatia”. Bwana huyo akarejea kwake na asubuhi iliyofuata, akakuta dinari mbili chini ya mto wake.” Asubuhi iliyofuata akakuta tena dinari mbili chini ya mto wake.
Lakini asubuhi ya kesho yake hakukuta kitu. Akafazaika na kutoka kwenda kuukata mti huo. Kwa mara nyingine Ibilisi akamtokea katika umbile lilelile la binadamu. Ibilisi akauliza, “unataka kufanya nini?”
Bwana huyo akajibu, “nataka kuukata ule mti unaoabudiwa badala ya MwenyeziMungu.” Ibilisi akasema, “unasema uongo”. Hakuna njia kwako ya kuweza kuukata mti huo.”
Mtu huyo akatoka hapo kwenda kuukata mti huo. Ardhi ikammeza na kumkaba hadi akakaribia kuuawa. Ibilisi akauliza, “hivi, wewe unajua mimi ni nani? Mimi ndiye Ibilisi. Nilikutana nawe kwa mara ya kwanza ulipokuwa na hasira za kutafuta radhi za Allah ambapo mimi sikuwa na uwezo juu yako.
Nikakudanganya kwa dinari mbili nawe ukaacha kile ulichokuwa umenuia kukifanya (kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah). Lakini safari hii umekuja kwa sababu ya hasira tu za kukosa dinari mbili, nami ndiyo hivyo nimepata mamlaka juu yako”. (Taz. Ibn al-Jauzi, Talbiis Ibliis, uk.43).
(Mwandishi wa Kitabu hiki, al-Ashqar kadokeza kuwa usahihi wa kisa hiki unahitaji kuthibitishwa. Yaelekea zaidi kuwa hiki ni kisa cha Kiisrailiyati au visa vya Wayahudi na Wakristo. Al-Ashqar kasema kuwa kisa hiki kinabainisha namna mchaMungu anavyoweza kumshinda Ibilisi. Haina maana kwamba kinaonesha kuwa mtu huyo aliyedhamiria kuukata mti kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah alishindwa kuishinda hila ya shetani dhidi yake. Allah Ndiye Mjuzi wa Yote).
Vilevile MwenyeziMungu ametufahamisha katika Kitabu chake kuwa mtu mmoja alipewa Aya za MwenyeziMungu na akazifahamu lakini baada ya hapo akazitelekeza zote na MwenyeziMungu akamuacha shetani amtawale. Shetani akamwandama na kumpoteza na matokeo yake akawa fundisho kwa wengine na akawa hadithi ya kusimuliwa. MwenyeziMungu anasema;
“Na wasomee habari za wale tuliowapa Aya zetu, kisha wakajivuna nazo (wasizifuate). Na shetani akawaandama, wakawa miongoni mwa waliopotea. Na kama tungelitaka, tungewanyanyua kwazo lakini wao waligandamana na dunia na wakafuata matamanio yao. Basi hali yao ni kama hali ya mbwa, ukimpigia kelele anahema, na ukimuacha pia huhema. Hiyo ndiyo hali ya watu waliozikadhibisha aya zetu. Basi simulia hadithi huenda wakatafakari (7:75-76).
Ni dhahiri kuwa kisa hiki cha mfano kinamuhusu mtu anayeujua ukweli na kuukataa kama Mayahudi ambao walimjua Mtume Muhammad (Salallahu alaihi wasalam) kuwa alikuwa Mtume wa kweli wa Mwenyezi lakini wakamkataa.
Baadhi ya watu wanasema kuwa aya hiyo inamzungumzia Balaam ibn Bauura ambaye alikuwa mchaMungu na baadae akawa kafiri. Wengine wanasema kuwa Aya hiyo inamzungumzia Umayya ibn Abu as-Salit ambaye alimuabudu Allah katika zama za ujahili na akakutana na Mtume lakini akakataa kumuamini kutokana na husuda. Yeye alikuwa na matarajio kuwa ndiye angetumwa kuwa Mtume. Hatuna matini sahihi inayofahamisha kwa uwazi ni nani hasa aliyezungumziwa na aya hii.
‘Kupokea Aya za MwenyeziMungu na kisha usiziamini’ ni maelezo juu ya mtu anayefanana kabisa na Ibilisi. Hii ni kwa sababu Ibilisi aligeuka kuwa kafiri baada ya kuujuwa na kutambuwa ukweli wazi wazi. Hili ndilo jambo miongoni mwa mambo ambayo Mtume (Salallahu alaihi wasalam) aliyachelea zaidi kwa umma wake.
Al-Hafidh Abu Yala kanakili Hadith kutoka kwa Hudhaifa bin al-Yaman kuwa Mtume wa MwenyeziMungu kasema: “katika mambo ninayoyahofia kwenu ni mtu kusoma Qur’an hadi ukaona utukufu wake kwake. Vazi lake likawa Uislamu na akalivaa mpaka Allah akapenda na baada ya hapo akalitupa nyuma ya mgongo wake na kumshambulia jirani yake kwa upanga na kumshutumu kwa ushirikina. (Hudhaifa) akauliza, “ewe Mtume wa Allah yupi hapo auliwe, yule anayeshambulia au anayeshambuliwa? Mtume (saw) akasema, “Yule anayeshambulia.” (Ibn Kathiir kasema, “isnadi yake ni safi”. Taz. Tafsiir ibn Kathiir, juz. 3, uk. 252).
Shetani huwaogopa na kuwakimbia baadhi ya waja wa Allah
Iwapo mja anashikamana barabara na Uislamu, ana Imani ya dhati kabisa moyoni mwake na anachunga mipaka iliyowekwa na MwenyeziMungu basi shetani humgwaya na kumkimbia. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alimwambia hivi Umar,
“Kweli kabisa, kabisa Shetani anakukimbia Umar”. (Hii imenakiliwa na Ahmad, at-Tirmidh na ibn Hiban kwa Isinad Sahih. Taz. Al-Albani, Sahih al-Jaami, juz. 2. uk. 74).
Pia Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alisema hivi juu ya Umar;
“”Kwa hakika nawaona mashetani wa kijini na kibinadamu wakikukimbia Umar”. (Imenakiliwa na al-Tirmidh kwa isnadi sahihi. Taz. Sahih al-Jaami, juz. 2, uk. 329).
Lakini jambo hilo si kwa Umar pekee. Yeyote yule mwenye imani thabiti huweza kumshinda shetani,’humbwaga’ na ‘kumtweza’
Inaelezwa katika Hadith;
“Muumini humnyongesha (hummiliki au humuendesha) shetani wake kama vile vile mmoja wenu anavyomnyongesha (anavyomuendesha) ngamia wake wakati akisafiri naye.” (Hii imenakiliwa na Ahmad. (shuaib al-Arnauut na Adil murshid wanasema kuwa Hadith hii ni dhaifu kwa sababu inamjumuisha Abdullah ibn Lahiya ambaye alikuwa na upungufu wa kumbukumbu. Taz. Shuaib al-Arnauut na adil Murshid, Musnad al-Imaam Ahmad (Beirut: Muasassah al-Risaalah, 1997), juz. 14, uk. 504.
Isinadi pia ina upungufu mwingine ambao hawakuutaja. Upungufu huu ni kwamba yeye huyo huyo Lahiyya alikuwa akikariri tadliis (ambapo akawa anatumia neno la kutatanisha ambalo halikubainisha jinsi alivyopokea Hadith) na katika riwaya hii akatumia neno tata katika Isinadi yake. Ndiyo kusema basi mtu hawezi kupata uhakika ni kwa nani hasa Lahiya aliisikia Hadith hii.
Baada ya kuinakili Hadith hiyo, ibn Kathiir kasema: “ (mtu) kumkamata shetani wake maana yake ni kumnyaka utosini na kumtenzanguvu kama anavyofanywa ngamia pale anapotoroka na kukamatwa tena. (Taz. Ibn Kathiir, Al Bidaayatu wa al-Nihaayah, juz. 1,.uk. 73) Sherehe hii ya ibn Kathiir inaegamia kauli isiyo sahihi ya Hadith. Allah ndiye Ajuaye.
Inaweza hata kutokea kuwa Muislamu huweza kuwa na athari kubwa kwa “mshirika” au Swahibu wake kutoka jamii ya majini ambaye huweza kusilimu. Muslim na Ahmad wamenakili Hadith hii kutoka kwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam);
“Hakuna hata mmoja kati yenu asiye na “jamaa” (partner) yake kutoka jamii ya majini” Watu wakauliza, “hata wewe Mtume wa Allah?” Mtume (saw) akajibu, “hata mimi isipokuwa tu MwenyeziMungu amenisaidia dhidi yake na hivyo, (jini huyo) huniamrisha kufanya mema tu.”
Imam Ahmad naye pia kainakili Hadith hii kutoka kwa Ibn Abbas ikiwa na kauli hii, “lakini MwenyeziMungu amenisaidia dhidi yake na amesilimu”. Muslim naye kanakili kutoka kwa Aisha, “lakini Mola wangu kanisaidia dhidi yake mpaka kajisalimisha.”
Inaendelea ..../8
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


