Kutoa Sadaka Kwa Kipato Cha Kazi Ya Kuuza Pombe

 

SWALI:

 

Ndugu katika imani

Asalam alaykum; mimi ni  ukhti ***** **** ***** wa p.o box ***, ******** ******, naomba kuuliza maswali mawili na la mwisho nimeulizwa na wenzetu toka upande wa pili [wakristo].

Mimi nimeajiliwa katika kampuni ya soda na bia hivyo nauza soda,bia na maji ya chupa[maji ya kunywa] na  najitahid sana katika ibada za kila siku, pamoja na kujisitiri kuvaa mavazi ya stara kwa mujibu wa dini yangu ya kiislamu, michango mbali mbali natowa msikitini, je hili pato langu lafaa kutolea sadaka?



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali. Ieleweke kuwa Uislamu una kanuni zake za kibiashara na mambo mengine ambayo mara nyingi yanakwenda kinyume na nchi tunazoishi. Hivyo zipo biashara zilizohalalishwa na zipo zilizoharamishwa. Biashara mojawapo iliyoharamishwa ni ya uuzaji wa pombe.

 

Kwa ajili hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelaani aina kumi za watu wanaohusika na ulevi: “Mwenye kugema ulevi, mwenye kutaka afanyiwe, mwenye kunywa na mwenye kubeba, mwenye kubebewa, mwenye kunywisha, mwenye kuuza, mwenye kula thamani yake, mwenye kununua na mwenye kununuliwa” (at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Wakati ilipoteremka Aayah ya kuharamisha ulevi (5: 90-91) moja kwa moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Hakika Allaah Ameharamisha ulevi, basi mwenye kuisikia Aayah hii ilhali anao ulevi, basi asinywe wala asiuze” (Muslim).

 

Kwa kuwa unafanya biashara ya haramu, pato lako ni la haramu, hivyo sadaka zako hazikubaliwi na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri” (Muslim).

 

Tazama hata Maquraysh kabla ya kusilimu kwao walikuwa ni washirikina wakubwa na wenye kufanya maovu chungu nzima. Hata hivyo, mwaka wa 605 Miladi pale al-Ka‘bah ilipoharibiwa na mvua kubwa walianza kuijenga na wakaamua kuwa isiingie mali ya haramu na yeyote aliyejulikana kuwa ameleta hiyo alikuwa akirudishiwa. Nasi ni muhimu tuwe na msimamo wa zaidi ya huo.

 

Nasaha zetu kwako ni kuwa uache kazi hiyo mbaya na ya haramu na badala yake utafute kazi nyingine ili mambo hayo mema yako yasiwe ni yenye kupotea bure.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share