Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (8)

(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea

 

 

Majini walivyotiishwa kumtumikia Suleiman

                            

MwenyeziMungu aliwatiisha Majini na mashetani wote kumtumikia Nabii Suleiman (as) na wakamfamfanyia vile alivyotaka. Alikuwa akiwaadhibu na kuwatia kifungoni wale waliokataa kutii. Katika Qur’an, MwenyeziMungu anasema,

“Na wengine wafungwao minyororo (wanapokhalifu amri zake)  (38:38)                               

Pia Anasema,

“Na kwa Suleiman (Tukatiisha) upepo (uliokwenda) safari yake ya asubuhi (mwendo wa) mwezi mmoja, na safari yake ya jioni (mwendo wa) mwezi mmoja. Na Tukamyeyushia chemchem ya shaba. Na katika Majini (kulikuwa na) waliofanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake. Na kila anayejitenga na Amri yetu miongoni mwao Tunamuonjesha adhabu ya Moto uwakao. (34:12).                                                                                     

Utiifu huu kwa Suleima ni majibu ya dua ambayo Suleiman aliiomba kwa MwenyeziMungu,

“Akasema: “Mola wangu! Nisamehe na Unipe ufalme, asiupate yeyote baada yangu. Bila shaka wewe ndiwe Mpaji (38:35)                                                                                       

Ilikuwa ni dua hii ambayo ilimzuia Mtume Muhammad (saw) kumdhibiti na kumdhihirisha yule jini aliyewahi kumkamata ambaye alimuwekea Mtume kijinga cha moto usoni na kutaka kumtupia. Katika Sahihi Bukhar imenakiliwa Hadith hii kutoka kwa Abu al-Dardai:

“Mtume wa Allah alikuwa amesimama wima (kusali) na akasikiwa akisema, “Najikinga kwa Allah kuepukana nawe”, baada ya kusema hivyo, akasema, “Nakulaani kwa laana za Allah.”

Mtume alisema maneno haya mara tatu kisha akanyoosha mkono wake akionesha kama anakamata kitu fulani. Alipomaliza kuswali, akaulizwa, “Ewe Mtume wa Alllah, wakati ukiswali, tulikusikia ukisema jambo fulani ambalo hatujawahi kukusikia ukilisema katika Sala, na tukakuona ukikunjua mkono wako”.

 Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akawaambia, “Adui wa Allah, Ibilisi alinijia na kijinga cha moto kuniwekea usoni, ndiyo sababu nikatamka mara tatu, ‘nakulaani kwa laana za MwenyeziMungu’. Halafu nikasema mara tatu, “najikinga kwa Allah kuepukana nawe”. Lakini bado hakuondoka. Ndipo nikajaribu kumkamata. Wallah kama si dua ya ndugu yangu Suleiman, angedhibitiwa na kugeuzwa dubwasha la kuchezewa na watoto wa Madina”.

Mkasa kama huo ulitokea zaidi ya mara moja. Imam Muslim kanakili Hadith ifuatayo kutoka kwa Abu Huraira; Mtume wa Allah kasema, Afriit (aina ya shetani) wa kijini alichapuka kunivurugia sala usiku wa jana, lakini MwenyeziMungu akanijaalia nguvu za kumshinda, hivyo nikamkamata na kutaka kumfunga kwenye nguzo moja ya msikiti, lakini papo hapo nikakumbuka dua ya ndugu yangu Suleiman, ‘Basi MwenyeziMungu akamgeuza kuwa duni na dhalili”                   

                        Wayahudi walimsingizia uwongo Suleiman

Wayahudi na wale wanaowaiga katika kuwatumia majini kwa njia ya sanaa ya uchawi, hudai kuwa Suleiman alitumia uchawi ili kuwatawala majini. Wengi miongoni mwa wanazuoni wa awali wanaeleza kuwa, pale Suleiman alipotawafu, mashetani wakaandika vitabu vya uchawi na kufuru na kuviweka kwenye kiti chake cha ufalme, halafu wakasema, “Suleiman alikuwa akitumia vitabu hivi kuwatawala Majini”

Jambo hili likawafanya watu wengine waseme kuwa kama sanaa hii ya uchawi ni haramu mbona Suleiman aliifanya! MwenyeziMungu akashusha wahai huu,

Na walipojiwa na Mitume kutoka kwa MwenyeziMungu, mwenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nao, kundi moja miongoni mwa wale waliopewa Kitabu lilitupa kitabu cha MwenyeziMungu nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui (2:101).

Kisha MwenyeziMungu akabainisha kuwa walifuata yale waliyosomewa na mashetani wakati wa uhai wa Suleiman, kisha Allah akamfutia Suleiman tuhuma hizo za uchawi na kufuru

“...na Suleiman hakukufuru bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruta na Maruta (kakika mji wa) Babil. Wala Malaika hao hawakumfundisha  yeyote mpaka wamwambie, “hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru  (2:102)

                             Majini hawana uwezo wa kufanya miujiza

Majini hawawezi kufanya miujiza kama  ile ya Mitume ambayo ni uthibitisho wa ukweli wa mafundisho yao. Baadhi ya Makafiri walidai kuwa Qur’an  ilitokana na maandiko ya Shetani, ndipo Allah akashusha wahai huu,

“Wala mashetani hawakuteremka nayo (hii Qur’an kama walivyodai hao makafiri). Wala haiwi kwao (kuiteremsha Qur’an) na hawawezi. Bila shaka wao wamezuliliwa kusikiliza (yanayosemwa na malaika mbinguni) (26:210-212)                                                                                   

MwenyeziMungu anatoa changamoto kwa binadamu na majini wote katika aya ifuatayo:

“Sema: “Hata wakijikusanya watu (wote) na majini ili kuleta mfano wa hii Qur’an basi hawangaliweza kuleta mfano wake hata kama watasaidiana vipi wao kwa wao    (17: 88)

         

Majini hawawezi kutokea kama Nabii katika uoni wa macho au ndoto

Majini hawawezi kujitokeza kwa sura ya Mtume katika upeo wa macho. Tirmidh kanakili Hadith kwa Isinadi sahihi kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema,

“Yeyote anayeniona mimi, basi ni mimi, kwani mashetani hawawezi kijitokeza kama mimi.” Na katika Sahih zote mbili, kauli ni hii, “yeyote anionaye mimi, basi uoni wake ni sahihi kwani mashetani wa kijini hawawezi kujitokeza kwa umbile langu”. 

Maana inayodhihiri katika Hadith hii ni kuwa mashetani hawana uwezo wa kujipa umbile la Mtume wa Allah. Lakini hii haina maana kuwa hawawezi kujitokeza kwa maumbile ya watu wengine na kudai utume.

Hivyo, haijuzu kujenga hoja kwa kutumia Hadith hii kuwa kila amuonae yule anayemdhania kuwa ni Mtume katika ndoto basi amemuona kweli Mtume isipokuwa labda mtu huyo anayeonwa atimimize wasifu wa Mtume(Salallahu alaihi wasalam) unaokutikana katika vitabu vya Hadith. Watu wengi hudai kumuona Mtume ndotoni lakini wasifu wanaoutoa unatofautiana na ule ambao umenakiliwa katika vitabu sahihi.

Majini hawewezi kuvuka mipaka waliyowekewa mbinguni

MwenyeziMungu anasema katika Qur’an, 

"Enyi jamii ya  majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi basi penyeni! Hamtapenya ila kwa nguvu zangu. Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha? Mtaletewa mwako wa moto wa shaba wala nyinyi hamtaweza kujilinda navyo.  (55: 33-35)

Licha ya nguvu na kasi yao ya mwendo, hawana uwezo wa kuvuka mipaka hiyo, na wakithubutu, wataangamia.

 

Majini hawawezi kufungua milango iliyofungwa

kwa jina la Allah

Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema,

“Fungeni milango na isomeeni jina la Allah, kwani Shetani hushindwa kufungua mlango uliofungwa (kwa kusomewa jina la Allah) (Hadith hii imenakiliwa na Abu Dawd, Ahmad,ibn Hibban na al-Haakim kwa isnadi sahihi. Taz. al-Albani, Sahihi al-Jaami, Juz. 1, uk. 229).

 Aidha kuna Hadith hii katika Sahih zote mbili;

“Kwa hakika, Shetani hafungui  mlango uliofungwa. Funikeni ndoo zenu na zisomeeni jina la Allah, hata kama ni kuweka kitu kidogo tu humo. Na zimeni taa zenu. (Sahihi al-Jaami, juz. I, uk.270)

“Fungeni milango yenu na funikeni vyombo vyenu na fungeni viriba vyenu vya maji na zimeni taa zenu, kwani Shetani hafungui mlango uliofungwa wala hafunui mfuniko wala hafungui viriba vya maji.”

 

Majini kuwajibika kwa matendo yao

Lengo kuu la kuumbwa kwao:

Majini waliumbwa kwa lengo lilelile waliloumbiwa wanadamu. (al-Dhaariyat 56).

Kwa hiyo, majini wanawajibika kwa matendo yao na wameamrishwa kufanya baadhi ya mambo na kukatazwa kufanya mengine. Yule anayetii, MwenyeziMungu atakuwa radhi naye na ataingia Peponi. Yule asiyetii au anayeasi, hupata adhabu ya Moto wa Jahanamu. Aya na Hadith nyingi zinabainisha jambo hili.

Siku ya hukumu, MwenyeziMungu atawaambia viumbe wote wawili, majini na wanadamu maneno haya: Enyi makundi ya majini na wanadamu ! je hawakuwafikieni mitume miongoni mwenu kukubainishieni aya zangu na kukuonyeni mkusanyiko wa siku yenu hii leo? Watasema tumeshuhudia juu ya nafsi zetu[kuwa sisi wabaya]yaliwadanganya maisha  duniya. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri          (al-Anam 130)

Aya hii inathibitisha kuwa maamrisho ya Mungu yamewafikia majini na kwamba wamefikiwa na Mitume waliowaonya na kuwafikishia ujumbe. Aya za kuthibitisha  kuwa majini wataadhibiwa katika Moto wa Jahanamu ni nyingi:

Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu badala ya MwenyeiMungu?’’ watasema “wametupotea’’ na watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri... Atasema [Mwenyezi Mungu siku ya kiyama kuwaambiya]:”Ingieni motoni pamoja na nyumati zilizopita kabla yenu za majini na watu

(al-Araaf 37-38)

‘’ Na bila shaka tumewaumbiya moto wa jahanam wengi katika majini na wanadamu[kwa sababu hii] nyoyo wanazo, lakini hawafahamu kwazo na macho wanayo, lakini hawaoni kwayo, na masikiyo wanayo lakini hawasikii kwayo na hao ni kama wanyama;bali wao wamepotea zaidi. Hao ndio alioghafilika[al-Araaf 179)

“Kwa yakini nitaijaza jahanamu kwa wote hawa ;majini na watu

(al-Sajdah 13)

Na ushahidi kuwa majini walioamini wataingia Peponi ni huu:

’Na mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya mola wake atapata mabustan[pepo]mawili (alRahman 46-47)

Aya hii  na na hizo nyingine zilizonukuliwa  na kwa ujumla Sura nzima inawahusu viumbe wote wawili, Majini na Wanadamu. Sura hiyo inazungumzia neema za Allah kwa majini na kuingia kwao Peponi.

 Laiti kama majini hawangekuwa viumbe wa kupata neema hii ya Pepo, iweje basi ielezwe kuwa ni neema kwao.  Katika kitabu chake, al-Furu, Ibn Mufleh kasema:

Majini huwajibika kwa vitendo vyao, hii ni kulingana na rai ya pamoja (ya Maulamaa). Wale ambao sio waumini  wataingia motoni, jambo hili linaafikiwa na (Maulamaa) wote. Waumini  miongoni mwao wataingia Peponi, hii ni kwa mujibu wa Malik na Shafii. 

Kwa rai yao hii, majini hawatageuzwa udongo kama wanyama na kwamba malipo ya waumini miongoni mwao ni kunusurika tu kukaa katika moto wa Jahanamu ambapo rai hii inatofautaina na ile ya Abu Hanifa, al-Laith ibn Saad na wengineo.

Ni wazi kuwa rai ya kwanza ndiyo sahihi. Majini watakuwa Peponi pamoja na Wanadamu kulingana na mizani ya amali zao. Hii pia inatofautiana  na ile rai kuwa majini hawatakula wala kunywa Peponi; jambo hili lilisemwa na na Mujaahid.

Na vilevile hii inatofautiana na rai iliyoshikiliwa na Umar ibn Abdul Aziz ambayo inasema kuwa majini watakuwa pembezoni mwa Pepo. Ibn Hamad yeye kasema katika kitabu chake kimoja, “majini wako sawa na wanadamu katika kuwajibishwa kwa vitendo na kwa Ibada.” (hii imenukuliwa kutoka Lawaami al-Anwaar, juz. 2, uk. 222-223).      

                          Majini huwajibishwa kwa kadri ya uwezo walionao

Ibn Taimiya kasema hivi,

Majini wameamrishwa kufanya  matendo ya msingi na matendo ya ziada kulingana na uwezo (wasaa) walionao. Hawafanani na binadamu kwa haiba na maumbile. Yale mbayo wao wameamrishwa kuyafanya au wamekatazwa kuyafanya, hayafanani kabisa na yake ambayo wameamrishwa au kukatazwa wanadamu. Ila wanalingana katika kuhukumiwa kwa yale ambayo wameamrishwa kuyafanya, na  yale ambayo wamekatazwa kuyafanya. Ninavyojua hakuna khitilafu juu ya jambo hili miongoni mwa Waislamu. (Taz. Ibn Taimiya, Majmuu Fatawa, juz. 4, uk. 233).

                                  Hakuna ushirika kati ya majini na Allah (SW)

 Majini, kama ilivyoelezwa, ni miongoni mwa viumbe vya Allah ambao, kama walivyo viumbe wengine, wanatii Kwake. Majini waliumbwa kwa ajili ya kumuabudia na kumtii Allah tu na wanawajibika kutekeleza maamrisho Yake.

Maelezo hayo yanafutilia mbali zile imani za kishirikina zilizokuwa zimeshamiri kutokana na dhana potofu juu ya msingi sahihi wa mambo au kutokana na ukosefu wa elimu.

Wayahudi na washirikina wa Kiarabu walikuwa wakiamini kuwa MwenyeziMungu alioa wake kutoka jamii ya majini na matokeo ya uhusiano huo ndio wakapatikana malaika (Subhana-Allah). Katika Qur’an, MwenyeziMungu analitaja jambo hili na kusema kuwa ni la uzushi. MwenyeziMungu anasema:

"Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa".  

"Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia."

(al-Saffaat 158-159).

Katika sherehe yake ya aya hii, Ibn Kathiir kaandika hivi:

Mujahid kasema, “washirikina walisema, ‘malaika ni watoto wa kike wa Mungu, SubhanaAllah’. Abubakar akawauliza, “mama zao ni kina nani?” Wakajibu, (mama zao) ni mabinti wa majini bora.”

Ibn Zaid na Qatada wote wawili walitoa maelezo kama hayo ya Mujahid...Al-Aufi naye kasimulia Hadith kutoka kwa ibn Abbas, ‘maadui wa Allah walidai kuwa MwenyeziMungu  na Ibilisi ni ndugu. Na Allah ametakasika na uzushi huo mzito,”

 

 

Inaendelea ……9