Mfululizo Wa Mada Ya Majini (9)
(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)
imefasiriwa na Shaibu H.Kifea
Majini wameumbwa kwa moto, wataunguaje motoni?
‘Baadhi ya watu wamezusha ubishi au shaka wakisema kuwa, “nyie si mnakubaliana na ukweli kuwa majini wameumbwa kwa moto. Sasa mbona tena mnasema kuwa makafiri miongoni mwao wataadhibiwa motoni, na yule anayethubutu kuiba habari a mbinguni hutupiwa kimwondo. Huu moto utawadhuru vipi ikiwa wao wenyewe wameumbwa kwa huo huo moto?’
Jawabu ni kwamba kwa asili wameumbwa kwa moto lakini baada ya kuumbwa kwao hawakuwa moto tena. Wakawa viumbe tofauti na moto. Jambo hili linaweza kutolewa mfano wa binadamu ambao wameumbwa kwa udongo. Baada ya kuumbwa kwao wakawa tofauti kabisa na udongo.
Iwapo mtu atampiga mwenziwe na dongo, atamuumiza sana au hata kumuua kabisa. Mwanadamu akifukiwa udongoni, atakosa hewa na kufa. Ndiyo kusema basi, ingawaje yeye mwenyewe katokana na udongo, bado udongo huo huo humdhuru. Basi hali ni hiyo hiyo kwa Majini na moto.
Je wahy (ufunuo) huwafikiaje Majini?
Kwa kuwa majini watahukumiwa kwa matendo yao, basi hapana shaka kuwa wahai wa MwenyeziMungu lazima uwafikie na kuwa “ushahidi” dhidi yao. Lakini jambo hili huwatokeaje? Je na wao wana Mitume miongoni mwao kama walionao binadamu au Mitume wao ndio hao hao wa jamii ya wanadamu?
MwenyeziMungu anasema katika Qur’an,
“Enyi makundi ya majini na wanadamu! Je hawakukujieni Mitume miongoni mwenu kukubainishieni Aya zangu na kukuonyeni juu ya mkusanyo wa siku yenu hii ya leo?” (6:130).
Aya hii inabainisha kuwa MwenyeziMungu aliwatumwa Mitume kwa majini lakini aya hii haijasema wazi hao Mitume wenyewe walikuwa ni majini wenzao au binadamu? Neno ‘miongoni’ au “minkum” kwa Kiarabu ambalo Mfasiri wa Kiingereza Picktball amelifasiri kwa maneno, “Of your own” laweza kuwa na maana kuwa ama Mitume hao walikuwa wa jamii yao wenyewe au laweza kuwa maana kuwa Mtume mmoja wa kibinadamu katumwa kwa viumbe wa jamii zote mbili.
Kwa hali hiyo, kuna tofauti ya rai kuhusiana ipi hasa maana ya aya hii. Kimsingi, kuna rai mbili juu ya jambo hili. Rai ya kwanza ni kwamba majini walipelekewa Mitume wa jamii yao wenyewe. Hii ni rai ya al-Dhuhhaak. Ibn al-Jauz kasema hii ndiyo maana ya wazi zaidi ya aya hii
Ibn Hazm kasema kuwa hakuna Mtume yeyote wa jamii ya binadamu aliyetumwa kwa majini kabla ya Mtume Muhammad (Salallahu alaihi wasalam).
Rai ya pili ni kuwa Mitume wote waliotumwa kwa Majini walikuwa wanadamu. AlSuyuuti kaeleza katika kitabu chake, Luqat al-Marjaan kwamba wengi miongoni mwa wanazuoni wa awali na wa baadae wamesema kuwa majini hawakuwahi hata mara moja kuwa na Mtume au nabii wa jinsi yao. Rai hii ilisimuliwa kutoka kwa ibn Abbas, Mujahid, al-Kalbi na Abu Ubaid. (
Taz.Lawaami al-Anwaar, juz. 2, uk. 223-4).
Kinachoifanya rai hii ya pili ionekane kuwa na nguvu zaidi ni ile kauli ya majini baada ya kuisikia Qur’an;
(Majini) wakasema, “Enyi watu wetu! Hakika Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa......” (46:30) Hata hivyo aya hii si uthibitisho wa wazi wa jambo husika. Swala linalobishaniwa hapa halihitaji ijitihadi yeyote kwa upande wa Waislamu na wala hakuna aya iliyowazi kuhusiana nalo. Kwa hiyo basi, hakuna haja ya kulijadili kwa kina zaidi.
Ujumbe wa Muhammad (Salallahu alaihi wasalam) kwa majini na wanadamu
Mtume Muhammad (Salallahu alaihi wasalam) alitumwa kwa wote majini na watu. Ibn Taimiyya kasema, “Kuna makubaliyano ya rai juu ya jambo hili miongoni mwa Maswahaba na wale waliofuta baada yao na maimamu wa Waislamu na makundi mbalimbali ya Waislamu, ahl al-sunna wa al-jamaa na wengineo. MwenyeziMungu awawie radhi.” (Taz. Ibn Taimia, Majmuu al-Fatawa, juz. 19, uk. 9.
Kinachoitia nguvu rai hii ni changamoto ya Qur’an kwa majini na binadamu ikiwataka watunge kitabu sawa na Qur’an. MwenyeziMungu anasema katika Qur’an.
“ Sema, ‘hata wakijikusanya watu (wote) na majini ili kuleta mfano wa hii Qur’an basi hawangaliweza kuleta mfano wake hata kama watasaidiana (vipi) wao kwa wao.” (17:88)
Baadhi ya majini haraka wakabadilika na kuwa waumini walipoisikia Qur’an ikisomwa. Qur’an inasema: “Sema, ‘imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikia (Qur’an) likasema, ‘hakika tumeisikia Qur’an ya ajabu, inaongoza katika uongofu, kwa hivyo tumeiamini wala hatutamshirikisha yeyote tena na Mola wetu.’” (72:1-2).
Wale walioisikiliza na kuiamini Qur’an ni wale wanaotajwa katika aya ifuatayo kutoka surat al-Ahqaaf, “Na (wakumbushe) tulipokuletea kundi la majini (kuja kwako) kusikiliza Qur’an. Basi walipoihudhuria wakasema (wakaambiana) ‘nyamazeni (msikilize maneno ya MwenyeziMungu)’. Na ilikwisha (somwa) wakarudi kwa wenzao wakiwaonya, ‘enyi wenzetu! Hakika tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake na kinachoongoa katika haki na katika njia iliyonyooka. Enyi wenzetu! Muitikieni mlinganiji (muitaji) wa MwenyeziMungu na mumuamini, atakusameheni (MwenyeziMungu) madhambi yenu na atakukingeni na adhabu iumizayo. Na wasiomuitikia Muitaji wa MwenyeziMungu, basi wao hawatamshinda hapa katika ardhi wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotofu (upotevu) uliodhahiri.”(46:29-32).
Walipoisikia Qur’an, wakaiamini na kurejea kwa wenzao kuwalingania wailekee tawhiid na imani na wakawapa habari njema pamoja na kuwaonya.
Kisa cha majini hawa kumsikiliza Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kimenakiliwa katika Bukhari na Muslim kwa mapokezi ya ibn Abbas. Ibn Abbas kasimulia kuwa Mtume wa Allah alikuwa akisafiri na baadhi ya Maswahaba, wakiwa na madhumuni ya kwenda sokoni eneo la Ukaz.
Katika kipindi hicho, kulikwishakuwa na kizuizi kwa majini kupata habari za mbinguni ambapo vijinga vya moto vilikuwa vikirushwa dhidi yao. Kwa hiyo majini (waliokwenda mbinguni) wakarudi kwa wenzao ambako waliulizwa kulikoni.
Wakajibu, “vizuizi fulani vimewekwa baina yetu na habari za mbinguni’. Wakaambiana, “yawezekana labda kuna jambo limetokea. Kwa hiyo nendeni sehemu za mashariki na magharibi ya dunia mkaone nini kimetokea na kusababisha vikwazo hivi baina yetu na habari za mbinguni. Wakafanya hivyo.
Kundi moja likaenda hadi kufika Tihama ambao ni msitu wa michikichi ulio jirani na soko la Ukaz. Muda huo Mtume (Salallahu alaihi wasalam) alikuwa akiwaswalisha Maswahaba swala ya Alfajir. Majini hao waliposikia kisomo cha Qur’an, wakaambiana, ‘tusikilize jamani’. Kisha wakasemezana, ‘hii ndiyo imesababisha vizuwizi baina yetu na habari za mbinguni.” Majini hawa wakarejea kwa wenzao na kuwaambia, “Enyi wenzetu, sisi wenzenu tumesikia kisomo cha ajabu (Qur’an ya ajabu) ambayo inaongoza katika njia iliyonyooka nasi tunaiamini”. Kisha MwenyeziMungu akamshushia aya hii,
“Sema, ‘Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikia...”(Qur’an) (72:1). Hii ni kwamba MwenyeziMungu alimfahamisha Mtume kile walichosema majini.
Ujumbe wa majini
Tukio lililosimuliwa hapo juu lilikuwa ni tukio la kwanza kwa majini kuusikia ujumbe wa Mtume (Salallahu alaihi wasalam). Waliisikiliza Qur’an bila Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kujua kama walikuwepo (hakuwaona). Kundi moja kati yao likaamini na kurudi kwa wenzao kuwasambazia ujumbe huu.
Baada ya tukio hilo, ujumbe wa majini ukamfikia Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kupata elimu fulani kwake. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akawapa ahadi na baadae akakutana nao na kuwafundisha yale ambayo MwenyeziMungu kayaaamrisha kwao. Na akawasomea Qur’an na kuwapa habari za mbinguni
Tukio hili la pili lilitokea Maka kabla ya Mtume kuhamia Madina. Muslim katika Kitabu chake, Sahih, na Ahmad katika kitabu chake Musnad wamenakili Hadith kutoka kwa Alqama kuwa alipata kumuuliza Abdullah ibn Masud kama kulikuwa na mtu yeyote aliyemsindikiza Mtume (Salallahu alaihi wasalam) usiku huo aliokutana na majini, Ibn Masud akasema “hapana, hakuna yeyote kati yetu aliyekwenda.
Lakini tulikuwa pamoja na Mtume (Salallahu alaihi wasalam) usiku huo na tukapotezana nae. Tukamtafuta hadi kwenye mabonde na vilima na tukaambizana, “huenda labda amechukuliwa (na majini) au ameuawa kwa siri.
Akasema, “ Tuliishi katika usiku m-baya ambao watu hawakuwahi kuishi’. Alfajiri ndio tukamuona anakuja akitokea upande wa Hiraa. Tukamwambia, ‘Mtume wa Allah tulipotezana nawe na kukutafuta lakini hatukukuona na tukaishi katika usiku mbaya ambao watu hawajapata kuishi’
.
Mtume (Salallahu alaihi wasalam) akasema, “alikuja kwangu jamaa fulani kuniita kwa niaba ya majini, na nikaondoka naye (hadi kwa wenziwe) ambako niliwasomea Qur’an’. (Ibn Msud) akasema, ‘Halafu (Mtume) akaenda nasi kutuonesha mabaki ya vijinga vyao vya moto’. Majini hao walimuuliza Mtume kuhusu chakula chao, naye akawaambia, ‘Kila mfupa uliosomewa jina la Allah ni chakula chenu. Muda ule ule mfupa unapotua mikononi mwenu, utavikwa nyama. Na kinyesi cha ngamia ni chakula cha wanyama wenu.’”
Na pia ipo riwaya hii kutoka kwa ibn Masud katika kitabu cha al-Tabari, “Nilipitisha usiku mmoja nikiwasomea majini Qur’an mahali paitwapo al-Hujuun (ndani ya Maka).
Miongoni mwa aya alizowasomea ni ni Surati al-Rahmaan. Katika Hadith nyingine Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema, “Nilisoma (surati Rahman) kwa majini katika usiku wa majini nao wakiitikia kwa mwitiko bora kuliko mlivyofanya nyinyi. Nilipofikia sehemu inayosema, “ni ipi kati ya neema za Mola wenu mnayoikanusha?” Wakaitikia, ;hakuna neema yoyote kati ya neema zako tunayoikanusha. Na sifa ni zako” (hii ilinakiliwa na al-Bazaar , al-Hakiim na ibn Jarir ikiwa na isinadi sahihi. Taz. Al-Albani, Sahih al-jaamii, juz. 1, uk. 30)
Haikuwa mara hiyo moja tu Mtume kuwasomea majini bali mikutano yake na majini ilifanyika mara nyingi baadae. Katika sherehe yake ya surati al-Ahqaaf, ibn Kathiir kanakili Hadith mbalimbali ambapo Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kakutana na majini.
Katika baadhi ya Hadith hizo, inaelezwa kuwa ibn Masud alikuwa karibu sana na Mtume (Salallahu alaihi wasalam) usiku huo.
Katika Hadith iliyonakiliwa katika Sahih al-Bukhari, kuna maelezo ya baadhi ya majini waliotoka sehemu iitwayo Nasiib nchini Yemen kwenda kumtembelea Mtume (Salallahu alaihi wasalam). Bukhari kanakili Hadith kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mtume (Salallahu alaihi wasalam) kasema,
“Ujumbe wa majini wa Nasiib (sehemu ya Yeman) ulinijia-nao walikuwa ni majini wema walioje-na wakaniuliza vyakula vyao, Nikawaombea dua kwa MwenyeziMungu kuwa wasiupite mfupa wowote au kinyesi cha mnyama isipokuwa wakuta chakula chao juu yake.”
Majini kuwahubiria binadamu
Katika baadhi ya Hadith sahihi kuna riwaya kuwa baadhi ya majini walichangia kuwaongoa wanadamu kadha wa kadha. Katika Sahih Bukhari, imenakiliwa kuwa Umar ibn al-Khatab alimuuliza mtu mmoja aliyekuwa mtabiri zama za ujahili kuhusu jambo moja la ajabu ambalo jini wa kike wa mtabiri kapata kumfahamisha
Mtabiri huyo akamwambia Umar hivi, “siku moja mwanamke huyo jini alinijia katika hali ya hofu. Akasema, ‘Hivi wewe hujaiona hali ya kukata tamaa na kushindwa waliyonayo majini (yaani hali ya kushindwa kupata habari za mbinguni), na kwa sababu hiyo, sasa wanawafuata waendesha ngamia tu’”.
Umar akasema, ‘huo ndio ukweli’ (Mtabiri huyo) akasema, nilikuwa nikilala jirani na masanamu ambapo alikuja mtu mmoja aliyekuwa na ndama wa ng’ombe ambaye alimtowa muhanga kwa ajili ya sanamu. Ndama huyo akapiga yowe ambalo sijawahi kusikia mfano wake.
Ndama huyo alisema, ‘”ewe Julaih, ewe muovu jeuri, una jambo la mafanikio mbele yako. Mtu mwenye kauli njema, anasema, ‘Hakuna wa kuabudiwa isipokuwa MwenyeziMungu’.
(watu kusikia hivyo, wakapatwa na woga), wakatimua mbio kutoka mahali hapo. Yowe hilo likaja kusikika tena. Mimi nikaondoka halafu siku chache baadae, watu wakawa wanasema, ‘Nabii katokea..”’
Baada ya kunakili Hadith katika sherehe yake ya Surat al-Ahqaaf. Ibn Kathiir kaandika hivi: “Hii ni matini ya Bukhari. Al-Baihaqi naye kanakili kitu kama hiki kutoka kwa ibn Wahb.” Kisha akasema, ‘ni wazi kuwa riwaya hii inafuata dhana ile ile potofu kuwa alikuwa ni Umar aliyepiga yowe hilo wakati mnyama huyo akitolewa muhanga. Jambo hili linabainishwa kwa Hadith dhaifu kutoka kwa Umar. Riwaya nyingine zote zinamtaja mtabiri kuwa ndiye aliyesimulia kile alichokiona na kukisikia. MwenyeziMungu ndiye ajuaye.” Kisha akaongeza kuwa, “mtu huyo aliyekuwa mtabiri alikuwa ni Sawaad ibn Qaarib”.
Kuamrisha mema na kuwa mashahidi kwa Waislamu
Ile Hadith ya Mtume (Salallahu alaihi wasalam) inasema kuwa jini wa Mtume alisilimu na akawa anamuhimiza Mtume kufanya mambo mema tu kama itakavyoelezwa huko mbele.
Abu Sa’id al-Khudhri alimwambia Abu sasa al-Ansari, “Mimi nakuona wewe kama kondoo na pori. Hivyo, unapokuwa na kondoo wako au uwapo porini, piga adhana ya Sala, basi ima binadamu au jini au kiumbe yeyote yule atakuwa shahidi wa adhana hiyo Siku ya Kufufuliwa”. Abu Sai’id akaongeza kusema, “mimi nilisikia hivyo kwa Mtume wa Allah” (imenakiliwa na Bukhari). Akasema kuwa majini waliosikia adhana ya Sala watakuwa mashahidi wake Siku ya Kufufuliwa.
Majini wana daraja tofauti za wema na uovu
Majini wana matabaka mbalimbali. Baadhi yao ni watiifu watendao mema na kuishi maisha ya uchaMungu. Wengine wako katika kiwango chini cha wema na uchaMungu, na wengine ni wakaidi, na wengine ni makafiri kabisa, na hawa ndio wengi mno.
MwenyeziMungu anawaezea hivi wale majini walioisikiliza Qur’an;
“Na hakika katika sisi wako wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tumekuwa njia mabalimbali.”
(72:11). Kwa maneno mengine baadhi yao ni wachaMungu kwelikweli, baadhi ni wachaMungu wa wastani na wengine ni wapotevu. Na wao wana njia na fikra tofauti kama walivyo wanadamu.”
MwenyeziMungu anawanukuu majini wakisema;
“Nasi wamo miongoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu wanaosilimu hao ndio waliofuata uwongofu. Na wanaokengeuka hao watakuwa kuni za jahanamu” (72:14-15).
Kwa maneno mengine baadhi yao ni Waislamu na wengine wamedhulumu nafsi zao kwa ukafiri. Yeyote yule ambaye amesilimu amejielekeza katika njia ya uwongofu kwa matendo yake na ambaye amedhulumu nafsi yake atakuwa kuni Jahanamu.
Asili ya Ibilisi
MwenyeziMungu amewapa majini hiyari ya kuwa waumini au makafiri ambapo huyu Ibilisi mwanzoni alikuwa akimuabudu Allah pamoja na Malaika. Kabla hajawa muasi.
Alipoasi akauridhia uovu na kuuhangaikia ijapokuwa uovu utakuwa sababu ya kuadhibiwa kwake. Aliridhia kufanya maasi na kuwachochea wengine kufanya maovu
“(Shetani) akasema, ‘Na-apa kwa haki ya utukufu wako, bila shaka nitawapoteza wote (hao watoto wa adui yangu-Adam). Isipokuwa wale waja wako waliosafishwa”. (38:82-83)
Hali ni hiyo hiyo kwa binadamu. Nafsi ya mtu ikiwa ovu, hutamani kile kinachoidhuru na huridhika na matendo maovu. Kwa hakika nafsi hiyo, kwa mapenzi huyafurahia maovu hata kufikia kiwango cha kumuharibu mtu, kuharibu dini, kuharibu maadili, afya ya mwili na mali.
Itoshe tu kutoa mfano wa wale wanaokunywa pombe, au wanaovuta sigara. Vitu hivi humdhuru hata kumuua yule anayevitumia. Ingawaje vinaweza kumsababishia mtu kifo lakini bado mtu hushindwa kuviacha isipokuwa kwa ugumu.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
