Skip navigation.
Home kabah

Mfululizo Wa Mada Ya Majini (10)

(Na Prof. Dkt. Sheikh Umar Suleiman al-Ashqar)

imefasiriwa na Shaibu H.Kifea

 

Majini Kuwahubiria Binaadamu
Je Jini, Shaytwaan Anaweza Kusilimu?


Katika baadhi ya Hadith sahihi kuna riwaya kuwa baadhi ya majini walichangia kuwaongoa wanadamu kadha wa kadha. Katika Sahih Bukhari, imenakiliwa kuwa Umar ibn al-Khatab alimuuliza mtu mmoja  aliyekuwa mtabiri zama za ujahili kuhusu jambo moja la ajabu ambalo jini  wa kike wa mtabiri huyo kapata kumfahamisha.

 Mtabiri huyo akamwambia Umar hivi, “siku moja mwanamke huyo jini alinijia katika hali ya hofu. Akasema, ‘Hivi wewe hujaiona hali ya kukata tamaa na kushindwa waliyonayo majini (yaani hali ya kushindwa kupata habari za mbinguni), na kwa sababu hiyo, sasa wanawafuata waendesha ngamia tu’”.

Umar akasema, ‘huo ndio ukweli’ (Mtabiri huyo) akasema, nilikuwa nikilala jirani na masanamu ambapo alikuja mtu mmoja aliyekuwa na ndama wa ng’ombe ambaye alimtowa muhanga kwa ajili ya sanamu. Ndama huyo akapiga yowe ambalo sijawahi kusikia mfano wake.

Ndama huyo alisema, ‘”ewe Julaih, ewe muovu jeuri, una jambo la mafanikio mbele yako. Mtu mwenye kauli njema, anasema, ‘Hakuna wa kuabudiwa isipokuwa MwenyeziMungu’.  

(watu kusikia hivyo, wakapatwa na woga), wakatimua mbio kutoka mahali hapo. Yowe hilo likaja kusikika tena. Mimi nikaondoka halafu siku chache baadae, watu wakawa wanasema, ‘Nabii katokea..”’

Baada ya kunakili Hadith hii katika sherehe yake ya Surat al-Ahqaaf. Ibn Kathiir kaandika hivi: “Hii ni matini ya Bukhari. Al-Baihaqi naye kanakili kitu kama hiki kutoka kwa ibn Wahb.” Kisha akasema, ‘ni wazi kuwa riwaya hii inafuata dhana ile ile potofu kuwa alikuwa ni Umar aliyepiga yowe hilo wakati mnyama huyo akitolewa muhanga. Jambo hili linabainishwa kwa Hadith dhaifu kutoka kwa Umar. Riwaya nyingine zote zinamtaja mtabiri  kuwa ndiye aliyesimulia kile alichokiona na kukisikia. MwenyeziMungu ndiye ajuaye.” Kisha akaongeza kuwa, “mtu huyo aliyekuwa mtabiri alikuwa ni Sawaad ibn Qaarib”

                                          Kuamrisha mema na kuwa mashahidi kwa Waislamu

Ile Hadith ya Mtume (salallahu alaihi wasalam) inasema kuwa jini wa Mtume alisilimu na akawa anamuhimiza Mtume kufanya mambo mema tu kama itakavyoelezwa huko mbele.

Abu Sa’id al-Khudhri alimwambia Abu sasa al-Ansari, “Mimi nakuona wewe kama kondoo na pori. Hivyo, unapokuwa na kondoo wako au uwapo porini, piga adhana ya Sala, basi ima binadamu au jini au kiumbe yeyote yule atakuwa shahidi wa adhana hiyo Siku ya Kufufuliwa”.

Abu Sai’id akaongeza kusema, “mimi nilisikia hivyo kwa Mtume wa Allah” (imenakiliwa na Bukhari). Akasema kuwa majini waliosikia adhana ya Sala watakuwa mashahidi wake Siku ya Kufufuliwa.

                                       Majini wana daraja tofauti za wema na uovu

Majini wana matabaka mbalimbali. Baadhi yao ni watiifu watendao mema na huishi maisha ya uchaMungu. Wengine wako katika kiwango chini cha wema na uchaMungu, na wengine ni wakaidi, na wengine ni makafiri kabisa, na hawa ndio wengi mno.

MwenyeziMungu anawaezea hivi wale majini walioisikiliza Qur’an;

“Na hakika katika sisi wako wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo, tumekuwa njia mabalimbali.” (72:11).

Kwa maneno mengine baadhi yao ni wachaMungu kwelikweli, baadhi ni wachaMungu wa wastani na wengine ni wapotevu. Na wao wana njia na fikra tofauti kama walivyo wanadamu.”

 MwenyeziMungu anawanukuu majini wakisema;

“Nasi wamo miongoni mwetu waliosilimu na wamo miongoni mwetu wanaokengeuka, na waliosilimu, hao ndio waliofuata uwongofu. Na wanaokengeuka hao watakuwa kuni za jahanamu” (72:14-15).

Kwa maneno mengine baadhi yao ni Waislamu na wengine wamedhulumu nafsi zao kwa ukafiri. Yeyote yule ambaye amesilimu amejielekeza katika njia ya uwongofu kwa matendo yake na ambaye amedhulumu nafsi yake atakuwa kuni Jahanamu.

Asili ya Ibilisi

 

MwenyeziMungu amewapa majini  hiyari ya kuwa waumini au makafiri ambapo huyu Ibilisi mwanzoni alikuwa akimuabudu Allah pamoja na Malaika. Kabla hajawa muasi.

Alipoasi akauridhia uovu na kuuhangaikia ijapokuwa uovu utakuwa sababu ya kuadhibiwa kwake. Aliridhia kufanya maasi na kuwachochea wengine kufanya maovu.

“(Shetani) akasema,  ‘Na-apa kwa haki ya utukufu wako, bila shaka nitawapoteza  wote (hao watoto wa adui yangu-Adam). Isipokuwa wale waja  wako waliosafishwa”. (38:82-83)

Hali ni hiyo hiyo kwa binadamu. Nafsi ya mtu  ikiwa ovu, hutamani kile kinachoidhuru na huridhika na matendo maovu. Kwa hakika nafsi hiyo, kwa mapenzi huyafurahia maovu hata kufikia kiwango cha kumuharibu mtu, kuharibu dini, kuharibu maadili, afya ya mwili na mali.

Itoshe tu kutoa mfano wa wale wanaokunywa pombe, au wanaovuta sigara. Vitu hivi humdhuru hata kumuua yule anayevitumia. Ingawaje vinaweza kumsababishia mtu kifo lakini bado mtu hushindwa kuviacha isipokuwa kwa ugumu.

 

                                      Je shetani wa kijini anaweza kusilimu?

 

 Ni dhahiri kuwa kwa mujibu wa Hadith, inawezekana kwa shetani wa kijini kusilimu kama alivyosilimu shetani wa kijini wa Mtume (salallahu alaihi wasalam). Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wanaikataa kauli hii na kusema kuwa shetani wa kijini hawezi kuwa muumini. Mufasiri wa al-Aqiida al-Tahaawiya yeye rai yake ni hiyo ya pili.

Watu wa kundi hili wanatoa hoja kuwa neno aslam (lililotajwa katika Hadith kuhusiana na kusilimu kwa shetani wa kijini wa Mtume lina maana kuwa jini-shetani huyo alitii sheria za Kiislamu (bila yakini wala imani).

Baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa kauli sahihi ni ile ya Mtume (saw) kusema, “mimi nimesalimika naye”. Mfasiri wa al-Tahaawiya yeye ana rai kuwa kuliweka neno aslam katika kiima ni makosa. 

Lakini al-Nawawi, katika tafsiri yake ya Sahihi Muslim kasema, “Hizo ni kauli mbili zilizothibitishwa.” Yeye anasema kuwa al-Khaatabi anaona kuwa kauli  yenye nguvu zaidi ni ile yenye dhamma (yaani ile yenye neno katika kiima).

Miongoni mwa wale wasemao kuwa shetani wa kijini anaweza kusilimu ni ibn Hiban. Akisherehesha Hadith iliyotajwa hapo, kasema, katika riwaya  hii, kuna ashahidi kuwa shetani wa kijini wa Mtume ((salallahu alaihi wasalam) alisilimu na hakumchochea Mtume ((salallahu alaihi wasalam)) kufanya kingine chochote ila mambo mema. Pamoja na hivyo Mtume wa Allah alikuwa amesalimika hata kama shetani alikuwa kafiri.”

Kuna hatihati kuhusiana na rai ya Mfasiri wa al-Aqiida al-Tahaawiya kwamba shetani wa kijini anabakia kuwa kafiri tu. Kama ana maana kuwa neno shetani hutumika tu kwa majini waliokufuru, basi rai hiyo ni sahihi.

Lakini kama ana maana kuwa shetani wa kijini hawezi kubadilika na kusilimu , basi rai yake iko mbali na usahihi ambapo Hadith hiyo ni ushahidi dhidi yake.

Kwa mtazamo wa kisheria, haionekani kuwa sahihi kwamba majini waliokufuru wawajibike kwa matendo yao halafu tena, wakati huo huo, wasiweze kusilimu.

Majini wataadhibiwa ikiwa ujumbe umewafikia na kuukanusha. Hii tu inaonesha kuwa na wao wana uhuru wa kuwa waumini au makafiri. Ndiyo kusema, na wao pia wanaweza kuwa Waislamu kama wanataka kuwa hivyo.

     Uadui kati ya Ibilisi na Mwanadamu

Sababu ya uadui, historia yake na ukubwa wake

Uadui kati ya wanadamu na Ibilisi mzizi wake ni kadhia iliyotokea muda mrefu huko nyuma. Msomaji rejea nyuma kabisa hadi siku ambayo MwenyeziMungu Alimuumba Adam, kabla hajampulizia roho iliyotokana na Yeye.

Shetani akamzunguukia na kusema, “(we Adam) ukipewa mamlaka juu yangu, kwa kweli, mimi nitakuasi. Na nikipewa mamlaka juu yako, nitakuangamiza.”

Katika Sahihi Muslim, imenakiliwa Hadith kutoka kwa Anas kuwa Mtume ((salallahu alaihi wasalam)) kasema, “MwenyeziMungu alipomuumba Adam Peponi, alimuacha kwa kitambo alichotaka ambakishe huko. Ndipo Ibilisi alipomzunguukia kutaka kuona kuwa yeye ni kitu gani hasa, na alipoona kuwa yu mtupu kwa ndani, akatambua kuwa kiumbe mpya kaumbwa akiwa na umbile ambalo lisingejimiliki lenyewe”.

MwenyeziMungu alipompulizia Adam roho iliyotokana naYeye, akawaamuru Malaika wamsujudie. Ibilisi  alikuwa akimuabudu Allah pamoja na Malaika, hivyo, naye amri hii ilimuhusu.

Lakini yeye akajiona bora na kwa majivuno, akakataa kumsujudia Adam. Alijigamba, “mimi ni bora kuliko Yeye. Mimi umeniumba kwa moto na Yeye umemuumba kwa udongo.”

Na pale Adam alipofumbua macho yake akaona ishara ya utukufu na fadhila, Malaika wakimsujudia. Lakini pia aliona uadui mkubwa ukimsubiri, ni uadui wa kumpotosha na kumpeleka yeye na kizazi chake katika maangamizi.

Ibilisi alitolewa nje ya Pepo kutokana na majivuno yake lakini akaomba muda kwa MwenyeziMungu aachwe hai hadi Siku ya Hukumu

 “Akasema, ‘nipe muda (nisife) mpaka Siku watakapofufuliwa (viumbe).”  (7:14). Kiumbe huyu aliyelaaniwa alitoa ahadi na kula kiapo kuwa atakipoteza kizazi cha Adam na atawafanyia hila.

“(MwenyeziMungu) Akasema: “Utakuwa miongoni mwa waliopewa muda.’ Akasema, ‘Kwa kuwa umenuhukumia upotevu basi nitawakalia (waja) wako) katika njia Yako iliyonyooka. Kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta (hutawaona) wenye kushukuru”. (7:15-17).

Kauli hii ya mwisho inaonesha ukubwa wa vita vyake vya kuwapotosha wanadamu. Atatega kila njia aiwezayo dhidi yao, kuliani kwao, kushoto, mbele na nyuma yao.

Atawapiga vita kila upande. Katika sherehe yake ya aya hii, Alzamakhshari kaandika hivi: “atawajia pande zote nne kama ilivyo kawaida ya adui, yeye ndio atakuwa mchochezi wao. Pia atawarubuni kwa njia yoyote aiwezayo. Qur’an inasema;

“Na wavute uwawezao miongoni mwao kwa sauti yako, na uwakusanyie (jeshi lako la) wapanda farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali (yao) na watoto (wao), na waahidi (ahadi za uwongo). Lakini shetani hawapi waadi ila kwa udanganyifu.” (17:64).