Skip navigation.
Home kabah

Tawassul - 1 Nini Tawassul Au Wasila?

 





Idara ya 'Da'awah, Habari, Utafiti, Tahariri Na Uandishi

Ansaar Muslim Youth Centre

"Tawassul" Ni neno lenye kusikika Sana hasa siku hizi ambapo kumejitokeza baadhi ya walimu humu mwetu kutetea Tawassul zisizofaa kisheria kwa sababu tu walimu hao wamezifanya ndio kitega uchumi kikubwa katika maisha yao. Hivyo pale walipojitokeza vijana watetezi wa Dini na sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)(ANSWAAR) kuhadharisha ndugu zao Waislam na utapeli unaofanywa na walimu hao kwa jina la dini basi walimu hao wamekua wakali sana kutetea ‘ulua’ huo, na kutumia Aya na Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kuzifasiri wanavyotaka wao au kutumia Hadithi za Uongo ilimradi tu "ulua" wao uendelee.

Kwa sababu Waislamu wengi waliingia katika mtego huu ilikua mtu hawezi kuanzisha biashara, kuhamia nyumba mpya au kununua gari mpaka amwite mwalimu amsomee ‘Tawassul’ ima ya ‘Nabahan’ au ‘Ahalalbadri’ au nyinginezo bila ya kujua hakika ya Tawassul hizo na hukmu yake kisheria.

Makala hii itaweka wazi kila jambo linalohusiana na Tawassul, nini maana ya Tawassul kilugha, nini maana ya Tawassul kisheria (kidini) ni aina gani ya Tawassul zilizokubaliwa kwa mujibu wa mafunzo ya Qur’aan na Sunnah sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na ni Tawassul gani zisizofaa na kwa nini? Hoja zinazotegemewa na watetezi wa Tawassul zisizofaa na majawabu yake. Lengo la makala hii ni kumuelimisha Muislamu mambo yaliyofichwa muda mrefu na walimu wetu ima ni kwa uchache wa elimu au kwa sababu ya maslaha yao ya kidunia.

Ewe ndugu yangu msomaji wa makala hii jitahidi kufuatilia mfululizo wa makala haya na InshaAllah utajikuta katika hali ya kujikomboa kidini na kiuchumi, na kutokubali kuchezewa tena. Nakutakia usomaji mwema na wenye manufaa.

NINI MAANA YA TAWASSUL KILUGHA?

Neno moja linaweza kuwa na matumizi mawili, matumizi ya kawaida ya kilugha, na matumizi maalum ya kiistilahi (kielimu) mfano neno "Swala" ni la kiarabu maana yake kilugha ni "Dua" lakini kisheria au kidini ni: maneno na vitendo maalum anavyofanya mtu (Ibada) hufunguliwa na Takbira na hufungwa na salamu yaani hii Swala tunayo Swali misikitini.

Hivyo hivyo neno "Wasila" lina matumizi ya kilugha na matumizi ya kidini, hebu tuangalie kamusi zinasemaje. Katika kamusi Al-muhiit ya mwanachuoni Feiruz Abaadiy (amekufa mwaka 817 H) anasema hivi:-

‘Wasila’ Ni heshima maalum mbele ya mfalme au cheo na kujikurubisha (uk. 1379) Na katika kamusi ya "Mukhtaru Swihah" ya Muhammad Arraaziy (alikufa mwaka 666 H) anasema:-

"Wasila ni kila kinachotumika kumkurubisha mtu kwa mwingine (uk. 721).

Kwa maana hizo hapo juu, lolote afanyalo mtu kujikurubisha na chengine chochote basi itakua ni "Wasila" kilugha. Hii inamaana hata mtu akimpa mtu mwingine, kama vile Bosi wake kazini akimpa Rushwa au Glasi ya pombe Ili apendeze na kujikurubisha kwake ili apate cheo basi hiyo Rushwa au Glasi ya pombe kilugha itakua ni "Wasila"

NINI MAANA YA WASILA KIDINI (KISHERIA)?

Neno Wasila kisheria lina maana mbili:-

Kwanza: Ni ile heshima maalum "Manzila" Atakayo pewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)huko peponi nako ni kupewa pepo ya daraja ya juu, na maana hii tunaipata katika Hadithi ya Mtume (s.a.w.). Ifuatayo:

Imepokewa Na Abdullah bin Amru Al-Aaswi (Radhiya Allaahu ‘anhu)kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akisema: Mtakapomsikia muadhini basi semeni Kama anavyosema, kisha niswalieni, kwani mwenye kuniswalia mara moja Mwenyeezi Mungu (S.W.) Atamswalia mara kumi, na kisha niombeeni (kupata) "WASILA" ambayo Ni (heshima maalum) Manzila huko peponi. Haitomstahikia ispokua mja mmoja katika waja WA Mwenyeezi Mungu, nami ninatarajia kuwa mja huyo, na mwenye kuniombea "Wasila" atapata uombezi (wangu siku ya kiyama)

"Imepokewa na Muslim".

MAANA YA PILI YA WASILA KISHERIA.

Ni kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  kwa matendo ya ibada na Twaa kama alivyotufundisha Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kama vile kuswali, kufunga, kutoa zaka, kuhiji, kuomba dua na kutekeleza yale yote aliyotuamrisha Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na kujiepusha aliyotukataza nayo.

Na maana hii inajitokeza katika Qur’aan Aya ya 35 sura ya Al-maida, Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  Aliposema:

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyeezi Mungu na tafuteni "Wasila" (na tafuteni njia ya kumfikilia Mwenyeezu Mungu).

Wamekubaliana wafasiri wote katika Maswahaba na Taabiina kwamba wasila ulio kusudiwa hapo juu ni kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu na kumtii. (Angalia tafsiri ya Qurtubiy Aya hii juzuu ya 6 uk.201, Tafsiri ya Ibni Kathiiry Aya hiyo Na Tafsiri ya Fathul Qadiir ya Shaukani na nyinginezo.

Na marehemu Sheikh Abdallah Saaleh, katika kusherehesha maana ya aya hii anasema hivi:-

"Al-wasila ni jambo linalo mfikisha mtu mahala Fulani au (linalo mpatia) kitu Fulani. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)amekwisha kusema katika Hadithi zake sahihi kuwa hakuna la kumsogeza mtu likamfikisha katika radhi ya Mwenyeezi Mungu, kama kutekeleza aliyomwamrisha na kujiepusha na aliyokataza." ( Angalia Tafsiri ya Sheikh Abdallah Saaleh Farsiy).

Basi kwa maana hii ya "Wasila" kisheria tuliyoifafanua , itafuta yale yote finyu waliyokuwa nayo Waislamu wengi kwamba wasila ni zile dua maalum tu, wanazoombewa na walimu kama vile kutawassal kwa jaha ya Masharifu wanapo fikwa na misiba/majanga au anapotaka mtu kheri fulani akasomewa. Na hayo ni mawazo yaliyopandikizwa na baadhi ya walimu hao kupotosha watu kusudi au kwa kutokujua maana halisi ya wasila kama ilivyo kusudiwa kisheria.

AINA ZA WASILA:

‘Wasila’ kwa maana pana hiyo tuliyoieleza hapo juu kisheria ni aina nyingi kwani ni mambo mengi sana aliyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)ya kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) , na mtu hawezi kuyajua ila arejee kwenye Qur’aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)sahihi, kwani kadri tunavyojiona ni Wacha Mungu au twaijua kheri inayotukurubisha kwa Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  basi hatumfikii Mtume (s.a.w.). na yeye ameshatufundisha aina zote za wasila zinazofaa kujikurubisha nazo kwa Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) .

Sio rahisi kutaja wasila zote alizotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)ila imekua ni wajibu kwetu kubainisha WASILA WA DUA, kutokana na utatanishi uliotiwa na baadhi ya walimu kwa nia ya kutaka watu wamshirikishe Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  na viumbe vyake, na kwa sababu ya kulinda maslahi yao ya kidunia, vile vile kutokana na mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)amesikiwa na Swahaba Nu’umaan bin Bashiir Akisema:

"Dua ndio Ibada hasa"

(Imepokewa na Tirmidhiy)

Hivyo imetupasa kuwabainishia Waislamu Ibada hii kama alivyotufundisha Mtume (s.a.w.), kwa sababu Ibada yoyote aifanyayo mtu ili akubaliwe na Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  ni lazima atekeleze masharti mawili makubwa:

1.       Mwenye kuifanya aifanye kwa kumkusudia Mwenyeezi Mungu tu peke yake (Ikhlaaswi).

2.       Ibada hiyo iwafikiane na sheria kama alivyobainisha Mtume (s.a.w.).

Isipo timia sharti yoyote katika sharti hizo mbili tendo Hilo la Ibada haliwezi kuhesabiwa kua ni la KHERI au kutakabaliwa na Mwenyeezi Mungu. Kwa hiyo DUA kwa maana ya kumwita au kumuomba kwa unyenyekevu unaemuhitajia, tunaona Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  ametaka aombwe Yeye tu na asishirikishwe na yeyote kwa sababu ni Yeye tu Alietajiri wa kweli na Anaestahiki kudhalilikiwa na viumbe vyake vyote vinamuhitajia Yeye tu, ndio maana Akasema:-

"Na Amesema Mola wenu: Niombeni Mimi Nitakujibuni"

(Al Muumin: 60)

Na Amesema tena Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) :

"Na waja wangu watakapo kuuliza Hakika Yangu (waambie kua) Mimi Niko Karibu Nao Naitika Maombi ya Mwombaji Anaponiomba"

(Al- Baqarah: 86)

"Na Amesema:

Na Wala Msiwaombe Badala ya Mwenyeezi Mungu Wale Ambao Hawawezi Kukunufaisheni Wala Kukudhuruni Basi Ukifanya (hivyo) Utakua Miongoni Mwa Madhalimu".

(Yunus: 106)

Aina za Wasila katika Ibada ya Dua Kwa mujibu WA Qur’aan Na Sunnah sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Ni Tatu nazo Ni hizi zifuatazo:-

Kwanza: Ni kumuomba Mwenyeezi Mungu moja kwa moja kwa kupitia majina Yake Matukufu, kwa agizo lifuatalo.

Amesema Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) :

"Na Mwenyeezi Mungu Ana Majina Mazuri, Basi Muombeni Kwa Majina Hayo"

(Al-A’araaf: 180)

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Ametuelekeza namna ya kuomba kupitia Majina Matakatifu ya Mwenyeezi Mungu. Kuna

Hadithi nyingi zinazotupa muongozo huo, na baadhi yake ni kama ifuatayo:-

Imepokewa Na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu)kwamba Mtume (s.a.w.): Alikua Akihuzunishwa Na jambo Akisema: "Yaa Hayyu (Ewe ulie hai) Yaa Qayyum (Ewe msimamia kila jambo). Ninataka Msaada Kwa Rehema Yako.

(Imepokewa na Tirmidhiy)

Na katika Hadithi nyingine:

Imepokewa na Muadh bin Jabal, kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Alimsikia mtu akisema: Yaa dhal Jalaali Wal Ikraami (Ewe Mwenye Utukufu Na Heshima) Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Umeshaitikiwa Mwito Wako, Omba (utakalo).

(Imepokewa na Tirmidhiy)

Na maana hii ya Tawassul Kwa majina ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  katika Dua bila kupitia Kwa watu au mambo mengine, ndio dua ya Asili, Na hili linakubaliwa Na hata watetezi wa bid’aa,

Kwa mfano katika kitabu cha Muhammad Alawiy Al-Malikiy (tegemeo la watu wa Bid’aa alichokiita "Mafahiim yajib an tuswahah" Uk 118 amesema hivi:"Wasila ni kila alichokijaalia Mwenyeezi Mungu kua ni sababu katika kujikurubisha, na kiungo cha kukidhi haja kutoka kwake".

Na amesema katika UK. 116 WA kitabu chake (chapa ya 4 mwaka 1990):

Hakika kutawassal (kuomba Kwa kupitia viumbe) sio jambo la lazima au la dharura Na kujibiwa hakutegemei (Tawassul) hiyo, bali lililokua la asili, ni kumuomba Allah moja kwa moja, kama alivyosema Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) . "Atakapo kuuliza mja wangu kuhusu Mimi basi Mimi niko Karibu.

Basi hili ndio tamko rasmi la bunge la watu wa Bid’aa, nae anakiri kwamba kutawassal kwa jaha ya Masharifu waliokufa sio jambo la lazima wala Tawassul hizo hazina gerentii ya kujibiwa,

Kwani Tawassul yenye gerentii ni ile ya kumuomba Mungu moja Kwa moja kwa Majina yake Matukufu kwani Yeye yuko Karibu sana na muombaji kumkidhia haja yake. Sasa basi mbona watetezi wa Bid’aa hawatekelezi mafunzo ya Mashekh na Masharifu wao, kwani Ahlul Bid’aa wamefanya Tawassul kwa jaha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na Masharifu wa hadharamaut (Yemen ya Kusini) ndio tegemeo lao kubwa, wakitegemea kwamba kujibiwa Dua zao kwa jaha ya watu hao ni jambo la gerentii, na wamewadanganya Waislamu muda mrefu sasa kua Dua hizo ni "mujarrab" (Experimented) yaani hapo kwa hapo hujibiwa, kila mwenye kusomewa atapata atakacho, hivyo wametengeneza vijitabu maalum kama vile ,Wasilatu Shafii, " thalathu wasail" "Ahlul Badri" na kuwapa walimu wao kujitengenezea rizki zao kwa njia ya mkato, na watu wengi walihadaika na utapeli huu ikawa kila mwenye kufungua duka au kuanza biashara yoyote , au kununua gari jipya au kuhamia nyumba mpya, basi humuita mwalimu kumsomea Tawassul hizo kwa jaha ya Masharifu hao waliokufa wakiitakidi kwamba dua hizo ni gerentii zitakubaliwa mara moja.

Na watu wengi waliingia mtegoni kiasi cha mtu kushindwa kuomba Dua mwenyewe kwa kutumia Majina ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  kama ile dua fupi aliyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alipomsikia mtu akisema "Yaa dhal Jalaali wal Ikrami Akamwambia omba, Mungu atakuitikia mara moja" Dua kama hizi si rahisi Ahlul Bid’aa kuwabainishia watu, kwa sababu ni nyepesi mno na zina gerentii kuliko Dua za kutawassal kwa jaha za Masharifu kama alivyo bainisha sharifu lao Al Maalikiy" kama tulivyoona hapo nyuma, na wanafanya hivi kusudi kwa sababu watu wakigundua wepesi huo basi itakua wamejizibia madongo katika riziki, ndio maana Ahlul Bid’aa wal Hawaa wametengeza hadharani usiku wa tarehe 20.11.93, uhalali wa jambo hili, Ili wateja wao wasivunjike nguvu lakini wapi! Unaweza mdanganya mtu siku moja lakini huwezi kudanganya watu wote siku zote, Elimu sasa ziko wazi wazi zinatolewa bila ya khiyana, na sio elimu za choyo ambazo mtu hapati ila kwa kuwadhalilikia Mashekhe na Masharifu wanaopenda kuabudiwa na kusota hadi kutoboa makanzu chini ya miembe, halafu mtu anavishwa kilemba cha ukoka nae kwa ujinga anajiona amesha maliza elimu zote na kutakabbar.

Waislamu Leo wamechoka kudhulumiwa Na InshaAllah watakombolewa hivi karibuni Na makucha ya madhaalim.

Tutatoa ushahidi kamili hapo baadae juu ya kutofaa kwa tawassul za jaha ya Masharifu. Na ushahidi wa kimatendo unao onyesha kwamba tawassul za kupitia jaha ya Masharifu hazifai ni pale Ahlul Bid’aa walipokua wakiomba usiku na mchana Tawassul hizo ili kuwaangamiza watu wa Ahlul Sunnah, na kuwaahidi waislamu kwamba vijana hawa walokuja na dini mpya tutawasambaratisha kwa Dua za Tawassul matokeo yake Sunnah imezagaa na kuenea kila pahala na watu kuijua haki na kutoka katika ujinga. Alhamdulillahi na tunasema Waislamu kwa Idhni ya Allah wataelimika na kuendelea kutoka katika ujinga kwani Elimu ya haki imeenea kila pahala.

AINA YA PILI YA TAWASSUL KATIKA DUA:

Huku ni kuomba dua kwa kupitia matendo mema aliyofanya mtu binafsi katika uhai wake, yawe ni matendo ya moyo au kiwiliwili, kama vile kusema:

"Ewe Mwenyeezi Mungu, Kwa ile imani ya mapenzi yangu kwako, Kwa kumfuata kwangu Mtume wako basi nisamehe madhambi yangu".

Au Kwa kule kumpenda kwangu Mtume wako Na kumuamini basi niondolee au nipe jambo kadhaa.

Na Tawassul hii ya matendo ya mtu ayafanyayo moyoni kama vile kumpenda Mwenyeezi Mungu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Itakua ni ya maana na ya kweli itastahiki kujibiwa pale tu atakapo dhihirisha mtu mapenzi yake katika kutii na kumfuata Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na katika kutawassal kwa Dua ya kupitia matendo ya moyo kama vile imani. Amesema Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  kuhalalisha aina hii ya Tawassul:

"Ambao Wanasema:" Mola wetu, Hakika sisi tumeamini basi Tughufirie Madhambi yetu, Na tuepushe Na Adhabu ya Moto"

(Aali – Imraan: 16)

Na Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) :

"Mola wetu, Tumeyaamini uliyoteremsha, Na Tumemfuata Mtume, basi tuandike pamoja Na Mashahidi’’

(Aali - Imraan: 53)

Na katika ushahidi wa kutawassal kwa Dua ya kupitia matendo mema binafsi ya mtu aliyoyafanya kwa Ikhlaaswi,

Ni kile kisa mashuhuri alichopokea Swahaba Ibni Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na mukhtasari wake ni kama ifuatavyo: Watu watatu katika umma ulio tangulia walikua safarini, na ulipofika wakati wa kulala wakaingia pangoni, bahati mbaya likaanguka jiwe wakati wao wamo ndani likaziba mlango wa pango wakasema: Hakuna jambo litakalo tusaidia isipokua kuomba Dua kwa "Kutawassal" kwa matendo yetu mema. Hivyo mmoja akaomba Kwa kutaja alivyo watendea wema wazazi wake wawili Ili Mwenyeezi Mungu awafariji Na msiba huo. Basi hapo hapo sehemu Fulani ya jiwe lililoziba likanyanyuka Kwa kiasi cha kushindwa wao kutoka. Wa pili akaomba kwa kutaja kisa chake na binti ammi yake, alimpenda sana, na akamtaka kuzini nae, lakini yule Binti alikataa, hivyo alimdanganya kwa kumpa pesa Dirham mia na ishirini (120) ili amkubalie atakalo, na Mwanamke akakubali. Mume alipokua tayari kupata atakacho, Mwanamke akamkumbusha yule Mwanamme kua si haki kufanya hivyo, basi pale pale yule Mwanamme akakumbuka na kuacha tendo lile ovu, basi akaomba "Ewe Mola wangu nikiwa nilifanya hivyo kwa ajili yako basi tutoe kwenye dhiki hii tuliyo nayo! Pango likanyanyuka lakini Kwa kiasi ambacho hawakuweza kutoka. Wa tatu akataja aliwaajiri watu akawalipa mishahara yao isipokua mtu mmoja aliwacha malipo yake kwake akaondoka, Yule akaikuza mali hiyo hadi ikawa nyingi, baada ya muda akaja yule ambae aliacha mshahara wake akasema "nipe ujira wangu nilio acha" yeye akajibu "Ngamia, ng’ombe, mbuzi na watumishi wote hawa unaowaona ni mali yako, Ujira wako" yule bwana akasema: usinifanyie masikhara, ndipo akachukua haki yake yote. Basi akasema "Ewe Mola, ikiwa nimefanya tendo hili kwa kutaka radhi zako, basi tupe faraja yako katika hali hii tuliyonayo" Basi lile jiwe likafunguka lote ndipo walipotoka Na kwenda zao.

(Hadithi hii sahihi ipo Kwa urefu kwenye kitabu cha Bukhari)

AINA YA TATU YA KUTAWASSAL KWA DUA:

Ni kuwataka ndugu zako au ndugu yako alie hai mwema na Mcha Mungu akuombee dua ili Mwenyeezi Mungu akufariji na msiba ulio kufika. Au kuita kheri ya namna Fulani. Aina hii ya tawassul ina mifano mingi sana lakini tutataja baadhi kwa faida ya msomaji.

Wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.), watu wengi walimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kumtaka awaombee dua kwa kua na yakini kwamba dua za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)ni makubuli

Katika Hadithi iliyopokewa Na Tirmidhiy: Swahaba mmoja kipofu alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamwambia:

"Niombee kwa Mwenyeezi Mungu, Ewe Mtume wa Mwenyeezi Mungu anirejeshea uoni wangu, basi Mtume (s.a.w) Akamuombea, na ndipo Mwenyeezi Mungu akamrejeshea (bwana yule) uoni wake, akarejea (uzima wake) kama kwamba hajawahi kupatwa na dhara."

Hivyo hivyo anasimulia Swahaba Anas bin Maalik (r.a): Kwamba siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alikua akihutubia juu ya mimbari basi akajiwa na Bedui mmoja akamtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)awaombee Dua ili wapate mvua kutokana na ukame mkubwa uliowafika kiasi cha kupata balaa la njaa, basi pale pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)Akaomba mvua na Mwenyeezi Mungu akaitakabali dua ile na mvua zikanyesha hadi kuondoka balaa lile.

(Kisa hiki utakipata kwa urefu katika sahihul Bukhari)

Hali kama hii ilitokea zama za utawala wa Khalifa Ummar bin Al Khattaab huko Madina, na alichofanya Ummar (Radhiya Allaahu ‘anhu)ni kumwendea Swahaba Al- Abbaass bin Abdil Muttalib kutokana na wema na ucha Mungu wake, nae kweli aliwaombea Waislamu mvua, Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala)  Akateremsha mvua kiasi cha kuondoa shida ile.

(Kisa hiki utakipata kwa urefu katika sahihul Bukhari)

Hali kama hii pia ilijitokeza zama za utawala wa Swahaba Muawiya bin Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu)huko Damascus, alimuomba bwana mmoja Mcha Mungu anaitwa Yaziid bin Al-Aswad Al-Jurashiy awaombee dua basi yule bwana aliomba na hapo hapo Mwenyeezi Mungu akaitika dua yake na wakapata mvua ya kutosha.

(Kisa hiki sahihi utakipata kwa urefu kwenye kitabu Al – Aswaaba cha Ibni Hajar Al – Askalaaniy juzuu ya 3/sahifa 634).

Mambo tunayo jifunza katika visa hivyo hapo juu:

Kwanza: mtu yeyote Muislamu anaweza kumtaka nduguye Muislamu amuombee dua kwa kumdhania ni mtu mwema, na sio lazima awe ni koo ya Mtume (s.a.w.). Na hili linathibitishwa na Mwenyewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kwamba hata Yeye aliwahi kumtaka Swahaba wake Ummar bin Al – Khattaab amuombee dua katika hadithi iliyopokewa na Abuu Daaud na Tirmidhiy, alisikika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akimwambia Ummar (Radhiya Allaahu ‘anhu)wakati akitaka kwenda kufanya Ibada ya "Umrah" huko Makkah!

"Usitusahau ewe ndugu yangu katika Dua yako".

Mafundisho haya yanapinga ile itikadi iliyojengwa na Masharifu na Mashekhe bandia kujifanya wao ni wacha Mungu, kiasi ambacho, mtu kama si sharifu (koo ya Mtume) basi dua yake haikubaliwi hivyo hastahiki kuombea wenzie.

Hii ndio ilivyopelekea humu mwetu kila kukiwa na shughuli basi hutangulizwa sharifu (koo ya Mtume) kuombea watu dua ya ufunguzi wa shughuli hata kama inafahamika wazi kwamba sharifu yule si mtu mwema asilani, ana tabia ya uzinifu, mywa ulevi, mtafuna mirungi n.k. yote haya hawajali kwa madai kwamba sharifu yeyote ana makarama, basi akiomba tu hutakabaliwa, wamesahau mwongozo wa Mwenyeezi Mungu (Qur’aan) iliposema mwenye karama zaidi mbele ya Allah ni Mcha Mungu zaidi kwetu bila kujali koo yake.

Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)

"Hakika alie Mtukufu zaidi mbele ya Mwenyeezi Mungu Ni Mcha Mungu"

(Al – hujuraat: 13):

Pili: Haifai kuomba kupitia kwa mtu aliekufa kwa sababu tu ya jaha yake. Na lau kama ingefaa basi Ummar bin Al-khattaab (Radhiya Allaahu ‘anhu)asingeliacha kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)ambae ni bora kuliko Al-Abbaass, akapitisha maombi yake kwa alie hai Al-Abbaass (Radhiya Allaahu ‘anhu)ilihali kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)lipo hapo hapo Madina? Hii ina maana kwamba kuomba kwa jaha ya mtu ni kuomba kwa jaha ya Ucha Mungu wa mtu alie hai nako ni kumuendea binafsi na kumtaka atuombee, na sio jaha ya koo ya mtu aliekufa au alie mbali na sisi.

Aina hii ya "Tawassul" ndio iliyoleta mzozo mkubwa baina ya waislamu leo, kwani kuna watu wanaotaka kulinda maslahi yao ya kidunia, usharifu na utapeli, hivyo wameng’ang’ania kuzitetea Tawassul kwa jaha ya Masharifu waliokufa, na wanawadanganya watu kwamba Dua za kupitia kwa jaha ya Masharifu ni Mujarrab (Angalia utangulizi wa Tawassul ya nabahani na Ahlul Badri yaani zina gerentii ya kujibu ndio wanawaendea wenye Mahoteli kuwasomea Tawassul kila siku asubuhi ili wapate chai, machapati na michuzi ya bure! Hawa ni matapeli kuna haja ya Waislamu wawafungulie mashtaka ya utapeli! Wamejitahidi watu waovu hawa kutumia Hadithi za Uongo au kufasiri Aya na Hadithi wanavyotaka wao ilimradi tu ziende sambamba na matakwa yao, Tutawabainishia waislamu zile hoja zote zinazotegemewa na wazushi hawa na tutazijibu moja baada ya moja kwa hoja madhubuti za Qur’aan na Sunnah sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)InshaAllah.

Makala ijayo ambayo itataja Shubha za watetezi wa Tawassul zisizofaa na majawabu yake InshaAllah.

 

 

Makala hii imetolewa na:-

Idara ya Da’awah, Habari na Utafiti, Tahariri na Uandishi ANSSAR MUSLIM YOUTH CENTER. SLP 1542 TANGA TANZANIA.



 

Inaendelea.../2