Tawassul - 2 Tawassul Zisizofaa Kisheria
Idara ya 'Da'awah, Habari, Utafiti, Tahariri Na Uandishi
Ansaar Muslim Youth Centre
Katika makala iliyopita, tulifafanua maana ya Tawassul Kilugha na Kisheria kisha tukataja aina za Tawassul zisizofaa kwa ushahidi wa Qur’aan na Sunnah sahihi za Mtume (s.a.w.) hususan tawassul za Dua.
Hakuna Ikhtilaafu baina ya Waislam kwamba haifai kwa Muislam kutumia ‘Wasila’ kwa maana ya kilugha tuliyoitaja awali kupata mradi wake bila kuchunga misingi na mipaka ya kisheria Aliyoweka Mwenyeezi Mungu (S.W).
Kwa mfano mtu anataka kurithi Mali ya Baba yake kwa haraka, hivyo akatumia ‘Wasila’ wa kumuua ili apate kurithi Mali hiyo. Urithi namna hiyo ni batili; Au mzazi kumtumia mwanae kama ‘Wasila’ wa kujipatia riziki yake, kama ni mwanamke kumshakiza kufanya umalaya, na kama ni wakiume kumshakiza kufanya kazi za kuuza unga (madawa ya kulevya). ‘Wasila’ wa namna hii ni batili kwa hali yoyote na hakuna mwanachuoni hata mmoja alieruhuasu hali hii hata kama tukiona watoto wa baadhi ya Mashekhe wanafanya hayo.
Kuna ‘Wasila’ zisizofaa kisheria lakini Kwa sababu zimeegemezwa katika dini basi watu wengi wametatanishwa nazo kiasi cha kuona kwamba zinafaa ili hali hazina tegemezi yoyote kisheria. Katika makala hii tutataja Tawassul zisizofaa katika dini kwa kuzingatia kwamba ndio zilizoleta utatanishi baina ya Waislam.
‘KUTAWASSAL’ KWA JAHA ZA MITUME WALIOKUFA NA WATU WEMA’
Hii ni aina ya Tawassul ambayo inatetewa sana na watetezi wa Bid’aa Wanachodai ni kwamba kama ilivyokua inajuzu kumwendea Mtume (s.a.w.) wakati wa uhai wake au mtu mwema akuombee dua, basi vile vile inafaa kumwendea Mtume au Mtu huyo kaburini mwake ukamuomba akuombee dua, au kuomba popote pale ulipo kwa jaha ya Mtume kabla ya kuzaliwa kwake au baada ya kufa au Mtu yeyote mwema alie kufa au alie mbali kama vile kusema: "Ewe Fulani ulie kaburini nipelekee maombi yangu kadhaa kwa Mwenyeezi Mungu," au akasema: "Ewe Mwenyeezi Mungu ninakuomba kwa jaha au kwa haki ya Fulani alie kufa au alie mbali!"
Hali Kama hii ndio Mtume (s.a.w.) aliyo wakuta nayo wakiifanya washirikina wa Makkah ambao walikua wamejiwekea masanamu ya watu wema kisha wakataka yawaombee kwa Mwenyeezi Mungu, Mtume (s.a.w.) aliwakataza vitendo hivi, lakini walitoa hoja kwamba wao hawakusudii kuyaabudu hayo masanamu isipokua wanayatumia kujikurubisha kwa Mwenyeezi Mungu tu.
Qur’aan iliwapa majawabu yafuatayo:-
"Mola WA kuitakidiwa (kuabudiwa Kwa Ikhlaswi) Ni Mwenyeezi Mungu tu; lakini wale wanaowafanya wengine kuwa waungu badala yake (husema): "sisi hatuwaabudu hawa ILA wapate kutufikishia karibu kabisa Na Mwenyeezi Mungu, Hakika Mwenyeezi Mungu atahukumu baina Yao katika Yale wanayohitilafiana. Bila shaka Mwenyeezi Mungu hamuongoi (hamuongozi) alie muongo, alie Kafiri.
(Azzumar: 3)
Na amesema Allah (S.W.)
"Nao wanaabudu (waungu) wasiokua Mwenyeezi Mungu wasioweza kuwadhuru (wanapoacha kuwaabudu) wala kuwanufaisha (wakiwaabudu) Na wanasema: Hao ndio waombezi wetu mbele ya Mwenyeezi Mungu, sema: "Je! Mnamwambia Mwenyeezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi?" Ameepukana Na upungufu, Na Ametukuka Na hao wanaowashirikisha naye.
(Yunus: 18)
HOJA ZINAZOTEGEMEWA NA WATETEZI WA TAWASSUL
ZISIZOFAA KISHERIA NA MAJAWABU YAKE:
HOJA YA KWANZA:
Kwamba inafaa kutawassal Kwa jaha ya Mtume (s.a.w.) kabla ya kuumbwa kwake. Na wanadai kwamba kuna hadithi ya Mtume (s.a.w.) Eti amesema:
"Adam alipofanya kosa alisema: "Ewe Mola! Ninakuomba Kwa haki ya Muhammad upate kunisamehe. Akasema Mwenyeezi Mungu: Ewe Adam! Na ulimjuaje Muhammad Na ilihali sijamuumba? Akasema: Ewe Mola Kwa sababu pale ulipo niumba Kwa mkono wako ukanipulizia roho yako, nilinyanyua kichwa nikaona juu ya matendegu ya Arshi kumeandikwa ‘LAA ILAHA ILLA LLAH MUHAMMADU RASULU LLAH’ (Hakuna apasae kuabudiwa Kwa haki isipokua Allah na Muhammad ni mjumbe wake) basi nikajua kwamba hakukuongezwa kwenye jina lako isipokua (alie) kipenzi zaidi kwako kuliko viumbe vyote. Akasema Mwenyeezi Mungu: Umesema kweli Ewe Adam, Hakika yeye Ni kipenzi zaidi kwangu kuliko viumbe vyote, niombe Kwa haki yake Na nimeshakusamehe, Na lau Kama si Muhammad nisingekuumba.
(Imepokewa Na Al Haakim katika kitabu chake Al –Mustadrak).
Hadithi hii inayo daiwa kua ni maneno ya Mtume (s.a.w.) ni tegemeo kubwa kwa watetezi wa Tawassul zisizofaa, na wamewataja wanachuoni wengi na vitabu vyao eti wameiona hadithi hii ni sahihi. (Angalia kitabu ‘Mafahim yajib an tuswahah uk.119 chapa 1990 cha Sharifu Al – Maalikiy) – Tegemeo kubwa la Mashekhe na watetezi wa tawassul hizi zisizofaa)
Jambo ambalo tunataka kuwaelimisha Waislam kwanza kuhusiana na hadithi za Mtume (s.a.w.) si kila linalo nasibishwa na Mtume (s.a.w.) basi linakua ni sahihi, na hata kama kuna baadhi ya watu wanadai kwamba Hadithi Fulani ni sahihi, ni lazima kuchukua hadhari katika kupokea hadithi kama alivyotahadharisha mwenyewe Mtume (s.a.w.) kwa kusema:
"Mwenye kunisingizia uongo kwa kusudi basi na ajiandalie makazi yake motoni."
Hii inaonyesha kuna watu maadui wa Uislamu watapenyeza mafunzo yasiyo sahihi katika Uislam na kuyanasibisha na Mtume (s.a.w.) ili kuwatia watu katika ushirikina au kuwapotoa katika dini yao. Ndio maana wanachuoni wetu kwa hadhari iliyotolewa ndani ya Qur’aan Aliposema Allah (S.W.):-
"Enyi mlio amini anapo wajia Mtu muovu (asiekuwa wa kutegemewa) na habari (yoyote ile msimkubalie tu) Bali pelelezeni (kwanza), msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu ya yale mliyo yatenda.
(Al Hujuraat: 6)
Wameweza kuzichambua Hadithi na kuzibainisha zilizosahihi na zilizombovu kwa mizani maalum, iliyokubalika na wanachuoni wa somo la Hadithi.
Kwa mujibu wa mizani ya somo la Hadithi, Hadithi ya matendegu, iliyotajwa hapo juu inahesabika ni maudhui (ya uongo) kwa sababu zifuatazo:-
Kwanza: Maneno yaliyomo ndani ya hadithi hii yanapingana na Aya za Qur’aan zilizoeleza kwa uwazi juu ya kisa cha Nabii Adam (a.s.) alivyofanya kosa na namna alivyoomba msamaha kwa Mola wake. (Anasema Allah (S.W.):
"Kisha Adam akapokea maneno (ya maombi) Kwa Mola wake, (akaomba), Na Mola wake akapokea toba yake; Hakika Yeye ndie mwingi wa kusamehe Na mwingi wa kurehemu."
(Al – Baqarah: 37)
Aya hii inaonyesha wazi kwamba ni Mwenyeezi Mungu (S.W.) ndie alie mfundusha Adam (a.s.), maneno ya kuombea msamaha na hii ni kinyume na tulivyoona katika hadithi kwamba Adam (a.s.) kwa ujanja wake tu, na umbea ndio uliyompelekea kunyanyua kichwa mbinguni na kuona jina la Muhammad (s.a.w.) hivyo akaomba msamaha kwa jaha yake, jambo ambalo eti Mwenyeezi Mungu lilimshangaza kiasi cha kumuuliza Adam (a.s.) vipi alijua siri zilizopo kwenye matendegu ya Arshi!
Isitoshe Mwenyeezi Mungu (S.W.) amezidi kutufungulia utata kwa kuyataja hasa hayo maneno aliyomfundisha Adam (a.s.) aliyoombea msamaha.
Amesema Allah (S.W.):-
"Wakasema Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, Na Kama hutatusamehe Na kuturehemu, Bila shaka tutakua miongoni mwa wenye hasara."
(Al – a’araaf: 23)
Basi hayo ndio maneno halisi aliyoombea Adam (a.s.) na Mama Hawaa, msamaha kwa Mola wao, haya, mbona hatujaona neno "Kwa jaha ya Mtume" au "Kwa haki ya Mtume?
Pili: Moja ya masharti ya kukubaliwa hadithi ni wapokezi wawe waadilifu na inafahamika katika hadithi hii kuna mmoja katika wapokezi anaitwa Abdul Rahmaan bin Zaid si muadilifu, hivyo upokezi wake haukubaliki. Na hao waliotajwa kua wameiona hadithi ya Adam (a.s.) ni sahihi ndio hao hao waliosema mpokezi huyo ni Dhaifu na muongo.
(Angalia kitabu ‘Al-Madkhal ila swahih Juzuu 1 uk. 114 na uk. 154, cha Al-Hakim huyo huyo mwenye kitabu cha Al-Mustadrak, angalia Dalaailu Nnubuwwah’ cha Al-Bayhaqiy Juzuu 5 uk.489 vile vile Suyuutwi katika kitabu chake takhrijul Ahaadiythi Shifaa uk.30, Azzurqaaniy katika Sharhul Mawaahib na wengi wengineo).
Kwa yeyote aliyesoma somo la hadithi au kulipitia juu juu, hawezi kuona hadithi imeandikwa pahali kua ni sahihi basi akamuamini na kumkubali huyo aliesema bila kufanya utafiti. Hawa ndugu zetu watetezi wa tawassul hiyo walipopata kitabu cha ‘Sharifu’ Al Maalikiy kiitwacho: ‘Mafahim Yajib an tuswahah’ basi walikigeuza "Msahafu", kila kilichotajwa humo walikishikilia neno kwa neno kutetea Bid’aa zao, ilihali mwenyewe Al Maalikiy anakiri kuwa kitabu chake kinaweza kua na makosa, anasema hivi katika utangulizi wa kitabu chake:
"Kitabu changu hiki ni kama vitabu vingine, kinakubali kufanyiwa marekebisho na marejeo, nami kwa fadhila za Mwenyeezi Mungu, ninakiri hilo katika kila kitabu nilichoandika, na ninasema mwisho wa yale niliyoandika:"Hakika ninamuomba Mwenyeezi Mungu Tawfiq na usawa wa yale niliyoandika, ikiwa ni sawa basi inatokana na Mwenyeezi Mungu, na ikiwa ni kosa basi inatokana na nafsi yangu na jitihada yangu, na ninataraji kwa mwenye kukisoma ataniongoza na kunionyesha makosa yangu…" (Uk.6 chapa 1990 Tafsiri kwa Kiswahili ni yetu).
Basi haya ndio maneno yanayosemwa na msomi, tafauti na walivyojengwa wanafunzi wa mashekhe wenye kutetea mambo ya bid'aa.
Hii ndio iliyowapelekea hata kama wamefanya kosa la kielimu basi hawakubali kukosolewa asilani, na wataleta kila taawili na kupindua maneno hadi wawaridhishe watu kwamba kila walichosema ni sawa, hii ni dalili ya uchache wa Elimu uliowazi.
Na ushahidi kwamba sio kila asemalo mwanachuoni kuhusu usahihi wa hadithi Fulani, ni pale mwanachuoni Assuyyutwi aliedaiwa kua amesema hadithi ya Adam na matendegu tuliyoitaja hapo nyuma kua ni sahihi katika kitabu chake Al – khaswaisu Annabawiya.
Mwanachuoni huyu huyu ametaja hadithi za kutukana watu weusi na akang’ang’ania kua ni sahihi! Na kwa Mtume (s.a.w.) amezinasibisha Mfano wa hadithi hizo ni, eti Mtume (s.a.w.) Amesema:-
"Mtu mweusi akishiba anazini na akishikwa na njaa anaiba".
(Imepokewa na Abu Said Al Ashaj)
Hadithi hii Suyuutwi ameitetea sana katika kitabu chake alichokiita Al – Aaliy uk.272 kua ni sahihi, pamoja na wanachuoni wote wanaipinga kwa kua maneno yake yanapingana na maadili ya kiislam. Mwanachuoni namna hii kwa upande wa mafunzo na sera za watetezi wa tawassul zisizofaa, maadam amesema hadithi hiyo ni sahihi na wao wanamuitakidi ni kigogo chao basi hadithi hiyo kwa upande wao pia ni sahihi. Je, wao wanaikubali na kuitekeleza hadithi hiyo?
Tunadhani imeeleweka sasa kwa nini Ansaar wakaweka Qur’aan na Sunnah sahihi za Mtume (s.a.w.) ndivyo vya kufuatwa na sio kila lisemwalo na Shekhe Fulani.
Tatu: Katika hadithi ya Adam iliyotajwa hapo nyuma, kuna maneno yanadaiwa aliyasema Mwenyeezi Mungu kumwambia Adam nayo Ni:-
"Lau kama si Muhammad nisingekuumba (wewe Adam)". Na maneno kama haya ndio yaliyoandikwa ndani ya Tawassul aliyoandika Nabahani:-
"Lau lahu maa kunnaa walaa baqiyna" (lau si yeye (Muhammad) tusingelikuwako wala tusingelibaki)
Ugomvi wetu sisi na Ahlul Bid’aa ni kua kama aliekusudiwa hapo ni Muhammad basi ‘Wasila’ huo utakua haufai kwa sababu umekiuka maadili ya Qur’aan Tukufu, kwani tunajifunza katika Qur’aan Tukufu kua lau kama si kuabudiwa Mwenyeezi Mungu basi tusingeliumbwa sisi Wanaadamu wala Majini.
Amesema Allah (S.W.):-
"Sikuwaumba Majini na Watu ila wapate kuniabudu".
(Adhaariyaat: 56).
Nae Mtume (s.a.w.) ni mmoja katika hao watu, lakini hadithi hiyo ya Adam (a.s.) inatuambia kinyume na Aya hii sasa tushike Aya ilio wazi au hadithi ambayo haina usahihi wowote ni katika hadithi zilizotungwa na za Uongo ili kumpa Mtume Muhammad (s.a.w.) cheo kama alichopewa yesu mbele ya wakristo kua ni mwana wa Mungu na kabla ya kuletwa hapa duniani alikua na Baba yake huko mbinguni. Na kama si yeye kusingeumbwa kitu kama inavyoelezwa katika Biblia (Agano jipya) ambayo inasema hivi:-
"Hapo mwanzo kulikuweko NENO, naye NENO alikuweko kwa Mungu, naye NENO alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; Wala pasipo yeye Hakikufanyika chochote kilichofanyika."
(Yohana 1:1 – 4).
Je, maneno haya yana tafauti gani na yale yaliyomo kwenye hadithi ya Adam na matendegu? Au na yale yanayosoma kwenye Tawassul ya Nabahani? (Lau kama si Muhammad basi tusingelikuweko wala tusingelibaki).
HOJA YA PILI YA WATETEZI WA TAWASSUL ZISIZOFAA:
Watetezi wa Tawassul zisizofaa wametoa ushahidi wa Aya ifuatayo kama ni hoja kwao: Amesema Allah (S.W):-
"Na kilipowafikia (wakati wa Nabii Muhammad hiki) Kitabu kitokacho kwa Mwenyeezi Mungu kisadikishacho yaliyo pamoja nao (walikadhibisha); na zamani walikua wakiwafungulia Makafiri (khabari ya Mtume huyo) lakini yalipowafikia yale waliyokua wakiyajua waliyakataa. Basi laana ya Mwenyeezi Mungu iko juu ya Makafiri (hao).
(Al – Baqarah: 89).
Wanadai watetezi wa Tawassul zisizofaa kwamba eti wamekubaliana wafasiri wote kua Aya hii imeshuka kwa Mayahudi waliokuwa wakiishi khaibar huko Madina, na walikua wakiomba dua ifuatayo: - "Ewe Mwenyeezi Mungu, sisi tunakuomba kwa haki ya nabii huyu ambae umetuahidi kumleta kwa ajili yetu. Aakheri zamaan (Zama za mwisho) Ili utupe ushindi juu yao (hao maadui zetu wa kabila la Ghatfani wagomvi wetu). (Hoja hii utaikuta katika kitabu Raddul matiin cha kiongozi mmoja wa watetezi wa Tawassul zisizofaa hapa Tanzania, uk.10 na uk.11).
Hoja iliyojengwa hapo juu ni kwamba inawezekana kutawassal (kuomba) kwa jaha ya mtu kama vile Mtume (s.a.w.) kabla hata hajazaliwa. Na Mayahudi walifanya hivyo na walifaulu waliyoyataka.
JAWABU LA HOJA HIYO:
Tatizo la watu wa Bid’aa kwanza hufanya jambo wakalinasibisha na dini bila hoja halafu baadae wakitakiwa hoja ndipo hulitafutia ushahidi basi hawajali usahihi wa ushahidi huo ilimradi wawe na kitu cha kujiegemeza hata kama hadithi ni dhaifu au za uongo. Na hayo tuyasemayo si ya kusingizia tutawapa mfano wa tamko la kiongozi huyo wa watetezi wa Tawassul zisizofaa alilolisema katika utangulizi wa kitabu chake. Raddul matiin akitetea kufaa kwa Tawassul zisizofaa. Anasema hivi:-
"Wameniuliza baadhi ya Wanafunzi niwatajie hoja mbalimbali juu ya kufaa kupiga dufu, kufaa kwa Tawassul na Talaqiin kwa sababu wanasikia makelele mengi dhidi ya mambo haya. Nikasimama muda mrefu (kushindwa kujibu) kutokana na uchache wa Elimu nilokua nayo juu ya ushahidi wa kufaa mambo hayo, lakini kuendelea kwao kuniuliza kumenilazimisha kusema…" (Angalia Raddul matiin uk. 2).
Maneno hayo hapo juu yanaonyesha wazi kwamba watu wengine wanajifanyia tu mambo bila mwongozo wala Elimu. Na hivi sivyo inavyotakiwa kwa Muislam.
Inavyotakiwa kwanza kabla ya kufanya jambo hasa la kidini kulihakikisha kielimu kisha ndio kulifanya na sio kujifanyia tu kichwa mchunga ukiulizwa ndio utafute japo jani la mgomba ulikamate.
SASA HEBU TUJIBU HOJA HIYO HAPO JUU.
Kwanza: Sio kweli kama alivyodai huyo kiongozi wa watetezi wa Tawassul zisizofaa , kwamba Aya hiyo hapo juu, kwa makubaliano ya wafasiri wote imeshuka kwa Mayahudi wa khaibar waliokuwa wakitawassal kwa Dua ya kupitia jaha ya Mtume, kwa sababu ukipekua vitabu vya Tafsiri utakuta kuna wafasiri waliotoa maelezo tofauti kabisa na hayo hapo juu. Angalia Tafsiri ya Ibn Jariir ya Aya hiyo au Tafsiri ya Ibn Kaathiir ya Aya hiyo, na sera ya Muhammad bin Is’haaq uk.63. Amenukuliwa Ibn Is’haaq katika upokezi sahihi akisema hivi kwa mukhtasari:-
"Amenisimulia Aasim bin Amru kupitia kwa Qatada Al – Answaar kutoka kwa Mashekhe wake (Maswahaba) kwamba Aya hii imeshuka kwa ajili ya Maswahaba wa Mtume (s.a.w.) na mayahudi waliokua jirani zao pale Madina. Katika Zama za ujahilia (Ushirikina) wao walikua na nguvu kuliko Ahlul Kitaab hivyo wakiwapiga mara kwa mara. Na Mayahudi nao walikua wakisema: hivi karibuni atatumwa Mtume (yaani Mtume Muhammad (s.a.w.) nasi tutamfuata hivyo tutakua pamoja nae kuwapiga vita nyinyi kama walivyopigwa kaumu ya Aadi na Irmi. Basi Mwenyeezi Mungu (S.W) alipotuma Mtume wake kutoka kabila la Quraysh, sisi Answaar (Waarabu wa Madina) ndio tuliomfuata na wao (Mayahudi) wakamkufuru na kumkataa katakata ndipo iliposhuka Aya hii:
Hebu tuangalie Shekhe Abdullah saaleh Farsiy katika Tafsiri yake kuhusu Aya hii:-
"Kabla ya kuja Mtume Muhammad (s.a.w.) Mayahudi walikua wakiwapa khabari Waarabu kuwa karibuni atadhihiri Mtume.
Ama kusema kua hao Mayahudi walikua wakiomba kwa jaha ya Mtume na wakishinda maadui zao kua ndio muradi wa Aya hii – maneno haya hawakuyasema wale wafasiri wa mwanzo kabisa (salaf) wenye kutegemewa, kama Imam Ibn Jariir. Tazama kwenye juzuu ya pili ya Tafsiri yake iliyoshereheshwa na kina Shakir – tangu sahifa 332 mpaka 335 – hutaiona Tafsiri hiyo wala hawakuitaja vile vile wale wafasiri wanaotegemea Hadithi sahihi za Mtume, kama Ibn Kathiir. Tazama juzuu ya kwanza sahifa 124, hutaona tafsiri hiyo. Wala Maimamu hawakutaja hadithi sahihi za Mtume – na wakataja tafsiri ya Qur’aan hawa pia hawakuitaja tafsiri hiyo; ila wametaja kama walivyotaja Maimamu hawa; ni Ibn Jariir, Ibn Kathiir, Ibn Mundhir, Al–Bayhaqiy, Ibn Is’haaq na Abu Nuaym, kama ilivyo katika sahifa 99 ya Fat–hul Qadyr ya Imam Ash-shaukany. Na ndivyo alivyofasiri Imam Al–Bukhary, kama ilivyo katika sahifa 124 ya juzuu ya nane. Fat–hul Bary (Pamoja na kuisoma hiyo Fat–hul Bary). Basi hiyo yakua waliomba kwa jaha ya Mtume siyo NDIYO. Ingawa imetajwa na wafasiri wengi wa nyuma baada ya hao Salaf wa kutegemewa.
Haikuja Hadithi ya Mtume Sahihi inayosema watu wamuombe Mwenyeezi Mungu kwa jaha ya viumbe vyake wala Majina Yao; wala haikusihi katika Dua za Mtume (s.a.w.) Dua ya kuomba kwa jaha ya viumbe.
Imekuja katika Qur’aan na Hadithi sahihi kuombwa Mwenyeezi Mungu kwa Majina Yake. Basi tufupizike na alivyotwambia Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Wallahi hatutokua watovu kwa kufupizika juu ya haya.
Ama kuomba maiti badala ya kumuomba Mwenyeezi Mungu – Kama ilivyo kwenye Dua ya SA’ALTUKA – haya yamepundukia mipaka – yametia maji maziwani!"
Maelezo haya ya Sheikh Abdullah Saaleh Farsy katika Tafsiri yake yanam’bainishia Muislam yeyote mpenda HAKI kwamba mambo haya ya kubainisha Tauhidi na ubaya wa Ushirikina na Bid’aa katikaTawassul, hayakuanzishwa na vijana waliosoma Saudia kama wanavyodai baadhi ya Masheikh na walimu waovu kuwadanganya watu kua kuna vijogoo vinavyowika mapema! Ili ionekane vijana hawa wameleta dini mpya au wanataka kupindua vyeo vya Masheikh wazee. Haya yote si ya kweli, ni maneno ya mfa maji, kwani tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Farsy mwenyewe anasema katika uk. Vii ameanza kuiandika tangu mwaka 1950 wakati huo hata hao vijana waliokwenda kusoma Saudi Arabia wengi wao walikua hawajazaliwa na hadi kuchapishwa rasmi Tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Farsy mwaka 1969 na Islamic Foundation – Nairobi hapakua na hata kijana mmoja ambae ametoka kwenda Saudia kusoma na kama yupo basi alikua hajamaliza masomo. Sasa je, Sheikh Abdullah Farsy nae amesoma Saudi Arabia? Au nae Ni kijogoo kiwikacho mapema? Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi! Kuna hoja nyingine ya watetezi wa Bid’aa kumdharaulisha Marehemu Sheikh Abdullah saleh Farsy kama ilivyo kawaida yao kumtukana mtetezi wowote wa haki, eti yeye aliwahi kuhudhuria maulidini hii sio hoja ya kielimu, kwani mtu anaweza kufanya jambo kwa kutokujua, na Muislamu wa kweli ni yule anaeacha jambo baya pindi anapojua ubaya wake, sio kulishikilia kichwa mchunga kisa umewaona mababu zako unaowapenda wakilifanya – Dini haiendi namna hii! Na inafahamika wazi Marehemu Sheikh Abdullah Farsy ni mwanachuoni mkubwa Afrika Mashariki na watu wa mwanzo waliompiga vita baada ya kutangaza HAKI ni Masharifu na Mashekhe wanaopenda kuabudiwa, kwa hiyo sisi tunapotukanwa kuitwa majina mabaya mabaya, tunamshukuru Mwenyeezi Mungu (S.W.) kwani haya ndio yaliyo wafika watu wema wote waliotangulia. Ama kwa upande wa watetezi wa Batili, ile wao kuambiwa haki ndio kutukanwa kwao.
Kwa hiyo maelezo haya yaliyotangulia yanaonyesha wazi kwamba Mayahudi hawakua wakiomba Dua (Tawassul) kwa jaha ya Mtume (s.a.w.) kama inavyodaiwa bali walikua wakitaraji ujio wa Mtume (s.a.w.) ambao kwao waliona ni nusura hapo atakapo fika atawasaidia kivita.
Pili: kisa kilichoelezwa na watetezi wa ‘Tawassul’ zisizofaa ni cha Uongo na Hadithi iliyotaja kisa hicho ni mbovu kwa sababu katika upokezi wake kuna mtu anaitwa Abdul Malik bin Haarun bin Antarah huyu anahesabiwa ni muongo kwa mujibu wa masharti ya kukubalika Hadithi sahihi. Amesema Suyuutwi katika Addurrul Manthuur kwamba upokezi wa kisa hiki ni dhaifu, na amesema Al Hakim katika kitabu chake ‘Al–Madkhal’ juzuu 1/uk.170 kwamba Abdul Malik amepokea Hadithi nyingi kutoka kwa Baba yake za Uongo na amesema Adhahabiy katika kitabu chake "Attalkhiys" kwamba Abdul Malik ni wa kupuuzwa na ni mtu alieangamia).
Basi hii ndio hakika ya hoja iliyotolewa na watetezi wa Tawassul zisizofaa, kwanza wao wana kawaida ya kujifanyia mambo bila mwongozo wa Qur’aan wala Sunnah ya Mtume (s.a.w) wakibanwa na maswali basi hujitafutia hoja yoyote ile ili mradi iambiwe nao wana hoja, hata kama hoja hizo ni Batili.
Mfano mzuri wa kwamba watetezi wa Bid’aa hujifanyia tu majambo bila ya Elimu, ni pale kiongozi mwingine mkubwa wa watetezi wa Tawassul zisizofaa alipoulizwa na wanafunzi wake juu ya ushahidi wa kufaa kwa ‘Tawassul’ basi mwenyewe alikiri kuwa alikua akijifanyia tu mambo haya muda mrefu bila ya kujua ushahidi wake kwa uchache wa Elimu aliokua nayo juu ya kufaa kwa mambo haya, lakini amelazimika kujibu baada ya kughasiwa na maulizo ya mara kwa mara ya wanafunzi wake. (Angalia kauli yake halisi katika kitabu chake Raddul Matiin uk.2).
Mambo ya dini hayataki msimamo kama huu, huwezi kujifanyia jambo la dini hasa Ibada bila Elimu ya jambo hilo. Huwezi kuswali bila kujifunza masharti ya swala, hivyo hivyo ‘Tawassul’ ya Dua ni Ibada kama tulivyoona hapo awali, huwezi kujifanyia tu bila mwongozo, Mwenyeezi Mungu (S.W.) Ametukataza tabia hii Aliposema:-
"Wala usifuate (Ukiyasema au ukiyafanya) usio na Elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; hivyo vyote vitaulizwa".
(Al–Israa/ Bani Israil. 36).
Basi huo ndio msimamo unaotakiwa, na sio ule msimamo wa kudai ya kua haya mambo ya Bid’aa tumeyakuta kwa Mashekhe wetu waliotangulia basi nasi lazima tuyafate kichwa mchunga bila ya Elimu, ukitakiwa ushahidi unakua mkali kama simba na kutangaza inadi kwamba utalinda itikadi za mababu kufa kupona ziwe nzuri au mbaya mbele ya wengine. Huu sio msimamo anaotakiwa awe nao Muislam, Bali huu ni msimamo waliokua nao Washirikina ambao walikua wakijifanyia mambo tu kichwa mchunga.
Anasema Allah (S.W.) kuweka wazi tabia walizokua nazo Washirikina ili tujiepushe nazo:-
"Na wanaabudu badala ya Mwenyeezi Mungu (Miungu) ambayo (Mwenyeezi Mungu) hakuteremsha Amri (ya kuabudiwa), na ambayo hawana Elimu nayo. Na madhaalim hawatakua na wa kuwasaidia.
Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki juu ya nyuso zao wale waliokufuru. Hukaribia kuwashambulia wale wanaowasomea hizo Aya zetu. Sema: je, nikuambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni moto! Mwenyeezi Mungu Aliwaahidi wale waliokufuru, na ni marejeo mabaya hayo".
(Al – Hajj: 71, 72)
Ndugu Muislam, katika makala ijayo tutaendelea kukuletea hoja za watetezi wa Tawassul zisizofaa na zitajibiwa moja baada ya moja kwa ushahidi wa Qur’aan na Sunnah sahihi ya Mtume (s.a.w.).
« « « «
|
MAKALA HII HUTOLEWA NA:- IDARA YA DA’AWAH, HABARI, UTAFITI, NA TAHARIRI ANSAAR MUSLIM YOUTH CENTER STR. NO. 19 S.L.B. 1542, TANGA, TANZANIA µ µ µ |
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
