Skip navigation.
Home kabah

Tawassul - 3 Hoja Za Watetezi Wa Tawassul Zisizofaa Kisheria






Idara ya 'Da'awah, Habari, Utafiti, Tahariri Na Uandishi

Ansaar Muslim Youth Centre 





Katika makala iliyopita, tuliona jinsi watetezi wa Tawassul zisizofaa wakiegemeza matendo yao hayo katika hoja zisizotegemewa katika dini. Na hii nikule kujifanyia majambo kwa kuiga iga tu bila ushahidi. Na pale wanapotakiwa ushahidi, basi hukamata chochote kilioko karibu ilimradi iambiwe wana hoja za kutegemewa. Tuliwabainishia Waislam baadhi ya hoja kubwa zinazotegemewa na watu hao na tukazijibu kielimu kwa hoja madhubuti zilizomo ndani ya Qur’aan na Sunnah sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Katika makala hii tunaendelea kuwatajia hoja nyingine zinazotegemewa na watetezi wa Tawassul zisizofaa na zitajibiwa ipasavyo.

Kabla ya kutaja hoja za watetezi wa Tawassul zisizofaa, ingepaswa kuwatanabahisha Waislam juu ya tafsiri ya Qur’aan. Ni jambo lenye kueleweka wazi kwamba Qur’aan, kwa ujumla, inatafsiriwa kwa Qur’aan yenyewe au kwa kauli na matendo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). na Maswahaba ambao wamejifunza tafsiri ya Qur’aan kutoka kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au ‘Taabiina’ waliojifunza kutoka kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kwa rai zilizokubalika kisheria. Na kama inavyofahamika kua Qur’aan imeelezea baadhi ya visa vya nyuma (Mataifa) vilivyotangulia ili viwe ni mazingatio kwetu. Visa hivi ni baadhi ya matukio mbalimbali ambayo yameelezwa kwa mukhtasari katika sehemu mbalimbali za Qur’aan. Na katika visa vilivyoelezwa kwa wingi ni visa vya Waisrael na Manabii wao. Visa hivi havikuelezwa katika mfumo wa hikaya kama hizi za ‘Paukwa pakawa’ Bali ni maelezo mafupi yenye kutaja sehemu zenye mazingatio kwetu sisi wanaadamu, kama alivyosema Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu Wa Ta’ala) katika Qur’aan Tukufu:-

“Bila shaka katika visa vyao hivi limo fundisho (zingatio) kwa wenye akili” (Yusuf: 111)

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile amebainisha kwa undani baadhi ya mambo waliyokua nayo watu wa nyuma (Mataifa) waliotangulia wakiwemo wana wa Israeli na Manabii wao. Na maelezo yoyote aliyoyatoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yakithibiti upokezi wake, basi ni wajibu kwa Muislam kuyakubali kwa sababu yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hatamki kwa matamanio yake bali ni wahyi (ufunuo) utokao kwa Mola wake. Kuna hali iliyojitokeza wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na baada ya kufa kwake. Nayo ni watu wa dini mbalimbali kuingia katika Uislam baada ya kubainikiwa na haki. Watu hawa waliposilimu walikua bado wana baadhi ya itikadi au fikra za dini zao za awali. Mfano mzuri tunaupata ni pale Adiy bin Haatim alipomsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma Aya ya 31 katika Sura ya Attawbah inayotaja habari za wakristo walivyokua wakiwaabudu viongozi wao. Yeye (Adiy) alikanusha kitendo hicho kwa mujibu wa mafunzo ya kikiristo aliyolelewa nayo. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkosoa na kumwambia kutii kila asemalo kiongozi wa kidini kichwa mchunga ni namna ya kuwaabudu. Na sio Adiy tu, kuna Maswahaba wengine kama vile Kaab bin    Al – Ahbaar, Wahab bin Munabih, Abdullah bin Salaam, Tamimu Addariy na wengineo ambao walikua ni katika Ahlul kitaab (Mayahudi na Manasara) kabla ya kusilimu kwao.

 Wao baada ya kusilimu kwao walitoa masimulizi mbalimbali ya kufafanua baadhi ya visa vilivyoelezwa ndani ya Qur’aan kwa mujibu wa mafunzo ya dini zao za awali yaliyomo ndani ya Taurat na Injili. Na walifanya hivi kwa nia nzuri pamoja na kwamba baadhi ya visa walivyoelezea ni katika yale mafunzo ya Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu Wa Ta’ala) yaliyoharibiwa na viongozi wao kwa kubadilishwa kwa kusudi kama alivyobainisha Mwenyeezi Mungu Katika Qur’aan:

“Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao tuliwalaani na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu (hazisikii kheri. Wamekua) wanayabadilisha maneno (ya Mwenyeezi Mungu katika Taurat na Injili) na mahali pake. Na wameacha (sahau) sehemu kubwa ya Yale waliyokumbushwa.(Al – Maidah: 13).  

Na hali hii ndio iliyompelekea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwakataza Maswahaba kupokea mafunzo kutoka kwa Ahlul Kitaab (Mayahudi na Manasara) na alisikika akisema:-

“Enyi Waislam, vipi mnawauliza Ahlul Kitaab (Mayahudi na Wakristo) ilihali kitabu chenu ambacho kimeteremshwa kwa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na kitabu cha mwisho mnakisoma na hakijaharibiwa? Na hakika Mwenyeezi Mungu ameshawaeleza kwamba Ahlul Kitaab wamebadilisha Kitabu cha Mwenyeezi Mungu, wamekigeuza na wameandika Kitabu kwa mikono yao (kuongeza yao), kisha wakasema kua Kitabu hicho kinatoka kwa Mwenyeezi Mungu Ili wapate kukiuza (kukibadilisha) kwa ajili ya thamani ndogo tu (ya kidunia). Hivi Elimu iliyokujieni (kutoka kwa Mwenyeezi Mungu) haiwakatazeni kuwauliza wao? Wallahi hatujaona miongoni mwao hata mtu mmoja akiwaulizeni juu ya yale mlioteremshiwa nyinyi”.(Imepokewa na Bukhari).

Na mafunzo haya ndio yaliyomfanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaghadhibika sana alipomuona Umar bin Al khattwaab akisoma kitabu cha Ahlul kitaab. Alimkataza kitendo hicho.

Hata hivyo baadae Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaruhusu Maswahaba kusikiliza na kusimulia habari za wana wa Israeli aliposema:-

“Fikisheni (ujumbe) kwa niaba yangu angalau Aya (moja).  Na simulieni habari za wana wa Israeli na hakuna ubaya, na mwenye kunisingizia uongo kwa makusudi, basi na ajiandalie makaazi yake motoni”. (Imepokewa na Bukhari)

Ruhusa hii aliotoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haina maana kwamba watu wasimulie tu chochote wasikiacho toka kwa Ahlul kitaab hata kama ni cha uongo kwa sababu hii, ndio maana Imaam Shaafii (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika kusherehesha Hadithi hii amesema:-

“--- Ni jambo lenye kujulikana kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haruhusu kusimulia uongo, kwa hiyo maana (inayokusudiwa) simulieni habari za wana wa Israeli kwa yale ambayo hamjui uongo wake ---“.

(Angalia Fat hul Bari juzuu 6 uk.618)

Na hivyo hivyo Imaam Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika kusherehesha Hadithi hii anasema:-

“Muradi (hapa) ni kufaa kusimulia habari zao (hao wana wa Israeli), kwa lile lililokua ni zuri. Ama lile lililojulikana uongo wake, haifai (kulisimulia).

(Angalia Fat hul Bari juzuu 6 uk 617).

Imebidi tutoe maelezo marefu juu ya visa vya Ahlul kitaab na inavyotakiwa Muislam kupokea habari hizo, kwa sababu moja ya msiba uliotufika Waislam ni kwamba vitabu vingi vya Tafsiri na Hadithi  kwa bahati mbaya vimetiwa humo ngano nyingi kuhusu Mitume na watu waliotangulia. Mengi katika ngano hizo ni ya uongo, na ndio maana wanachuoni wengi wamehadharisha hatari ya kujichukulia tu kila kilichomo ndani ya vitabu hivyo. Na inafahamika katika vitabu vya Tafsiri vilivyokubalika lakini vimebeba visa vya uongo juu ya wana wa Israeli ni Tafsiri mashuhuri humu mwetu inayoitwa “Jalalein” iliyoandikwa na Wanachuoni wawili mashuhuri Jalaluddin Al Mahalliy na kukamilishwa na Jalaluddin Assyuutwi. Na imeitwa “Jalalein” kwa maana walioandika ni Jalal wawili hao waliotajwa.

Na kwa bahati, Tafsiri hii imeshereheshwa na baadhi ya wanachuoni mbali mbali, na mmoja katika wanachuoni hao ni sheihk Ahmad Asswaawiy wa madhehebu ya kimaaliky, na ni mashuhuri humu mwetu kwa kuitwa –“Tafsiri ya Swaawiy” na ni moja katika tegemeo kubwa la baadhi ya Masheikh wetu na walimu ambao hawajabahatika kusikia au kumiliki Tafsiri nyingine za zamani zaidi zenye kutegemewa. Kwa hiyo basi, imewapelekea walimu hao kila walichokikuta humo basi ni kama ‘wahyi’ toka mbinguni, wanakikubali tu bila kufanya utafiti wa kielimu juu ya waliyoyaona humo, ilihali inafahamika wazi mbele ya mabingwa wa somo la Tafsiri kwamba baadhi ya Tafsiri zina ngano nyingi za uongo. Na mfano mzuri utaona katika tafsiri ya Jalalein tegemeo kubwa la walimu wengi humu mwetu. Hebu tumsikilize Bingwa Sheihk Marwan Siwar katika utangulizi wake wa Tafsiri ya Jalalein iliyochapwa huko Beirut – Lebanon akisema maneno yafuatayo katika kumhadharisha msomaji juu ya yaliyomo ndani ya Tafsiri hiyo:-

“Imekuja katika Tafsiri ya jalaleini Tafsiri ya baadhi ya Aya ambazo Wanachuoni wamekhitalifiana juu ya muradi (maana) yake. Na wafasiri wawili (hawa) waliofasiri Jalaalein wamechagua baadhi ya rai ambazo wamewapinga wanachuoni na wafasiri wengi katika rai hizo”.

(Angalia Uk. – (d) – wa Tafsiri hiyo ya Jalaalein) ambayo pia yametanabahishwa yale yote yasiyokubaliwa katika visa vya wana wa Israeli).

HOJA YA TATU:

Katika hoja zinazotegemewa na watetezi wa Tawassul zisizofaa ni Tafsiri ya jalaalein na Swawiy ya Aya zifuatazo: - Amesema Allah (Subhaanahu Wa Ta’ala)

“Na Mtume wao (Hao wana wa Israeli) akawaambia: - Mwenyeezi Mungu amekuchagulieni Taalut kua Mfalme”. Wakasema: “vp atakua na ufalme juu yetu na hali sisi tumestahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, nae hakupewa wasaa wa mali? Akasema Mwenyeezi Mungu: - “amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa Elimu na kiwiliwili na Mwenyeezi Mungu humpa Ufalme wake amtakae na Mwenyeezi Mungu ni Mwenye wasaa (Na) Mwenye kujua”.

(Al – Baqarah: 247). Kisha Akasema (Subhaanahu Wa Ta’ala)

“Na Nabii wao akawaambia: - Alama ya Ufalme wake ni kukujieni lile Taabut (sanduku) ambalo mna ndani yake kitulizo (nyoyo zenu) kitokacho kwa Mola wenu na (mna) masazo (mabaki) ya yale waliyo yaacha watu wa Musaa na watu wa Haarun; wakilichukua Malaika (kukuleteeni). Bila shaka katika hayo mna dalili kwenu (ya ufalme wake juu yenu) ikiwa nyinyi mnaamini”.

(Al – Baqarah: 248)

Katika kufasiri Aya hiyo hapo juu, Suyutwi amefafanua maana ya neno Taabut lililotajwa katika Aya hiyo kwa kusema hivi: “Taabut” ni Sanduku lilikua na masanamu ya Manabii (wote) aliloteremshiwa (Nabii) Adam na Mwenyeezi Mungu---“(Rejea Tafsiri ya Jalaalein). Swawiy nae katika kusherehesha maneno ya Suyutwi asema hivi:-

“(Hilo Sanduku) lilikua la mbao aina ya shamshaar (mgunga) na urefu wake ni dhiraa tatu, dhiraa mbili upana, lilipakwa maji ya dhahabu. Na lilikua kwa (Nabii) Adam. Ndani yake mna masanamu ya Manabii wote na mna ndani sanamu ya (Mtume) Muhammad na nyumba yake na Maswahaba zake na huku amesimama anasali baina yao. Kisha wakarithiana kizazi cha Adam hadi likamfikia (Nabii) Musaa, nae alikua akiliwekea ndani yake Taurat, na akaweka humo masazo (mabaki) ya mbao zilizovunjika, kisha wakalichukua wana wa Israeli baada ya (Nabii) Musaa, na ilikua wakitoka kuelekea vitani basi hulitanguliza mbele yao. Na ilikua Malaika wakilibeba juu ya vichwa vya wapiganaji, kisha wanaingia vitani. Basi wanaposikia ukelele, wanapata yakini ya ushindi. Na walipokufa Manabii wao Mwenyeezi Mungu akawasaliti na (kabila) la Amalikah, kwa sababu ya ufisadi wao. Hivyo wakawanyang’anya (hilo) sanduku na wakaliweka sehemu ya mkojo na kinyesi. Na pale Mwenyeezi Mungu Alipotaka kumdhihirisha Mfalme Twaalut, akawasaliti na balaa. Ikawa kila mwenye kukojoa kwenye sanduku hilo, hupata balaa ya maradhi ya bawasiri hadi ikaharibika miji mitano katika miji yao. Khofu yao ilipoongezeka juu ya hilo, wakalitoa (sanduku) wangwani, kisha (ndipo) wakalibeba Malaika kumpelekea Twaaluti.

 (Na kauli ya Suyutwi) ni kwamba Mwenyeezi Mungu alimteremshia (hilo sanduku) (Nabii) Adam yaani kisha walirithiana kizazi chake baada yake. (kauli yake: wakashindwa na Amaalikah) yaani baada ya mauti ya Mitume wao. (Na kauli yake: ilikua wakitaka kwalo ufunguzi) yaani wakiomba ufunguzi na ushindi kwa (jaha) ya sanduku (na kauli yake hupata utukufu kwalo) yaani kupata matumaini linapotangulizwa (sanduku) kwa adui (yao) (na kauli yake: utulivu wa nyoyo zao) yaani ni kwamba utulivu hupatikana kwa ajili ya hilo (sanduku) na kwa ajili yake, na imesemwa, muradi wa utulivu (hapo) ni sanamu la madini ya aina ya ‘zabarjad’ katika mithili ya paka isipokua paka huyo ana mbawa mbili, basi anapotoa sauti ndani ya hilo sanduku, walijibashiria ushindi, na imesemwa muradi hapo wa utulivu ni yale masanamu ya Manabii---“.

(Mwisho wa kunukulu maneno ya Swawiy).

Hoja iliyojengwa katika kisa hiki ni kwamba inafaa kutawassal kwa Athar (masazo) ya Mitume na watu wema kwa vile wana wa Israeli walishinda vita kwa kutanguliza lile sanduku lenye mabaki ya Mitume na watu wema waliokufa, hivyo inafaa kutawassal kwa watu wakubwa wakati wowote.

JAWABU LA HOJA HIYO NI KAMA IFUATAYO

Kwanza:

 Kisa kilichotajwa hakina tafauti na Hikaya za ‘Abunuasi’ au ‘Esopo’ kwa sababu hakina Isinadi (mtiririko) wa wapokezi hadi kufikia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba. Na moja ya masharti ya kukubaliwa Hadithi ni lazima uonekane mtiririko (Isnadi) wa wapokezi uliounganika. Vile vile huangaliwa uadilifu wa wapokezi. Kisa hiki hapo juu hakina lolote katika tulivyotaja, hivyo hakiwezi kukubalika hata kama kimetajwa na Sheikh Mashuhuri kiasi gani. Kwani tumeona jinsi ya baadhi ya Mashekhe kutunakilia baadhi ya maneno ya kudharaulisha watu weusi na wakayashikilia kwamba ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Pili: 

 Katika Aya iliyotajwa hakuna maelezo hayo ya Suyutwi na Swawiy. Kwani Aya imeeleza kwa ufupi kwamba Bani Israeli walikua na sanduku, na wala haikutolewa maelezo juu ya hakika ya sanduku hilo kua limetengenezwa na nini ua asili yake limetoka kwa Nabii Adam (‘Alayhi wasalaam).

Aya imeweka wazi kwamba Sanduku hilo mna mabaki ya Nabii Musa (‘Alayhi wasalaam) na Haarun (‘Alayhi wasalaam) hawajatajwa Manabii wengine. Na Aya imeweka wazi kua hilo sanduku lilikua ni sababu ya utulivu kwa Bani Israeil, na likabebwa na Malaika ikiwa ni dalili ya ukweli kua ni Twaaluti ni Mfalme wao hakuna maelezo yoyote yaliyothibiti zaidi ya hayo juu ya sanduku hilo. Na katika maelezo yaliyotolewa na mfasiri wa zamani sasa ni mfasiri mashuhuri Ibni Jariri Attwabariy. Yeye ndie aliesema kua:-

Yaani walikua wakishinda vita kwa Baraka ya sanduku hilo; yaani wakitabaruku nalo. Na kauli hii haiwezi kua hoja kwani ni maoni yake tu Ibn Jariri, nae sio ‘maasum’ (hakulindwa kutokana na makosa). Isitoshe kutabaaruk na kutawassal ni vitu viwili tofauti. Tutaelezea hapo baadae Inshaallah nini maana ya Baraka, na kutabaaruku kilugha na kisheria, kutabaaruku kunakofaa na kusikofaa, na nini hukmu ya kutabaaruku kwa athari za Mitume?

Tatu:

  Maneno yaliyomo ndani ya kisa alichokieleza Swawiy kinapingana na mafunzo sahihi aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tunavyoelezwa katika kisa cha sanduku walilopewa wana wa Israeil kua ndani yake mlikua na masanamu ya Manabii wote akiwemo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake, akiswali baina yao. Kwanza la kushangaza ni kwamba sanduku dogo la dhiraa tatu kwa dhiraa mbili (3x2) litaingiaje vitu vyote hivyo; Masanamu ya Manabii, Maswahaba, nyumba ya Mtume na masazo ya Musa na Haarun na paka mwenye mbawa mbili! Inavofahamika ni kua Manabii aliowateua Mwenyeezi Mungu ni wengi sana. Wengine wala hatujapewa khabari zao. Na hao wenye kujulikana inasemekana ni laki moja na ishirini elfu (120,000). Na Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nao pia walikua wengi, kwani inafahamika kua wale aliotoka nao Madinah kwenda kuikomboa Makkah walikua sio chini ya elfu kumi (10,000). Haya hatujui sanduku hilo limeingiaje masanamu ya watu wote hao? Isitoshe, vipi Mwenyeezi Mungu ataruhusu watu watawassal au kutabaaruk kwa masanamu, kitendo ambacho kimepigwa vita na Mitume wote waliotangulia, akiwemo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Anasimulia Bi Aisha (Radhiya Allaahu ‘anhu). Yafuatayo:-

“Ilipokua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Anaumwa, baadhi ya wakeze walitaja (khabari) ya kanisa lililokua katika Ardhi ya Uhabeshi likiitwa ‘Mariyah’ na ilikua Ummu Salama na Ummu Habiba ni (katika) waliowahi kwenda katika Ardhi ya Uhabeshi. Basi wakataja uzuri wake (kanisa hilo) na Masanamu yake, akasema (Aisha):- “Basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua kichwa chake na Akasema: - “hao ni (watu) ambao alikua (akifa) Mtu mwema miongoni mwao hujenga Msikiti juu ya kaburi lake, kisha hufanya hayo masanamu mfano wa sura (ya huyo mtu mwema) hao ni katika viumbe waovu mbele ya Mwenyeezi Mungu siku ya qiyama”. (Imepokewa na Bukhari).

Katika kusherehesha Hadithi hii Mwanachuoni Ibn Rajab Hambaliy (amekufa mwaka 795 H) anasema hivi:-

“Hadithi hii inatoa dalili, (hoja) ya uharamu wa kujenga Misikiti juu ya Makaburi juu ya watu wema na kufanya masanamu yao humo kama wanavyofanya wakristo. Na hakuna shaka kila moja katika hayo mawili ni haramu peke yake, kwani kufanya sanamu za wana Adam ni haramu na kujenga Misikiti juu ya makaburi peke yake ni haramu, kama zinavyoonyesha dalili (hoja za kisheria) nyingine. Zitakuja tajwa baadhi yake” na akaendelea kusema: - “Yale masanamu ambayo yamo katika lile Kanisa alilolitaja Ummu Habiba na Ummu Salamah yalikua ukutani na mfano wake, na hayakua yenye kivuli. Hivyo basi, kutengeneza masanamu mfano wa sura za Manabii na Watu wema ili kutabaaruku kwa hayo au kutaka uombezi kupitia kwa hayo Imeharamishwa katika Dini ya Kiislam na huko ndiko kuabudu masanamu”.

(Mwisho wa kunukulu. Angalia kitabu Al – Kawaakibu dduraary juzuu ya 2: uk: 65/82).

Hayo basi, ndio mafunzo halisi ya Uislam. Na watetezi wa Tawassul zisizofaa wanataka kuturudisha kwenye Ibada ya masanam, na wanatetea sana mambo yao haya si kwa jingine isipokua wanataka na wao wakifa, kwa sababu ya ‘Usharifu’ wao, wajengewe makaburi na kuchongwa sanamu zao ili watu watawassal au kutabaruku kwa masanamu hayo. Ukiwauliza watasema: “Ehee inafaa! Mbona Bani Israeli walitawassal kwa sanduku lenye picha ya masanamu ya Mitume? Haya tena msomaji, Akili kichwani mwako kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au ngano za ‘Abunuasi’ Na ‘Esopo’?

Kuna Hadithi nyingi zilizokataza kufanya Ibada kwenye masanamu. Mfano wa Hadithi hizo ni ile iliyopokewa na Bukhari na Abdu Razzaak kwamba Ummar Ibn Al – khattaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipofika sham, mmoja katika wakubwa wa wakiristo walimualika chakula kanisani lakini Ummar Alikataa na kusema:-

“Sisi hatuingii Makanisani mwenu kwa sababu ya masanamu yaliyomo humo”.

Na katika riwaya nyingine aloitaja Bukhari:-

“Ilikua Ibn Abbaas (Swahaba) anaswali katika hekalu isipokua hekalu ambalo ndani yake hamna masanamu”.

Basi hayo ndio mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kama walivyofahamu Maswahaba zake, kinyume na wanavyotaka watetezi wa Tawassuul zenye ushirikina kwani wao kwa mujibu wa kisa walichopokea wao na kukitilia nguvu kama tulivyotangulia kutaja, wamemtia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndani ya sanduku (Taabuut) akiswali baina ya masanamu Na Manabii wote, jambo ambalo hata washirikina wa Makkah wangeelezewa kisa hiki wasingekubali kwa jinsi wanavyomfahamu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokua akichukia ushirikina wa kuabudu masanamu. Na ni Yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndie aliemwambi Bi Aisha kua hakika nyumba ambayo ina mapicha (masanamu) haingii Malaika.

(Hadithi hii ipo kwenye sahihi ya Bukhari).

Baada ya mafunzo yote haya sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). halafu aje mtu atwambie kwamba Malaika ambao hawaingii ndani ya nyumba yenye masanamu au mapicha halafu ndio hao hao waliobeba sanduku zima la masanamu au mapicha ili kuwasaidia wana wa Israeli wapate kutawassal au kutabaruku nalo ili wapate kushinda vitani!!

Jama mbona dini inachezewa namna hii!! Hivi Mwenyeezi Mungu ameruhusu ushirikina wa kuabudu masanamu? Inavyofahamika ni kua Qur’aan imetaja visa vya Mitume mbalimbali jinsi walivyopambana na ushirikina mbalimbali ukiwemo wa kuabudu masanamu.

Ndugu muislam InshaAllah katika makala ijayo tutaendelea kukuletea hoja za watetezi wa Tawassul zisizofaa na majawabu yake yenye hoja thabiti katika Qur’aan na Sunnah sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

MAKALA HII HUTOLEWA NA:-

IDARA YA DA’AWAH, HABARI, UTAFITI, TAHARIRI NA UANDISHI

ANSAAR MUSLIM YOUTH CENTER

SLB. 1542. TEL. 255 - 27- 2646620

TANGA, TANZANIA.