Skip navigation.
Home kabah

Tawassul - 5 Hoja Za Watetezi Wa Tawassul Zisizofaa Kisheria

Idara ya 'Da'awah, Habari, Utafiti, Tahariri Na Uandishi

Ansaar Muslim Youth Centre 


Katika makala iliyopita tuliona jinsi watetezi wa Tawassul zisizofaa kisheria walivyokuwa hawana hoja za kutegemewa juu ya wayafanyayo, kwani hawana Aya wala hadithi sahihi hata moja walioitoa. Bali wametukusanyia mahadithi mabovu na ngano za uongo, na kudai ya kwamba maadam hadithi hizo au ngano hizo zimetajwa na Mashekhe wao, basi wao hawana makosa wala hatuna haja ya kuwazogoma kwani wao ni watu wa kufuata yaliyo achwa na mababu zao tu kama walivyokua wakisema Makureishi zama za Mtume (s.a.w.) alipowabainishia haki.

Bado watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa hawajatupa mizani ya kufuata Mashekhe au mababu waliopita; je, ni mababu wa miaka mia moja iliyopita au ni miaka 1,400 iliyopita au ni Imam Shaafii na Mashekhe wa madhehebu ya Shaafii au Mashekhe wa Misri au Mashekhe wa Maimamu wa Kishia au vipi?

Sisi tulikwisha tangaza msimamo wetu zaidi ya mara moja kwamba babu yetu wa kumfuata ni Mtume (s.a.w.) ambae ni Maasuum (amelindwa na Mwenyeezi Mungu (S.W.) kufanya makosa). Kisha tunawafuata waliomfuata Mtume (s.a.w.) katika karne tatu bora alizozitaja Mtume (s.a.w.) Halafu tutamfuata kila aliekwenda sambamba na mafunzo ya Mtume (s.a.w.) awe amezaliwa zamani au karne yetu hii bila kumbagua. Tunachoangalia ni lile neno au tendo afanyalo na sio kabila au mahali alipozaliwa. Hatuwezi kuikataa haki eti kwa sababu aliesema ni mtu wa Singida au sio sharifu. Ni mwiko kwetu kufuata Shekhe kichwa mchunga, na hivi ndivyo ilivyo agiza Dini yetu, na ndivyo walivyotuagiza Maimamu wetu waliotangulia kama tulivyoona katika makala iliyopita. Sisi ni wafuasi wa Maimamu wote wanaofuata Sunnah ya Mtume (s.a.w.) bila ya kuwabagua, na tutafuata kauli zao pale zitakapokubaliana na muongozo wa Mwenyeezi Mungu (S.W.) na Mtume (s.a.w.). huu ndio msimamo wa wanachuoni waliosoma Fiqhi ya Imam Shaafii (r.a.) kama vile Sheikh Assubkiy. Katika risala yake:-

“Maana ya kauli ya Shaafii Almutwaliby: itakaposihi hadithi basi hiyo ndio madhehebu yangu”.

Amesema hivi mwandishi wa Risala hiyo Sheikh Taqiyuddin Assubkiy katika Juzuu ya 3 uk. 102:-

“Lililokuwa bora zaidi kwangu ni kufuata hadithi. Na mtu achukulie nafsi yake kama yuko mbele ya Mtume (s.a.w.) na akawa amesikia (jambo) lilotoka kwake, je, itafaa kwake kuchelewa kuitekeleza kauli hiyo? Hapana wallahi, - kila mmoja amekalifishwa kulingana na ufahamu wake”  

Vile vile tuliona katika makala iliyopita jinsi watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa kisheria walivyowaaasi Masheikh wao, wanaojigamba kwamba ndio wanaowafuata Maimamu hao, lakini katika yale masuala yanayo wanyima ‘Ulua’ au kuondoa maslaha ya kidunia, au kuwafanya wakiyasema watagombana na wateja wao basi wameamua kuyaasi au kutoyasema kwa kuogopa kuudhi watu.

Katika makala hii, tutaendelea kukutajia Msomaji baadhi ya mambo ambayo watetezi wa Bid’aa wamekaa kimya na wamewaacha watu wakiendelea kuwaasi Maimamu wao,

Kisha tutataja hoja nyingine zinazotegemewa na watetezi wa Tawassul zisizofaa kisheria na zitajibiwa ipasavyo InshaAllah.

Ni jambo lenye kueleweka katika Sunnah kwamba wakati wa kuzika haifai kunyanyua sauti ya aina yoyote hata kama iwe ni dhikri, kwa sababu Ibada inayokusudiwa wakati ule ni kukumbuka mauti ili mtu apate mazingatio akiwa hapa duniani na kurekebisha matendo yake kabla hajafa. Huu ndio msimamo wa madhehebu ya Kishaafii ambao umewekwa wazi zaidi na Imam Nawawiy (r.a.) katika kitabu chake Al-Adhkaar uk. 203 aliposema:-

“Jua kwamba lililo sawa na lililochaguliwa na waliokua nalo salaf (watu wema waliotangulia) (r.a.) ni kukaa kimya wakati wa kwenda na jeneza (maiti). Basi isinyanyuliwe sauti kwa kusomwa (Qur’aan) au dhikri wala jambo (jingine) lisilokua hilo. Na hikma katika hilo iko wazi; nalo ni kwamba huo ukimya unatuliza mawazo yake na unakusanya fikra zake kwa yale yanayohusiana na jeneza (maiti) na hilo ndilo litakiwalo katika hali hii. Basi hii ndio haki. Na wala usighurike (usihadaike) na wingi wa wenye kukhalifu hilo kwani amesema Abuu Aliy Al-Fudhail bin Ayaadh (r.a.) (maneno) yenye maana (ifuatayo):- “Jilazimishe na njia za uongofu wala usidhurike na uchache wa wenye kuzipita, na ole wako (jihadhari) na njia za upotovu na wala usighurike na wengi wa wenye kuangamia...“. (Al-Adhkaar, uk. 203).

Maneno haya ni kinyume kabisa na matendo ya Waislam humu mwetu. Jeneza linabebwa kwa makelele na dhikri za ‘Laa ilaha illa Llah’ na hivi sasa wameongeza Adhana. Akifa mwinyi wa mji, basi maiti yake itaadhiniwa kaburini. Huu ni uzuzshi ambao watu wa Bid’aa wameukalia kimya muda mrefu, na huku wasema wanafuata Mashekhe au mababu zao. Leo Imam Nawawiy nae amewekwa baoni, je, yeye si katika mababu zao?!

Mfano mwingine wa uasi waliomfanyia Mtume (s.a.w.) na Imam Shaafii (r.a.) ni lile katazo la kuyajengea makaburi ilivyopokewa na Swahaba Jaabir (r.a.):-

“Amekataza Mtume wa Mwenyeezi Mungu (S.W.) kulijengea kaburi, Na kukaa juu yake, na kujenga juu yake.” (Imepokewa na Muslim).

Na amesema Imam Shaafii (r.a.):-

“Na ninapenda yasijengewe wala yasijengwe (haya makaburi) kwani hilo linafanana na pambo na fakhari, na mauti sio mahala pa mojawapo katika hayo mawili. Na sikuyaona makaburi ya Muhajirina (Swahaba waliohamia toka Makkah kwenda Madinah) wala Answaar (Swahaba wenyeji wa Madinah) yamejengwa…”

Basi hiyo ndio hali waliokua nayo mababu zetu sisi Answaar, watetezi wa Sunnah ya Mtume (s.a.w.)! Sasa watueleze watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa kisheria; pale wanapojenga makaburi ya Masharifu na Mashekhe au watu wengine wanakuwa wanafuata mababu gani? Na kama wao pia wanapinga hayo mbona hawayakemei kwa madai ya kulinda itikadi za mababu zao akina Imam Shaafii (r.a.)? Bali tunaona wameshikilia kuzilinda zile itikadi za mababu zao wa hivi majuzi tu kama vile ‘maulidi’ kwa sababu ndani yake mna ubwabwa wa bure, au Tawassul ambazo ndani yake mna pato lisilo na jasho.

Pale makaburini (Mabawa, Tanga) kuna kaburi la sharifu limejengwa kama nyumba na limetiwa na mlango ili watu waingie ndani kutawassal kwa jaha ya sharifu na kugaragara ndani yake kama lilivyojengwa kaburi la Khomeini wa Iran ambaye ni adui mkubwa wa Abubakar (r.a.) na Umar (r.a.) na Uthmaan (r.a.). lakini hujasikia sharifu humu mwetu hata siku moja kulikemea au kulikosoa tendo hilo la kujengea makaburi, kwa sababu masharifu hawa wamesharubuniwa kutetea itikadi za Kishia na mababu zao. Pesa za Mashia zimewatia upofu hadi kukanusha itikadi za mababu zao wa Kisuni na hadi kuruhusu Mashia kujenga mafiriji (majokofu) ya maji baridi katika Hospitali zao na kuwataka watu wamshirikishe Allah (S.W.). kwa kunywa maji baridi kwa jina la Imam Hussein badala ya jina la Mwenyeezi Mungu (S.W.).  (Msomaji na aende akajionee mwenyewe hali hii katika Hospitali ya Tamta iliyopo barabara ya kwanza mjini  Tanga).

Hatujasikia sharifu hata mmoja hapa kwetu akikemea ushirikina huu ilihali kuna mafunzo sahihi ya Mtume (s.a.w.) alipowataka Waislam wakila au wakinywa basi iwe ni kwa jina la Mwenyeezi Mungu (S.W.) kwa ushahidi ufuatao:-

 Imepokewa na Umar bin Abi Salamah (r.a.) akisema: - nilikua kijana (mdogo) chini ya ulezi wa Mtume wa Mwenyeezi Mungu na ulikuwa mkono wangu ukitapatapa (pande zote) za sahani (ya chakula). Akaniambia Mtume wa Mwenyeezi Mungu: Ewe kijana; Taja jina la Mwenyeezi Mungu Alietukuka, Na kula Kwa mkono wako wa kulia, na kula katika sehemu iliyokuelekea”.

(Imepokewa na Bukhari na Muslim).

Vile vile katika Hadithi iliyopokewa na Ibn Abbaas (r.a.) amesema:-

“Amesema Mtume wa Mwenyeezi Mungu: msinywe mara moja Kwa mkupuo Kama unywaji wa ngamia, lakini kunyweni kwa (pumzi) mbili au tatu, Na tajeni jina la Mwenyeezi Mungu mnapotaka kunywa na mtukuzeni (mshukuruni) mtakapomaliza”.

(Imepokewa na Tirmidhiy).

Pamoja na ushahidi huu tuliotaja, watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa kisheria, kwa sababu ya kurubuniwa na Mashia, wanaweza pia kulitetea hilo la kunywa maji kwa jina la Imam Hussein (r.a.), kwamba kumtaja jina lake sio ushirikina bali ni aina ya kutawassal kwa jaha ya Ahlul Bait (Masharifu) ambayo kwa wao inafaa!! Ni watu majabari waliochuna nyuso, na kuwa ni inadi kutetea batili na kupiga vita Sunnah za Mtume (s.a.w.). Kwa hivyo, hilo halitowashangaza Waislam wenye kuitaka haki. Hivyo hivyo walipoweka Misalaba kwenye Hospitali zao, ukiwauliza watasema hiyo sio Misalaba ni alama za kujumlisha tu!!

 

HOJA ZINAZOTEGEMEWA NA WATETEZI WA TAWASSUL ZISIZOFAA KISHERIA

 

HOJA YA TANO:

Katika makala zilizopita tulitaja baadhi ya hoja zinazotegemewa na watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa kisheria na za ushirikina na tumegundua kwamba, hoja hizo Ima zimejengwa kutokana na hadithi mbovu au ngano na visa vya ‘Israiliyaati’ vilivyosimuliwa na wasiokua Waislam. Leo tutataja hoja ifuatayo inayotegemewa na watetezi wa Bid’aa na itajibiwa ipasavyo:-

“Ametaja Al – Hafidh Ibn Kathiir (katika kitabu chake Al – Bidaaya wa Nnihaaya Juzuu ya 6 uk. 324) kwamba mwito wa Waislam katika vita ya Al Yamamah ulikuwa – ‘Yaa Muhammadaa!!’ (Ewe Muhammad)”.

Hoja iliyojengwa hapa ni kwamba Waislam walishinda vita ya Yamamah baada ya kutawassal kwa jina la Mtume (s.a.w.) ilihali ameshakufa. Kwa hiyo, hii inaonyesha kwamba inafaa katawassal kwa jaha za watu wema waliokufa ili kupata ushindi vitani na kwengineko (Hoja hii imetajwa na gogo la watetezi wa Tawassul zisizofaa kisheria katika kitabu chake Mafaahim Yajib an Tuswahah uk. 147 chapa ya 1990 na imetumiwa na wanafunzi kama hoja juu ya wanayoyatetea

Jawabu la hoja hiyo ni kama ifuatavyo: 

Kwanza:

 Neno ‘Yaa Muhammadaa!! Katika lugha ya kiarabu hujulikana kama “Usluubu – Nnudbah” yaani ni lugha maalum anayoitumia mtu aliefikwa na msiba wenye kutia huzuni, kama vile mtu akifiwa na kipenzi chake, hupiga mayowe kwa kumwita yule aliyekufa au kupata ajali Ewe Baba ee!! Au Ewe Mama ee!! (Angalia kitabu Dhwiyaau Ssaalik Juzuu. 3 uk. 282 cha Ibn Hishaam na Annahwul Muswaffaa cha Muhammad Eid uk. 512 kwa faida ya msomaji). Kwa hiyo, tamko hilo halileti maana yoyote ya kutawassal kama wanavyodai watetezi wa Tawassul zisizofaa kisheria.

Pili:

 Habari hizi za Maswahaba kutaja jina la Muhammad (s.a.w.) kama alama (mwito) wa vita ya Yamamah zimetajwa na Mwanachuoni Ibn Kathiir bila kutaja wapokezi wa khabari hizo. Hata hivyo, inaonyesha amenukulu kisa hicho toka kwenye kitabu ‘Taarikhul Umami wal Muluuk” kilichoandikwa na Mwanachuoni Mashuhuri Ibn Jariir, na ni ndie alietaja majina ya wapokezi wa kisa hicho. Katika hao wapokezi kuna Seif, Adhwahaak bin Yarbuu na mtu katika Banii Assahiymiy.

Wapokezi hao waliotajwa kwa mujibu wa somo la uchambuzi wa Hadithi wamehesabiwa kua na ila zinazopelekea kisa hicho kutokubaliwa. Kwa mfano, huyo Seif bin Umar amehesabiwa kua si chochote, ni mwenye kuachwa na ametuhumiwa kuwa ni mzandiki (muongo). Hivyo hivyo kuna Adhwahaak na yule mtu katika kabila la Sahiymiy ni watu wasiojulikana (Angalia Miyzaanul I’itidaali Juzuu. 2 uk. 255 kwa faida).

Na kisa japo kimetajwa na Mwanachuoni mkubwa “Ibn Jariir”, lakini kinachozingatiwa ni upokezi wake kua ni sahihi au la. Kama sio sahihi, basi hakiwezi kukubaliwa kama hoja ya jambo lolote. Na inafahamika na kila msomi kua vitabu vya Taariykh (Historia) vimejazwa humo visa vingi vya uongo, na ndio maana waandishi mara nyingi huhadharisha msomaji achukue tahadhari katika kunakili kisa kilichoandikwa katika vitabu vyao. Na ndio maana Mwanachuoni huyo tuliemtaja Ibn Jariir ameyaweka wazi haya katika utangulizi wa kitabu chake hicho tulichokitaja ‘Taariykhul Umami wal Muluuk’ Juzuu. 1 uk. 8 aliposema:-

 “Habari yoyote niliyoitaja katika kitabu changu hiki kuhusu baadhi ya watu waliopita na ambayo msomaji wake ataikana au msikilizaji ataichukia (ataiona kigegezi) kwa kua hakujua (hakuona) usahihi (wake) wala (hakuijua) maana (yake) kwa uhakika, basi ijulikane kwamba habari hiyo haikuletwa na sisi isipokua kwa hakika imeletwa na baadhi ya walioinakili kwetu. Na sisi tumeinakili kama ilivyonakiliwa kwetu”.

Tatu:

 Watetezi wa Bid’aa na Tawassul zisizofaa hawajafaulu kuleta hata hadithi moja sahihi inayoonyesha kua inafaa kutawassal kwa jaha ya Mtume (s.a.w.) baada ya kufa au akiwa mbali wakati wa uhai wake. Bali tunaona kuna wakati Mtume (s.a.w.) alituma askari wake sehemu mbali mbali kupigana na makafiri na katika sehemu hizo jeshi la Kiislam lilishindwa hadi kukimbia, kama vile vita ya Mu’utah. Mbona hakuwafundisha Dua ya kutawassal kwa jaha yake ilihali anajua kutawassal kwa jaha yake kuna gerentii ya kuleta ushindi? Na hivyo hivyo baada ya kufa Mtume (s.a.w.), Maswahaba na Taabiina wanaokaribia sabini elfu (70,000) waliuawa, kitika vita ya ‘Swifiin’ na katika vita ya ‘Jamal’ waliuawa Maswahaba na Taabiina karibu elfu tisa (9,000) na katika walioshiriki katika vita hivyo ni Amiirul Mu’uminina ‘Aliy bin Abiitaalib (r.a.) Ibn Ami yake Mtume (s.a.w.), na Mama wa waumini Bi, Aisha (r.a.) mkewe Mtume (s.a.w.) na wajukuu zake Mtume (s.a.w.). Lakini hatujasikia hata mmoja katika walioshiriki vita hivyo akitawassal kwa jaha ya Mtume (s.a.w.), au kwa jaha ya Aliy (r.a.) au kwa jaha ya Hassan (r.a.) au Hussein (r.a.). Na ilikua ndio mahali pake hasa inapotakikana ili isaidie angalau kupunguza idadi ya vifo!! Iwe Leo mtu akitawassal kwa jaha mathalan Masharifu wa Hadhramaut (Yemen ya kusini) ndio afaulu vitani? Sijui katika vita vya ghuba jaha za masharifu zilikua wapi? Na inafahamika wazi kwamba, Iraq ni sehemu ambayo wamezikwa masharifu wengi sana, mbona Tawassal kwa jaha ya masharifu hao, hazikusaidia watu kufa? Lakini tunaambiwa ‘Tawassul’ hizo husaidia kulinda mabasi yasipinduke!! Utapeli huu una mwisho wake!

Ewe Mwenyeezi Mungu (S.W.) tuepushe na Shari ya waovu hawa, usije ukatuteremshia adhabu sote kwa makosa yao, shuhudia kwamba tumeyakataza na tumefikisha ujumbe wako!

Ewe Mwenyeezi Mungu (S.W.) zijaalie nyoyo zao ziwe zenye kuikubali haki, kwani wamewapoteza wengi kwa sababu ya kiburi na kutetea utukufu na maslahi ya kidunia – Amin!