Skip navigation.
Home kabah

Utaratibu Sahihi Wa Kufanya Ruqya - 1 Tiba Kwa Njia ya Qur-aan na Sunnah

(Na Fathi Al-Jundii)

Imefasiriwa na Ummu Ashraf

Kutafuta tiba kwa njia ya Ruqya na Qur’an ni suala zito linalohitaji ufafanuzi na mjadala wa wazi kutokana na ukweli kuwa yamezuka mambo mengi ya uzushi na ushirikina ambayo hayana ushahidi wa Qur’an, Sunna wala vielelezo kutoka kwa Maswahaba wa Mtume (saw).

Mambo haya yamekuwa yakifanywa kwa jina la Ruqya au ponyo la Qur’an. Ingawaje Ruqya hutafsiriwa kama “uganga,” au “uganga wa kitabu” lakini ainisho hili, kwa kiasi fulani, ni potofu na linabeba maana mbaya sana katika lugha ya Kiswahili.

Wakati neno uganga huhusishwa na mambo ya kishirikina (uchawi na mauzauza), ruqya maana yake ni usomaji wa Qur’an na uombaji wa dua kwa Allah (SW) ili kupata msaada wake katika tiba ya ugonjwa na matatizo mengine na haihusiani kabisa na mambo ya uganga.

Ibn Hajr Al-Asqalanii kasema kuwa ainisho la ruqya linajumuisha ta’awwuth ambayo maana yake ni kuomba ulinzi. Kwa maneno yake kasema hivi:

“Hakuna khitilafu yoyote miongoni mwa wanazuoni kuhusiana na suala la kumuelekea MwenyeziMungu kumuomba msaada na ulinzi kwa hali yoyote itokeayo au inayotarajiwa kutokea. (Fath Al-Barii)

Suala la ruqya huendana na Aqida na Akhlaq za Kiislamu na ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la MwenyeziMungu kuwa Waislamu wamtegemee MwenyeziMungu tu katika mambo au matatizo yao yote.

Jambo la kusikitisha ni kwamba umezuka mtindo wa kufanya ‘tiba’ kwa ruqya kinyume na maana na lengo la ruqya. Hali hii imepelekea watu kupata “ajira isiyo rasmi” ya kufanya’uganga’ kwa maslahi binafsi huku wakijihami kwa kisingizio cha ruqya.

Sio siri hata kidogo kuwa kuna watu wamejipa uwezo wa “kuwatibu’ au’kuwaombea dua’ wengine ilihali hao wanaotibiwa au kuombewa dua hawana hata dalili moja ya imani juu ya MwenyeziMungu. Matokeo yake, “wateja” humtegemea zaidi “mganga” kuliko MwenyeziMungu.

‘Tiba’ kwa kisingizio cha ruqya sio tu imekuwa “kitega uchumi” bali pia kumekuwepo na ukiukaji wa maadili kwa baadhi ya wale wanaosemekana kuwa ni “wataalamu wa tiba ya ruqya”.

Kama ilivyokwishaelezwa kuwa ruqya sahihi huendana na Aqida na Akhlaq au maadili ya Kiislamu, lakini baadhi ya waganga magirini wamekuwa wakilitumia jambo hili kama mtego wa kunasia “akina dada na akina mama”.

Wateja hawa wa kike sio tu hutoa “ada” au “malipo” ya pesa kwa ajili ya ‘kufanyiwa ruqya’ bali wakati mwingine huwa wahanga wa maumbile yao.

Hushikwashikwa miili yao, hupapaswa maungo ya siri, huchojolewa nguo, hukogeshwa maji ya ‘dawa’ uchi’ au humwagiwa maji juu ya kanga ili igandamane na mwili mganga apate kukidhi matamanio yake, na wengine hufanyiwa kabisa uchafu wa zinaa!

Utafiti unaonesha kuwa wateja wengi wa “Matabibu hawa wa ruqya” huwa ni akina dada na akina mama, baadhi yao wakiwa ni wake za watu. Tamaa ya ngono kwa “tabibu wa ruqya”, mara nyingine huchochewa na “shida za akinadada” wanaotaka “kuombewa ili wapate waume!”

Kwa kweli kuna mambo ya ajabu sana ambayo japo yanafanyika chini ya mwamvuli wa ruqya lakini yanakiuka kabisa msingi, maana na lengo la ruqya!

Yawezekana makala hii ikawaudhi wahusika lakini lazima waukubali ukweli kuwa hii wanayofanya siyo ruqya iliyofundishwa na Mtume (saw). Hayo wanayoyanya wao ni kwa ajili ya matamanio ya nafsi zao na maslahi yao tu.

Kwa ajili hiyo, lazima wakubali kuwa, shughuli wanayofanya inawajengea ushirikiano wa karibu na shetani badala ya kuwakurubisha kwa MwenyeziMungu.

Lengo la ruqya sahihi ni kuwakurubisha waja kwa Mola wao. Na lengo la makala hii ni kuonesha tofauti kati ya ruqya inayoruhusiwa katika Uislamu na ‘ruqya feki’ inayofanywa na waganga magirini wanaohaha kuganga njaa zao.

Kwa minajili hiyo, makala hii, kwanza kabisa, inawahadharisha watu juu ya mambo ya uzushi yanayofanyika kwa jina la ruqya. Njia sahihi ya kuepukana na ghiliba zozote zile za ‘waganga’ ni kutafuta elimu sahihi ya Uislamu, kumuamini Allah na kumtegemea Yeye pekee.

                            Moyo wa mwanadamu

Moyo wa mwanadamu, kwa kawaida, hujaa mambo fulani na huwa hauruhusu kitu chochote kuingia mpaka kwanza kingine kilichomo ndani yake kitoke nje.

Ibnul-Qayyim kasema “ili mahali paweze kuruhusu kitu fulani kukaa basi ni shurti kuondosha kitu kingine kilichopo hapo. Hii ndiyo kanuni ya kimaada na ndiyo kanuni ya imani na nafsi pia. (Taz. Al-Fawa’id)”

Mja muumini humjuwa ipasavyo Muumba wake, anajuwa kwa nini yeye ameumbwa na anajuwa mwisho wa safari yake

Pia mja anayemuamini Allah anajuwa kuwa wanadamu na majini hawana uwezo wa kuwadhuru wala kuwanufaisha viumbe. Na wala hawana mamlaka juu ya maisha ya uhai wao, mauti yao au kufufuka kwao bila ya idhini ya MwenyeziMungu.

Kwa hali hiyo, Muumini mwenye tauhiid huishi maisha ya utulivu kwani anajuwa fika kuwa hakuna mwenye uwezo juu yake isipokuwa MwenyeziMungu kama Anavyosema katika Qur’an:

“Hakika waja wangu wewe hutakuwa na mamlaka juu yao isipokuwa wale wenye kukufuata katika hao wapotevu”. (15:42).

“Na kama MwenyeziMungu akikugusisha madhara basi hakuna yeyote awezaye kuyaondoa ila Yeye; na kama akikugusisha kheri, Yeye ndiye Muweza juu ya kila kitu”. (6:17).

Mtume (saw) alimwambia Abdullah ibn Abbas, “Ewe Kijana! Jichunge na MwenyeziMungu, Naye Atakuchunga. Chunga Haki Zake, Naye daima atakuwa pamoja nawe, ukilazimika kuomba basi muombe Yeye pekee; na ukihitaji msaada, Muombe msaada Allah pekee. Na kumbuka kuwa kama watu wote wakitaka kukunufaisha, hawataweza kukupa chochote isipokuwa kile tu alichokukadiria MwenyeziMungu na ikiwa wote wanataka kukudhuru basi hawataweza kukudhuru isipokuwa kile tu alichokupangia MwenyeziMungu. Kalamu zishasimamishwa na kuwekwa kando na wino wa (kuandikia) Kitabu (kadari) ushakauka”. (Ahmed na Tirmith).

Kinyume cha hivyo, imani dhaifu katika kumpwekesha  Allah, ulegevu wa imani katika kumtegemea MwenyeziMungu na ukosefu wa elimu sahihi huufanya moyo uwe kichaka cha kufichia mambo ya kishetani, mambo ya udanganyifu na mambo ya kipuuzi.

Kuhusiana na hali hii ya hatari ya moyo, Ibnul Qayyim kaandika hivi: Mashetani, mara nyingi, huwachezea wale wenye uelekeo hafifu wa dini yao, na wale ambao nyoyo na ndimi zao zimekimbiwa na imani-hawa ni watu ambao hawamkumbuki MwenyeziMungu na hawana njia ya kuimarisha imani yao. Pale mashetani wanapokutana na mtu dhaifu, asiye na silaha, na mtupu, huweza kumuandama na kumshinda (Attib An-Nabawii).

Aidha Ibn Qayyim kasema: “Uchawi wa wachawi huwadhuru watu wenye nyoyo dhaifu na  watu waliogandamana na hadaa na tamaa za dunia...na wasioshughulika kusoma Qur’an na nyiradi alizofundisha Mtume kila siku).

Wanazuoni wamesema: ‘wanaorogeka (wanaopatwa na uchawi) ni wale wanaoruhusu wenyewe kurogwa, kwani mara zote unakuta nyoyo zao zimekamatana na kushughulishwa na jambo hilo; na hivyo, nyoyo zao hizo hutetereshwa na jambo hili kulingana na kiwango ambacho zimeshikamana nalo, Allah ndiye Ajuwaye zaidi.”  (Al-Fawa’id).

Ufumbuzi wa tatizo hilo ni kuujaza moyo na kukijaza kichwa mambo ya  kumuabudia, kumfikiria na kumkumbuka Allah. Maisha yote ya mtu yatawaliwe na mambo haya. Kwa njiya hii imani hugeuka kuwa silaha kubwa ya kupambana na wale wanaotafuta uchawi na kiini macho ili kupata maslahi fulani.

                                  Uhalali wa kutafuta Tiba

Hapana shaka kuwa Uislamu ulikuja na nguvu ya kutibu moyo na kiwiliwili. Mtume (saw) aliitafuta tiba na pia aliwahimiza Maswahaba zake kufanya hivyo. Jabir kasimulia kuwa Mtume(saw) amesema:

kuna dawa kwa kila ugonjwa na dawa hiyo inapotumika kutibu ugonjwa, ugonjwa hutibika kwa idhini ya MwenyeziMungu Sunhaanahu wataala.” (Muslim).

Akisherehesha Hadith hii; Ibn Qayyim kaandika hivi: “Mtume (saw) aliamrisha tiba kwa kutumia dawa inayowiyana na ugonjwa. Kila ugonjwa una dawa. Kupona ugonjwa shurti kuendane na dawa inayowiana na ugonjwa huo.

Hivyo dawa ikizidi mno kiasi, itasababisha ugonjwa mwingine. Kinyume chake, dawa ikitumika  chini ya kiasi kinachohitajika itashindwa kupambana na ugonjwa na kwa hali hiyo itaonekana kutofaa.

Hivyo basi, daktari asipogundua tiba halisi au iwapo tiba haihusiani na ugonjwa, suala la kupona huwa ni muhali. Zaidi ya hivyo ikiwa tiba inatolewa katika muda usiofaa, dawa haitasaidia kitu, au kama mwili haukubali dawa au mwili hauna nguvu kabisa ya kumudu dawa hiyo, au kuna kitu fulani kinachozuwia isifanye kazi, dawa haitasaidia. Lakini kinyume cha hivyo kama dawa inawiana na ugonjwa, tiba itafanya kazi kwa idhini ya Allah.” (Attib An-Nabawii).

Jambo la ajabu ni kwamba, kuna baadhi ya watu wanaopuuzia njia za kisasa za tiba na badala yake husingizia kukumbwa na majini, kurogwa au kutazamwa kwa jicho baya. Ujinga huu huweza hata kusababisha kifo kwa mgonjwa wakati watu wakipoteza muda kumtowa majini mgonjwa.

Hivyo, ni muhimu kwanza kugundua aina ya ugonjwa na kisha kujaribu kutafuta dawa sahihi inayoweza kutibu ugonjwa huo. Kwani kama mtu hana uhakika na aina ya ugonjwa, anawezaje kutoa tiba ya kufaa?

Baadhi ya watu wanaweza kuuliza je kutafuta tiba kunapingana na imani ya kumtegemea MwenyeziMungu (tawakkul). Kwa hakika Hadith chungutele za Mtume (saw) ikiwemomoja iliyokwishatajwa hapo juu zinaunga mkono mtazamo huu kuwa kutafuta tiba ya dawa ni jambo linalokubalika kabisa, na limehimizwa katika Uislamu. Upo muafaka wa pamoja wa wanachuoni wa Kiislamu juu ya jambo hili.

       Muungozo wa Mtume kuhusiana na Kinga na Tiba

Muongozo bora kabisa wa maisha yetu unapatikana kwa kuyasoma maisha ya Mtume (saw) ambaye alituonesha namna ya kufanya mambo yetu katika mazingira yoyote yale.

MwenyeziMungu anamzungumzia Mtume hivi: “yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na mwenye huruma.” (9:128).

Kwa hakika Mtume (saw) katuongoza katika mema yote na kutuonya dhidi maovu yote. Muongozo wake unajumuisha na kinga dhidi ya aina zote za maradhi pamoja na njia za kupambana nayo pale yanapotokea.

Hapa tutaziangalia njia za kujikinga na maradhi alizofundisha Mtume (saw) pamoja na tiba mbalimbali za kutibu madhara ya kijicho na uchawi.

Kinga dhidi uovu kwa ujumla hupatikana kwa nguvu ya tauhiid (imani ya kumpwekesha MwenyeziMungu), kumsabihi kwa Majina na Sifa Zake tukufu, kufanya Ibada Zake kwa ikhilasi, kutii amri Zake, kumtegemea yeye tu,kumpenda na kumkumbuka mara kwa mara.

Hii ndiyo njiya ya kutafuta ulinzi wa jumla wa MwenyeziMungu. Aidha kuna maelezo kuhusu namna ya kutafuta ulinzi wake kwa njia mahususi, kama vile kuomba dua kabla ya kufanya tendo la ndoa ili kumkinga mtoto atakayezaliwa, kusoma Surati Baqara nyumbani, na kusoma Ayatu Kursiyu pamoja na sura tatu za mwisho za Qur’an, Ikhilas (QulhuAllahuAhadu), Falaq (Qulaudhubirabilifalaq) na Surat n-Nasi (Qulaudhubirabinnas). Sura hizi hujulikana kama Al-Muawwithat

Hata hivyo, ni muhimu kubainisha kuwa kuna tofauti kubwa kati ya maneno yanayotamkwa kwa ikhilasi kutoka ndani kabisa ya moyo na maneno yanayotokea mdomoni tu.

Kinachohitajika hapa ni dhikri inayohusisha moyo na ulimi. Ibnul-Qayyim kailezea hali hii kama ni “aina ya mapambano”, akisema: “Mpiganaji huweza kumshinda aduwi yake iwapo silaha anayotumia ni madhubuti na ikiwa yeye mwenyewe ni mkakamavu (shupavu) katika kutumia silaha hiyo.

Endapo moja kati ya masharti haya mawili halitimizwi, basi silaha haitakuwa na maana. Na mambo yatakuwa mabaya zaidi kama masharti yote mawili hayatimizwi” (Attib An-Nabawii).

 

Inaendelea...../2