Skip navigation.
Home kabah

Hekima Ya Falsafa Ya Ibada Katika Uislamu

 

(Na Imam Ibnul  Qayyim)

Imefasiriwa na Shaibu H. Kifea

KATIKA kitabu chake mashuhuri, Madarij-us-Salikiin, Ibnul Qayyim, mwanazuoni na mtafiti mkubwa wa Mas-a-la ya Uislamu anaelezea vipengele mbalimbali vya Ibada katika Uislamu.

Anayaainisha makundi mbalimbali ya watu yaliyojitokeza katika Umma wa Kiislamu kwa mitazamo yao tofauti juu ya Ibada. Baadhi ya makundi haya yakiwa yameathiriwa na mawazo yasiyokuwemo katika Uislamu.

Imama Ibn Qayyim anaiweka mitazamo hiyo katika makundi manne. Matatu kati yao ni potofu na moja tu ndilo kundi la wafuwasi wanaofuwata muongozo sahihi.

KUNDI LA KWANZA - AL-JABARIYYAH

 

Kundi la kwanza, Al-Jabariyyah linawajumuisha wale wanaokanusha kuwepo kwa hekima, lengo au sababu katika Ibada ya Allah. Watu hao wanaifinya Ibada kuwa ni kufuata tu amri ya Mungu, yaani ni kutii tu maamrisho yake pasina kuuhusisha umuhimu wa ibada zao na mafanikio na furaha katika dunia hii au Akhera.

Kwa mujibu wa watu hawa, MwenyeziMungu hakuumba maumbile kwa lengo au hekima yeyote. Viumbwa  si Mas-ul wala hawana msukumo wowote wa kimaumbile.

Hakuna cha kuulizwa wala cha kupatilizwa iwe katika ulimwengu wa kanuni za maumbile au katika Sharia ya Allah. Kwa watu hawa, halali na haramu ni sawa tu kwa asili. Wakiwa na maana kuwa vitu haviharamishwi kwa sababu ya madhara bali kwa sababu ya amri tu ya Mungu.

Ibada ya watu hawa ni kavu na ngumu, haina ladha na raha rohoni. Ibada yao hii haitulizi macho yao wala ule utekelezaji wao wa amri za Allah hauziletei furaha nyoyo zao na kuvinawirisha (kuvipa siha) viwiliwili vyao.

Wengi wao hukanusha uwezekano wa kuwepo kwa mapenzi ya kumpenda Allah moyoni mwa mja kwani mtu anachokipenda ni thawabu na rehema za Allah na si kuipenda Dhati ya Allah.

Hivyo, wanakana msingi na maana nzima ya Uungu ambayo ni  ile ya Mungu kuwa Kipenzi Kikuu cha mwisho. Ibada, kwa uhalisia wake, ni mapenzi makubwa kuliko yote yanayoambatana na unyenyekevu, utukuzo na taadhima.

KUNDI LA PILI – AL-QADARIYYAH

Kundi la pili, AlQadariyya, ni la wale wanaofinya  hikima na lengo la Ibada. Kwao wao hikima hii hukomea katika thawabu na muruwa wa watu lakini ibada haina maana au lengo zaidi ya hilo.

Watu hawa husema kuwa matendo ya ibada ni biashara ya amali ambapo mja hupata malipo na radhi za Allah Peponi. Ibada ni kazi ya utumishi ambayo mtu hupata ujira kwayo.

Wanatoa dai hili kwa kutumia aya hii...”Hii ndiyo Pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya (amali)”. (7:43) na wanatumia aya nyinginezo mfano wa hii.

Wanasema tu kuwa Jazaa na Thawabu ndiyo mambo ambayo MwenyeziMungu kayataja mara kwa mara kwa mnasaba huu wa  malipo ya amali. Aidha wanatoa hoja ya mizani ambapo mema na maovu yatapimwa kulinganishwa uzito.

Wanaona mwenyeziiMungu kaweka sheria kwa ajili ya usalama tu wa watu na wanaona kuwa jambo la kuabudu linaishia tu katika amali na jazaa yake na kwamba kama kuna kitu ambacho MwenyeiMungu atamlipa mja wake bila amali basi ni sadaka.

Hivi ni  nani alishiyeshindwa zaidi kumjua Allah na aliyezidisha majivuno kuliko yule anayelinganisha Radhi na Rehema kwa mja Wake na sadaka ya mja kwa mja mwenziwe? Kiasi cha kusema kuwa malipo ya Allah kwa amali alizozifanya ni bora  na mazuri zaidi kuliko Hisani yake?

Kundi hili na lile la Jabariyyah ambalo kama tulivyoona, lina msimamo tofauti wa kuzitoa amali thamani na maana, yote mawili yako makosani kwani yametoka katika njia sahihi ambayo kwayo MwenyeziMungu kamuumba mtu na ni katika njia hiyo Mitume wote waliwaita (waliwalingania) watu ambapo Vitabu vilishushwa kwao.

Njia hiyo Sahihi ni hii kwamba amali ndiyo sababu zipelekeazo mtu kupata malipo mema au adhabu. Amali njema hutokana na idhini na rehema za MwenyeziMungu. Zote hizo ni Hisani Yake tu kwa waja Wake.

MwenyeziMungu Ndiye Aliyeumba niya ndani ya nafsi ya mja Wake na Ndiye Aliyempa mja uwezo wa kutenda au kufanya hizo amali. MwenyeziMungu Ndiye Aliyeumba  ile hali ya kupendwa kwa amali hizo na akazipamba moyoni mwa mja.

Iweje basi amali hizi alizoziumba MwenyeziMungu ziwe bidhaa za kuthaminishwa na Rehema Zake hapa duniani na Akhera? Amali hizi haziwezi kuuzwa kwa bei ya rehema za MewnyeziMungu.

Kimsingi, hakuna thamani ya mabadilishano ya kibiashara baina ya amali hizi za mja na  Rehema na Malipo ya MwenyeziMungu, si hapa duniani wala si Akhera. Katu amali hizi hazina bei ya kununuliwa au hazina thamani ya kulipwa.

 Lengo la amali hizi, kama zitafanywa kwa ikhilasi kwelikweli na kwa utaratibu sahihi kabisa, ni kuonesha shukurani kwa MwenyeziMungu kwa baadhi tu ya neema Zake. Laiti MwenyeziMungu angelitutaka tumshukuru kikamilifu kwa neema Zake, tusingeweza kabisa kumshukuru.

Ndiyo kusema basi, kama Angewaadhibu viumbe wote Duniani, Asingekuwa dhalimu. Au vinginevyo, kama Kahiyari kuwa na Rehema juu ya waja Wake wote, basi, kwa hakika, Rehema Zake hizo zina thamani kubwa kuliko amali zao.

Kwa sababu hii,  Mtume (Swalallahu alaihi wasalam) kasema, “hakuna atakayeingia Peponi kwa amali Zake.” Nao Maswahaba wakauliza, “ukiwemo na wewe Mtume wa MwenyeziMungu?” Mtume akajibu, “ndiyo, pamoja na mimi isipokuwa MwenyeziMungu Anifunike kwa Rehema Zake.”

Wakati ambapo MwenyeziMungu kasema “ingieni Peponi kwa yale mliyokuwa mkiyayafanya", hakuna mapingano kati ya kauli hizi mbili. Kwani amali sio bidhaa za kubadilishana thamani na malipo ya MwenyeziMungu. Bali zenyewe ni sababu tu za waja kurehemewa na Mola wao na hivyo kuruzukiwa Pepo.

Kundi lile la pili la Qadiriyyah ndilo lisilomjuwa zaidi MwenyeziMungu. Ni ujinga mkubwa ulioje kutojuwa kuwa viumbe wa mbinguni na ardhini hawaishi isipokuwa kwa Rehema za MwenyeziMungu na kwamba raha na furaha yao huwepo kwa kuzitambuwa na kuzikumbuka rehema hizi.

“Wanakusumbua kwa kuingia kwao katika Uislamu, Sema, “Msifanye kuwa ni hisani kwangu kusilimu kwenu, bali MwenyeziMungu Ndiye Aliyekufanyieni hisani kwa kukuongozeni katika Uislamu, ikiwa nyinyi ni wakweli. (49:17).

Hivyobasi aya za Qur’an na Hadith za Mtume zinayabatilisha makundi yote mawili. Yote mawili yamekanusha sehemu ya ukweli

KUNDI LA TATU – WANAFALSAFA NA MASUFI

Kundi la tatu ni lile la wanafalsafa na Masufi. Hili ni kundi la wale wanaodai kuwa faida ya ibada ni mazoezi tu na maandalizi ya roho kwa ajili ya elimu zaidi, maono na kinga dhidi ya matamanio na matashi ya kinyama.

Ibada hutakasa roho na kuifungua  pingu za shughuli na maisha ya kawaida na kuitayarisha kupokea ujuzi na utambuzi. Makundi mawili yana mtazamo huu:

Mosi, wale wanaowaelezea Mitume kuwa ni sawa na wanafalsafa wanaoamini umilele wa duniya (qidanil-aalam), wakikanusha kusambaratika kwa mbingu na kutetea kutokuwepo kwa uhuru wa hiyari.

Pili, wale waliokuwa wanafalsafa miongoni mwa masufi. Hawa hudai kuwa ibada si chochote bali ni mazoezi na utakaso tu wa nafsi zao na kinyanyua daraja kutoka katika ulimwengu wa matamanio ili ipokee elimu ya siri ya Mungu.

Baadhi yao hawaoni ulazima wa ibada isipokuwa kwa lengo hilo na hivyo hudai kuwa punde maono yanapopatikana, mtu anaweza kuhiyari kufanya au kutofanya ibada. Baadhi wanaona kusoma uradi ndilo jambo la lazima huku walipuuzia ubada za faradhi.

 KUNDI LA NNE – WAFUASI WA KWELI WA MUHAMMAD NA IBRAHIM

Kundi la nne ni kundi la wafuwasi wakweli wa Muhammad (saw) na Ibrahim (as). Wafuwasi wakweli wa Muhammad (saw) na Ibrahiim (as) ndio wanaomjuwa MwenyeziMungu., ndio wanaofahamu hikima ya Sharia za Mungu na ndio wanaotambua lengo na maana ya Ibada.

Makundi matatu ya mwanzo yamefungwa macho kutoiona njia sahihi kutokana na dhana zao potofu na zisizo na msingi wowote. Kundi hili la nne la wafuwasi wa kweli wa Mitume hao linajuwa barabara kuwa undani wa ibada, lengo la ibada na hikima ya ibada ni mambo yanayofahamika kwa wale tu wanaozijuwa sifa tukufu za MwenyeziMungu.

Hawa ndio wanaotambua dhati ya Uungu (uluuhiyyah) wa Allah, Mungu pekee wa kweli na wanajuwa kuwa ibada kwa MwenyeziMungu ndio lengo pekee aliloumbiwa binadamu, ndilo lengo ka kutumwa Mitume, ndilo lengo la kushushwa Vitabu vya ufunuo, ndilo lengo la kuumbwa kwa Pepo na Moto wa jahanamu.

“Je mlidhani ya kwamba tumekuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?” (23:115).

“Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu.” (51:56)

“Ambao humkumbuka MwenyeziMungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala. Na hufikiria umbo la mbingu na ardhi (‘Namna gani MwenyeziMungu alivyoumba’ na Kusema): “Mola wetu! Hukuviumba hivi bure. Utukufu ni wako. Basi tuepushe na adhabu ya Moto.” (3:191).

“Na mwenyeziMungu ameziumba mbingu na ardhi  kwa haki na ili  kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa. (45:22).

Kwa hiyo MwenyeziMungu kaeleza wazi kuwa kaumba ulimwengu kwa haki na haki hiyo inajumuisha maamrisho na makatazo Yake na malipo na adhabu itakayokuja ambayo itatokana na hayo.

Ikiwa basi ulimwengu mzima umeumbwa kwa ajili ya kumuabudia MwenyeziMungu, iweje tena mtu aseme kuwa hakuna sababu, lengo wala hikima ya Ibada kama linavyodai kundi la Jabariyya.?

Au ibada ni fidia tu ya malipo kwa neema tuzipatazo? Au ibada ina kazi tu ya kuziandaa nafsi zetu kwa ajili ya kupata utambuzi wa kiakili na kuacha shughuli nyingine?

Mdadisi anayetumia akili, mara moja, ataona kuwa hakuna pa kupenyezea hoja ya kuhalalisha mitazamo hii na kwamba makundi matatu ya mwanzo yamemvunjia heshima na kumkadiria visivyo MwenyeziMungu:

“Na hawakumuheshimu MwenyeziMungu heshima ipasayo. (39:67).

Undani wa ibada ni: Mapenzi kwa Allah Pekee. Usipende chochote zaidi ya Allah, na kisha mapenzi yako yote kwa wengine yawe kwa ajili ya Allah. Kuyapata mapenzi ya Allah kwajumuisha utekelezaji wa amri Zake na kuepuka makatazo Yake. MwenyeziMungu kafanya jambo la kumtii na kumfuata Mtume kuwa ndiyo sharti la kupata mapenzi Kwake.

“Sema, ‘Ikiwa nyinyi mnampenda MwenyeziMungu, basi nifuataeni; MwenyeziMungu atakupendeni na kughufirieni madhambi yenu. (3:31)

Kupenda kingine chochote zaidi ya MwenyeziMungu au Mtume Wake ni shirki. MwenyeziMungu Anasema:

Sema, “kama baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazoogopa kuharibikiwa na majumba mnayoyapenda; (ikiwa vitu hivi) ni vipenzi zaidi kwenu kuliko MwenyeziMungu na Mtume Wake na kupigania dini Yake, basi ngojeni mpaka MwenyeziMungu alete amri Yake, na MwenyeziMungu hawaongozi watu maasi (njia iliyonyooka).