Skip navigation.
Home kabah

Je, Una Mpango Gani Wa Maisha Ya Hapa Duniani?


Muhammad Shaykh ‘Umar

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ


Swali moja linalokera au kuudhi watu sana ni pindi mtu atakapokuuliza una mpango gani katika maisha yako? Au mtu akutamkie kuwa huna mpango wowote wa kimaisha. Ama uwe nao au usiwe nao bila shaka linaudhi.

Swali moja muhimu katika maisha ya mwanadamu ni kujiuliza nini lengo lakekatika maisha yake hapa duniani? Wewe unayesoma makala haya tafadhali acha kusoma makala haya kwa muda wa dakika moja na ujibu swali hili kwa uoni au imani yako …….

Je, maisha yako hapa duniani ni kwa ajili ya kusoma elimu ya kilimwengu ukiwa na matumaini ya kufaulu vizuri na kupata kazi nzuri na hatimaye ajira nzuri, na kuna ubaya gani kuwa na nia hiyo? Au ni kutafuta maisha mazuri kwa njia yoyote ile?

Tunatoa mapesa na muda wetu mwingi kuwasomesha watoto wetu elimu ya kilimwengu tu, tukitarajia wajitosheleze pindi watakapofikia umri wa kujitegemea kama ilivyo desturi yetu. Je, kwa lugha ya kidini huku kujitosheleza si ndiyo inayoitwa rizki?

Imani yetu inatuambia yakuwa hakuna mmoja wetu isipokuwa rizki yake imeshakadiriwa kabla hajatoka tumboni mwa mama yake. Mola wetu Amesema katika Qur-aan Tukufu,

 

NA HAKUNA mnyama yeyote katika ardhi ila rizki yake iko kwa Mwenyeezi Mungu. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha. (11:6)  

 

Mwenyeezi Mungu Humkunjulia rizki Amtakaye, na Humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo. (13:26)

 

Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia rizki zao! Mwenyeezi Mungu Anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye Ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. (29:60)

 

Amesema Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo Kutoka kwa AbuAbdur-Rahmaan   Abdullaah Ibn Masu'ud    (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye alisema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye ndie mkweli, anaesadikiwa alitueleza haya:

Hakika umbo la kila mmoja wenu linakusanywa pamoja katika tumbo la mama yake kwa muda wa siku arubaini, ikiwa katika hali ya mbegu, baadaye tone la damu kwa muda kama huo, tena huwa ni kipande cha nyama kwa muda kama huo, tena hupelekwa Malaika anayempulizia pumzi za uhai na anaamrishwa mambo manne:  kuandika rizki yake, maisha yake, amali yake na akiwa atakuwa (mtu) mbaya au mwema. Kwa Allaah ambaye hakuna Mungu isipokuwa Yeye, mmoja katika nyinyi hufanya vitendo vya watu wa peponi mpaka baina yake na pepo ikawa dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni.  Na mmoja katika nyinyi hufanya amali ya watu wa motoni mpaka baina yake na moto ikawa dhiraa, na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa peponi akaingia peponi. Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim.

Je, ndugu Muisilamu haya ndiyo malengo yetu tuliyoletwa kwayo hapa duniani? Bila shaka wengi wetu tulio na elimu chache ya dini tutakiri yakuwa dunia sio lengo letu bali lengo la kuwepo hapa duniani ni kuchuma kwa ajili ya maisha ya Akhera. Je si kweli matendo yetu na nia zetu zinaonyesha kinyume na hilo? Maisha yetu yote yamefungamana na PESA (Mali); kwa uzuri au kwa ubaya. Kunaye anayetarajia apate asaidie maskini, na mwengine awatambie maskini ‘alaa kulli haal, zinatushgulisha sehemu kubwa ya maisha yetu.

Swali linalofuatia sasa ni, je, unataka tuachane na hayo yote tuwasomeshe watoto wetu dini tu? Na swali hili linaulizwa kwa maana yakuwa kusoma elimu ya dini pekee ni kujitakia umaskini. Mimi binafsi sioni ubaya wowote. Lakini suala hili ndilo linalobainisha hali ya imani yetu juu ya RIZKI tunaelewa vyema ya kuwa rizki zetu zimeshakadiriwa Sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema katika Qur-aan Tukufu:

Sema: Hakika Mola wangu Mlezi Humkunjulia rizki na Humdhikisha Amtakaye. Lakini watu wengi hawajui. (34:36)

 

Mwenyezi Mungu Humkunjulia rizki Amtakaye, na Humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo. (17:26)

 

Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu Humkunjulia rizki Amtakaye na Humdhikisha Amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanaoamini. (30:37)

 

Imesimuliwa na Abu Ad-Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu) Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), Ameshaamua kwa kila mja wake katika viumbe Vyake mambo matano: Kifo chake, Matendo yake, makazi yake, maeneo yote atakayo tembelea na rizki yake. Imepokelewa na Ahmad. 

Ndugu Muislamu mifano ya kututhibitishia maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni mingi tuliyonayo ndani ya ulimwengu huu wa leo tunaoishi.

Tumeona Rais anatoka kwenye Urais hadi jela, kama ilivyotokea kwa Jenerali Noriega wa Panama. Na mwengine atoka jela hadi kwenye Urais (Nelson Mandela). Leo tunaye tajiri mkubwa duniani ambaye hakumaliza hata shule yake ya sekondari, naye ni mmiliki wa kampuni kubwa ya mambo ya kompyuta, bilioneya Bill Gates. Na mifano ni mingi wala haina idadi, na kila mtu anamjua mwengine kama huyo katika wale wanaosemwa hii leo ‘aliyebahatika kwa utajiri wa mali’.

Ndugu Muislamu tujaribu kutofautisha IMANI na ELIMU, ni kweli imani inahitaji elimu lakini mtu anaweza kuwa na elimu lakini asiwe na imani. Sote tunajua/tuna elimu kuwa anayeturuzuku ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), vipi basi tunatetereka tena? Jawabu ni kuwa, ima hatuna imani, au imani yetu ni dhaifu sana.

Vipi tutaepukana na janga hili?

Ni umbile la mwanadamu kupenda maisha mazuri na vinavyonasibiyana kwayo. Hata huko kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni kwa ajili ya kutaraji hayo maisha mazuri (Pepo) na kuepukana na maisha mabaya (Jahanamu). Mpaka tubadilishe desturi tuliyokuwa nayo ya kuweka maslahi ya huu ulimwengu tunaoishi zaidi ya huko tunakokwenda (Akhera). Kwa lugha nyingine, tubadilishe lengo. Lengo letu lisiwe mapato ya hapa duniani bali kila kitu tutachotaka kukifanya hapa duniani tufikirie kesho Akhera. Na mambo yote inshaAllaah yatakaa vizuri yenyewe. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wanasema katika Aayah na Hadiyth zifuatazo:

Na Anayemcha Mwenyeezi Mungu Humtengezea njia ya kutokea (65:2)

 Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. Na anaye mtegemea Mwenyeezi Mungu Yeye Humtosha. Hakika Mwenyeezi Mungu Anatimiza amri Yake. Mwenyeezi Mungu Kajaalia kila kitu na kipimo chake. (65:3)

Na anayemcha Mwenyeezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi. (65:4)

Imesimuliwa na ‘Umar ibn al-Khatw-Twaab (Radhiya Allaahu 'anhu), kwamba alimsikia Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ukiweka imani yako kikamilifu kwa Allaah, atakuandalia rizki yako kama vile Alivyowaandalia ndege. Ndege wanatoka asubuhi na hali hawana kitu matumboni mwao na jioni wanarudi hali yakuwa yamejaa” Imepokelewa na At-Tirmidhiy.

Ndugu mpendwa Muislamu, kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) sio kukesha usiku kucha kwa ibada tu bali khaswa ni kufuata aliotuamrisha na kuacha aliotukataza.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliyekuumba wewe na mimi Anasema:

Nami Sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. (51:56)

 

Ndugu mpendwa, hili ndilo lengo letu la kuwepo hapa duniani na sio kutafuta mali tu. Hebu tuchukulie mfano wa maneno kama umri ungekuwa miaka elfu. Leo hii mtu akikuambia mfanyie kazi kwa muda wa miaka mia na ujira wako utalipwa kwa muda wa miaka 900 iliyosalia. Bila shaka hakuna atakayepinga kuwa huu utakuwa ujira mzuri sana usio na kifani. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuandalia ujira zaidi ya huo, si miaka elfu tu, wala miaka laki moja au milioni moja, bali ni milele. Ndugu mpendwa Muislamu kweli tunaridhia kuterekeza ujira wa milele kwa hii miaka sitini au sabini ya hii duniya?

Halahala ndugu mpendwa Muislamu, imani si matamanio bali ni matendo.

Ewe Mola wetu! Twakuomba Tujaalie ni katika wale wenye kusikia maneno (mengi) na kufuata yale yaliyo mazuri.