Skip navigation.
Home kabah

Umuhimu Wa Zakaah - 3: Zakaah Ya Mapambo Ya Dhahabu

 

 

 

Abu ‘Ammaar

 

ZAKAAH YA MAPAMBO YA DHAHABU

Mapambo ya dhahabu ni suala bado linawapa utata akina mama wa Kiislamu kuhusu hukmu yake kisheria kwa sababu ya kuwa na rai tofauti kama ni wajibu kutoa Zakaah au si wajibu.

Tumezungumzia Dhahabu kwa sababu ndiyo pambo lilokuwa maarufu miongoni mwa jamii za Kiislamu wanaozungumza Kiswahili.

Tofauti hizi zimekuja kutokana na kupokewa Hadiyth kutoka kwa Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) ambazo zinaeleza hukumu tofauti.

 

Rai ya kwanza: Ni wajibu kutolewa Zakaah

Kutokana Hadiyth ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam):

  

Mama mmoja alikuja kwa Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na mwanawe wa kike ambae amevaa bangili nzito za dhahabu mkononi mwake, Mtume alimuuliza; “je umezitolea zaka hizo?” Akasema; “laa,” Akamuuliza tena, “je utapenda Allah siku ya Qiyaama kukupa bangili za moto mikononi mwako?” Yule mama akazivua na kumpa Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na akasema anazitoa kwa ajili ya Allah na Mtume Wake ( kwa ajili ya kutumika kwa njia aya Allah)

Na pia imepokewa kutoka kwa Bi Ummu Salamah, Allah (Amuwie radhi), kwamba:

كنتُ ألبس أوضاحًا من ذهبٍ  فقلت: يا رسول الله، أكنزٌ هذا؟ فقال: ما بلغ أن تُؤدَّى زكاته فزُكِّيَ فليس بكَنْزٍ. رواه أبو داود والحاكم

Nilikuwa nikivaa dhahabu inayong’aa ni nikamuuliza Mtume; “Je hii ni hazina? Akasema Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam): “Kitakachotimia kiwango basi kitoe Zakaah na si hazina” Abu Daaud na Al Haakim.

 

Na pia imenukuliwa kutoka kwa Bi Aishah, Allah (Amuwie radhi), kwamba

"دخل عليَّ النبي ـ صلى الله عليه وسلم ـ فرأى في يدي فَتَخَاتٍ من وَرِقٍ (فقال: ما هذا يا عائشة؟ قلت: صنعتُهنَّ أتَزَيَّنُ لكَ يا رسول الله. قال: أتُؤَدِّينَ زكاتَهُنَّ؟ قلت: لا. قال: هو حسبك من النار"    

. رواه أبو داود والحاكم

Siku moja aliingia Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) (katika chumba changu) akaona katika vidole vyangu pete nzito ya fedha na akauliza: “Ni kitu gani hiki Ewe ‘Aishah?” Nikasema: “Nimezitengeneza kwa ajili yako ewe mjumbe wa Allah” Mtume akauliza: “Je unaitolea Zakaah yake?” Nikasema: “Hapana” Mtume akasema: “Adhabu yake ya motoni itakutosha” Abu Daaud na Haakim.

 

Rai ya pili: Si wajibu kutolewa Zakaah

Kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na Maalik kwamba:

أن عائشة كانت تَلِي بنات أخيها يتامَى في حِجْرها ولهنَّ الحُليُّ فلا تُخرج عنه الزكاة

Bi Aishah alikuwa akiwalea watoto wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na wala hakuwa akiyatolea Zakaah

 

Na pia imepokewa na ‘Amr bin Diinaar, Allah (Amuwie radhi), akisema

 ـ قال: سمعتُ رجلًا يسأل جابر بن عبد الله عن الحُليِّ، أفيه زكاة؟ قال: "لا. قال: وإنْ كان يبلغ ألف دينار؟، قال: وإنْ كثُر". (رواه الشافعي والبيهقي).

Nilimsikia mtu akimuuliza Jaabir bin Abdillahi kuhusu mapambo: je yanatolewa Zakaah? Akasema: “Hapana” Akasema hata ikifikia Diinaar elfu moja? Akasema “hata kuzidi” Ash-Shaafi’iy na Al-Bayhaqiy

 

Pia aliwahi kunukuliwa Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akisema kuwaambia akina mama:

                  "تَصدَّقنَ ولو من حُلِيِّكُنَّ"

Toeni sadaqa japo katika mapambo yenu

 

Wanasema Maulamaa lau kama ingelikuwa ni wajibu basi Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) asingepigia mfano wa mapambo katika ibadah ya Tattawau’ (isiyokuwa wajibu).

 

Rai ya tatu: Hutolewa mara moja tu kuitoharisha kisha haitolewi tena

Kauli hii imepokewa kutoka kwa Anas, Allah (Amuwie radhi), kama ilivyosimuliwa na Bayhaqiy.

Hata hivyo kauli hii si mashuhuri sana na ni kauli mbili zilizotangulia ambazo hutumika. Hata hivyo kuna baadhi ya Maulamaa wanaitumia kauli hii katika hukmu ya Zakaah ya mapambo.

Sababu ya kutofautiana ni kama riwaya ziolivyokuja tofauti. Katika kauli za Maulamaa wa zamani ni Abu Haniyfah pekee aliyewajibisha Zakaah katika mapambo ya dhahabu na Maalik, Shaafiy na Ahmad bin Hanbal wote walisema haipaswi kutolewa Zakaah kwa sababu ni mapambo hivyo hayapaswi kupewa hukmu ya dhahabu safi ya biashara au yenye malengo mengine.

Hata hivyo Maulamaa wa karibuni wengi wao wamekubaliana na hukmu ya Abu Haniyfah kwamba mapambo ni wajibu kutolewa Zakaah kwa mujibu wa Hadiyth zilizothibiti. Sh. Yusuf Qardhawi amekubaliana na rai ya Jamhuur Ulamaa kwamba si wajibu kutolewa Zakaah katika kitabu chake mashuhuri cha Fiqh Zakaah.

Na kwa upande wetu tunapendekeza ikiwa dhahabu ya mapambo ya mwanamke itakuwa imefikia kiwango basi ni bora kuitolea Zakah kuliko kuacha kuitolea kwa sababu ya kuepukana na hizi tofauti kwani ikiwa ni sawa basi utakuwa tayari umeitekeleza nguzo na ikiwa si sawa mali yako itakuwa imetolewa katika njia ya sadaqa. Tofauti na kama haijatolewa kwani ikiwa ni sawa basi ni kheri na vyema na ikiwa si sawa basi yawezekana kuwa na dhimma  ambayo huenda  tukaulizwa siku ya Qiyaama.

Hata hivyo ikiwa mapambo haya hayakutolewa Zakaah basi kuna miongoni mwa masahaba, mataabiina na wanazuoni ambao hawakujuzisha Zakaah kwenye mapambo ya mwanamke ikiwa ni kwa ajili ya kujipamba tu.

 

 

MAPAMBO

Mapambo ya dhahabu kwa akina mama siku hizi yamekuwa yanatumika kwa njia zaidi ya moja. Kwani yakinunuliwa kwa ajili ya mapambo tu ni sawa lakini hapo hapo hununuliwa kwa ajili ya akiba (asset) basi tayari nia na makusudio yamebadilika na pia baadhi ya Maulamaa wameweka masharti kwa mapambo haya kama ifuatavyo:

1.     Yawe ni kwa ajili ya kujipamba tu na kusiwe na malengo mengine ndani yake.

2.     Yasizidi mazoea na utamaduni wa jamii husika katika uvaaji yaani yasikithiri ada na utamaduni husika.

3.     Angalau yavaliwe katika mwaka japo mara moja na kama hayakuvaliwa basi yataingia katika hukmu ya akiba (asset) au yaazimishwe katika mwaka ule ili yaepukane na hukmu ya kuwa hazina ikiwa hayajatumika kwa mwaka mzima.

 

DHAHABU YOYOTE HUTOLEWA?

Dhahabu imegawika katika ubora. Kuna iliyo safi zaidi na kuna iliyochanganywa. Dhahabu inayopaswa kutolewa Zakaah ni iliyo safi au hata kuchanganywa lakini mchanganyiko huu dhahabu huwa ni nyingi zaidi kuliko madini mengine.

Kwa kufafanua zaidi tuangalie ubora wa dhahabu kwa kipimo chake cha kitaalamu kinachoitwa “Karat”

KARAT

ASILIMIA YA DHAHABU

MAELEZO                            HUKUMU

24

100%

Hii ni dhahabu safi na laini sana na mara nyingi huchanganywa na shaba

Inatolewa Zakaah

22

91.7%

Bado huwa laini kwa mapambo mengi hivyo huchanganywa

Inatolewa Zakaah

18

75.0%

Ni dhahabu inayotumika sana kutengenezea mapambo bila ya kuchanganywa na madini mengine

Inatolewa Zakaah

12

50.0%

Hutumika mara chache kutengenezea mapambo

Inatolewa Zakaah

10

41.7%

Dhahabu ni chini ya asilimia 50

Haipaswi kutolewa Zakaah

 

Hukumu ya kisheria ni kwamba dhahabu yoyote itakayozidi asilimia 50 basi huhesabika kama ni dhahabu safi na inapaswa kutolewa Zakaah ikiwa itakuwa imefikia kiwango na kutimiza masharti mengine yanayohusiana na Zakaah bila ya kujali mchanganyiko uliopo.

 

 

ANAYEPASWA KUITOA ZAKAAH YA MAPAMBO

Kwa mujibu wa sheria Zakaah kwanza hutolewa katika jinsi ya kitu chenyewe. Hivyo kisheria kama mtu ana dhahabu basi itabidi itolewe dhahabu ila tu Maulamaa wameruhusu kutolewa thamani yake hasa wakati huu kwani ni munasaba zaidi kwa mlengwa atakayepewa Zakaah (mafakiri na masikini na wengineo).

Na atakayepaswa kuitoa Zakaah ni mwenye kuimiliki mali kama tulivyoona kwenye masharti yanayomuawajibikia mwenye kutoa Zakaah. Hivyo ikiwa mapambo ni ya mwanamke basi ni wajibu kwake kutoa Zakaah na ikiwa ni ya mtoto mdogo na yametimia kiwango yatatolewa kwa niaba yake. Na hapa ieleweke kwamba si sahihi kuchanganya mapambo ya dhahabu ya mama na mtoto/watoto katika kujua uzito/uzani wa dhahabu bali kila moja itapimwa kivyake. Na kama ikipimwa kwa upande wake hayatotimia kiwango basi kimsingi wote hawajatimiza masharti na hivyo si wajibu kwao kutoa Zakaah.

Ikiwa mume atataka kumtolea Zakaah mkewe inakubalika kisheria ikiwa atamjulisha na kutia nia kwa ajili hiyo. Na mume atalipwa ujira wake kwa kutoa Sadaqa kumsaidia mkewe kuweza kuitekeleza nguzo. Hata hivyo mume wakati wa kusaidia asikusudie kama yeye ndiye anaitoa Zakaah kwa niaba ya mkewe kwani si wajibu kwake.

Hali hii inaweza kujitokeza pale ambapo mke anaweza kuwa anamiliki mapambo ya dhahabu lakini hana kitu chengine cha kuitolea Zakaah yake. Kwani kisheria atapaswa kutoa sehemu ya dhahabu yake (2.5%) kama Zakaah ima kwa kwenda kuipunguza au kutafuta mtu wa kuweza kumsaidia kutekeleza wajibu wake.

 

 

HUTOLEWA THAMANI YAKE AU UZANI?

إن الذهب لا يؤخذ منه شيء حتى يبلغ عشرين دينارا فإذا بلغ عشرين دينارا ففيها نصف دينار‏,

رواه أحمد  وأبو داود  والبيهقي  وصححه  البخاري

Hakika dhahabu haitolewi kitu mpaka ifikie Dinari 20 ambapo hutolewa (Zakaah) nusu dinari… Ahmad Abu Daawuud na Al-Bayhaqiy na imesahihishwa na Al-Bukhaariy

Kwa mujibu wa Hadiyth hii kinachoangaliwa ni uzani wa dhahabu na sio thamani yake. Na Nisaab kwa dhahabu ni Mithqaal 20. Zilipimwa Dinari za kizamani (Dinari zote zilizopimwa tokea enzi za Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) zilikuwa na uzani takriban unaolingana) na uzito wake kila dinari moja ni gramu 4.25. Hivyo ukizidisha mara 20 ni gramu 85.00.

Hivyo dhahabu ikipita mwaka na tayari imevuka Nisaab basi hupimwa uzito wake wakati wa kutolewa na kisha kuangaliwa bei ya dhahabu kwa wakati ule ni kiasi gani.

Hivyo dhahabu ikipita mwaka na tayari imevuka Nisaab, hupimwa uzito wake wakati wa kutolewa na kisha kuangaliwa bei ya dhahabu kwa wakati ule ni kiasi gani.

Kwa mfano hivi Septemba 2007 bei ya dhahabu mpya kwa wakia (troy ounce) moja hapa Uingereza ni £362.00.

Na wakia moja ni sawa na gramu 31.00 au gramu moja ni sawa na £12 takriban.

Mfano:

Nina dhahabu gramu 220.

220×12 = £ 2640 (Thamani ya dhahabu kwa bei iliyopo)

Kiwango cha Zakaah kinachotolewa ni:

£ 2640 × 2.5 = £ 66.00 (ndicho kiwango nitakachopaswa kukitoa)

 

 

HUTOLEWA DHAHABU YENYEWE AU THAMANI YAKE?

Asli ya kutolewa Zakaah ni kutolewa jinsi ya kitu chenyewe. Hata hivyo Maulamaa wamejuzisha kutolewa thamani yake kwani ndiyo itakayokuwa na manufaa zaidi kwa mlengwa kuliko dhahabu yenyewe.

Ni vyema kwa mwenye kutaka kutoa Zakaah kupima na kujua thamani ya mapambo yake na kuhakikisha anatoa kiwango kinachostahiki.

 

 

HUTOLEWA THAMANI YA DHAHABU ILIYOTUMIKA AU MPYA?

Thamani inayotolewa ni ya dhahabu inayopaswa kutolewa Zakaah na si thamani ya dhahabu mpya. Hivyo thamani ya iliyotumika ndiyo ya kuzingatiwa kwa kwenda kuitia thamani kwa sonara au kwa mtaalamu wa vyombo vya mapambo. Hivyo thamani ya dhahabu hii inawezekana kupungua mwaka hadi mwaka endapo itafikia au kupita gramu 85 za dhahabu safi.

Tanbihi:

Thamani inayoangaliwa kama dhahabu ile itauzwa kwa wakati ule na si thamani ya sonara au mtu mwengine ambaye labda akiinunua ataweza kuiuza kwa bei ya juu zaidi.

Kwa mfano uliopita dhahabu gramu 220 iliyotumika

Thamani ya gramu  moja ya dhahabu iliyotumika ni £8.00

£220 × 8 = £1760

Kiwango kinachotolewa:

£1760.00 × 2.5 = £ 44.00

 

 

HUKUMU YA DHAHABU ILIYOKAA MUDA MREFU BILA YA KUTOLEWA ZAKAAH

Kama Muislamu amenunua mapambo ya dhahabu lakini hajayatolea Zakaah kwa muda wa miaka mingi vipi hukmu yake ni kuitoa kwa miaka yote iliyopita au kuanza kuitoa kwa mwaka atakapoamua kuitolea?

Kwa kuwa suala hili wametofautiana Maulamaa hivyo kutokutoa Zakaah kwa mapambo pia ni moja katika kauli za Maulamaa hivyo hatopaswa kutoa Zakaah kwa miaka iliyopita bali atawajibika kuanza mwaka ambao ameona au kuamua ni wajibu au kuwa na hadhari kwa kutoa.

 

 

KUBADILISHA DHAHABU KWA DHAHABU NYENGINE NDANI YA HAWL

Ikiwa mwenye kuimiliki mapambo ya dhahabu, akauza na kununua au kubadilisha nyengine katika Hawl hatopaswa kuanza mwaka mwengine wa Zakaah bali ataendelea na hesabu yake ya mwaka wake wa Zakaah alioanzia. Kwa sababu ya asli ya kilichopo na kilichobadilishwa ni kitu hicho hicho (dhahabu kwa dhahabu) endapo tu kilichonunuliwa au kubadilishwa kitakuwa pia kimetimia au kuvuka kiwango cha mwanzo kutolewa.

Laa kama ni kitu chengine kisichokuwa dhahabu, mwaka wa Zakaah utakatika na kuanza tena kwa kitu kilichobadilishwa ikiwa ni miongoni mwa vitu vinavyopaswa kutolewa Zakaah.

 

 

DHAHABU YA KUCHOVYWA (GOLD PLATED)

Hukmu ya mapambo ya dhahabu ya kuchovywa itategemea na kiwango cha dhahabu kilichomo kwa mujibu wa maelekezo tuliyoainisha kwenye ubora wa dhahabu (karat). Ingawa kawaida ya dhahabu iliyochovywa asilimia kubwa huwa ni madini mengine yasiyokuwa dhahabu.

Hivyo ikithibitika kwamba asilimia kubwa iliyomo si dhahabu haitopaswa kutolewa Zakaah kwa kutotimiza masharti.

 

Itaendelea InshaAllaah…